Showing posts with label KITAIFA. Show all posts
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts

05 January, 2016

Serikali Yanunua Mashine Mpya Ya CT-Scan Katika Hospitali Ya Taifa Ya Muhimbili

Serikali imenunua mashine  mpya ya CT-Scan yenye thamani ya  takriban dola  za Marekani milioni 1.7  yenye  uwezo wa hali ya juu kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali  katika Hospitali  ya Taifa ya Muhimbili(MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Ununuzi wa mashine hiyo, umefanyika kufuatia agizo la Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoifanya hivi karibuni ambapo aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma zake na kuhakikisha vifaa tiba na dawa   vinapatikana ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya.

Hayo yamegundulika jana baada ya ziara ya Naibu  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi  Kingwangala aliyoifanya jana katika hospitali hiyo, ambapo alitembea Idara ya  Magonjwa ya Dharura,Idara ya Mionzi,  sehemu  mpya ya wagonjwa waliopo chini ya ungalizi maalum(ICU), ambayo inafanyiwa ukarabati na wodi mojawapo.

Akizungumzia kuhusu mashine ya CT-Scan Mkuu wa Idara ya Mionzi, Dkt. Flora Lwakatare alisema mashine hiyo , iliyotengenezwa na kampuni ya  Siemens  mpya imefungwa siku mbili zilizopita na imeshaanza kufanya majaribio  kwa wagonjwa 26  tangu ilipofungwa.

 Dkt. Flora aliongeza kwamba mashine hiyo iko moja tu nchini na katika nchi za Afrika Mashariki nchi nyingine iliyonunua mashine hiyo ni Kenya katika Hospitali ya Aghakhan.

“ Mashine hii inatoa huduma za hali ya juu kwa magonjwa ya moyo, ubongo, tumbo, kifua na inauwezo wa kupima kifua na tumbo kwa sekunde sita,” alisema.

Akizungumzia kuhusu mashine hiyo Naibu Waziri huyo, alisema imenunuliwa kwa fedha za Serikali wala sio mkopo.

“Tunatarajia kununua mashine hii katika hospitali ya Dodoma na Mwanza,” alisema Waziri Kingwangala.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Laurence   Maseru alisema mashine hiyo ina sahani 128 mara 2 ikilinganishwa na iliyokuwepo ambayo ilikuwa inatumia  sahani sita.

 Kwa upande wa mashine ya MRI alisema tangu ilipofanyiwa matengenezo makubwa Novemba 26, mwaka jana  hadi sasa imesha hudumia wagonjwa 560.

 Dkt. Kingwangala  alitembea katika Idara  cha huduma za dharura na kuangalia jinsi huduma zinavyotolewa, ambapo alielezwa na  Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura Dkt. Juma Mfinaga kuwa huhudumia wastani wa wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku na wanafanya kazi kwa kutumia mfumo maalum wa kompyuta bila kutumia karatasi.

Naibu Waziri huyo, mbali na kupongeza maboresho yaliyofanyika na huduma nzuri, alitoa maagizo kwa uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma  zinazotolewa hospitalini hapo kuwa za kitaifa zaidi.

 Alitolea  mfano  huduma  kulipa kwa kuongeza vitanda na matumizi ya choo kimoja kila chumba ili kuweza kuvutia wateja.

 “Sisi tunaweza kufanya biashara kwa kuboresha huduma za kulipa ili zimpendeze na kuvutia wateja. Na fedha zitakazopatikana zitatumika kununua dawa , vifaa tiba na kuwapatia wafanyakazi motisha, "alisema.

Aliutaka uongozi huo pia kuhakikisha inawalipa wafanyakazi fedha za  malipo ya ziada kwa wakati ifikapo tarehe 25 ya mwezi unaofuata,kutumia mfumo wa kompyuta sehemu zote, kupunguza msongamno wa wagonjwa na kuwa wabunifu.

04 January, 2016

Waziri Mbarawa Atoa Siku Tatu Ukarabati Reli Ya Kati Iliyosombwa na Mafuriko


Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka watendaji wa Shirika la Reli nchini (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (RAHCO) kuhakikisha sehemu ya reli iliyosombwa na mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro inaunganishwa ndani ya siku tatu na huduma za treni kurejea. 
 
Prof. Mbarawa amesema hayo baada ya kukagua sehemu ya reli hiyo kutoka Kilosa hadi Magulu- Kidete kuona athari zilizosababishwa na mafuriko yaliotokana na mvua zilizonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma. 
 
“ Fanyeni kazi usiku na mchana ili ikifika alhamisi mawasiliano ya reli kati ya mkoa wa Morogoro na Dodoma yawe yamerejea na abiria waendelee kupata huduma ya treni ,” amesema Waziri Prof. Mbarawa. 
 
Amewahakikishia wananchi wa vijiji vya Munisagara, Mkadage, Mzaganza, Magulu na Kidete ambao usafiri wao pekee wa uhakiki ni wa kutumia reli watoe ushirikiano kwa serikali ili ukarabati na ujenzi wa reli hiyo ukamilike kwa haraka. 
 
Amewataka wananchi waishio pembezoni mwa reli katika wilaya ya Kilosa kupanda miti ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaosababisha mafuriko kwa urahisi wakati wa mvua na kubomoa reli kila wakati.
 
“Pandeni miti, lindeni miundombinu ya reli na acheni vitendo vya uharibifu wa mazingira ili ujenzi wa mwaka huu uwe wa kudumu na reli isiathiriwe kirahisi na kuwasababishia kero wananchi,” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa. 
 
Naye Diwani wa kata ya Kidete Bw. Mohamed Seleman Mbunda amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wananchi wake watashirikiana na serikali kulinda mazingira ili kudhibiti mafuriko yanayoharibu miundombinu ya reli kila wakati wilayani humo. 
 
Mafuriko wilayani Kilosa ni matokeo ya mvua zinazonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma ambayo husababisha maji ya mto mkondoa kuacha mkondo wake na kubomoa tuta la reli katika eneo la Msagali hadi Kilosa kila wakati. 

Mvua za hivi karibuni zilizonyesha mkoani Iringa na Dodoma zimesomba reli katika eneo la Magulu-Kidete kilomita 315 kutoka Dar es Salaam na kukata mawasiliano ya reli kwa siku tatu sasa. 
 
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa TRL na RAHCO kutafuta suluhisho  la kudumu katika madaraja 32 yaliyo katika mtandao wa reli ya kati ili yasiathiriwe na mvua wakati wote.

03 January, 2016

Bajeti ya Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar Yatengwa.......Kinachosubiriwa ni ZEC Kutangaza Tarehe Ya Uchaguzi

Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema bajeti ya uchaguzi wa marudio imeshatengwa na wanachosubiri ni Mwenyekiti wa Tume ya  Uhaguzi Zanzibar (ZEC) atangaze tarehe hiyo ya kufanya uchaguzi.

Amesema bajeti hiyo haitatofautiana na ile iliyotumika katika uchaguzi wa Novemba 2015 iliyofikia karibu ya shilingi bilioni saba.

Amekanusha kauli kuwa uchaguzi huo hautafanyika kwa vile matokeo yanayolazimisha kutangazwa na CUF yameshafutwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi, Balozi Seif amesema mazungumzo yanayoendelea ni ya kuhakiksha amani inaimarika Zanzibar na si suala la uchaguzi uliofutwa.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 52 sherehe za Mapinduzi Balozi Seif amewabeza wanaosusuia sherehe hizo kwa madia kuwa Rais Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein kuwa si halali ni upotoshwaji mkubwa.

Amefahamisha kuwa rais huyo yupo kihalali na hata mawaziri wake wote na watamaliza ukomo wao atakapoapishwa rais mwingine kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 28 (1) a cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na si kama inavyeleezewa kuwa ukomo wake umeisha tangu tarehe 2 Novemba.

Tazama video hii kumsikia akiongea na kujibu maswali ya waandishi kuhusu marudio ya uchaguzi Zanzibar.

02 January, 2016

Magufuli Awakuna Wananchi Wenye Ulemavu, wamshukuru kwa kutimiza ahadi ya kuwakumbuka katika uongozi wake

lianza na Dkt. Abdallah Possi, wakafuata Profesa James Epiphan Mdoe na Mhe. Amon Anastaz Mpanju na kusababisha mshangao wa furaha miongoni mwa wananchi wenye ulemavu kwa kile wanachokitaja kama kukumbukwa katika uongozi wa Serikali ya awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 
 
Rais alipomteua Dkt. Abdallah Possi kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na walemavu wengi walifurahi kuona Mtanzania wa kwanza mwenye ualbino anaingia katika Baraza la Mawaziri 
 
Furaha hiyo ilizidi alipowateua Mhe. Amon Anastaz Mpanju mlemavu wa kuona kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria na Profesa James James Epiphan Mdoe kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, ambaye ni mlemavu wa miguu.
 
 Mhe Mpanju, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na ambaye pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge la Katiba, alishangaza kila mtu wakati alipokula kiapo mbele ya Rais bila kusoma mahali kama ilivyo desturi. 
 
“Huyu bwana pamoja na ulemavu wake hakika ni mtu wa kazi” alisikika mmoja wa wageni waliohudhuria hafla ya kuapishwa Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu wakuu Ikulu siku ya Mwaka mpya. 
 
Akiwa amesindikizwa na mke wake, Mhe. Mpanju alipokea Biblia Takatifu na kuinyanyua juu na kuanza kula kiapo, ingawa mkewe alikuwa ameshika karatasi ya maandiko ya vitone ambayo ilikuwa aitumie. Hata Rais alitabasamu kwa hilo. 
 
Huko mitaani, ambako tukio hilo la kuapishwa Makatibu wakuu lilikuwa likirushwa ‘live’ na vituo kadhaa vya TV na Redio na mitandao, wengi walishikwa na butwaa, huku wakimsifia Rais Magufuli kwa kuwakumbuka watu wenye ulemavu. 
 
Waliendelea kufurahi walipomuona Profesa James James Epiphan Mdoe, ambaye ni msomi aliyebobea katika Kemia,  akisogea mbele kwa mikongojo miwili na kula kiapo cha kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini. 
 

 Dkt. Abdallah Possi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na walemavu - siku alipoapishwa rasmi Ikulu jijini Dar es salaam Desemba 13, 2015


 Profesa James James Epiphan Mdoe akila kiapo kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini mbele ya Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam jana January 1, 2016


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Amon Anastaz Mpanju akiongozwa na msaidizi wake kujiunga na viongozi wenzie ili kutia saini Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma  mbele ya Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam  jana January 1, 2016

01 January, 2016

Profesa Ndalichako Atoa Siku 30 Kwa Katibu Mtendaji NACTE Kuvichunguza Vyuo Vyote Nchini Kujua Ubora Wake


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametoa siku 30 kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk Primus Nkwera kufanya ukaguzi wa vyuo vyote na kumkabidhi ripoti ili kujiridhisha na ubora wa elimu inayotolewa.

Pia, amewataka watendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuandaa mitalaa yenye matokeo ya kujenga wanafunzi watakaozalisha kwenye jamii.

Waziri huyo ambaye amewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), alitoa maagizo hayo jana wakati wa ziara yake katika ofisi hizo ikiwa ni siku tano baada ya kuapishwa kuiongoza wizara hiyo.

Alisema anawafahamu vyema watendaji wote wa taasisi hizo na hatavumilia kuona ubora wa elimu ukiendelea kuporomoka nchini.

Aliitaka TET kuhakikisha mtalaa wa KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu) kwa darasa la kwanza na la pili unapelekwa shuleni kabla ya Januari 13.

“Lakini pili, ningependa muanze kutumia walimu wastaafu kwenye uandaaji mitalaa hiyo na ukaguzi uimarike kwa wanafunzi, mnaweza kuwa na mitalaa mizuri lakini ufuatiliaji ukikosekana haitasaidia,” alisema.

Kuhusu ubora wa elimu alisema: “Ningependa uonekane kwa matokeo baada ya kumaliza shule, sihitaji kusikia amefaulu kwa alama ngapi ila amejengewa uwezo gani kichwani,” alisema.

Alisema kasi ya uwajibikaji TET imekuwa ndogo kwani kitabu cha kurasa 16 kinatengenezwa kwa mwaka mmoja. 

“Ninaweza kuja hapa mnipatie nafasi halafu tujipime na nyie tuone, naomba mbadilike nimeona mko nyuma sana ya kasi yangu,” alisema.

Mbali na maagizo hayo, Profesa Ndalichako aliiagiza Nacte kufanya usajili wa vyuo kwa kuzingatia mahitaji ya soko badala ya kusajili holela bila ufuatiliaji kwa kuwa baadhi vinajiendesha kwa ujanja ujanja.

Alisema suala la ubora wa elimu linamkosesha usingizi. Alilitaka baraza hilo kungeongeza kasi ya ushawishi katika uwekezaji wa shule za ufundi badala ya kujikita kwenye upandishaji wa hadhi ya vyuo na kuondoa dhana ya biashara katika sekta ya elimu.

“Lakini pia ningependa wafanyakazi wote mbadilike, tuache kufanya kazi kwa mazoea. Katika upandishaji hadhi ya vyuo, lazima tujiridhishe na mahitaji ya Taifa, pia kwa suala la udahili wa wanafunzi, ningependa vyuo ambavyo havijatambuliwa kwenye mfumo wa Necta viingizwe ili kuondoa udanganyifu wa vyeti wa usajili,” alisema.    

25 December, 2015

post-feature-imageJeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watu wanne wakiwemo mke wa marehemu dereva na mtunza bustani kwa tuhuma za mauaji ya aliekuwa mkuu wa kitengo cha ulinzi na usalama wa shirika la hifadhi za Tanapa Emili Kisamo aliyeuwawa kwa kukatwa shingo na kutelekezwa ndani ya gari lake Nissan Mazda No T 435 CSY eneo la Lemala jijini Arusha tarehe kumi na nane ya mwezi huu.

Kamanda Polisi mkoa wa Arusha Lebaratus Sabas amesema baada ya tukio hilo jeshi la polisi lilifanya uchunguzi na kuwakamata watu hao lakini mtunza bustani Ismail Swalehe amekiri kufanya mauajki hayo kwa tamaa ya fedha kiasi cha shilingi milioni tano na kati ya hizo milioni nne zimepatikana zikiwa zimefukiwa chini nje ya nyumba ya marehemu na kudai alimkata shingo kwa panga akiwa sebuleni  anakunywa uji ili aweze kuelekea kazini.

Kamanda Sabas amesema uchunguzi wa jeshi la polisi pia umegundua panga moja liliokuwa na damu ambalo lilikutwa kwenye stoo ya nyumba ya marehemu vitu vingine ni taulo nne kitambaa cha mezani suruali ya mtuhumiwa ambazo zilifichwa kwenye migomba karibu na banda la kuku nyumbani kwa marehemu ambazo zinadaiwa ndiyo zilizo tumika kupigia deki baada ya kuuwawa.

Mwalimu jela kwa ‘kufuga’ wanafunzi watoro

post-feature-imageMahakama ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imemhukumu mwalimu wa Shule ya Msingi Nonwe, Raphael Matima kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh600,000 ili afiche wanafunzi watoro.


Hakimu Mkazi Mfawidhi, Robert Oguda alitoa hukumu hiyo jana baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewana upande wa mashtaka.
Alisema mshtakiwa huyo aliomba fedha hizo kwa wazazi wa wanafunzi watatu wa shule hiyo iliyopo katika Halmashauri ya Ushetu.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Kahama, Kelvin Murusulu alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha Sheria ya Elimu.
Murusulu alimuomba hakimu wa mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo kwa kuwa kuomba na kupokea rushwa kwa wazazi wa watoto hao ni kosa na anadidimiza elimu. Alidai licha ya taasisi yake kuweka mtego wa kumkamata, mshtakiwa huyo anapaswa kutumikia kifungo kikubwa.
Hakimu Oguda alimhukumu kifungo hicho cha miaka mitano ili iwe fundisho kwa walimu wengine wenye tabia kama hiyo.

Wakati huohuo, Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Ushetu, Focus Kahendaguza amekutwa na kesi ya kujibu kwenye tuhuma zinazomkabili za kutumia madaraka vibaya ikiwamo kugushi nyaraka na kujipatia fedha zaidi ya Sh4,000,000 kinyume cha sheria.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo na Takukuru wilayani Kahama. Murusulu alidai kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka vibaya akiwa mtumishi halali ya Serikali na kujipatia kesi hicho cha fedha.
Madai mengine yanayomkabili ni pamoja na kutosambaza viti kwa watendaji wa vijiji wakati huo ikiwa halmashauri ya wilaya ya Kahama kabla ya kugawanywa . Hakimu Oguda aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 19, mwakani mshtakiwa huyo atakapoanza kuwasilisha utetezi wake.
-Mwananchi

17 December, 2015

Magufuli amfuta mkuu wa kupambana na rushwa

Magufuli
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dkt Edward Hoseah, na pia akawasimamisha kazi maafisa wa nne wa taasisi hiyo.
Rais Magufuli amesema hajaridhishwa "na namna taasisi hiyo ilivyokua ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es salaam.”
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema Dkt Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Bw Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.
Kwa mujibu wa Bw Sefue, Dkt Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa "utendaji kazi wa Takururu chini ya Dkt Edward Hoseah hauwezi kuendana na kazi anayoitaka”.
Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takururu ambao walisafiri nje ya nchi licha ya Rais Magufuli kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.
Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Bw Sefue amesema atakayekiuka agizo la rais "atachukuliwa hatua kali”.
Hii si mara ya kwanza kwa Dkt Magufuli kuwachukulia hatua maafisa wa Serikali tangu achukue madaraka mwezi uliopita. Siku chache baada ya kuingia afisini, a libadilisha usimamizi wa hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kufanya ziara ya kushtukiza huko na kutoridhishwa na utoaji huduma.
Majuzi alivunja bodi inayosimamia bandari.

15 December, 2015

Wabunge walioukataa Uwaziri, Mapigano ya wakulima, wafugaji, aliyevamia kwa MWINYI bila taarifa…#MAGAZETINI

MTANZANIA
Wabunge wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametajwa kukataa uteuzi wa nafasi ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne zilizokuwa wazi, imebainika.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12, mwaka huu.
Wabunge hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini walidai kuwa kasi ya Rais Magufuli inawatia hofu.
“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito na kwangu ni ngumu na nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya taarifa hizi nasikia na wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.
“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada ya kupima nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge wangu,” alisema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri, Desemba 10, mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo na kwamba anaendelea kuwatafuta.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliteua manaibu waziri wa wizara hizo, huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake baadaye atakapomaliza mchakato.
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo naibu wake ni Dk. Ashatu Kijaji.
Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii, ambayo naibu wake ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.
MTANZANIA
Mkazi wa Ilala Mtaa wa Lindi, Hafidhi Ally, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni akikabiliwa na tuhuma za kuvamia kisha kuingia nyumbani kwa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.
Mbele ya Hakimu Ester Kihiyo, karani wa mahakama hiyo, Mosses Mchome, alidai kwamba mtuhumiwa alifanya kosa hilo Desemba 10, mwaka huu saa 7:30 usiku nyumbani kwa Mzee Mwinyi,  Mikocheni B, Dar es Salaam.
Karani Mchome aliiambia mahakama hiyo kwamba, Hafidhi aliingia hadi ndani ya nyumba hiyo bila ruksa kutoka kwa mlinzi aliyekuwapo kwenye lindo, Nuru Saidi, ambapo alimweleza kwamba hana mahali pa kuishi.
“Mtuhumiwa ulikaidi amri ya mlinzi aliyekuwepo zamu siku hiyo, aliyekutaka urudi ulipotoka, kisha ulisisitiza kwamba huna sehemu ya kuishi, lakini pia wewe ni mtoto wa rais huyo mstaafu wakati huo ukielekea ndani kitu ambacho ni kinyume cha sheria,” alidai Mchome.
Mtuhumiwa alikana kosa hilo na upelelezi bado unaendelea.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 28, mwaka huu na mtuhumiwa alirejeshwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo alitakiwa apeleke wadhamini wawili waaminifu wenye barua kutoka kwa ofisa mtendaji wa kata anakoishi.
MTANZANIA
Mtu mmoja amefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa, akiwamo askari polisi mmoja baada ya kutokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Dihinda, Kata ya Kanga, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Dihinda, Hariri Kilama, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 11, saa 11 jioni.
Kwa mujibu wa Kilama, tukio hilo lilisababishwa na mfugaji mmoja aliyejulikana kwa jina la Shaban Ramadhan, kuingiza ng’ombe wake katika shamba la mkulima aliyetambuliwa kwa jina la Bakari Mlunguza ambao waliharibu mazao.
“Baada ya uharibifu wa mazao hayo, uongozi wa kijiji ulimwita Bwana Shamba wa Kijiji, Mathew Limbanywa, kwa ajili ya kufanya tathimini ya  mazao yaliyoharibiwa na mifugo hiyo.
“Baada ya tathmini hiyo, ilibainika, kuwa uharibifu uliofanyika ulikuwa mdogo na bwana shamba huyo aliomba suluhu ifanyike ili kutatua mgogoro huo.
“Pande hizo zilipokaa pamoja, mkulima aliomba alipwe fidia ya shilingi laki tatu, lakini mfugaji alikataa na kusema yupo tayari kulipa shilingi laki mbili.
“Makubaliano hayo yalipofanyika saa nane katika ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Wiliam Masanyika, mfugaji aliondoka na saa 11 jioni alirudi na kundi la wenzake na kuanza kupiga miruzi ya kuita ng’ombe wake waliokuwa chini ya ulinzi ofisini hapo.
“Wakulima walipoona kuna dalili za mapigano, nao walijibu mapigo, ambapo wafugaji walimpiga mkulima mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Mohamed ambaye alifariki dunia wakati akipelekwa katika Hospitali ya Mission ya Bwagala wilayani humo.
“Pamoja na mauaji hayo, ng’ombe 71 nao waliuawa na wengine 120 walijeruhiwa vibaya na wakulima hao,” alisema Kilama.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, Mwigulu Nchemba, aliliagiza Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kuimarisha ulinzi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuwakamata waliohusika katika vurugu hizo.
Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema polisi mkoani hapa wanawashikilia watu 19 wakiwamo watatu wanaodaiwa kuwaua ng’ombe hao kwa kuwakatakata kwa mapanga
MWANANCHI
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema watu wanaomiliki mashamba bila kuyaendeleza huku wakiyatumia kama dhamana ya kukopea fedha benki watanyang’anywa.
Lukuvi, akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuripoti kazini jana pamoja na naibu wake, Angelina Mabula, alisema kuna watu wamehodhi mashamba makubwa lakini hawayaendelezi, hawayalipii kodi, na mbaya zaidi wanayatumia kukopa fedha benki.
“Mkuu wa idara anayehusika na ardhi ninaomba Jumatatu ijayo orodha ya watu tuliowapa ardhi lakini wameitumia kuombea mikopo ambayo wanaitumia kwa shughuli nyingine.
Hao nitalala nao mbele,” alisema Lukuvi baada ya kujitambulisha kwa wakuu wa idara za wizara hiyo.
“Nipeni pia orodha ya watu wanaotakiwa kulipa kodi ya ardhi lakini hawalipi na tukikutana wiki ijayo nielezeni taratibu zinazotakiwa kuchukuliwa dhidi yao,” alisisitiza.
Akisisitiza kuhusu hilo, Lukuvi alisema wiki ijayo atakwenda kuchukua shamba lililohodhiwa na mwekezaji lenye ekari 1,600 huko Mbarali mkoani Mbeya na kuwarudishia wananchi.
Japokuwa Lukuvi hakumtaja mwekezaji atakayenyang’anywa shamba hilo wilayani Mbarali, lakini shamba la ukubwa huo lililokuwa na mgogoro kwa muda mrefu ni la Kapunga.
Akiwa kwenye kampeni mkoani Mbeya, mgombea urais wa CCM ambaye sasa ni Rais John Magufuli, aliahidi kurejesha shamba hilo kwa wananchi ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu.
Aidha, Lukuvi aliwaagiza maofisa hao kuwasiliana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuangalia wawekezaji waliopewa ardhi kama wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Tukikutana Jumatatu ijayo nipewe taarifa za kila mwekezaji na ukubwa wa ardhi aliyopewa; aliomba kwa madhumuni gani, na je, anaitumia ardhi hiyo kwa madhumuni aliyoombea?” alihoji. Kuhusu upimaji wa ardhi,
Lukuvi alisema asilimia 10 ya ardhi nchini ndiyo imepimwa na kwamba juhudi zinahitajika ili kupima ardhi zaidi. Tunataka tukikutana wiki ijayo, ofisa anayehusika na upimaji aje na mpango wa upimaji ardhi na umilikishaji na atueleze utagharimu kiasi gani ili tuweze kuona serikali itawekeza vipi katika upimaji wa ardhi nchi nzima,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa nyumba za kupangisha, Lukuvi alisema kumeibuka kampuni nyingi zinazofanya biashara ya kujenga nyumba kubwa na kuzipangisha lakini hakuna chombo chochote cha serikali kinachosimamia sekta hiyo. “Hii ni biashara kubwa ambayo inakua siku hadi siku, hivyo ni lazima sasa wizara isimamie kwa kuweka chombo maalumu. Hivi sasa biashara inafanyika lakini hatupati kodi kwa sababu si rasmi,” alisema.
Waziri Lukuvi alimtaka mkurugenzi wa nyumba wa wizara hiyo kuandaa mpango wa namna ya kuwasaidia watu maskini ili kuwa na nyumba bora.
“Tunataka atueleze serikali ifanye nini ili kuwasaidia wananchi maskini kuwa na nyumba bora ili waondokane na nyumba zilizoezekwa kwa nyasi,” alisema.
MWANANCHI
Wizara ya Nishati na Madini, imezindua matumizi ya mfumo mpya wa malipo ya ada za leseni za madini kwa njia ya kielektroniki (OMCTP) Kaimu Kamishna Mkuu wa Madini, John Nayopa jana alisema mfumo huo ulianza kutumika wiki iliyopita na utawawezesha wateja kutuma maombi ya leseni na taarifa za utendaji kazi kwa njia ya mtandao.
“Mfumo huu ni salama kwa fedha za wateja na kuanzia sasa malipo ya ada za leseni yatafanyika kwa njia ya mtandao pekee. Ofisi zetu za madini zitatoa msaada kwa wateja wanaohitaji maelekezo,” alisema.
Alisema utawawezesha pia wateja kupata ramani za kijiolojia, takwimu mbalimbali za madini na kufanya malipo kwa njia ya miamala ya simu za mkononi, Maxmalipo na kupitia benki (EFT).
Nayopa amewataka wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya madini na kuchakata mchanga wenye madini ili wanufaike na Serikali iongeze mapato kwa kupitia ulipaji wa kodi.
Mfumo huo unalenga kurahisisha utoaji wa leseni wachimbaji wadogo, kupunguza mlundikano wa maombi ofisi za madini, kurahisisha mawasiliano kati ya wizara na wamiliki, kujua taarifa za leseni na utoaji wa taarifa za madini kwa wakati
MWANANCHI
Mradi wa kuchakata gesi asilia kutoka Madimba Mtwara­Songosongo hadi Dar es Salaam umekamilika na kuwezesha uzalishaji umeme katika mitambo ya Kinyerezi, Ubungo, Tegeta na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Kwa sasa mradi huo unazalisha asilimia 70 ya umeme wote unaotumika nchini kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC), Dk James Matagio alisema jana kuwa nchi inaelekea katika uchumi wa gesi kutoka katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta na maji. Alisema ujenzi wa bomba jipya la gesi umeongeza uzalishaji kwa asilimia 30.
Dk Matagio lisema mradi wa usambazaji gesi asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam pia unalenga kusambaza gesi katika nyumba 30,000 na magari 8,000.
Alisema upembuzi yakinifu na usanifu wa michoro umekamilika na kwa sasa wanatafuta fedha kutekeleza mradi unaotarajia kugharimu Dola 150 za Marekani.
Meneja wa Mawasiliano wa TPDC, Maria Msellemu alisema kutokana na ugunduzi wa mafuta nchini Uganda, Serikali ya nchi hiyo ilitia saini makubaliano na Tanzania kwa kushirikiana na TPDC na Kampuni ya Total.
Alisema makubaliano hayo yanalenga kuangalia uwezekano wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka nchini humo kupitia Bandari ya Tanga hadi kwenye soko la nje.
“Tumeanzisha kampuni tanzu za Gaso ambayo inashughulikia gesi, Copec uagizaji wa mafuta na Kampuni ya International Business biashara za kimataifa,” alisema Msellemu.
MWANANCHI
Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), kimekamata shehena ya makonyo na karafuu kavu iliyodaiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa njia ya magendo katika Bandari ya Milango Mikavu kisiwani hapa.
Kamanda wa KMKM Pemba, Silima Haji Haji alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku. Alisema watu waliokuwa wakivusha shehena hiyo walikimbia na kutelekeza magunia 31 za makonyo na manne ya karafuu kavu baada ya kuwaona askari wa kikosi hicho wakienda kuwakamata.
Alisema kabla ya tukio hilo, askari waliokuwa doria waliwatilia wasiwasi na walipowafuatilia watuhumiwa hao walikimbia.
Kamanda Silima alisema katika kipindi hiki ambacho karafuu zinaendelea kuchumwa, askari wake wameongeza ulinzi baharini na nchi kavu ili kuwadhibiti watu wanaotaka kuhujumu uchumi wa nchi kwa masilahi yao binafsi.
Mdhamini wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) Pemba, Abdalla Ali Ussi amepongeza juhudi zinazochukuliwa na kikosi cha KMKM kupambana na biashara ya magendo ya karafuu.
Aliwataka wananchi kujiepusha na biashara hiyo haramu inayowanufaisha kwa kuwa inadhoofisha uchumi wa nchi. Alisema wananchi wameitikia wito wa Serikali wa kuuza karafuu katika vituo vya ZSTC na kwamba fedha zinazopatikana hutumika katika kukuza maendeleo.
Baadhi ya wananchi wanaouza karafuu katika Kituo cha Shirika Bandarini Wete, wameviomba vyombo husika kufanya uchunguzi ili watuhumiwa wakamatwe.
Mmoja wa wakazi hao, Yussuf Said Rashid alisema ni vema Serikali kupitia ZSTC kuandaa utaratibu maalumu wa kuwakagua wananchi wenye mikarafuu ili kujiridhisha kama wanaziuza kwenye vituo vya shirika hilo.
Alisema vitendo vya magendo vinatakiwa kukomeshwa kwa kuweka mikakati kabambe ya kuvidhibiti ikiwamo wananchi kutoa taarifa wanapoona matukio kama hayo.
MWANANCHI
Maandalizi ya upangaji wa ada elekezi kwa shule binafsi nchini yameibua mvutano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) baada ya kulalamikia kutopewa nafasi ya ushiriki katika hatua za awali.
Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamini Nkonya alisema jana kuwa chama hicho kiliwachagua mawakili wake wanne kwa ajili ya kutoa ushirikiano kwa wizara hiyo katika upangaji na uchambuzi wa ada elekezi, lakini haijawatumia.
Alisema Serikali imekuwa ikiwatumia wamiliki wa shule binafsi wasiokuwa na uwakilishi wa mawazo ya chama hicho. Waliochaguliwa na chama hicho kuwakilisha maoni yao ni mwenyekiti wake, Mrinde Mnzava, makamu mwenyekiti Jeremiah Bwegenyeza, Katibu mkuu, Benjamin Nkonya na mhasibu, Mapenzi Yona.
Hata hivyo, Kamishina wa Elimu Wizara hiyo, Profesa Eusella Bhalalusesa alipinga ofisi yake kupokea majina ya wawakilishi wa chama hicho.
Alisema utafiti bado unaendelea, hivyo wanayo nafasi ya kuwasilisha maoni yao. “Sijapata majina yao, lakini kwa nini tugombanie fito wakati nyumba ni moja? Wadau ni wengi na siyo rahisi kumfikia kila mmoja, wataalamu watakapokamilisha ripoti yao kabla ya mwaka wa masomo 2016, tutaichambua na wadau wote kabla ya kuanza majaribio yake.
“Lakini katibu huyo wa Tamongsco (Benjamini Nkonya) nilimuona kwenye televisheni akisema wameshiriki vizuri kutoa maoni yao,” alidai Profesa Bhalalusesa.
Profesa Bhalalusesa alitaja baadhi ya vigezo vitakavyotumika kupanga ada elekezi kuwa ni huduma zinazotolewa na shule, eneo la shule inakopatikana na mmiliki wa shule husika.
Alipoulizwa kuhusu kutenganisha mtoa huduma na mfanyabiashara ili kutoza kodi alisema: “Ndiko tunaelekea huko, tutaangalia shule inayotoa huduma na inayofanya biashara ili iweze kutozwa kodi.”

05 August, 2015

Kwenye StoriKubwa >>> Ya MAGUFULI, Rais JK.. Lowassa? mastaa waliokatwa YANGA …

222222MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan jana walichukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku Rais Jakaya Kikwete akisema wapinzani wataisoma namba.
Ofisi ndogo za makao makuu ya CCM zilizoko Lumumba na za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilifurika mashabiki waliovalia nguo za rangi ya njano na kijani, ambazo hutumiwa na chama hicho, huku wakazi wengine wanaofanya kazi au kuishi maeneo jirani na barabara za Morogoro, Bibi Titi na Ohio, wakilazimika kusimamisha shughuli zao kwa muda kushuhudia msafara wa wagombea hao ukipita.
Walinzi  wa ofisi za NEC walilazimika kufanya kazi ya ziada kudhibiti wafuasi wa CCM waliosindikiza wagombea hao kutoka ofisi ndogo za CCM kabla ya msafara huo kuondoka baada ya wawili hao kuchukua fomu, kurejea Lumumba, ambako mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete aliupokea.
“Wakwere wanasema chihendo na mwene mwana, yaani shughuli na mwenye mtoto,” alisema Rais Kikwete mara baada ya msafara kuwasili akieleza sababu za yeye kuwapo eneo hilo kwa kutumia maneno ya shughuli za kitamaduni za jandoni, unyagoni na mkoleni za kabila la Wakwere.
“Nimekuja hapa kujiridhisha kama kweli fomu zimechukuliwa. Na kweli nimeziona. Baada ya hatua hii wale wanaodhani kuwa CCM ni chama cha mchezo mchezo, wataisoma namba.”
Huku akikatiza hotuba yake kwa kuitaka bendi ya TOT ya chama hicho kuimba wimbo wa “Shangilia Ushindi Unakuja”, Rais Kikwete alisema kwa kuwa yeye ni baba alilazimika kuja kuangalia kama mwanaye ametekeleza alichotuma.
Kikwete, ambaye alitumia mifano iliyovunja mbavu wafuasi hao, alirusha kijembe kwa wanachama walioihama CCM akisema ni tamaa na kuahidi kufanya mkutano mkubwa wa uzinduzi wa kampeni.
CCM shangilia ushindi unakuja, tena ushindi wa uhakika na si wa wasiwasi. Baada ya hapa kitakachofuata ni uzinduzi hapo Agosti 22 kwenye mkutano utakaotisha. Hatumwi mtoto siku hiyo, unakuja mwenyewe,” alisema.
“Watu wanasumbuliwa na tamaa na wakati mwingine ni tamaa iliyopitiliza kutaka madaraka.”
Magufuli alitoka ofisi ya CCM Lumumba akiwa amepanda gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa wazi juu akiwa na msafara wa magari yapatayo 10 kuelekea ofisi za NEC. Baada ya kufika eneo la makutano ya Barabara ya Ohio na Bibi Titi, alishuka na kupanda gari nyingine iliyokuwa wazi nyuma na kuamsha kelele za shangwe.
Aliwasili ofisi hizo saa 5.22 asubuhi na baada ya kuchukua fomu za kuwania urais, msafara wa kurejea ofisi za chama hicho zilizoko Lumumba ulianza tena na kufika ofisi hizo ndogo za CCM, ambako ulipokelewa na Rais Kikwete.
“Matatizo ya Watanzania nayajua na  ninaahidi kuwa nitakuwa mtumishi wenu mtiifu,” alisema Dk Magufuli baada ya Rais Kikwete kumuomba aketi ili azungumze na wafuasi wa chama hicho.
“Nafahamu kuwa Watanzania wanahitaji ajira na hawataki usumbufu kwenye biashara zao kama mamantilie, wana kero kwenye huduma mbalimbali. Ninawaahidi kuwa nitazishughulikia.
Napenda nimhakikishie mwenyekiti na wananchi mliokusanyika hapa kuwa CCM itashinda na wala simuoni mtu wa kutushinda. Nashukuru kwa moyo mliouonyesha wa kunisindikiza mimi pamoja na Samia. Mmetoa jasho na mmepoteza muda wenu. Napenda kuwahakikishia kuwa muda wenu hautapotea bure.”
Alirudia wito wake wa kuwataka wananchi kuendeleza mshikamano uliopo bila kujali itikadi zao wala makabila ili kuliletea Taifa maendeleo kwa kuondoa kero zinazowakabili.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ilikuwa kazi kubwa kumshawishi Juma Duni Haji kukiacha chama hicho na kujiunga Chadema ili awe mgombea mwenza wa Edward Lowassa.
Duni, ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF, alitangazwa kujiunga na Chadema jana, ikiwa ni makubaliano ya mkakati maalumu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wa kukabiliana na kikwazo cha kisheria cha kupata mgombea mwenza kutoka chama tofauti na kilichosimamisha mgombea urais.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka Makamu wa Rais kutoka chama kilichoshinda kiti cha urais na hivyo Duni amejiunga na Chadema akiwa mwakilishi wa Ukawa kwenye Serikali iwapo umoja huo, unaoundwa na CHADEMA, CUF, NLD na NCCR – Mageuzi utashinda Uchaguzi Mkuu.
Lakini kabla ya Duni kukubali ushauri huo, Maalim Seif alisema walikuwa na kibarua kigumu.
“Tulimwita Babu Duni, tukamwambia azma hii, akasema; ‘hivi kweli niende Chadema mie?’” alisema Maalim Seif akimnukuu Duni wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chadema jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Nikamwambia kwa hili tunalotaka la mabadiliko, lazima uende Chadema.”
Maalim Seif, ambaye alikuwa mmoja wa wageni waalikwa waliopewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo ambao ni chombo cha juu cha uamuzi cha Chadema, alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu kuhakikisha kuwa upinzani unatwaa Dola katika uchaguzi ujao wa Rais, wabunge na madiwani.
Maalim Seif, ambaye alijitangazia ushindi wa kiti cha urais wa Zanzibar, pia alimtangaza Lowassa, ambaye pia aliondoka CCM na kujiunga na Chadema wiki iliyopita, kuwa ameshashinda mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mgombea mwenza na wanachosubiri sasa ni kuapishwa tu.
“Huu ni wakati wa kujiamini na kuamini kuwa tunaweza kuchukua dola,” alisema Maalim Seif ambaye pamoja na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba waliiongoza CUF katika kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK).
Wakati Maalim Seif akitangaza ushindi kwa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alionya kuwa kazi ya kuiondoa CCM si rahisi na kwamba nguvu ya Watanzania inahitajika kufanikisha azma hiyo.
HABARILEO
Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Ujambazi Mkoa wa Morogoro, Elibariki Pallangyo , amepigwa risasi na kufa papo hapo nyumbani kwake eneo la Yombo jiji Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alisema kuwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa tisa usiku, kundi la watu zaidi ya kumi lilivamia nyumbani kwa Pallagyo eneo la Yombo kwa kuruka ukuta, kisha kuvunja mlango na kuingia ndani walikopora fedha na simu za mabinti wanne waliokuwa ndani kabla ya kufanya mauaji.
“Hili tukio ni la kusikitisha kwani watu hawa wanaonesha walikuwa na lengo la kumuua tu na si kupora mali, kwani wamechukua fedha Sh 130,000 pamoja na simu za mkononi 4 ambazo walikuwa nazo hawa wasichana waliowakuta sebuleni,Satta.
Alisema baada ya watu hao kupora simu na fedha kutoka kwa mabinti, waliekea kwenye chumba cha Pallangyo, wakampiga risasi moja kifuani na kumuua.
Wauaji hao walitokomea kusikojulikana huku wakisahau kifaa kinachotumika katika milipuko. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Temeke na utapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi kabla ya maziko.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kufanya kampeni za kistaarabu, kwakuwa nchi ya Tanzania inayo sifa ya kuendesha mambo yake kwa njia ya amani na utulivu.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akihutubia mamia ya wakazi kwenye hafla maalumu ya kuwaaga wananchi wa mkoa wa Tanga, iliyofanyika katika uwanja wa Mkwakwani jijini hapa.
Katika hafla hiyo, ambayo Rais Kikwete aliongozana na Mama Salma Kikwete alipata fursa ya kupokea zawadi za aina mbalimbali kutoka kwa wawakilishi wa wananchi kutoka wilaya za Tanga, Mkinga, Pangani, Muheza, Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi ambazo zinaunda mkoa huo.
Alisema kwa kuwa kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi wa Oktoba zitaanza rasmi Agosti 21 mwaka huu ni vyema wananchi kila mmoja kwa nafasi yake, wahakikishe zinafanyika kwa ustaarabu na utulivu ili kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
“Tanzania ina sifa ya kuendesha vitu kwa amani na utulivu …naomba kampeni zitakazofanyika za kuwanadi wagombea wa udiwani, ubunge na urais ziwe za kistaarabu hakuna sababu ya kufanya vurugu bali kila mtu apewe nafasi ya kumwaga sera zake, asikilizwe kwa utulivu”, alisema.
Aidha, Rais Kikwete aliwashukuru wakazi wa Tanga kwa kuiunga mkono CCM sambamba na kumuunga mkono kwa kiwango kikubwa kwenye chaguzi zote, zilizomuweka madarakani mwaka 2005 na 2010, ikilinganishwa na baadhi ya mikoa mingine nchini.
“Wito wangu kwenu ichagueni CCM tu katika serikali inayokuja, chama hiki kitawajengea Chuo Kikuu cha Serikali kwa sababu hapa Tanga hamna… naomba wananchi tujiandae vizuri kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo mkuu,” alisema.
Awali, akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Saidi Magalula alisema “Wananchi wa mkoa huu wameniagiza niwasilishe kwako maombi ya vitu vifuatavyo ujenzi wa daraja la Mligazi linalounganisha wilaya ya Handeni na Miono, pia ujenzi wa barabara ya Tanga- Pangani–Bagamoyo kwa kiwango cha lami, Bandari ya Tanga, kufufuliwa kwa viwanda mbalimbali vya uzalishaji na kufufuliwa kwa reli ya Tanga – Moshi hadi Musoma”.
HABARILEO
Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Chiku Abwao ndiye atakayepeperusha bendera ya ACT kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa mjini katika uchaguzi mkuu ujao, huku akitamba kwamba atambwaga mbunge anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Mbali na Abwao aliyejiunga na ACT Wazalendo hivi karibuni, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chadema, Abuu Changawa naye ameiacha Chadema na kujiunga ACT Wazalendo, huku akitangaza kuwania udiwani katika Kata ya Mivinjeni, mjini hapa.
Abwao aliyewahi kuwa mbunge wa NCCRMageuzi, alisema; “Nimeondoka Chadema baada ya kubanwa kila kona na Mchungaji Msigwa akidhani kwamba mimi nilikuwa Chadema kwa sababu ya kutaka cheo.”
Alisema pamoja na kunusurika maisha yake wakati akipigania ushindi wa Mchungaji Msigwa 2010, mahusiano yao kisiasa yamekuwa mabaya kwa kipindi chote kwani kila alilokuwa akijaribu kulifanya kwa niaba ya chama hicho alitafsiriwa analenga kugombea ubunge jimbo la Iringa Mjini.
Alisema ili kumuonesha nguvu yake kisiasa na kwamba yeye sio mwanasiasa anayetaka tu uongozi lakini mwenye dhamira na maono ya dhati ya kusaidia kuleta mabadiliko nchini atagombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini kupitia ACT Wazalendo.
JAMBOLEO
Siku mbili baada ya mawaziri watano kushindwa katika kura za maoni ya ubunge ndani ya CCM, waziri mwingine, Gaudentia Kabaka anayeshughulikia Kazi na Ajira, naye amedondoshwa katika jimbo la Tarime Mjini.
Kabaka, kabla ya kujitosa katika siasa za majimbo, alikuwa mbunge wa muda mrefu wa viti maalumu. Aidha, katika kura hizo zilizofanyika kote nchini, zimewaacha katika hali mbaya wabunge wanne, baada ya kushindwa katika kura za maoni majimboni mwao.
Hao ni Nyambari Nyangwine, Gaudence Kayombo, John Lwanji na Salome Mwambu.
Matokeo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini ambako Nyangwine ameanguka, yamethibitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu Wazazi Wilaya ya Tarime, Mathias Lugola aliyetangaza rasmi matokeo ya majimbo hayo.
Awali, matokeo hayo ya kura za maoni yaliahirishwa kutangazwa kutokana na kuwepo kwa tuhuma za kuwapo kwa wizi wa kura. Kwa jimbo la Tarime Mjini, Lugola alifafanua kuwa Michael Kembaki ndiye aliyeibuka mshindi kwa kura 3,908 akifuatiwa na Kabaka aliyepata kura 2,411.
Katika Jimbo la Tarime Vijijini, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Christopher Kangoye ambaye amejaribu zaidi ya mara tatu kuusaka ubunge, lakini bila mafanikio aliibuka mshindi akivuna kura 15,928 dhidi ya 12,205 za John Gimunta ambaye ni Mweka Hazina wa CCM wilayani Tarime.
Nyangwine na Gimunta, baadaye walilalamikia matokeo hayo wakisema mchakato wa kura za maoni ulitawaliwa na hujuma.
Kayombo azidiwa Mbinga Katika Jimbo la Mbinga Vijijini, matokeo yaliyotangazwa saa 5:45 usiku baada ya mvutano wa kutangaza matokeo unaodaiwa kudumu kwa takribani saa 12, yameonesha kuwa mbunge wa jimbo hilo aliyekuwa amejitokeza kutetea kiti chake, Gaudence Kayombo ameshindwa katika kura za maoni ndani ya CCM.
Aliyeibuka mshindi ni Martin Msuha, aliyepata kura 13,354 dhidi ya 12,068 za Kayombo, ambaye pia kwa mwaka mmoja na nusu kati ya Januari 12, 2007 na Agosti 2, 2008 alikuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.
Wengine walioshiriki katika mchakato wa ubunge jimboni humo na kura zao kwenye mabano ni Humphrey Kisika (545), Dk Silverius Komba (1,289), Edesius Kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga (3,941) na Deodatus Ndunguru.
Wabunge Singida hoi MCHUANO wa makada mbalimbali wa CCM kuwania nafasi za ubunge katika mkoa wa Singida umekamilika, huku wabunge waliokuwa wakitetea nafasi zao na baadhi ya vigogo kwenye chama hicho wakiwa wamebwaga vibaya.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Singida, Mary Maziku, wabunge wawili waliokuwa wakitetea nafasi zao hawakuweza kupata kura za kutosha kwenye kura za maoni. Nao ni Salome Mwambu wa Jimbo la Mkalama na John Lwanji wa Manyoni Magharibi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai ambaye aligombea jimbo la Mkalama alifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kupata kura 3,908 nyuma ya Allan Kiula aliyezoa kura 5,823. Jimbo hilo lilikuwa na wagombea 16.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, amesaini miswada mitano ya sheria, iliyopitishwa na Bunge la 10 Julai, mwaka huu.
Imo iliyozua tafrani na kusababisha wabunge 45 wa Ukawa kutimuliwa bungeni na wengine kususia mkutano wa 20.
Katika tukio la kihistoria lililofanyika Ikulu, jana na kuhudhuriwa na mawaziri, watumishi wa wizara na wadau wa mafuta na gesi, Rais alisaini miswada hiyo baada ya mawaziri husika kuwasilisha maelezo ya miswada hiyo.
Miswada hiyo ni wa sheria ya mafuta, sheria uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia, muswada wa sheria ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi pamoja na muswada wa sheria ya Tume ya walimu.
Vile vile muswada wa sheria ya usimamizi wa masoko ya bidhaa yote ya mwaka 2015.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema tukio hilo ni la kihistoria kwa Tanzania kwa miswada mitano kusainiwa katika hadhara kubwa ya watu.
Alisema miswada ya sheria ya gesi na mafuta inaweka utaratibu mzuri wa kimfumo, kisheria na udhibiti mzuri wa kusimamia uchumi wa gesi na mafuta, kujibu kilio cha Watanzania kuwa rasilimali ziwanufaishe na kizazi kijacho.
Balozi Sefue alisema pia watanzania wataunganishwa na ulimwengu wa gesi kwa biashara watakazoanzisha na kutekeleza katika uchumi huo, ikiwa ni pamoja na kuwa na uchumi nyumbulifu katika kulinda mahitaji ya vizazi vijavyo na cha sasa.“Tunafanya walichofanya wengine duniani na kuepuka yaliyoleta matatizo katika nchi nyingine,” alisema Balozi Sefue.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema muswada wa sheria ya mafuta unalenga kuleta sheria mpya ya kusimamia sekta ndogo ya mafuta nchini kwenye masuala ya utafutaji; uendelezaji; uzalishaji; usafirishaji; uagizaji; uchakataji; uhifadhi na biashara ya mafuta na gesi asilia nchini.
“Malengo ya muswada wa sheria ni kuimarisha usimamizi wa sekta ili kuhakikisha maslahi ya nchi katika tasnia ya mafuta yanalindwa kikamilifu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, kuweka mfumo madhubuti wa kisheria utakaoimarisha usimamizi wa shughuli za mafuta katika mkondo wa juu, wa kati na wa chini kupitia sheria moja,” alisema  na kuongeza:
“Masuala muhimu ni kuweka utaratibu ambao serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar zitashirikiana katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uendelezaji wa vitalu vya mafuta na gesi katika yaliyo kwenye maeneo yanayugusa pande zote mbili,” alibainisha.
Simbachawene alisema sheria hiyo itawezesha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Pura) ambayo itasimamia shughuli zote za udhibiti katika masuala ya kiufundi na kibiashara katika mkondo wa juu.
NIPASHE
Mbunge wa Mkuranga mkoani Pwani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,  Adam Malima, amesema kuwa kura za maoni zilizopigwa jimboni humo hazikuwa huru na haki kwa madai kwamba waliopiga kura walikuwa wachache lakini kura za matokeo zikawa nyingi.
Malima ambaye alisema kuwa hakuridhishwa na mwenendo mzima wa kura za maoni kwa vile umechukua siku tatu bila mawakala kusaini fomu za matokeo.
Matokeo ya kura za maoni katika jimbo hilo yalitangazwa juzi usiku, huku Malima akiwaambia wananchi na wapambe wake wasifanye fujo na kuwataka warudi nyumbani na kwamba vikao vya juu vya maamuzi vitatoa jina la nani apeperushe bendera ya chama.
“Mchakato uligubikwa na udanganyifu mkubwa, kura haziendani na uhalisia, pia mawakala hawakutia saini baada ya kumalizwa kwa upigaji kura katika vituo vyao, lakini ninaviachia vikao vya maamuzi vifanye kazi yake,” Malima.
Alisema kuwa ana nafasi nyingi ndani ya chama na miongoni mwa watu walioaminiwa na Rais Jakaya Kikwete kuandaa ilani ya uchaguzi, na kuwa anashangaa kusikia kuwa hawezi kuwaletea wananchi maendeleo katika jimbo hilo.
“Watu kama hao ni timu za wenzangu ambazo zinatumika kusema eti wataenda upinzani, siwezi kuzuia kambi zisiongee kitu chochote, lakini mimi sihami CCM ingawa kura hizi zina walakini,’” alisema.
Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi wa  Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, Hadija Kusaga, alisema kuwa waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 46,904, kura zilizopigwa ni 26,949 na kwamba kura 904 ziliharibika.
Alisema kuwa katika matokeo ya kura hizo, mkuu wa wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Abdallah Ulega, aliibuka na ushindi kwa kupata kura 16, 294 huku Malima akipata kura 8, 212.
NIPASHE
Mgombe urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli jana alichukua fomu za kuwania nafasi hiyo huku Mwenyeti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiwaasa wanachama wa chama hicho wasimpuuze adui yeyote katika uchaguzi mkuu mwaka huu na kutamba watafunga magori uwanjani huku wapinzani wakiwatazama.
Magufuli alichukua fomu hizo katika ofisi za Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (Nec) kwa mbwembwe akiwa kwenye msafara wa magari, pikipiki, matarumbeta na muziki.
Akizungumza na wanachama wa CCM jana mchana katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete aliwasihi wanachama wa chama hicho kutodharau adui yeyote watayepambana naye katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Licha ya Rais Kikwete kutofafanua kauli yake hiyo, katika uchaguzi mkuu ujao CCM inatarajia kupambana vikali na mgombea urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa aliyehama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hivi karibuni.
Lowassa alikihama CCM huku akisema kwamba ameamua kufanya hivyo kutokana na kubakwa kwa demokrasia ndani ya chama hicho kikongwe nchini.
Kikwete alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, chama hicho kitafunga magori uwanjani huku upinzani ukitazama na kwamba kitapata ushindi wa kishindo na hilo hana wasiwasi nalo.
Rais Kikwete jana alionekana mwenye furaha muda wote huku akiomba kikundi cha kwaya cha TOT, kimuwekea wimbo wa ‘acha waseme CCM kina wenyewe, shangilia ushindi unakuja’.
Wakati wimbo huo ukipigwa, Kikwete aliamua kuucheza akiwa jukwaani huku akishangiliwa na wananchi waliokusanyika katika ofisi za CCM.
Hata hivyo, Rais Kikwete hakuzungumzia juu ya kuondoka  Lowassa ndani ya CCM, na kwenda kujiunga na Chadema kisha kuteuliwa kugombea urais kupitia umoja huo.
Alisema dunia nzima inajua maendeleo mazuri yaliyofikiwa kupitia utawala wake na kwamba katika kampeni watakwenda kuwaeleza wananchi mambo mazuri yaliyofanywa.
Alijivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika utawala wake na kusisitiza kuwa anaondoka madarakani huku akiiacha nchi ikiwa na amani, umoja na mshikamano.
Wakati wa kwenda kuchukua fomu ya kugombea urais, Dk. Magufuli jana aliambatana na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), huku wakisindikizwa na viongozi mbalimbali waandamizi wa CCM.

02 August, 2015

#VIDEO>> TAZAMA MZUNGU HUYU ANVYOIMBA WIMBO WA TANZANIA TANZANIA NAKUPENDA.

Jakaya-Kikwete


Ni fahari iliyoje kuona wenzetu wakisifia na kuuimba uzuri wa TANZANIA, tena katika ardhi ya nchi yao?
 Mrs Bernadette Mathias akiimba Wimbo wa Tanzania Nakupenda Kwa kiswahili akimpongeza Mhe. Dr Jakaya Mrisho kikwete Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa Kutunukiwa Shahada ya heshima ya Udaktari wa Sheria (Doctor of Laws honorific causa) na Chuo Kikuu cha Newcastle cha nchini Australia.

Tazama video hiii ya  Mrs Bernadette Mathias Akiimba TANZANIA TANZANIA NAKUPENA

18 July, 2015

Ubunge CCM Kama Urais

wabunge+pixWANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaowania kibali cha chama hicho ili wagombee ubunge, wamejitokeza kwa wingi katika baadhi ya majimbo na kufanya mchakato huo kuwa na mvuto wa aina yake, unaofanana na ule wa urais.

Jana ikiwa siku ya pili tu tangu kufunguliwa kwa pazia la uchukuaji fomu za kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali nchini, idadi ya wanachama waliochukua fomu katika baadhi ya majimbo, imekuwa kubwa na kuelekea kulingana na wawania urais katika chama hicho, ambao walifikia 42. Jimbo jipya la Mbagala ndilo lilitia fora kwa kuwa na wasaka ubunge 17, waliolipa Sh laki moja na kuchukua fomu ya kuomba wanaCCM wapendekeze mmoja wao kuwania nafasi hiyo katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa Katibu Muenezi wa Wilaya ya Temeke, Rutami Masunu, mpaka jana siku ya pili ya utoaji fomu, waliojitokeza katika Jimbo hilo jipya ni wanachama hao 17.
Alitaja baadhi ya aliowakumbuka kuwa ni pamoja na Peter Nyalali, Richard Tambwe Hiza, Lucas Malegeli, Issa Mangungu, Mindi Dominck Haule, Ally Makwilo, Kivuma Msangi na wengine.
Katika Jimbo la Temeke waliojitokeza kuchukua fomu ni Mbunge wa jimbo hilo anayemaliza muda wake, Abbas Mtemvu, Hamis Salim maarufu kama Chicago, Maimuna Chicago pamoja na Joseph Mhoha.
Masunu alisema kwa upande wa Jimbo la Kigamboni waliojitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Dk Faustine Ndugulile anayetetea nafasi yake pamoja na wanachama wengine watatu.
Kwa Wilaya ya Ilala, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Ernest Charles aliliambia gazeti hili kuwa jumla ya waliojitokeza katika wilaya hiyo ni wanachama 26.
Aliwataja baadhi ya wanachama hao na majimbo yao kwenye mabano kuwa ni Mussa Azzan Zungu, Mrisho Gambo, Waziri Kindamba (Ilala), Zahoro Lyasuka, Bona Kalua, Apruna Jaka, Siasa Chuma na Nicholaus, Baraka Omary, Christopher Japhet, Scholastica Kevela, Simon Kambe na Tunza Kanabe (Segerea).
Kwa jimbo la Ukonga ni Meya Jerry Slaa, Anthony Kalokola, Jacob Kasema, Hamza Mshindo, Fredrick Rwegasira, Ramesh Patel, Peter Kaseleko, John Machuta, Magesa Magesa, Amos Hangaya, Thomas Masegese, Edwin Moses na Ammo Mkuno.
Taarifa kutoka majimbo mengine ya Dar es Salaam, zilieleza kuwa katika Jimbo la Kinondoni walijitokeza wagombea tisa, Ubungo sita na jimbo jipya la Kibamba 10.
*Morogoro Kusini
Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, lililopo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini nalo lilijikuta likipata wasaka ubunge 12, akiwemo mbunge anayemaliza muda wake, Dk Lucy Nkya.
Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro Vijijini, Shaibu Mtawa, alitaja baadhi yao aliowakumbuka kuwa ni Upendo Konyaki, Abdallah Mohammed, Athuman Maneno, Issa Dilunga na Semeni Mwinyimvua Kingalu.
Chilonwa, Morogoro
Mkoa mwingine ambao umepata wasaka ubunge wengi katika jimbo moja ni Dodoma, katika Jimbo la Chilonwa, lililokuwa likiongozwa na Hezekiah Chibulunje, ambaye alitangaza kutogombea tena ubunge. Waliochukua fomu mpaka jana mchana walifikia wagombea 12.
Miongoni mwa waliojitokeza kuwania jimbo hilo ni Godrick Ngoli, Paschal Ndolosi, Charles Ulanga, Peter Mlugu, Amos Kusakula na Chiuti Masagasi Jimbo la Mtera, mbunge anayemaliza muda wake, Livingstone Lusinde, naye amejikuta akikabiliwa na ushindani wa makada sita, akiwemo Charles Ulanga, Essau Mzuri na Dk Charles Msendekwa.

10 July, 2015

Kama uliikosa hotuba nzima ya Rais Kikwete July 9 2015.

20101207 - Brussels , Belgium - European Development Days - The Energy Evolution - Mobilising Energy for Sustainable Development - H. E. Jakaya Mrisho Kikwete , President of the United Republic of Tanzania © European Union
Kama ulikosa time ya kumtazama au kumsikiliza Rais Kikwete kwenye hotuba yake akilivunja Bunge Dodoma June 9 2015 unaweza kuutumia muda wako kumsikiliza hapa chini.
Amezungumzia ishu nyingi sana ikiwemo Wasanii na alivyowasaidia, soka, miaka yake kumi ya uongozi na aliyoyafanya pamoja na mambo mengine

09 July, 2015

Hotuba ya Rais kikwete leo july 9

.Mh Dr Jakaya Kikwete ambaye ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania amemaliza kulihutubia Bunge la kwa mara ya mwisho kwenye muhula wake wa urais muda mfupi uliopita.









Usisumbuke Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO, SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>mawere_mtoka_mbali,

Kilichojadiliwa kwenye Kikao cha CCM Dodoma, Waziri Mkuu, Urais, Makundi.. Maneno ya Rais JK

Rais JK
Stori kuhusu Siasa zinapewa nafasi kubwa sana sasa hivi, Tanzania inaingia kwenye Uchaguzi Mkuu Mwezi October 2015… Tayari wapo waliotangaza Kugombea nafasi mbalimbali lakini macho ya wengi yako kwenye nafasi ya Urais, mpaka sasa kuna majina zaidi ya 35 ya watu waliotangaza Kugombea nafasi ya Urais kupitia CCM.



 Hii ni Tweet ya Rais JK aliyoweka muda mfupi uliopita


Rais Kikwete yuko Dodoma, imenifikia hii Ripoti ya kilichoendelea jana wakati wa Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili cha CCM

Usisumbuke Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO, SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>mawere_mtoka_mbali,

06 July, 2015

NEWS toka Mahakama ya Kisutu Dar, Hukumu ya Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona..

breaking-news-youtube-cover-free-2560-1440-pixels
Stori kutoka Mahakama ya KISUTU Dar es Salaam ziliingia kwenye Headlines za vyombo vya Habari mfululizo baada ya Mahakama hiyo kuahirisha kusoma hukumu ya Mawaziri wawili wa zamani, Basil Pesambili Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Hazina kwa mara mbili mfululizo kutokana na sababu mbalimbali.
Leo July 06 2015 imesikika tena toka Mahakamani hapohapo, Hukumu imetolewa… Basil Mramba na Daniel Yona wamekuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na faini ya Milioni 5 kila mmoja, alafu Grey Mgonja ameachiwa huru baada ya Mahakama kumwona hana hatia.

Usisumbuke Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO, SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>mawere_mtoka_mbali,  
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

05 July, 2015

MAGAZETINI JULY5: Wabunge 42 UKAWA watimuliwa, Zitto ataja walioficha mabilioni na Risasi zarindima BVR.

Image result for sunday newsMWANANCHI
Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano ambalo uhai wake unaisha Julai 9, linaonekana dhahiri kwenda mrama baada ya wabunge 23 kumlazimisha Spika kuwatimua kikaoni wakipinga kuwasilishwa kwa miswada mitatu kwa hati ya dharura.
Kwa siku tatu mfululizo, Spika Anne Makinda amekuwa akipata shida kuendesha chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na mbinu waliyogundua wapinzani ya kupiga kelele kukwamisha shughuli za Bunge.
Juzi, kiongozi huyo wa Bunge aliamua kuwapeleka wabunge 11 mbele ya Kamati ya Maadili kwa makosa ya kudharau kiti chake na chombo hicho kikaibuka na adhabu ya kuwafungia wabunge wanne kutohudhuria vikao vyote vilivyosalia, wengine wawili kufungiwa vikao viwili.
Jana, hali iliendelea kuwa ya mapambano baada ya wabunge hao kuhoji uhalali wa adhabu hiyo, huku wakihoji sababu ya miswada hiyo kuwasilishwa kwa dharura.
Ezekia Wenje, mbunge wa Nyamagana, aliendelea kubishana na Spika na kusababisha atangaze kumzuia kushiriki vikao vitano, uamuzi uliosababisha wabunge wengine wa upinzani kusimama na kupiga kelele wakitaka nao waadhibiwe.
Spika Makinda alisema kuwa ametumia kanuni ya 74(i) kuwatimua wabunge hao kwa kushindwa kuheshimu kiti kwa kupiga kelele.
Wakati wabunge waliopewa adhabu wakiongezeka, wenzao ambao hawakuwapo sasa wamehamasishwa kwenda mjini Dodoma kuendelea na walichokiita mapambano, hali inayoweza kusababisha Bunge hilo likavunjwa likiwa limepukutika wabunge wa upinzani.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba amesema CCM inakabiliwa na kazi ngumu ya kupata mgombea wa urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka huu, akionya kuwa makundi ya urais yasipomalizwa yanaweza kufika hadi ngazi ya kata.
Makada 38 wamejitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho tawala ya kugombea urais katika kipindi ambacho kuna ongezeko kubwa la nguvu ya vyama vya upinzani, huku vyama vinne vikiwa vimeamua kusimamisha mgombea mmoja.
Tayari vikao vya kujadili jinsi ya kumpata mteule wa kupeperusha bendera ya chama hicho vimeshaanza kwa wenyekiti na makamu wao kukutana na jana Kamati Kuu ilikuwa inakutana mjini Dodoma.
Akiangalia hali hiyo, Jaji Warioba aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho tawala kinatakiwa kuwa makini katika mchakato huo, kwa maelezo kuwa unaweza kuacha majeraha makubwa kutokana na makundi yaliyoibuka.
“CCM inakabiliwa na wakati mgumu wa kupitisha jina la mgombea urais kutokana na waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 38, na mpaka sasa imekuwa ni vigumu kutabiri atakayepitishwa, jambo ambalo halikujitokeza wakati wa upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995 na 2005,”  Jaji Warioba
Alisema kila unapofika Uchaguzi Mkuu kunakuwa na changamoto zake, lakini mwaka huu CCM inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kwa sababu uchaguzi huo utamleta rais mpya na mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Alisema jambo la kwanza lililotokea katika mchakato wa kumpata mgombea urais litakalokifanya chama hicho kuwa na wakati mgumu ni kitendo cha baadhi ya wagombea kueleza sera zao, wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya uchaguzi.
“Waliotangaza nia wamekuwa wakieleza sera zao na ukiwasikiliza unaona kama walikuwa wagombea binafsi hivi kwa sababu CCM ina sera, wanayo ilani ambayo ipo tayari na yeyote atakayepeperusha bendera ya CCM lazima ajikite kwenye ilani ya chama,” alisema jaji Warioba.
“Kama mtu ametangaza sera na vipaumbele vyake na havifanani na vipaumbele vya ilani ya chama unafanyaje? Ni mtihani mwingine huo.”
Alisema jambo la pili ni kukiukwa kwa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote anayehusika kwenye ngazi ya maamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais, huku akiwatolea mfano wajumbe wote wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao ndio humchagua mgombea urais wa chama hicho.
“Nimeambiwa kwamba wajumbe wa mkutano mkuu walikatazwa kudhamini wagombea, lakini tulivyoona ni kwamba viongozi wengi wameonyesha waziwazi wapo kundi gani, wapo waliojitokeza na kusema na wengine hawakusema lakini wanajulikana wanamuunga mkono mgombea gani,” alisema.
“Hawa ndio watakwenda kuchuja, sasa hapa itakuwa kazi ngumu na inawezekana kukawa na mgongano wa maslahi na hilo lisipoangaliwa linaweza kufanya mchujo ukaonekana kuwa haukuwa wa haki. Jambo hili linatakiwa kuangaliwa na hasa kwa kuwa kuna makundi.”
MWANANCHI
Wakati watu watano wakijeruhiwa, wawili kwa kupigwa risasi, kwenye uandikishaji wa wapigakura eneo la Makunduchi, mkutano baina ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wadau umevunjika kutokana na mzozo wa mgwanyo wa majimbo.
Vurugu hizo zimetokea baada ya watu waliokuwa wamekusanyika katika Msikiti wa Kubini kwa madhumuni ya kupinga kazi hiyo ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura wakituhumu kuwapo kwa mamluki waliokuwa wakiandikishwa, lakini wakajikuta wakivamiwa na kundi la askari wasiokuwa na sare ambao walikuwa na silaha za moto.
Waliojeruhiwa kwa risasi ni Kheri Makame Hassan na Ramadhani Hija Hassan wote wakazi wa Makunduchi wakati Ali Seif Issa, Ali Hassa Hassan kutoka Paje akiwa amepigwa kwa magongo na nondo na kuumia vibaya miguuni, na Hassan Ali Ameir.
Majeruhi wao walisema walikuwa katika kituo cha Nganani, Shehia ya Nganani Kusini Unguja ndipo walipokuja watu waliovaa vinyago na kuwaamuru waondoke eneo hilo wakati uandikishaji ukiendelea.
“Ilikuja gari na watu waliojifunika nyuso zao wakatuambia tuondoke na sisi tukakataa kwa sababu tulikuwa tunazuia kuandikishwa mamluki katika eneo letu. Baada ya kubishana pale wakaenda kuchukua gari nyingine wakaanza kutupiga,” alisema Kheri ambaye amepigwa risasi ya pajani.
“Watu waliojifunika nyuso walikuja mara mbili na kuondoka kabla ya kufanya shambulio na kufanikiwa kuondoka katika eneo la tukio la Nganani kwa kutumia magari mawili,’ alisema Faki huku akilalamika kusikia maumivu.
Shuhuda wa tukio hilo, Ameir Mussa, mkazi wa Makunduchi, alisema kwamba waliamua kukusanyika eneo la msikiti wakitafakari jinsi ya kuzuia uandikishaji wa wapigakura mamluki, ambao ni pamoja na walio na umri mdogo.
“Lilikuja kundi la watu mara mbili na kuondoka. Walikiwa wamefunika nyuso zao na waliporudi kwa mara ya mwisho walitushambulia kwa kutumia silaha za kienyeji na baadaye kufyatua risasi za moto na kujeruhi watu wawili,Mzee Ameir.
Daktari wa zamu wa Hospitali ya Al Rahma, Seif Suleiman alithibitisha kupokea majeruhi na kusema kwamba katika hatua za awali wanazuia damu kuvuja kutoka kwenye majeraha.
Alisema wanaendelea na vipimo ili kujua majeraha hayo yamesababishwa na nini. “Tumewafanyia x-ray ili kujua majeraha yao yanatokana na nini lakini yanaonesha wazi kuwa ni majeraha kama ya risasi kwa kuwa risasi jeraha lake linakuwa ni kitobo kidogo inapoingia lakini kitobo kikubwa inapotokea risasi.” Dk Suleiman alisema majeruhi hao wanaendelea vizuri baada ya kutibiwa na wengine wataruhusiwa watakapopata nafuu.
“Wapo walioumia sana hao wataendelea kuwepo hospitali kwa sababu wametokwa damu nyingi sana na kutoka Makunduchi hadi Mjini ni mbali kwa hivyo wanahitaji kupumzishwa kwanza hadi hapo watakapopata nafuu,”  Dk Suleiman.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saadi alisema kuwa katika mkoa wake kuna uandikishaji wananchi kuwaingiza kwenye Daftari la Wapigakura, lakini hana taarifa za watu kupigwa risasi na kwamba anachojua ni risasi hizo kupigwa hewani na hivyo hazijajeruhi mtu.
MWANANCHI
Kiongozi mkuu wa chama chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe jana alianika orodha ya majina ya watu wanaotuhumiwa kuhodhi akaunti zenye mabilioni ya fedha nje ya nchi, lakini akasita kuyataja kutokana na sababu za kisheria.
Zitto aliwapa waandishi wa habari orodha hiyo akisema waende kufanyia kazi kwa kuwahoji wahusika kulingana na taaluma yao.
Orodha hiyo ina majina yenye asili ya kiasia isipokuwa wachache ambao wanaonekana wana majina ya kibantu.
Zitto alisema: “Majina ninayo haya hapa niwataje nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki kampuni kubwa.”|
Alisema Zitto alisema wamejaribu kuishinikiza Serikali ichukue hatua, lakini inaonekana kutotaka kufanya hivyo na kwamba anaamini waandishi wa habari kwa kutumia taaluma yao wataweza kuwaanika wahusika.
Wakati maofisa wa ACT wakigawa orodha ya majina hayo, wananchi walionekana kuwa na shauku ya kupata nakala ya karatasi hiyo yenye majina 99 ya wafanyabiashara hao maarufu ndani na nje ya nchi, lakini kiongozi huyo hakuwa tayari kuwapatia na badala yake akiwaambia wasome magazeti ya kesho (leo).
Zitto alisema kwamba kati ya majina ya raia hao wenye mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kuna wengine wanamiliki kihalali lakini wengine wamejirundikia isivyo halali.
‘’Nimeamua leo kuiweka orodha hii wazi kama shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi kabla ya Bunge kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa habari aliyepo kwenye mkutano huu nimempatia nakala yenye majina 99 ya Watanzania au watu wenye uhusiano na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya Uswisi. Jumla ya akiba katika akaunti benki hii pekee ni Dola 114 milioni za Marekani,’’
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ametawawa kuwa chifu wa mkoa na wazee wa Dar es Salaam na kuitaka serikali kuhakikisha inawarudishia wananchi chenji zinazotokana na ufisadi wa Escrow , EPA na Richmond.
Dk Slaa alisema ingawa wazee waliungana na Hayati Mwalimu Nyerere kupambana na maadui wa tatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini kwa sasa ameongezeka adui wa nne ambaye ni ufisadi.
“Ujinga alioupinga Mwalimu na wazee umeondoka? Lakini ujinga, umaskini na maradhi na kuna adui wa nne ambaye ni ufisadi,” alisema.
Alisema hakuna Mtanzania ambaye atakwenda dukani na Sh10,000 kununua chumvi na kibiriti halafu akaacha chenji yake dukani kwa makusudi na hivyo Watanzania bado wanadai fedha zao zilizopotea kutokana na ufisadi.
Kadhalika Dk Slaa alisema kitendo cha wazee hao kukutana katika kongamano hilo kinaashiria kuwa wana kiu, njaa na matumaini ya kutaka mabadiliko.
HABARILEO
Jitihada za Serikali kuhakikisha rasilimali adimu ya gesi yenye fursa ya kutokomeza umasikini kwa Watanzania wote inanufaisha umma zaidi, zimeendelea kupingwa ili rasilimali hiyo inufaishe sehemu ndogo ya jamii.
Katika kuhakikisha gesi inakuwa fursa ya kuondoa umasikini kwa umma wa Watanzania na kutimiza ndoto za Rais Jakaya Kikwete kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania masikini, mwishoni mwa wiki hii Serikali iliwasilisha bungeni miswada mitatu ya sheria ukiwemo Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015.
Mingine ni Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015.
Hata hivyo, kazi ya kuzuia manufaa hayo kwa umma iliyoanza tangu kuvumbuliwa kwa gesi nyingi baharini inayozidi futi za ujazo trilioni 55, iliendelea na kuvuruga vikao vya Bunge, ambavyo vimelazimika kuendelea leo na kesho kutwa, siku ya Sikukuu ya Sabasaba.
Sehemu ya kazi hiyo ilihusisha baadhi ya wabunge walioamua kuzuia jitihada hizo za Serikali, huku baadhi yao wakitamka wazi bungeni kwamba, wenzao wameshawishiwa na kampuni na wafanyabiashara wanaonyemelea kunufaika zaidi na rasilimali hiyo.
Gesi hiyo inayozidi futi za ujazo trilioni 55, pekee ni mtaji katika kuanzisha na kuendeleza miradi yoyote ya umma, katika sekta zote zinazogusa maisha ya Watanzania.
Profesa Sospeter Muhongo, amesema kiasi hicho ni sawa na mapipa bilioni 10 ya gesi na kwa bei ya chini ya dola za Marekani 50 kwa pipa, ni sawa na mtaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 500.
Mtaji huo ni sawa na karibu nusu ya bajeti ya nchi kubwa ya Uingereza ya mwaka 2014, ambayo ilikuwa Dola za Marekani trilioni 1.1. Uwazi, elimu.
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM) alisema miswada hiyo ikipitishwa na kuwa sheria, itaweka uwazi katika leseni na mikataba ya madini, gesi na mafuta.
Naye Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema miswada hiyo isipopitishwa kuwa sheria, itakuwa hasara kubwa kwa Watanzania, ikisubiri Bunge lijalo Serikali italazimika kuanza kuwajengea upya uwezo wabunge hao katika jambo hilo, wakati wabunge wa sasa walishapata elimu hiyo.
“Wabunge hawa wamejengewa uwezo, wameenda nchi mbalimbali kujifunza masuala ya gesi na mafuta na tangu mwaka 2010 tumeanza mchakato wa jambo hili, ndiyo sababu tunataka itungwe sasa vinginevyo itakuwa matatizo mbele,Simbachawene.
Hasara uchelewaji Simbachawene alisema masuala ya kujadili mikataba na kampuni za gesi, inachukua kati ya mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu, hivyo kama sheria haitakuwa tayari, uzalishaji uliopangwa uwe kati ya mwaka 2018 na 2019, utalazimika kucheleweshwa, maana yake muda utazidi kusonga mbele na itakuwa hasara kwa Watanzania.
“Suala la majadiliano ya mkataba si la wiki moja au mwezi, ni kati ya mwaka mmoja na zaidi, sasa unasema Bunge lijalo ndiyo lifanye kazi hiyo unajua litakuwaje?” Alihoji.
Alisisitiza kuwa Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji ukipitishwa, utafanya mikataba yote ya madini na gesi iwe wazi na halitakuwa jambo la siri kama ilivyo sasa.
HABARILEO
Hatimaye baada ya hujuma ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani kushindwa, Serikali imewasilisha bungeni miswada ya sheria kuhusu masuala ya mafuta na gesi, huku matumizi ya mapato ya gesi yakiwekewa vizingiti.
Akisoma hotuba ya Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 bungeni jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema muswada unaweka masharti kuhusu uanzishwaji wa Mfuko wa Mafuta na Gesi, ambao utakuwa na akaunti mbili zitakazotunzwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alizitaja akaunti hizo ni Akaunti ya Kupokea Mapato na Akaunti ya Kutunza Mapato na kwamba mfuko wa mapato yatokanayo na mafuta na gesi, unapendekezwa kuanzishwa kwa madhumuni ya kupokea na kugawa mapato yatokanayo na mafuta na gesi kwa kuzingatia malengo makubwa matatu.
Malengo hayo ni kuhakikisha uimara wa kifedha na kiuchumi, kugharamia uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kulinda rasilimali kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Katika muswada huo, Nchemba pia alitaja vyanzo vya mapato vya mfuko huo kuwa ni mirabaha, gawio na faida ya Serikali katika shughuli za mafuta na gesi.
Vingine ni kodi za mapato ya makampuni, ambayo hukatwa baada ya kupata faida ghafi na gawio litokanalo na tasnia ya mafuta na gesi pamoja na faida itakayopatikana kutokana na uwekezaji wa fedha za mfuko.
Nchemba alisema inapendekezwa katika muswada kwamba mapato yote ya mfuko yawekwe kwenye Akaunti ya Kupokea Mapato.
Baadaye, Akaunti ya Kutunza Mapato itapokea kiasi cha asilimia ya mapato kutoka kwenye Akaunti ya Kupokea Mapato kwa kuzingatia miongozo ya kibajeti.
NIPASHE
Kamati Kuu Maalum (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imekutana kwa dharura mjini Dodoma kupokea, kuchambua na kutoa baraka kwa vipaumbele na ahadi za Rais ajaye vilivyoainishwa katika ilani mpya ya uchaguzi ya mwaka 2015.
Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete; iliwaita Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam ya Kuandaa Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi, pamoja na wajumbe wake kwa ajili ya kuikabidhi na  kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo.
Kamati hiyo ilikuwa na kibarua kizito cha kutoa ufafanuzi kuhusu Rasimu za awali ambazo zilikuwa zimefanyiwa maboresho na kisha kupatikana kwa ilani mpya itakayotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kabla ya Rais Kikwete kuwasili mjini hapa saa, 8:37 mchana na kuendesha kikao hicho kwa zaidi ya saa nne; wapambe wa makundi ya baadhi ya wagombea wa kiti cha urais, walionekana wakirandaranda Makao Makuu ya CCM kwa lengo la kutaka kujua kinachoendelea baada ya kuitishwa ghafla kwa kikao hicho.
Wajumbe wa Kamati ya Wassira ni Anamringi Macha (Katibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali-Zanzibar, Ali Juma Shamhuna.
Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Anthony Mavunde, Mbunge wa Manyoni Mashariki, Kapt. John Chiligati, na Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Aboud; ndio walioitwa ili kukabidhi ilani hiyo.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya CC hiyo, vilieleza kuwa ajenda nyingine ilikuwa ni kuwajadili wenyeviti 18 wa mikoa wa CCM ambao wanadaiwa kujilipua kwa kumuunga mkono mmoja wa wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, kupitia chama hicho.
Ajenda ya tatu ilikuwa ni kupata mrejesho wa hali halisi ya mwenendo wa bunge; kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo inaundwa na vyama vinne vya Ukawa kuchafua hali ya hewa kwa siku mbili na kulazimika kuahirishwa ili kupata utulivu.
Awali, akifungua kikao hicho, Rais Jakaya Kikwete alisema, kikao hicho ni maalum kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.

NIPASHE
Wazee  wa Mkoa wa Dar es Salaam wamempa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, majukumu ya kuikomboa nchi kwa  mara ya pili kama alivyofanya mwalimu Julius Nyerere wakati akiitoa mikononi mwa wakoloni.
Jukumu hilo alipewa jana na wazee hao baada ya kumvisha vazi la uchifu na kumkabidhi vitu mbalimbali vikiwamo kisu, panga, shoka, jembe, nundu na usinga ikiwa ni ishara ya kumtawadha kushika madaraka hayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo sasa atatambuliwa kama Chifu Mwinyikambi.
Mzee Ally Mwinyikambi, ambaye alimkabidhi Dk. Slaa uchifu huo kwa niaba ya  wazee wa mkoa huo, alisema wanamtaka ahakikishe anakiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
Katika hotuba yake, Dk. Slaa alisema kuwa, kilichotokea kimekumbusha enzi za Nyerere wakati akiwa anatoka masomoni.
Alisema kitendo hicho kimekihakikishia chama hicho ushindi wa kuelekea Ikulu katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Aliwahakikishia wazee hao na Watanzania kwa ujumla kuwa, uchaguzi huu lazima washinde kwa kishindo.
Alisema licha ya Mwalimu Nyerere kuwataja maadui wa nchi kuwa ni umaskini, ujinga, maradhi lakini CCM katika utawala wake wote imeshindwa kuyaondoa hayo.
“CCM imekuwa ikikusanya wazee wa chama chao pekee kwenye ukumbi na kuwapa Sh. 5,000 bila kuangalia matatizo yao, sisi hatuna ubaguzi  na tunawatambua wazee wote wa nchi hii,” alisema.
Alisema licha ya CCM kutawala muda mrefu lakini huduma za jamii kama barabara, afya, elimu utekelezaji wake bado ni hafifu wakati wananchi wamekuwa wakitozwa kodi.
“Tunadai chenji zetu kwenye Richmond, Epa, Escrow kwa sababu hizi ni fedha za watanzania ambao ndio walipakodi,” alisema.
Dk. Slaa alisema watakapoingia madarakani miaka kumi watahakikisha nyumba zilizojengwa kwa nyasi zinatoweka huku huduma za afya zilipungua gharama zake kulingana na kipato cha Mtanzania.
Kuhusu mashine za kuandikisha wapiga kura za Kieletroniki Biometrick Voters Registration,  katibu huyo aliwataka wazee kutumia muda wao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji na kuhakikisha hawatoki vituoni hadi vinafungwa.
Akiongelea migogoro ndani ya nchi ukiwemo ule wa madereva ambao waligoma hivi karibuni, alisema kuwa serikali haipaswi kutafuta mchawi bali itafute muafaka.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, wakili mashuhuri, Mabere Marandu, alisema kuwa Chadema haina tamaa ya madaraka na kwamba wakiingia madarakani muda wake ukiisha na wananchi wakiona hawajafanya kitu, wapo radhi kuondoka.
Naye, mwenyekiti wa Wazee Tanzania, Hashimu Issa Juma, alisema kuwa Chadema ikiingia madarakani itatoa pensheni ambao haitapungua 100,000.
Pia alisema watatoa matibabu bure na huwahakikishia usafiri wa daladala utakuwa bure.


Usisumbuke Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO, SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>mawere_mtoka_mbali,

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...