Mwanauchumi mashuhuri duniani, hayati Milton
Friedman (1912-2006) aliwahi kusema kuwa hakuna kitu kama lanchi ya bure
(there's no such thing as a free lunch). Ingawa hakuna uthibitisho kama
Friedman ndio mtu wa kwanza duniani kutumia hiyo sentesi katika hotuba
yake, watu wengi sana walimhusisha na huo usemi kwa muda mrefu wakati wa
maisha yake. Milton mwenyewe aliwashangaza wasikilizaji wake wa taasisi
ya CATO (CATO institute) nchini marekani (tarehe 6 May, 1993) aliposema
kuwa vitu vizuri maishani vinapatikana bure (the best things in life
are free). Hizi sentensi mbili zinapingana kwa kiasi fulani ingawa
zinaelezea kitu kimoja. Si ajabu wanauchumi wengi duniani walipokea
habari za kifo cha Friedman mwezi uliopita kwa masikitiko makubwa sana.
Tafadhali marafiki zangu wa-jamaa (socialists)
msianze kubeza uamuzi wa kutumia mifano ya Friedman katika makala hii.
Nimeamua kutumia hotuba za Friedman ambaye wengi wenu mnamuita bepari
(capitalist), kwa sababu kubwa mbili. Kwanza, matokeo ya mechi kati ya
ubepari na ujamaa ni kwamba mabepari wameshinda 5-2. Pili, watanzania
wengi sasa wameutambua uongo wenu wa-jamaa kwa sababu ya mali za nchi
mnazojilimbikizia kila siku huku mkituambia watanzania wenzenu tufunge
mikanda. Friedman alifafanua usemi wake kwa kusema kuwa; hakuna mtu
anayetumia pesa za mwenzake kwa makini zaidi ya anavyotumia pesa zake
mwenyewe (nobody spends somebody else's money as carefully as he spends
his own).
Ni ukweli uliothibitishwa sasa, hakuna kitu cha
bure duniani. Hakuna chakula (lanchi) cha bure duniani. Kwa miaka mingi
sasa nchi maskini za kiafrika zimekuwa zinapokea misaada kutoka kwa nchi
tajiri duniani kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Ukweli wa mambo
unaonyesha kuwa misaada hiyo haijabadili hali zetu za maisha na badala
yake siku hadi siku watanzania na waafrika kwa ujumla tunazidi kuwa
masikini. Ninadhani kuwa ni wakati muafaka kwa waafrika kusoma tena
hotuba za Friedman ili kutambua kuwa hakuna kitu kama lanchi ya bure.
Hili lundo la misaada tunayoletewa sio ya bure kama wanavyoiita
wafadhili wetu. Hizi lanchi za bure tunazopewa hazitasaidia kabisa
juhudi zetu za kuondokana na umasikini. Wanauchumi wengi walishang'amua
hili; hizi lanchi za bure zinatudumaza na zitatuponza milele.
Kama huamini hebu jiulize maswali yafuatayo.
Karne nyingi zilizopita wakati wa mapinduzi ya viwanda (industrial
revolution), ni misaada gani ya nje ambayo wazungu wa Ulaya walipokea
ili kufanikisha mapinduzi hayo? Je ni fedha kiasi gani za kigeni benki
ya dunia iliwapa wazungu waliohamia Amerika na Australia kujiendeleza?
Ni misaada kiasi gani ilitakiwa ili kuwawezesha wazulu kujenga falme
zenye nguvu kabla ya ukoloni? Je, wamisri walipokea mikopo kiasi gani
ili kujenga mapiramidi? Majibu ya maswali yote hayo ni HAKUNA. Misaada
ya nje inadumaza badala ya kuendeleza. Misaada inayoitwa ya bure
inafanya watu kuwa wategemezi badala ya kufanya kazi kwa bidii ili
kujiletea maendeleo. Misaada ya nje inawapa viongozi wetu nafasi ya
kuifuja kwa sababu hakuna uhakika wa ni lini na ni wapi ilitolewa.
Ukweli wa mambo ni kwamba; hakuna msaada wowote tunaopewa na hawa
wanaojiita wafadhilli wetu. Hii ni njia mpya inayotumiwa na wanaojiita
wafadhili wetu kutudumaza.
Tuseme ukweli; nchi za kiafrika hazihitaji
misaada ya nje ili kuendelea au kutokana na umasikini. Nchi zetu
hazihitaji mipango ya wafadhili na wakopeshaji ili kufanikiwa. Nchi zetu
zinahitaji uhuru wa fikara (free minds) na juhudi zetu wenyewe badala
ya lanchi za bure. Nitamnukuu tena Friedman hapa; ni kweli hapa duniani
kuna lanchi ya bure, lanchi huru, lanchi isiyopimika, Lanchi yenyewe ni
soko huria na vitu binafsi (in the real economic world, there is a free
lunch, an extraordinary free lunch, and that free lunch is free markets
and private properties). Sina nia ya kuchanganya madesa hapa (nikitumia
lugha ya mlimani) kwa kuongelea soko huria na misaada ya nje katika
makala moja. Nia kubwa hapa ni kusisitiza umuhimu wa kupunguza ushawishi
wa nje (iwe wa serikali au wa wafadhili) katika kuleta maendeleo ya
Afrika.
Watanzania na waafrika inabidi tujifunze kutoka
katika historia ambayo inaonyesha kuwa maendeleo ya kweli ni yale
yanayozalishwa ndani ya nchi na wananchi wenyewe. Maendeleo ya kweli
yataletwa na sisi wenyewe na watoto wetu na wala sio wanauchumi wa Benki
ya dunia na shirika la fedha-IMF. Misaada ya nje ni sumu ya maendeleo
yetu na inatudumaza. Makala hii pia inawalenga wale vijana wanaokaa
vijiweni bongo bila kazi huku wakilalamika kuwa serikali haijawasaidia.
Hakuna hata siku moja serikali yetu itakuwa na pesa za kutosha za
kumsaidia kila mmoja wetu awe tajiri. Ni wakati wa kujishughulisha
wenyewe ili kujiletea maendeleo. Makala hii inawalenga baadhi ya
viongozi serikalini wanaofuja mali zetu huku wakisingizia kuwa tuko
masikini kwa sababu hatupati misaada ya kutosha kutoka nje. Tunaweza
kupata na ni vizuri tukipata wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili
kuleta ushindani wa kimaendeleo (nguvu ya soko huria). Lakini Kama
tutakaa chini na kusubiri kupiga wafadhili virungu (kuomba lanchi za
bure na misaada), basi tutazidi kuwa masikini milele zote.
No comments:
Post a Comment