Hii leo SSC Lazio watacheza na klabu ya Juventus katika raundi ya
15 ya Serie A ya msimu wa huu wa 2015/16.Ni mchezo wenye maswali mengi
sana kwa kuangalia hali ya timu zote mbili kwa sasa.
Je,Lazio watafuta uteja wa kutoifunga Juventus katika Serie A kwa miaka 12?
Lazio hawafanyi vizuri katika Ligi ya Italia kwa msimu huu kwani
wanashika nafasi ya 10 katika Ligi wakiwa na pointi 19 katika michezo 14
waliyocheza mpaka sasa.
Kocha wa Lazio Stefano Pioli yupo katika wakati mgumu sana na
inawezekana kufungwa na Juventus hii leo ikawa mechi yake ya mwisho
kuiongoza Lazio msimu huu.
Juventus wanarudi katika mji wa Roma kwa mara ya pili kwani tayari
wamekwishacheza katika mji huo dhidi ya AS Roma na Juventus kufungwa
magoli 2-0 katika uwanja wa Olimpico.
Safari hii Juventus wataendaje katika mji wa Roma?
Mpaka sasa klabu ya Lazio imepoteza michezo saba ya Ligi kwa msimu
huu ambayo ni mingi tofauti na msimu uliopita ambapo timu hiyo ilipoteza
michezo 11 tu katika michezo 38 ya Ligi ya Italia.
Kukosekana kwa beki wake wa kati Stefan De Vrij kumeonekana kuwa
pengo kwa Lazio kwani mabeki wawili wa kati wa sasa Santiago Gentiletti
na Mauricio hawajaweza kutengeneza ushirikiano mzuri ’chemistry’ nzuri
baina yao na hivyo Lazio kuruhusu magoli 22 katika michezo 14 mpaka
sasa.
Ubora wa kiungo Lucas Biglia unaweza kuwa chachu ya Lazio kupata
matokeo hii leo kwani anaonekana anaweza kupambana na wachezaji wa
kariba ya Claudio Marchisio,Stefano Sturaro na Mario Lemina.
Biglia
ni mfungaji bora namba mbili kwa upande wa Lazio akiwa na magoli matatu
huku Felipe Anderson akishika nafasi ya kwanza kwa kufunga magoli
manne.
Lakini pia Biglia ndiye mchezaji aliyepiga pasi nyingi sahihi
‘complete pass’ kwa Lazio kutoka eneo moja la uwanja kwenda eneo lingine
la uwanja akiwa na asilimia 81.6 ya kupia pasi sahihi.
Silaha nyingine ya Lazio itakuwa kwa mshambuliaji raia wa Brazil
Felipe Anderson ambaye ameonekana kuwa muhimili kwa Lazio hasa katika
ushambuliaji.
Felipe Anderson ana magoli 4 mpaka sasa katika Serie A ingawa tatizo
lake kubwa ni kuwa hana muendelezo mzuri wa uchezaji wake na hii imekuwa
ikiwapa Lazio wakati mgumu sana kupata matokeo kutokana na ubutu wa
safu yao ya ushambuliaji.
Miloslav Klose hayupo katika fomu yake lakini pia nyota wengine wa
Lazio kama Eddy Onazi ,Stefano Mauri na Senad Lulic wataendelea
kukosekana hii leo kwa sababu ni majeruhi.
Jambo la kusikitisha kwa upande wa klabu ya Lazio ni kuwa klabu hiyo
imepata ushindi wa Serie A mara ya mwisho tarehe 25/10/2015 katika
mchezo dhidi ya Torino kwa ushindi wa magoli 3-0.
Baada ya hapo Lazio haijashinda mchezo wowote wa Ligi Kuu ya soka nchini Italia mpaka sasa.
Kwa upande wa Juventus hakuna shaka kuwa fomu ya Paulo Dybala mwenye
magoli 6 na asisti 3 imeifanya safu ya ushambuliaji ya Juve kuwa na
makali kwa siku za hivi karibuni.
Kwani Juventus imeshinda michezo minne iliyopita ya Ligi ya Italia ikifunga magoli 9 na kufungwa magoli 2 tu.
Hapo kabla kocha wa Juventus Allegri hakuonekana kumpa nafasi Dybala
huku akijitetea kuwa mchezaji huyo bado hajakomaa kuweza kuanza kikosi
cha kwanza.
Lakini
hali imekuwa tofauti kwani Dybala amekuwa msaada mkubwa kwa Juventus
kwa sasa na anamuweka benchi hata mshambuliaji bora wa Juventus kwa
msimu uliopita Alvaro Morata.
Kutokuwepo kwa Paul Pogba katika mchezo wa kesho kunaweza kumpa
nafasi kiungo Stefano Sturaro kucheza sambamba na Claudio Marchisio na
Mario Lemina.
Kiungo Sami Khedira hajasafiri na timu na badala yake kiungo wa timu
ya taifa ya Ghana Kwawdo Asamoah amejumuishwa katika kikosi
kilichosafiri kwenda kucheza na Lazio leo.
Msimu uliopita Juventus walipata ushindi wa magoli 3-0 mbele ya Lazio
katika uwanja wa Olimpico.Mara ya mwisho kwa Lazio kushinda mchezo wa
Ligi kuu ya Italia dhidi ya Juventus ilikuwa tarehe 6 Desemba mwaka 2003
waliposhinda kwa magoli 2-0.
Magoli ya Lazio ya wakati huo yalifungwa na Bernardo Corradi na Stefano Fiore.
Naamini mashabiki wa soka wana kila sababu ya kuutazama mchezo huu na
kujua kama Juventus imerudi katika makali yake au itakuwa ndio mwisho
wa kocha wa Lazio Stefano Pioli.