|
Jamal Malinzi, Rais wa TFF |
Kwanza nikutakie heri ya mwaka mpya 2016 wewe msomaji wa safu hii ya
kujuzana mambo mbalimbali yanayotokea katika michezo hasa soka. Mengi
yamepita katika mwaka 2015, tumshukuru Mungu kuiona 2016.
Bila kuchelewa leo mada yangu inahusu kauli ya Rais wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwamba, klabu zisiilaumu TFF endapo
watapata matatizo ya kutopata leseni kutoka Shirikisho la Soka Afrika
(Caf) kwa kutokidhi vigenzo vya kushiriki michuano yake.
Baadhi ya vitu ambavyo klabu inatakiwa kuwa navyo ili kupata leseni
hiyo ni kuwa na uwanja binafsi wa mazoezi na angalau kuwa na timu moja
ya vijana inayoeleweka.
Tunapozungumzia uwanja wa mazoezi ni ule ambao timu inaweza kufanya
mazoezi yake muda wowote bila kuingiliana na klabu nyingine na uwe upo
kisheria kabisa siyo ubabaishaji.
Malinzi siku chache zilizopita katika mkutano wake na waandishi wa
habari alisisitiza kwamba, TFF isilaumiwe endapo klabu yoyote
itaondolewa katika michuano inayosimamiwa na CAF kutokana na kutokidhi
vigezo vya kupata leseni.
Nionavyo ni kwamba, Malinzi anakimbia jukumu lake kwani klabu
zinazoshiriki michuano ya CAF kutoka Tanzania Bara ni mbili tu Yanga na
Azam FC. Yanga inashiriki Ligi ya Mabingwa na Azam itacheza Kombe la
Shirikisho.
Kwa nini Malinzi asizikomalie klabu kuhusu kutimiza masharti ya
kupata leseni mapema mpaka anapoibuka hivi sasa na kutoa onyo hilo? Kuna
kitu amekiona mbele na hivyo anaanza kujihami mapema asionekana mbaya.
Ukitazama kanuni za Ligi Kuu Bara, kuna sehemu ya klabu kupatiwa
leseni na ili upate leseni ni lazima uwe na vitu nilivyotaja hapo juu
yaani uwanja wa mazoezi na timu ya vijana inayoeleweka.
Sasa kwa nini TFF inaziruhusu timu kucheza ligi kuu huku zikiwa
hazijatimiza masharti ya leseni? Upuuzaji wa vigezo vya leseni ulianza
kwa TFF kwa kuziogopa timu vigogo hasa Simba na Yanga na kuziacha
ziendelee kucheza ligi bila ya kutimiza masharti hayo.
Naamini kama TFF ingekuwa makini na kuzikomalia Yanga na Simba
kutimiza masharti hayo ya kupata leseni leo hii Yanga ingekuwa
imetengeneza pale Kaunda na Simba ingekuwa tayari ipo Bunju.
Tatizo lililopo ni TFF kuruhusu mambo kufanyika kienyeji bila kufuata
kanuni zinasemaje, leo hii kuna michuano ya Kombe la Shirikisho (Kombe
la FA), hapo timu za Ligi Daraja la Pili, la Kwanza na Ligi Kuu
zinachuana kupata timu moja itakayocheza Kombe la Shirikisho Afrika
mwaka 2018, lakini bado hakuna kinachoeleweka kuhusu ishu ya leseni au
kukidhi mahitaji ya CAF.
Chukulia mfano, timu ya daraja la pili inachukua ubingwa na kupata
nafasi hiyo ya CAF, je, itakuaje linapokuja jambo la kukidhi mahitaji ya
CAF? TFF itatoa tena tamko la kutohusika endapo timu itazuiwa kushiriki
michuano hiyo.
Kwa kutoa kauli kwamba wasilaumiwe endapo klabu itaondolewa katika
michuano ya CAF ni sawa na kukimbia lawama, kwani kabla ya CAF ni TFF
iliyokuwa na mamlaka ya kuzizuia klabu hata kucheza ligi kuu kwa
kutokidhi mahitaji ya kupatiwa leseni.
Maofisa wa CAF siyo wanaokuja kuzikagua klabu, bali ni TFF yenye
wajibu huo hivyo kabla ya CAF kufikia uamuzi wowote TFF ilipaswa kuwa ya
kwanza kuzifungia klabu kutocheza ligi kuu kwa kutokidhi vigezo.
Lakini kutokana na soka letu kuendeshwa kisiasa zaidi, TFF inashindwa
kuthubutu kutoa adhabu kwa klabu za ligi kuu tena bila sababu ya msingi
na sasa wanaibuka na kauli za kujihami.
Malinzi na timu yake asikimbie majukmu yake kwani alipaswa kulitazama
mapema ili jambo na kuzipa onyo klabu na ikiwezekana kuzizuia kucheza
ligi hadi zitimize masharti hayo.
Kwa jinsi mambo yanavyoenda, adhabu ya CAF inaweza kutua Yanga kwani
Azam tayari ina viwanja vyake vya mazoezi hadi mechi ndiyo maana Malinzi
anaanza mapema kujivua ili asionekane mbaya.
Hapa Malinzi hawezi kuepuka lawama kwani aliacha mwenyewe timu
ikacheza hadi ligi kuu bila ya kukidhi mahitaji ya leseni na sasa anaona
CAF ipo makini ndiyo anataka kukwepa lawama.
Tuwe wakweli tu kwamba, klabu ikizuiwa kucheza mechi za CAF, itakayolaumiwa ni TFF na siyo mtu mwingine.