Kisu kikali cha Kamati Kuu ya CCM (CC) leo kitaondoka na vichwa 33
kati ya 38 vya walioomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho
kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Ndugu Philip Mangula.
Kikao hicho ni hatua ya pili baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati
ya Maadili kilichokutana jana usiku chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais
Kikwete huku kikitawaliwa na usiri mkubwa, kuhama ukumbi na kila dalili
za kubadili ratiba iliyopangwa awali ili kuvuruga mipango ya kambi za
wagombea.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kulikuwa na uwezekano wa
kubadili ratiba ili vikao vya Kamati ya Maadili na CC ama vifuatane au
vifanyike usiku ili kuyanyima makundi nafasi ya kujipanga.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Alipoulizwa jana kuhusu vikao hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Nape Nnauye alidai kuwa hata yeye hakuwa na uhakika wa lini na muda
gani hasa kikao cha Kamati ya Maadili kingefanyika.
Awali, vifaa vya ukaguzi wa wajumbe vilikuwa vimewekwa katika Makao
Makuu ya CCM, White House lakini baadaye jioni viliondolewa na hapakuwa
na taarifa zozote zilizotolewa.
Habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kikao hicho cha Maadili
kilitarajiwa kufanyika Ikulu ya Dodoma kuanzia saa nne usiku wa jana.
Haya yanajitokeza wakati macho na masikio ya Watanzania yakiwa hapa
Dodoma kusikiliza namna kazi ya kuchuja wagombea itakavyofanyika na
kujua ni watu gani 33 watakaoanza kulambwa na kisu cha CC, hasa kwa
majina makubwa yanayotazamwa na wengi, mara tu baada ya kujadiliwa na
Kamati ya Maadili.
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana.
Kazi za Kamati Kuu leo
Kikao cha CC kina majukumu matatu leo ambayo ni kufikiria na kutoa
mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), majina yasiyozidi matatu
ya walioona kuwania urais wa Zanzibar ambayo imeombwa na Rais wa sasa,
Dk Ali Mohamed Shein pekee, kufikiria na kutoa mapendekezo kwa NEC
majina yasiyozidi matano ya walioomba kuwania urais wa Muungano na
kuandaa mkutano wa NEC.
Vigezo vya maadili
Kulingana na kanuni za Uongozi na Maadili, toleo la 2012 kifungu cha
4(ii), kuhusu taratibu za kuomba uongozi, wanachama wanaogombea uongozi
ambao uteuzi wao hufanywa na vikao vya kitaifa, watachunguzwa kwanza
uadilifu wao na chombo cha maadili cha CCM kwa ushirikiano na vyanzo
vingine.
Kanuni hizo zinasema mwanachama wa CCM anapoomba uongozi katika ngazi
yoyote, itikadi na mwenendo wake vitachunguzwa kwanza na Kamati ya
Usalama na Maadili inayohusika, ndipo maombi hayo yaliyoambatanishwa na
mapendekezo ya kamati hiyo yatakapofikishwa mbele ya kikao chenye
madaraka ya kutoa uamuzi.
Ikiwa mwanachama hakupendekezwa kwa sababu ya kukiuka Katiba ya CCM,
Kanuni za CCM na sheria ya nchi, hatakuwa na haki ya kukata rufaa kwa
mtu yeyote au kikao chochote. Lakini ikiwa mwanachama atakataliwa
kugombea kwa sababu ya madhambi yake katika chama, basi ni wajibu wa
Kamati ya Usalama na Maadili kumjulisha makosa yaliyomnyima haki ya
kugombea, naye anaweza kukata rufaa kwa mujibu wa haki zake kikatiba.
Mtu yeyote anayetuhumiwa mbele ya Kamati ya Usalama na Maadili ya
ngazi yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana na maadili au nidhamu ya
chama atasomewa na kutakiwa kuzijibu tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa
kamati hiyo ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa maandishi, lakini
hataambiwa nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa kama
imekwishajulikana mapema kutokana na mijadala ya vikao, vyombo vya
sheria au vyombo vya habari.
Kanuni ya maadili inaendelea kusema kuwa uchambuzi wa tuhuma hizo
utafanywa kwa kutumia njia mbalimbali pamoja na mashahidi
watakaopatikana.
Uchunguzi utakapokamilika na endapo itadhihirika kwamba tuhuma zina
uzito, mtuhumiwa ataitwa mbele ya kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili
ya ngazi inayohusika, kama ni lazima, ili apate kuhojiwa ana kwa ana.
Pia, kanuni inasema Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika
itatoa mapendekezo yake kuhusu suala hilo kwenye kikao cha uamuzi
kinachohusika. Mtuhumiwa atapewa nakala ya uamuzi kwa maandishi.
Wagombea wanne kukosa CC
Katika kikao cha CC kinachofanyika leo, wajumbe wanne ambao ni
miongoni mwa majina 38 yatakayojadiliwa katika mchujo huo watalazimika
kukaa kando ili kukwepa mgongano wa masilahi.
Wajumbe hao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria na
Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal na
Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM katika Vyombo vya
Dola, Toleo la Pili – Februari, 2005, ukurasa wa 25, kifungu cha 21 (3);
wajumbe wa vikao vya uchujaji na uteuzi wa wagombea kwa ngazi
inayohusika hawaruhusiwi kuendelea na kazi ya uchujaji na uteuzi iwapo
wao ni wagombea katika ngazi hiyo.
Kanuni hiyo pia imetoa miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi wa
wagombea na wajumbe wote wanatakiwa na kanuni kuzingatia maadili na
nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi.
Kanuni hizo zinasema ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa maneno au
vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji mmoja dhidi
ya mwingine, kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na
eneo analoishi au anakotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
Pia, ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya
uongozi au mwanachama yeyote aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi au
uangalizi au uratibu wa kura za maoni, uchujaji na uteuzi, kufanya
vitendo vya ukiukwaji wa kanuni.
Kuhusu misaada, kifungu cha tano (a) kinasema ni marufuku kwa mgombea
yeyote mtarajiwa au wakala wake, kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana
dhahiri kuwa ni sehemu ya kampeni za kuwania nafasi anayoitafuta kabla
ya muda rasmi wa uongozi unaohusika haujamalizika.
Kanuni imetoa adhabu kwa watakaovunja miiko hiyo na kwa kiongozi
atakayethibitika kuivunja atavuliwa uongozi na kwa mwanachama anayeomba
kugombea nafasi yoyote atakayethibitika kuivunja hiyo hatateuliwa
kugombea nafasi anayowania.
Chanzo: Mwananchi