Na FRANCIS MAWERE
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliamua kuanzisha mfumo wa kiuchumi
wa Ujamaa na Kujitegemea miaka michache baada ya Tanganyika kujipatia
uhuru wake.
Kwa kufanya hivyo alikuwa ameamua kufuata mawazo ya akina Adam Smith,
David Ricardo, Milton Friedman, Fredrich Hayek, Ayn Rand Robert Owen,
Pierre Leroux na Karl Marx kwa kuwataja kwa uchache; ambao wanatajwa
kama waasisi na watetezi wa Ujamaa.
Hii ni kwamba aliamua kusimama kinyume na mawazo ya ubepari ya akina
Stuart Mill, Albert Einstein, George Bernard Shaw, Leo Tolstoy na Emma
Goldman ambao katika anga za uchumi wanaheshimika kuwa waasisi na
watetezi wa ubepari.
Mwalimu Nyerere alitumia muda, akili na nguvu nyingi sana kuwasilisha
na kuwashawishi Watanzania kuupokea na kuukubali Ujamaa na Kujitegemea.
Mambo hayakwenda vizuri katika pande mbili. Mosi, kutokana na hali ya
uchumi wa kidunia na nafasi ya Ujamaa kwa wakati huo duniani;
utekelezaji wa sera za Kijamaa ulikuwa ni wa kutoa jasho mno. Pili,
Watanzania wengi waliupokea Ujamaa na Kujitegemea kwa shingo upande na
wale walioupokea kwa moyo mweupe inaonekana hawakumuelewa vizuri Mwalimu
Nyerere.
Upande wa kwanza ni nafasi ya Ujamaa duniani wakati Mwalimu Nyerere
alipokuwa anauleta Ujamaa uliokolezwa mapambo (Ujamaa na Kujitegemea)
hapa Tanzania. Ukweli ni kwamba hadi kufika miaka ya 1950 tayari Ujamaa
ulishakuwa kwenye hali mbaya ya kumalizikia kuanguka. Hii ina maana
Mwalimu Nyerere alikuwa anajaribu “bahati” ya kuijenga Tanzania imara
kiuchumi kwa kutumia mfumo wa uchumi ambao ulishakuwa katikati ya
changamoto kali sana za kushindwa.
Ushahidi wa kushindwa kwa Ujamaa katika miaka hiyo, tunaupata kutoka
kwa mataifa ambayo tunaweza kuyaita waasisi na miamba wa Ujamaa duniani.
Gazeti la Urusi liitwalo Pravda, Mei 1988 liliandika habari ya kitafiti
kuhusu hali tete ya uchumi wa Umoja wa Nchi za Urusi (USSR) kutokana na
kufuata sera za Ujamaa.
Katika habari hiyo, Pravda ilithibitisha kuwa matarajio ya Wajamaa
yanazidi kuyeyuka kutokana na matokeo mabaya kwenye uchumi. Kwa mfumo,
ilielezwa kuwa kati ya sekta 170 zilizoainishwa kuboreshwa na Ujamaa wao
hakukuwa hata na moja iliyofanikisha malengo walau kiasi cha
kuridhisha. Gazeti hilo lilihitimisha kwa kusema kuwa mfumo wa Ujamaa ni
sawa na machafuko yaliyokusudiwa.
Si hivyo tu, bali nyuma kabisa hapo mwaka 1920 wakati wa utawala wa
Lenins Bolsheviks kule Urusi, tayari wanauchumi wengi akiwamo
mwanauchumi wa Kiaustralia, Ludwig von Mises, walieleza kwa kina kuwa
Ujamaa ulishakuwa umeanguka.
Kwenye machapisho yake mawili maarufu sana, Economic Calculation in
the Socialist Commonwealth na Socialism, An Economic and Sociological
Analysis, Mises anasema kuwa kutokana na tabia, tamaduni, mazoea na
asili ya mwanadamu; kufanikisha Ujamaa ni sawa na kutengeneza sanamu
kisha kutaka uipe uhai.
Tunafahamu kuwa vita kubwa ya wafuasi wa Ujamaa na wale wa ubepari
chimbuko lake kubwa ni mgawanyo wa rasilimali zilizopo katikati ya
wanajamii. Ubapari wenyewe unasifa ya kuruhusu watu binafsi kuendesha
uchumi kwa watu binafsi kumiliki njia kuu za uzalishaji.
Kwenye ubepari, serikali inatakiwa kubaki kama mwangalizi tu na
inapaswa kuliacha soko kuamua. Wakati Ujamaa wenyewe unasisitiza kuwa
njia kuu za uchumi ni lazima zimilikiwe kwa pamoja na serikali iwe na
mamlaka kamili ya kuingilia chochote katika mwenendo wa kiuchumi.
Hapa ndipo penye kasheshe kubwa. Wale wapinzani wa Ujamaa huwa
wanaenda mbali na kumnanga Karl Marx na kusema kuwa hakuwa na sababu za
kiuchumi kuasisi Ujamaa. Marx yeye aliona kuwa ubepari ulikuwa
ukilinyonya tabaka la wafanyakazi hivyo alipofikiria Ujamaa alisema
utakuwa ni mfumo ambao utamlipa kila mtu kwa kadiri ya anavyofanya kazi.
Pengine tuanzie hapa kuutazama Ujamaa wa Mwalimu Nyerere hasa
tukiangalia ule upande wa pili wa namna ambavyo ulipokewa kwa shingo
upande na namna ambavyo haukueleweka. Mwalimu Nyerere alipoibuka na
mfumo wa Ujamaa aliuongezea viungo kwa kuuita “Ujamaa na Kujitegemea”,
lengo lake lilikuwa ni kuona Tanzania kama taifa likisimama na kumudu
mahitaji yake na ya watu wake pasipo kutegemea fadhila, kuombaomba ama
misaada.
Yakafanyika mambo mengi lakini makubwa mawili ni kuanzishwa kwa Vijiji
vya Ujamaa na kutaifishwa kwa mali binafsi kuwa za umma. Nia ilikuwa
nzuri lakini matokeo ya hatua hizi mbili hayakuwa mazuri pengine kwa
sababu wananchi hawakuuelewa vema huu Ujamaa na Kujitegemea.
Kutokana na hili, maelfu ya wananchi hasa wale waliohamishwa makazi,
waliopoteza mifugo yao, waliotakiwa kuacha mashamba na mazao yao na
kwenda kwenye vijiji vya ugenini waliuchukia Ujamaa na Kujitegemea
katika hatua za awali kabisa. Hata ubinafsishaji wa mali binafsi
zikiwamo hospitali, shule, viwanda, kampuni na mashirika ulileta
kizaazaa kwa sababu wamiliki wake walikuwa na wafuasi wengi na kama
hawakuridhika basi na wafuasi wao waliuchukia Ujamaa na Kujitegemea
ungali unaanza.
Pamoja na hilo inaonekana wananchi walioupokea Ujamaa na Kujitegemea
walielewa kipengele kimoja tu cha Ujamaa lakini hiki cha Kujitegemea
inaonekana hakikueleweka kabisa. Ili useme taifa linajitegemea ina maana
kuwa wananchi wanajitegemea. Kwenye Ujamaa na Kujitegemea serikali
ilihodhi njia kuu za uchumi na miundombinu ya kijamii, huku wananchi
wakibaki kufanya kazi “kijamaa”.
Suala hili lilisababisha wananchi wengi kama si wote kuitegemea
serikali kwa mambo mengi ikiwamo upatikanaji wa elimu, huduma za afya,
miundombinu na mengineyo. Serikali iliendelea kufurukuta kuwapa wananchi
bure huduma za kijamii hadi ikafika mahali ikajikuta haina ujanja tena.
Ndipo pale mahali Mwalimu Nyerere alipoamua kung’atuka na ghafla bin
vuu nchi ikawa haina ujanja zaidi ya kujisalimisha kwenye makucha ya
Benki ya Dunia (WB) na Shirika na Fedha (IMF).
Ilikuwaje Taifa la Ujamaa na Kujitegemea likashindwa kujitegemea? Jibu
ni rahisi. Ni kwa sababu wananchi wake katika ngazi ya mtu mmoja mmoja
walikuwa hawajitegemei. Badala yake walikuwa wakiitegemea Serikali kwa
kila kitu. Jambo hili halikutokea kwa bahati mbaya na wala halikutokana
na ubovu wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, isipokuwa una chimbuko lake
kutoka katika saikolojia na tabia za kibinadamu kama alivyosema
mwanauchumi Mises.
Kosa kubwa lililofanyika katika mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea ilikuwa
ni kutafuta usawa wa kijamii na kiuchumi kwa watu wote. Kiasili kila
mwanadamu ameumbwa tofauti na kupewa upeo, vipawa, karama, uwezo,
matarajio na maono yanayotofautiana. Tena kiasili mwanadamu hutafuta
kuwa tofauti, kufanya lile alipendalo na kutambuliwa na kujulikana kwa
yale ayafanyayo.
Hapa kwenye karama, maono, vipawa ndipo mahali ambapo humuwezesha
mwanadamu kusoma mazingira yake, kuangalia matatizo yaliyopo na
kuyatafutia ufumbuzi kwa kutumia karama, vipawa, maono na uwezo wake.
Namna hii ya utatuzi wa matatizo na changamoto ndiyo msingi na chimbuko
la ujasiriamali (Intrinsic Entrepreneurship).
Mchumi na mwanasaikolojia wa kale, John Stuart Mill, katika kitabu
chake cha Principles of Political Economy (1848) anasema, “Ukimlazimisha
mwanadamu awe sawa na wengine, afanye kila kitu kwa kuamuliwa na
mamlaka, basi atakuwa na hulka zifuatazo: Atakuwa mtu anayefanya mambo
nusunusu (passive), hatafanya mambo makubwa zaidi ya yale wanayofanya
wenzake hata kama ana uwezo na kubwa kabisa hataona umaana wa
kujipambanua katika kazi kwa sababu iwe atafanya sana ama atafanya
kidogo, maslahi anapata yale yale.”
Hapa ndipo mahali Ujamaa na Kujitegemea ulipoua vipawa vingi vya
kijasiriamali. Wafanyakazi hawakuona umuhimu wa kufanya zaidi, wananchi
hawakuwa na sababu ya kufanya zaidi kwa sababu Serikali ilitoa kila kitu
na vile vile ilikuwa na utaratibu unaobana unapotaka kufanya biashara.
Mathalani, ule mtindo wa kumbana mtu na kutaka ajieleze namna
alivyofanikiwa hata akajenga nyumba ama kununua kitu cha thamani
ulizalisha woga miongoni mwa Watanzania wengi.
Kivuli cha woga ule kinatutafuna hadi sasa, ndiyo maana nchi hii mtu
anapofanikiwa kiuchumi watu hawamuamini, wanamtilia shaka; eidha
watasema ni fisadi ama ni mshirikina ama ni mwizi. Ujamaa na Kujitegemea
ingawa haukuandika katika maandishi ya sera zake, lakini ulihesabu mtu
kuwa na utajiri kama “dhambi na unyonyaji”.
Kule Magharibi walianza kutumia msamiati wa ujasiriamali miaka ya
1700! Sisi Tanzania msamiati huu ndiyo kwanza unavuma miaka hii ya 2000.
Dhana ya ujasiriamali iliasisiwa na ubepari. Tulipokuwa tunacheza ngoma
ya Ujamaa na Kujitegemea tuliuita ubepari ni unyama. Kwa lugha nyepesi
ni kuwa Ujamaa na Kujitegemea ulipenyeza imani vichwani mwa Watanzania;
ya kuamini kuwa “ujasiriamali ni unyama”.
Hili tunaweza kulithibitisha kwa kutazama kile ambacho Watanzania
tunafahamu kuhusu ujasiriamali. Wengi wa Watanzania bado
wanashangaa-shangaa, wanasikiasikia tu lakini wanahisi kuwa ujasiriamali
si kitu kinachowahusu. Jirani zetu Wakenya ambao wamekuwa wabepari
nyakati zote; hadi watoto wa shule za msingi wananunua hisa katika soko
lao la hisa Nairobi. Sisi hapa Tanzania wasomi wetu wanahitimu vyuo
vikuu hawajui hata ABC hisa achilia mbali uwezo wa kutumia maarifa
waliyopata kujiajiri.
Nihitimishe kwa kusema kuwa kushindwa kwa Ujamaa na Kujitegemea
hakuwezi kuhesabiwa moja kwa moja kama ni kushindwa kwa Mwalimu Nyerere;
kwa sababu Ujamaa ulishakuwa umeshindwa kabla hata Mwalimu Nyerere
hajabuni Ujamaa na Kujitegemea.
Wachumi wanatuthibitishia kuwa miundombinu ya Ujamaa ndiyo chimbuko la
kuanguka kwake. Na moja ya sababu za kudondoka kwa viwanda na mashirika
mengi ya umma ilikuwa ni kushindwa kuzalisha kwa kuangalia mahitaji na
matakwa ya watumiaji (soko).
Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi tunapoendelea kumuenzi Mwalimu