Serikali
imesema tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini linatokana na
uchakavu na kuzidiwa kwa vituo vya kupoza umeme na miundombinu ya
usafirishaji na usambazaji nishati hiyo.
Katika
kukabiliana na tatizo hilo Tanesco inachukua hatua za kujenga mifumo ya
njia kubwa za umeme wa msongo wa kilovoti 400 (Iringa-
Dodoma-Singida-Shinyanga), gridi ya Kaskazini Mashariki (Dar es Salaam,
Chalinze,Tanga –Arusha), ya Kaskazini Magharibi (Geita- Kagera –Katavi-
Kigoma- Rukwa na Mbeya) na Makambako- Songea wa kilovoti 220.
Kauli
hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk
Medard Kalemani wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu, Boniventure
Kiswaga (CCM).
Kiswaga alitaka kufahamu serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la kukatika katika kwa umeme.
Pia
mbunge huyo alitaka kufahamu, Je serikali itakamilisha lini kupeleka
umeme katika vijiji vya jimbo hilo ikizingatiwa mpaka sasa ni asilimia
20 tu ya vijiji ndiyo vina umeme.
Kalemani
akijibu swali hilo, alisema tatizo la kukatika kwa umeme linatokana na
uchakavu na kuzidiwa kwa miundombinu ya kupoza umeme pamoja na matukio
ya kulipuka kwa transfoma yanayosababishwa na radi hasa kipindi cha mvua
pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma unaofanywa na wananchi wasio
waaminifu.
Alisema
Tanesco inakamilisha upanuzi wa usambazaji wa umeme katika majiji
makubwa ya Arusha, Dar es Salaam, na Mwanza ambapo kazi hizo zitahusisha
ujenzi wa njia mpya za umeme na kupanua vituo vya kupoza umeme.
“Kukamilika
kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA mkoani Kilimanjaro kumeimarisha
upatikanaji wa umeme maeneo ya Mirerani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (KIA),” alisema Kalemani.
Pia
vituo vya kupoza umeme katika jiji la Dar es Salaam vya Gongo la Mboto,
Kipawa, Mbagala, na Kurasini vitaunganishwa kwa njia ya sakiti mzunguko
kutoka Ubungo na Kinyerezi kuanzia Machi mwaka huu.