Mjumbe maalum wa Marekani katika
eneo la maziwa makuu amezitaka pande husika nchini Burundi kuafikiana
ili kulinusuru taifa hilo ambalo linaelekea kuangamia na vita.
Thomas Perrielo alikuwa akizungumza na BBC baada ya wapiganaji kuvamia kambi moja ya kijeshi katika mji mkuu wa Bujumbura.
Amesema
kuwa Burundi inaelekea kuwa taifa lililofeli .Amesema kuwa Marekani
inaunga mkono vikosi vya kuleta amani kutoka mataifa jirani badala ya
wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.
Serikali imesema kuwa jeshi
limewauwa wapiganaji 12 ambao walivamia kambi hiyo.Milio ya risasi
pamoja na milipuko imekuwa ikisikika katika mji huo kwa saa kadhaa.
Wakati huohuo mashirika ya ndege ya Kenya Airways na RwandAir
yamesitisha safari zake za kuelekea mji mkuu wa Burundi, Bujumbura,
kufuatia makabiliano ya risasi mjini humo.
Kwa mujibu wa afisa
mkuu wa mawasiliano wa shirika la ndege la Kenya, KQ, Wanjiku Mugo,
safari hizo zimesitishwa kutokana na ukosefu wa wafanyakazi katika
uwanja wa ndege wa Bujumbura.
Serikali ya Burundi imesema uwanja
huo haujafungwa ila tu shughuli zimetatizika kwa sababu wafanyakazi
hawakuweza kufika katika uwanja huo, kutokana na makabiliano makali ya
risasi kati ya wapinzani wa serikali walioakuwa wamejaribu kuvamia kambi
kadhaa za kijeshi mjini humo.
Shirika la kimataifa ya Msalaba
mwekundu ICRC nalo kwenye Twitter limesema kuwa halikufanikiwa kuingia
katikati mwa mji mkuu Bujumbura kutokana na vizuizi vilivyowekwa na
maafisa wa jeshi ambao wanaendelea na msako dhidi ya watu wanaomiliki
silaha.
Ripoti zinasema kuwa watu wanane wameuawa kwenye makabiliano hayo huku wengine wengi nao wakiwa wamejeruhiwa.
Mitaa
ya Mutakula na Musaga ndiyo iliyoathirika zaidi huku wakaazi wa mitaa
hiyo wakirpoti milio ya risasi kuanzia saa kumi alfajiri.
Huku hayo yakijiri Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza ameongoza mkutano wa baraza lake la mawaziri

Msemaji wa rais Willy Nyamitwe amesema lengo la mkutano huo limekuwa kujadili bajeti ya serikali ya mwaka ujao.
Kuhusu
makabiliano ya asubuhi, Bw Nyamitwe amesema kuwa watu wenye silaha
walijaribu kuvamia kambi kadhaa za kijeshi, katika kile alichokitaja
kama jaribio la kutaka kuwaachilia huru wafungwa.
Nyamitwe amesema kuwa juhudi hizo zimezimwa na Jeshi na kuwa hali ya utulivu imeanza kurejea.
Machafuko
yalianza nchini Burundi Aprili mwaka huu, wakati rais Nkurunziza
alipotangaza kuwa atawania muhula wa tatu kinyume na mkataba wa Arusha
uliosainiwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Umoja wa Mataifa
umesema kuwa zaidi ya watu 200 wameuawa tangu machafuko hayo kuanza huku
maelfu ya wengine nao wakikimbia nchi jirani.