Showing posts with label NEWS. Show all posts
Showing posts with label NEWS. Show all posts

05 January, 2016

Serikali Yanunua Mashine Mpya Ya CT-Scan Katika Hospitali Ya Taifa Ya Muhimbili

Serikali imenunua mashine  mpya ya CT-Scan yenye thamani ya  takriban dola  za Marekani milioni 1.7  yenye  uwezo wa hali ya juu kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali  katika Hospitali  ya Taifa ya Muhimbili(MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Ununuzi wa mashine hiyo, umefanyika kufuatia agizo la Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoifanya hivi karibuni ambapo aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma zake na kuhakikisha vifaa tiba na dawa   vinapatikana ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya.

Hayo yamegundulika jana baada ya ziara ya Naibu  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi  Kingwangala aliyoifanya jana katika hospitali hiyo, ambapo alitembea Idara ya  Magonjwa ya Dharura,Idara ya Mionzi,  sehemu  mpya ya wagonjwa waliopo chini ya ungalizi maalum(ICU), ambayo inafanyiwa ukarabati na wodi mojawapo.

Akizungumzia kuhusu mashine ya CT-Scan Mkuu wa Idara ya Mionzi, Dkt. Flora Lwakatare alisema mashine hiyo , iliyotengenezwa na kampuni ya  Siemens  mpya imefungwa siku mbili zilizopita na imeshaanza kufanya majaribio  kwa wagonjwa 26  tangu ilipofungwa.

 Dkt. Flora aliongeza kwamba mashine hiyo iko moja tu nchini na katika nchi za Afrika Mashariki nchi nyingine iliyonunua mashine hiyo ni Kenya katika Hospitali ya Aghakhan.

“ Mashine hii inatoa huduma za hali ya juu kwa magonjwa ya moyo, ubongo, tumbo, kifua na inauwezo wa kupima kifua na tumbo kwa sekunde sita,” alisema.

Akizungumzia kuhusu mashine hiyo Naibu Waziri huyo, alisema imenunuliwa kwa fedha za Serikali wala sio mkopo.

“Tunatarajia kununua mashine hii katika hospitali ya Dodoma na Mwanza,” alisema Waziri Kingwangala.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Laurence   Maseru alisema mashine hiyo ina sahani 128 mara 2 ikilinganishwa na iliyokuwepo ambayo ilikuwa inatumia  sahani sita.

 Kwa upande wa mashine ya MRI alisema tangu ilipofanyiwa matengenezo makubwa Novemba 26, mwaka jana  hadi sasa imesha hudumia wagonjwa 560.

 Dkt. Kingwangala  alitembea katika Idara  cha huduma za dharura na kuangalia jinsi huduma zinavyotolewa, ambapo alielezwa na  Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura Dkt. Juma Mfinaga kuwa huhudumia wastani wa wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku na wanafanya kazi kwa kutumia mfumo maalum wa kompyuta bila kutumia karatasi.

Naibu Waziri huyo, mbali na kupongeza maboresho yaliyofanyika na huduma nzuri, alitoa maagizo kwa uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma  zinazotolewa hospitalini hapo kuwa za kitaifa zaidi.

 Alitolea  mfano  huduma  kulipa kwa kuongeza vitanda na matumizi ya choo kimoja kila chumba ili kuweza kuvutia wateja.

 “Sisi tunaweza kufanya biashara kwa kuboresha huduma za kulipa ili zimpendeze na kuvutia wateja. Na fedha zitakazopatikana zitatumika kununua dawa , vifaa tiba na kuwapatia wafanyakazi motisha, "alisema.

Aliutaka uongozi huo pia kuhakikisha inawalipa wafanyakazi fedha za  malipo ya ziada kwa wakati ifikapo tarehe 25 ya mwezi unaofuata,kutumia mfumo wa kompyuta sehemu zote, kupunguza msongamno wa wagonjwa na kuwa wabunifu.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne Ya Januari 5

kutana na vichwa vya habari vilivyoko katika magazeti pendwa hapa nchini leo January 5,2016

Obama kutangaza kudhibiti silaha Marekani


Rais Obama anatarajiwa kutangaza mpango wa kuhakiki silaha katika masoko ya sihala hii leo wakati atakapotangaza mpango huo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo amesema anataka kutumia mamlaka yake ya urais kwa sababu bunge la congress limeshindwa kushughulikia tatizo hilo.
" Habari njema ni kwamba sio tu ni mapendekezo yaliyo ndani ya mamlaka yangu ya kisheria kama rais lakini pia nina matumaini ni jambo llililopokelewa na wamerekani wengi wakiwemo wamiliki wa silaha, wanaounga mkono na wanaoamini. Kwa hiyo katika siku chache zijazo tutatekekeleza mpango huu, tutahakiksha watu wanaelewa tutakavyofanya mabadiliko haya na tutakavyotekeleza."
Rais Obama ametoa angalizo kuwa mpango usitarajiwe kuondoa silaha zote mikononi mwa wahalifu
" Japo ni lazima tuwe wazi kwamba hatua hii haitaondoa tatizo la makosa ya jinai katika nchi hii, wala haitaweza kuzuia mauaji ya watu wengi, wala hautaweza kuondoa kila silaha mikononi mwa wahalifu, kubwa utaokoa kwa kiasi kikubwa maisha ya watu katika nchi hii na kupungunza maumivu ya familia kuondokewa na wapendewa wao kulikosababishwa tna silaha zilizokuwa mikononi mwa watu wasio sahihi."

04 January, 2016

Zinedine ZIdane atachukua nafasi yakua kocha wa Real Madrid baada ya Rafael Benitez kufukuzwa

2FB01D0B00000578-0-image-a-44_1451919445392
Real Madrid inatarajia kumfukuza kazi kocha wao Rafael Benitez baada ya club yao kuwa kwenye misukosuko ya kimatokeo na kiuongozi. Real Madrid kwa sasa ipo namba 3 kwenye msimamo wa ligi nyuma ya Barcelona na Atletico Madrid.
Benitez amejikuta kwenye pressure baada ya matokeo mabovu na kutokuelewana na wachezaji nyota hasa Ronaldo tangu aanze kukiongoza kikosi hicho. Rais wa club hiyo aliita meeting ya board ya club na baadae itafuatiwa na press conference ya kutoa taarifa.
Mtu ambae anatarajiwa kuchukua mikoba ya Benitez hadi mwisho wa msimu ni Zinedine ZIdane ambae alikua kocha wa kikosi cha vijana cha Real Madrid. Lakini inasemekana Jose Mourihno anatarajiwa kurudi mwishoni mwa msimu huu.
Rais wa club ya Real Madrid anabaki kuwa shabiki mkubwa wa kocha Jose Mourihno ambapo inaonekana kuwa ndio option pekee kwa club hiyo kwa sasa. Mara kadhaa rais wa club amekua akimpa support kocha wao licha ya kuwa na matokeo mabaya lakini hivi sasa imefika mwisho. Kama akifukuzwa itakua amedumu kwa muda wa miezi 6 tu.

Waziri Mbarawa Atoa Siku Tatu Ukarabati Reli Ya Kati Iliyosombwa na Mafuriko


Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka watendaji wa Shirika la Reli nchini (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (RAHCO) kuhakikisha sehemu ya reli iliyosombwa na mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro inaunganishwa ndani ya siku tatu na huduma za treni kurejea. 
 
Prof. Mbarawa amesema hayo baada ya kukagua sehemu ya reli hiyo kutoka Kilosa hadi Magulu- Kidete kuona athari zilizosababishwa na mafuriko yaliotokana na mvua zilizonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma. 
 
“ Fanyeni kazi usiku na mchana ili ikifika alhamisi mawasiliano ya reli kati ya mkoa wa Morogoro na Dodoma yawe yamerejea na abiria waendelee kupata huduma ya treni ,” amesema Waziri Prof. Mbarawa. 
 
Amewahakikishia wananchi wa vijiji vya Munisagara, Mkadage, Mzaganza, Magulu na Kidete ambao usafiri wao pekee wa uhakiki ni wa kutumia reli watoe ushirikiano kwa serikali ili ukarabati na ujenzi wa reli hiyo ukamilike kwa haraka. 
 
Amewataka wananchi waishio pembezoni mwa reli katika wilaya ya Kilosa kupanda miti ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaosababisha mafuriko kwa urahisi wakati wa mvua na kubomoa reli kila wakati.
 
“Pandeni miti, lindeni miundombinu ya reli na acheni vitendo vya uharibifu wa mazingira ili ujenzi wa mwaka huu uwe wa kudumu na reli isiathiriwe kirahisi na kuwasababishia kero wananchi,” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa. 
 
Naye Diwani wa kata ya Kidete Bw. Mohamed Seleman Mbunda amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wananchi wake watashirikiana na serikali kulinda mazingira ili kudhibiti mafuriko yanayoharibu miundombinu ya reli kila wakati wilayani humo. 
 
Mafuriko wilayani Kilosa ni matokeo ya mvua zinazonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma ambayo husababisha maji ya mto mkondoa kuacha mkondo wake na kubomoa tuta la reli katika eneo la Msagali hadi Kilosa kila wakati. 

Mvua za hivi karibuni zilizonyesha mkoani Iringa na Dodoma zimesomba reli katika eneo la Magulu-Kidete kilomita 315 kutoka Dar es Salaam na kukata mawasiliano ya reli kwa siku tatu sasa. 
 
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa TRL na RAHCO kutafuta suluhisho  la kudumu katika madaraja 32 yaliyo katika mtandao wa reli ya kati ili yasiathiriwe na mvua wakati wote.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatatu Ya Jaunuari 4


Nimekuwekea hapa habari zilizopo katika magazeti pendwa hapa nyumbani. Chukua muda kupitia

Matokeo ya mapema ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yanaonyesha Waziri Mkuu wa zamani Faustin Archange Touadera anaongoza.

Bozize
Wagombea 30 walishiriki kwenye uchaguzi huo ambao huenda ukaingia kwa duru ya pili kati ya wagombea wawili watakaoongoza tarehe 31 Januari.
Bw Touadera hakupigiwa upatu kupata kura nyingi.
Alikuwa waziri mkuu kwenye serikali ya rais wa zamani Francois Bozize, aliyeondolewa madarakani 2013 na wapiganaji wa Kiislamu wa kundi la Seleka.
Upigaji kura ulifanyika tarehe 30 Desemba, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakilinda vituo vya kupigia kura.
CAR kwa sasa inaongozwa na kaimu rais Catherine Samba-Panza.
Bw Touadera, 58, alikuwa mhadhiri wa somo la hesabu chuo kikuu kabla ya kujiunga na siasa. Aliwania urais kama mgombea huru, bila kutumia chama chochote cha siasa.
Baada ya kura kuhesabiwa mji mkuu Bangui, yuko mbele sana ya mpinzani wake wa karibu Anicet Georges Dologuele, ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani.
Kando na Bangui, kura nyingi hazijahesabiwa katika mikoa mingine ya CAR, sawa na za wakimbizi na raia wanaoishi nje ya nchi.
Bw Touadera ana zaidi ya kura 120,000 naye Bw Dologuele ana takriban kura 68,500.
Wa tatu ni Desire Kolingba, mwana wa rais wa zamani, tume ya uchaguzi imesema.
Wapiga kura 1.8 milioni walitarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Saudi Arabia yavunja uhusiano na Iran

Kifo
Saudi Arabia imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya Iran na huku kukiwa na hali mbaya ya mvutano kufuatia utekelezaji adhabu ya kifo kwa mhubiri maarufu wa dini ya Kiislamu.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Saudia, Adel al-Jubeir, ameishutumu serikali ya Iran kwa kusambaza silaha na kuanzisha jela na kuwafunga watu wanaodhaniwa magaidi katika ukanda wake .
Waziri huyo amesema wanadiplomasia wa Iran wanatakiwa kuondoka Saudia ndani ya saa arobaini.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, waandamanaji mjini Tehran waliuvamia ubalozi wa Saudia mjini Tehran, huku wakilaani utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa Sheikh Nimr al-Nimr na watu wengine 46.
Watu hao waliouawa inasadikiwa walikuwa na hatia ya makosa yanayohusiana na ugaidi.
Kiongozi mkuu wa Iran alimweleza Sheikh huyo kama shahidi ambaye alikuwa akitetea amani na kufanya maandamano ya amani.

CHANZO: BBC

03 January, 2016

Bajeti ya Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar Yatengwa.......Kinachosubiriwa ni ZEC Kutangaza Tarehe Ya Uchaguzi

Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema bajeti ya uchaguzi wa marudio imeshatengwa na wanachosubiri ni Mwenyekiti wa Tume ya  Uhaguzi Zanzibar (ZEC) atangaze tarehe hiyo ya kufanya uchaguzi.

Amesema bajeti hiyo haitatofautiana na ile iliyotumika katika uchaguzi wa Novemba 2015 iliyofikia karibu ya shilingi bilioni saba.

Amekanusha kauli kuwa uchaguzi huo hautafanyika kwa vile matokeo yanayolazimisha kutangazwa na CUF yameshafutwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi, Balozi Seif amesema mazungumzo yanayoendelea ni ya kuhakiksha amani inaimarika Zanzibar na si suala la uchaguzi uliofutwa.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 52 sherehe za Mapinduzi Balozi Seif amewabeza wanaosusuia sherehe hizo kwa madia kuwa Rais Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein kuwa si halali ni upotoshwaji mkubwa.

Amefahamisha kuwa rais huyo yupo kihalali na hata mawaziri wake wote na watamaliza ukomo wao atakapoapishwa rais mwingine kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 28 (1) a cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na si kama inavyeleezewa kuwa ukomo wake umeisha tangu tarehe 2 Novemba.

Tazama video hii kumsikia akiongea na kujibu maswali ya waandishi kuhusu marudio ya uchaguzi Zanzibar.

Habari kuu Magazetini leo January 3

HABARILEO
Makatibu wakuu na Naibu Makatibu Wakuu walioteuliwa na kuapishwa juzi wamekutana katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya semina elekezi iliyoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mada zilizoandaliwa katika semina hiyo jana, Katibu Mkuu Kiongozi Sefue, alisema semina hiyo ni ya kikazi zaidi na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha viongozi hao waandamizi wanatekeleza wajibu wa kusimamia utendaji kazi wa serikali vizuri.
Balozi Sefue alisema kila Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu anapaswa kutambua kuwa nafasi yake ni ya maamuzi, hivyo serikali inatarajia kuona wanafanya maamuzi kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazomuongoza kila mmoja katika majukumu yake.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inawatarajia viongozi hao kuwa wasimamizi wazuri wa fedha za umma na kwamba haitarajii kuwepo kwa hati za ukaguzi wa mahesabu zenye kasoro.
Balozi Sefue aliongeza kuwa Makatibu Wakuu hao na Naibu Makatibu Wakuu ni mamlaka ya nidhamu katika wizara zao, hivyo serikali haitarajii kuona wanakuwa na kigugumizi katika kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaokuwa na makosa.
Aliwakumbusha pia kwamba haikubaliki kwa mtumishi aliyefanya makosa katika sehemu moja ya kazi, kuhamishiwa katika sehemu nyingine badala ya kuchukuliwa hatua palepale alipo.
HABARILEO
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba amesema hakutakuwa na msamaha na huruma kwa watakaobainika kuhujumu sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini.
Nchemba alisema hayo baada ya kubaini kuwepo kwa utafunwaji wa mapato ya serikali ya vibali vya mifugo, yanayokusanywa katika Mnada wa Pugu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Alibaini kuwepo kwa hujuma hizo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza ya kukagua mnada huo na machinjio ya Vingunguti yaliyopo Manispaa ya Ilala juzi usiku.
Baadaye alitangaza hatua kadhaa, ikiwemo Mkuu wa Mnada huo wa Pugu na watumishi waliokuwa zamu Desemba 24 mwaka jana na Januari Mosi mwaka huu, kesho Jumatatu wafike ofisi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Pili, Mwigulu alisema kuanzia sasa amesitisha ukusanyaji wa ushuru kwenye eneo la Mnada wa Pugu, badala yake makusanyo yote ya fedha za Serikali, yatafanyika kwenye Machinjio la Vingunguti kwa kutumia mashine za kielektroniki za Mamlaka ya Mapato Tanzania (EFDs).
Alisema mnada wa Pugu sasa utakuwa unatumika kutoa vibali tu vya mifugo ili kudhibiti ubora wa mifugo inayotakiwa kuchinjwa. “ Sitakuwa na huruma na hatua stahiki zichukuliwe kwa mtu yeyote mwenye dhamana ya kusimamia sekta hiyo atakayebainika kutowajibika kwa mujibu wa Sheria,” alisema.
Akizungumza katika machinjio hayo, Nchemba alisema ubadhirifu uliopo ni wa uandikaji wa vibali kwa mifugo wachache kwa ajili ya kwenda machinjioni, tofauti na idadi ya mifugo inayoingizwa machinjioni hapo. Alisema mifugo mingi inaingizwa machinjioni bila kibali.
Katika ukaguzi huo, Mwigulu alibaini uwepo wa utafunwaji wa kodi ya mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa ushuru, kwa ajili ya kupelekwa katika machinjio hayo kutoka Mnada wa Pugu.
“Kwa hatua za awali nimekutana na ubadhirifu wa kutafunwa kwa kodi ya mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa ushuru kwa ajili ya kuja kwenye machinjio ya Vingunguti kutoka Mnada wa Pugu Desemba 26,2015,” alisema.
Aidha, Nchemba alisema alisikiliza kero na maoni ya wananchi wanaotumia machinjio hayo pamoja baadhi ya viongozi wenye dhamana na kusimamia juu ya uendeshwaji wa machinjio hayo.
Nchemba aliagiza uongozi wa machinjio hayo, kukutana kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kukiuka taratibu na sheria. Uchinjaji wa ng’ombe na mbuzi katika machinjio hayo, hufanyika nyakati za usiku kuanzia saa 4 hadi 10 alfajiri.
HABARILEO
Watu sita wamekufa papo hapo na wengine 25 kujeruhiwa na kulazwa hospitalini kutokana na ajali mbili tofauti. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema mjini hapa jana kuwa ajali ya kwanza, ilihusisha basi la abiria lililokuwa na abiria 42, ambalo liligonga kingo za daraja, likaparamia miti miwili kisha kutumbukia ndani ya mto Lukosi, Iyovi eneo la Msosa huko Mikumi wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, katika barabara kuu ya Iringa – Morogoro.
Alisema tukio hilo ni la Januari Mosi mwaka huu majira ya saa 8 mchana. Basi hilo lilitokea Dar es Salaam, lilikuwa linakwenda Mbeya. Kamanda Paulo alisema dereva wa basi hilo aliendesha gari kushoto zaidi, akaenda kugonga kingo za daraja hilo, akaenda kuparamia miti miwili kisha alilitumbukiza ndani ya mto huo.
Kamanda huyo alisema katika ajali hiyo, watu watatu walikufa akiwemo dereva wa basi hilo na kujeruhi wengine 16, ambapo majeruhi 14 walilazwa katika Kituo cha Afya cha Tandika kilichopo eneo la wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa. Majeruhi wengine sita walisafirishwa hadi Hospitali ya Mkoa wa Iringa na kulazwa.
Kamanda alisema basi hilo lilibeba abiria 42 na chanzo za ajali hiyo kilielezwa na mashuhuda kuwa ni uzembe wa dereva wa basi, aliyeshindwa kufuata sheria za usalama barabarani katika eneo hilo la safu ya milima ya Iyovi, lenye kona nyingi na mito yenye madaraja. Alisema maiti mmoja ametambulika na ni dereva wa basi hilo.
Maiti wawili, mmoja mwanamume na mwingine mwanamke, bado hawajatambuliwa na wamehifadhiwa katika chumba za maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Alitoa mwito kwa watu kufika kuwatambua.
Kamanda huyo wa Mkoa alisema ajali ya pili ilitokea Januari Mosi mwaka huu, ambapo watu watatu walifariki papo hapo na wengine watano kujeruhiwa na kulazwa katika Kituo cha Afya cha Gairo wilayani Gairo mkoani Morogoro.
Alisema ajali hiyo ilihusisha gari ndogo, lenye namba za usajili T 252 CGV aina ya Toyota Vitz, lililokuwa likiendeshwa na Bundala Charles Mahimbo, mkazi wa Dar es Salaam. Gari hilo liligongana uso kwa uso na lori, lenye namba za usajili T531 CFE lenye tela namba T 509 AFY aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na dereva, Ally Said Magimbi (33), mkazi wa Mtongani , Dar es Salaam.
Alisema ajali hiyo ilitokea jioni eneo la Ngiroli wilayani Gairo barabara kuu ya Morogoro- Dodoma. Gari ndogo lilikuwa likitokea Mkoa wa Tanga kwenda Mwanza wakati lori kubwa lilitokea Kagera kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Paulo alisema watu watatu waliokuwa katika gari ndogo, walikufa papo hapo na wengine watano walijeruhiwa, miongoni mwao mmoja ni abiria wa lori. Kamanda huyo wa Polisi aliwataja waliokufa katika ajali hiyo ni Bundala Mahimbo ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, Flora Mugabo na Emmanuel Mahimbo, wote wakazi wa Nyakato mkoani Mwanza.
Majeruhi waliolazwa Kituo cha Afya Gairo ni dereva wa lori, Ally Magimbi, mkazi wa Mtongani Dar es Salaam, Peter Mahinda ambaye ni mkazi wa Nyakato na Hassan Mwera. Walioruhusiwa ni Judith Joseph na Scolastica Fransis aliyekuwa abiria kwenye gari kubwa.
HABARILEO
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) wiki ijayo inakutana na wadau kujadili nauli zitakazotumika kwa mabasi yaendayo kasi.
Kwa sasa kampuni ya UDA-RT inapendekeza nauli ya chini kuwa Sh 700 na wanafunzi kulipa nusu yake.
Aidha, katika mapendekezo yake, UDA-RT inataka nauli ya safari kwenye njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1400 na wanafunzi nusu ya nauli hizo.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra ilisema maombi hayo kwa ajili ya kutoa huduma za mpito za usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika awamu ya kwanza ya mradi wa DART yatajadiliwa na wadau ili kuona uhalali wake.
Ilisema kwa mujibu wa sheria, Sumatra inapaswa kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kuridhia viwango vya nauli.
“Katika kutekeleza hilo, mamlaka imeandaa mkutano ili kupokea maoni ya wadau ikiwa ni pamoja na watoa huduma, watumiaji wa huduma na wananchi kwa ujumla,” ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo wa wadau utafanyika Januari 5, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi ambapo wadau wote wa usafiri wanaalikwa.
MWANANCHI
Kasi ya Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano jana ilichukua sura ya aina yake wakati mawaziri watatu walipoibuka kwenye machinjio ya Vingunguti, na kutoa maamuzi magumu kutokana na kukithiri kwa uchafu, ubadhilifu wa makusanyo ya fedha za ushuru.
Wakiwa katika eneo la machinjio hayo mawaziri hao, Mwigulu Nchemba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi), Dk Hamisi Kigwangalla (Afya), na George Simbachawene (Ofisi ya Rais­Tamisemi), walishuhudia hali ya uchafu wa eneo hilo na baadaye kubaini ubadhilifu mkubwa.
Baada ya kufanya ziara hiyo iliyoanza saa 4:47 asubuhi na kumalizika saa 5:32, mawaziri hao hawakuridhishwa na hali ya usafi kwenye maeneo ya kuwekea nyama.
Mbali na hayo walisikiliza kero za wadau ambao ni wachinjaji na wauzaji wa mifugo, waliodai wanatozwa ushuru mkubwa kama malipo ya Sh11,000 kwa ng’ombe mmoja, fedha ambazo hulipwa mnada wa Pungu (sh6,000) na Vingunguti (Sh5,000).
Catherine Severine, ambaye ni mchuuzi aliyekuwa zamu usiku wa Desemba 24 mwaka jana, aliwaambia mawaziri hao kuwa kumekuwepo udanganyifu wa utoaji wa vibali kwenye mnada wa Pugu.
Alidai kuwa siku hiyo walifikishwa mbuzi 1,407 huku wenye vibali wakiwa 300 , ng’ombe 700 lakini wenye vibali halali 492, hivyo kwa hesabu za haraka, zaidi ya Sh3.4 milioni zilipotea.
Alisema kwa ujumla wanatakiwa wakusanye kiasi cha Sh75 milioni kwa mwezi, lakini walikuwa wanakusanya Sh18 milioni huku Sh55 milioni zikiingia mifukoni mwa wajanja. Simbachawene alimpa siku tatu mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwaondoa wale wote waliokaa muda mrefu katika eneo hilo na kujimilikisha kila kitu.
“Kigwangalla naomba usitufungie, Jumanne nitataka kupata maelezo ya waliohusika na haya mabanda. Si kweli kwamba yamegharimu Sh100 milioni. Hadi Jumatatu umeme uwe umerudishwa kwenye hayo mabanda, yatumike ili kupunguza mbanano,” aliagiza Simbachawene.
Mwigulu aliwataka wote waliokuwepo mnadani Desemba 24, kufika kwa katibu mkuu wa Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Jumatatu na kuanzia leo waanze kutafuta kazi ya kufanya kwa sababu ya kujumlisha ng’ombe na mbuzi imewashinda.
Mwigulu alisema hayo baada ya juzi usiku kukuta machinjio ya Vingunguti kuna vibali 300 vya mbuzi, lakini kukiwa na mbuzi zaidi 1,000 na ng’ombe zaidi ya 200 hawakuwa na vibali, kitu alichosema kinaashiria wanafanya makusudi siyo kwamba hawajui kujumlisha.
“Kuanzia sasa vibali vyote vya wanyama wanaotakiwa kuchinjwa hapa, vitolewe kwenye mnada wa Pugu, huku wakusanya ushuru wa Serikali Kuu na Halmashauri watakusanya hapa katika machinjio ya Vingunguti.
Mnaolipia ushuru hakikisheni mnaondoka na risiti, lango la kuingizia ng’ombe lijengwe mara moja hata matatu, manne tena kwa fedha inayopatikana hapa hapa machinjioni,” alisema Mwigulu huku akishangiliwa.
Kigwangalla alisema anakubali ombi la Simbachawene la kutaka wasifungiwe kwa muda na watavamia wakati wowote kukagua maagizo waliyotoa kama yanafanyiwa kazi. Alisema mambo aliyoyaona akiwa katika Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa miaka miwili iliyopita ndiyo aliyoyakuta jana , hivyo hatawavumilia wanaohusika.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi limemkamata raia wa Nigeria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya ambazo thamani yake ni kubwa ingawa haijajulikana.
Kamanda wa polisi wa JNIA, Martin Ottieno alisema mtuhumiwa huyo, Ejiofor Ohagwu, alikamatwa na kilo nne za dawa hizo ambazo alisema licha ya kutofahamu thamani yake kwa sasa, inaweza kuwa kubwa kwa sababu hawajawahi kukamata dawa za kiwango hicho.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, kilo moja ya heroin kwa bei ya mitaani ni kuanzia Sh90 milioni. Ottieno alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa saa 8:00 usiku wa kuamkia jana kwenye sehemu ya ukaguzi ya eneo la wasafiri wanaoondoka.
Alisema awali polisi walipata taarifa za kiintelijensia kuhusu Ohagwu na alipopekuliwa alikutwa na dawa alizodai kuwa ni heroin zilizofungwa katika pakiti sita za plastiki.
“Mtuhumiwa huyo alikuwa anasafiri kuelekea mji wa Lagos, Nigeria, akitumia Shirika la Ndege la Ethiopia,” alisema. “Dawa hizi alizificha kitaalamu kwa kushonea pakiti zote pembeni mwa mabegi yake mawili ya nguo ili asibainike haraka na vyombo vya dola.” Alisema polisi bado inamshikilia mtuhumiwa huyo na upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Pia, alisisitiza kuwa kwa sasa viwanja vya ndege si vichochoro vya kupitisha dawa hizo, kwa kuwa polisi ikishirikiana na wadau wengine, imejipanga kupambana na aina hiyo ya uhalifu.
“Mbali na kuwakamata hawa, pia tumelenga kuwakamata mapapa wanaoagiza dawa hizi, ” alisema Kamanda Ottieno. Desemba 17 mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alikutana na maofisa wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam na kutaka wamueleze mipango ya kukabiliana na dawa za kulevya.
MWANANCHI
Wakati watu mbalimbali wakimminia sifa Rais John Magufuli kwa kubana matumizi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga amesema uwingi wa makatibu wakuu unakinzana na dhana ya yake ya kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri.
Lakini naibu waziri huyo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne amesifu hatua mbalimbali za kupambana na ufisadi anazochukua Rais Magufuli akisema amefanikiwa kutumbua majibu, lakini sasa anatakiwa awe na ubunifu katika kutatua matatizo ya wananchi.
Dk Mahanga alikuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira tangu mwaka 2008 na hakuwahi kuhamishwa wala kupandishwa hadi ngazi ya uwaziri hadi Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilipomaliza muda wake na baadaye kujiunga na Chadema.
Akizungumza na Mwananchi jana, mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Segerea (CCM) alisifu kazi inayofanywa na Rais Magufuli akisema inaonekana wazi. “Kweli ametumbua majipu ambayo hakika yalikuwa yameiva,” alisema Dk Mahanga. “Naweza kusema alikuta nyumba chafu na inanuka, ameisafisha.
Sasa tunapenda kuona baada ya kusafisha ataiweka katika hali gani? Atabuni nini ili kuwasaidia vijana dhidi ya tatizo la ajira ili wengi waweze kumudu gharama za maisha.
” Lakini katika waraka wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Dk Mahanga alimkosoa Rais Magufuli akisema ameongeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri baada ya kuteua makatibu wakuu 27 wakati anawaaminisha wananchi kwamba wizara ni 15 tu.
Dk Magufuli ameunda baraza lenye mawaziri 15, na manaibu waziri 19 na hivyo kufanya baraza lake kuwa na jumla ya mawaziri 34, tofauti na baraza lililopita lililokuwa na mawaziri 55. Uamuzi wa kupunguza idadi ya wizara ulikumbana na changamoto ya nafasi za makatibu, ambao hata hivyo baadhi amewarudisha wizarani ambako watapangiwa kazi na kubakiwa na makatibu 27.
“Si kweli kwamba kapunguza ukubwa wa Serikali, bali kaongeza ukubwa wake. Sina hakika kama wasaidizi wa Rais wamemshauri na kumweleza kwamba wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu,” alisema Dk Mahanga akifafanua kuwa katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu wa wizara na afisa masuhuli.
Alisema katibu mkuu ndiye mwenye dhamana ya utendaji na ndiyo maana hata katika ngazi ya kata, ofisi inaitwa ofisi ya ofisa mtendaji wa kata na si ofisi ya diwani.
Kwa maana hiyo, Dk Mahanga, ambaye kitaaluma ni mhasibu, alisema Rais alipounda Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambazo awali zilikuwa mbili tofauti na kuteua makatibu wakuu watatu, kiuhalisia hakuunganisha wizara mbili kuwa moja bali ameunda wizara tatu kutoka mbili za awali. “Ongezeko la gharama kwa kuongeza waziri mmoja ni ndogo sana kulinganisha na kuongeza katibu mkuu mmoja.
Waziri anapoteuliwa tayari anakuwa ni mbunge mwenye mshahara wake wa ubunge na kinachoongezeka ni kama laki tano tu juu ya ule mshahara wa ubunge na gharama nyingine ndogo za gari, pia mishahara na gharama za katibu muhtasi, msaidizi na dereva,” alisema Dk Mahanga.
Alisema kwa ujumla ahadi ya Rais Magufuli aliyotoa kwenye kampeni kwamba ataunda Serikali ndogo, hakuitimiza badala yake ameongeza ukubwa wa Serikali.
Wakati wa kampeni na alipoapishwa, Rais Magufuli alisema ataunda baraza dogo la mawaziri, hiyo ilijenga shauku kwa wananchi kufahamu kiwango cha ukubwa au udogo wa baraza hilo ikilinganishwa na mabaraza yaliyoundwa na watangulizi wake, tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961. Dk Magufuli pia alitoa ahadi hiyo alipozindua Bunge Novemba mwaka jana mjini Dodoma.
MWANANCHI
Wingu zito linaendelea kutanda kwenye anga za siasa visiwani hapa baada ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kusema mchakato wa kupanga bajeti kwa ajili ya marudio ya uchaguzi umekamilika, huku CUF ikishangazwa na kupinga tamko hilo.
Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein na katibu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad wako kwenye mazungumzo ya kujadili kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais, wawakilishi na madiwani na hadi sasa hawajatoa tamko la maendeleo ya mazungumzo yao.
Lakini viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa taarifa za kuwataka wafuasi wao wajiandae kwa marudio ya uchaguzi, huku CUf ikisema inachosubiri ni kutangazwa kwa mshindi wa uchaguzi wa Rais na haiku tayari kurudia uchaguzi.
Kauli nyingine ya namna hiyo ilitolewa jana na juzi na Balozi Seif alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, akisema kwa kuwa matokeo ya uchaguzi yalifutwa basi ni wazi kuwa hakuna utaratibu ambao utakaofanyika wa kuyamaliza matokeo yaliobaki isipokuwa kurudia uchaguzi upya.
“Tuache kusikiliza maneno ya porojo bali nawaambia suala la kurudia uchaguzi lipo kama kawaida na kilichobaki sasa ni kusubiri amri ya Tume (ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)) kutangaza siku ya uchaguzi huo,” alisema Balozi. “Kwa upande wetu CCM tupo tayari kushiriki uchaguzi huo.
Hata kama CUF hawatashiriki, sisi hawatubabaishi.” Kwa upande wa mazungumzo yanayofanyika Ikulu kwa kuwashirikisha viongozi wa wakuu wa Serikali, Balozi alisema kuwa hajui nini kinaendelea hadi sasa, lakini akawataka wananchi wasubiri taarifa rasmi mazungumzo hayo yatakapomalizika.
“Kikubwa zaidi nilichokisikia mimi katika mazungumzo hayo ni suala la kudumisha amani na utulivu ila kwa upana zaidi tusubiri mazungumzo hayo yatakapomalizika taarifa itatolewa kwa wananchi wote,” alisema.
Lakini kwa mara nyingine, CUF walipinga vikali kauli hiyo wakisema hawako tayari kurudia uchaguzi. Kaimu mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF, Ismail Jussa alisema matamko hayo yanashangaza wakati bado mazungumzo yanaendelea.
Jussa alidai kuwa kuna timu imejifungia mahali inafanya hujuma na inampotosha Dk Shein. Kuhusu sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif alisema kutoshiriki kwa viongozi wa CUF hakutaathiri sherehe hizo.
Alisema kamati ya maadalizi ya sherehe na mapambo tayari imeshajipanga vya kutosha na kilichobaki ni ufanikishaji wa maadhimisho hayo ambayo shamrashamra zake zilitarajiwa kuanza jana.
Alisema madhimisho hayo yapo kama kawaida na mwaka huu wamepanga siku ya kwanza ya shamrashamra zake kuitumia kufanya usafi wa mazingira ya mji wa Zanzibar.
Alisema kuwa shamrashamra nyingine za maadhimisho hayo zitaendelea kama kawaida kwa kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo
Trump
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab kutoka Somalia limetoa kanda ya video ya propaganda ambapo wanamtaja mgombea urais wa Marekani Donald Trump.
Hii imejiri wiki kadha baada ya Trump, anayeongoza kinyang’anyiro cha kutafuta atakayepeperusha bendera ya chama cha Republican, kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.
Kundi la al-Shabab, ambalo lina uhusiano na mtandao wa Al-Qaeda, linaelekeza ujumbe kwa Wamarekani weusi, likiwahimiza kusilimu na kushiriki kwenye Jihad au vita vitakatifu.
Kundi hilo linasema kwenye video hiyo kwamba ubaguzi wa rangi, ukatili wa polisi na chuki dhidi ya Waislamu vimesheheni Marekani.
Wasimamizi wa kampeni ya Bw Trump hawajazungumza lolote kuhusu video hiyo.
Miaka ya hivi karibuni, Wasomali-Wamarekani kutoka Minnesota wameripotiwa kwenda Somalia kujiunga na al-Shabab.

02 January, 2016

Magufuli Awakuna Wananchi Wenye Ulemavu, wamshukuru kwa kutimiza ahadi ya kuwakumbuka katika uongozi wake

lianza na Dkt. Abdallah Possi, wakafuata Profesa James Epiphan Mdoe na Mhe. Amon Anastaz Mpanju na kusababisha mshangao wa furaha miongoni mwa wananchi wenye ulemavu kwa kile wanachokitaja kama kukumbukwa katika uongozi wa Serikali ya awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 
 
Rais alipomteua Dkt. Abdallah Possi kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na walemavu wengi walifurahi kuona Mtanzania wa kwanza mwenye ualbino anaingia katika Baraza la Mawaziri 
 
Furaha hiyo ilizidi alipowateua Mhe. Amon Anastaz Mpanju mlemavu wa kuona kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria na Profesa James James Epiphan Mdoe kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, ambaye ni mlemavu wa miguu.
 
 Mhe Mpanju, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na ambaye pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge la Katiba, alishangaza kila mtu wakati alipokula kiapo mbele ya Rais bila kusoma mahali kama ilivyo desturi. 
 
“Huyu bwana pamoja na ulemavu wake hakika ni mtu wa kazi” alisikika mmoja wa wageni waliohudhuria hafla ya kuapishwa Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu wakuu Ikulu siku ya Mwaka mpya. 
 
Akiwa amesindikizwa na mke wake, Mhe. Mpanju alipokea Biblia Takatifu na kuinyanyua juu na kuanza kula kiapo, ingawa mkewe alikuwa ameshika karatasi ya maandiko ya vitone ambayo ilikuwa aitumie. Hata Rais alitabasamu kwa hilo. 
 
Huko mitaani, ambako tukio hilo la kuapishwa Makatibu wakuu lilikuwa likirushwa ‘live’ na vituo kadhaa vya TV na Redio na mitandao, wengi walishikwa na butwaa, huku wakimsifia Rais Magufuli kwa kuwakumbuka watu wenye ulemavu. 
 
Waliendelea kufurahi walipomuona Profesa James James Epiphan Mdoe, ambaye ni msomi aliyebobea katika Kemia,  akisogea mbele kwa mikongojo miwili na kula kiapo cha kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini. 
 

 Dkt. Abdallah Possi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na walemavu - siku alipoapishwa rasmi Ikulu jijini Dar es salaam Desemba 13, 2015


 Profesa James James Epiphan Mdoe akila kiapo kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini mbele ya Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam jana January 1, 2016


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Amon Anastaz Mpanju akiongozwa na msaidizi wake kujiunga na viongozi wenzie ili kutia saini Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma  mbele ya Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam  jana January 1, 2016

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...