01 August, 2015

Zama za ujasiriamali zilizoufukia ujamaa (MAKALA)

Nyerere2
Na FRANCIS MAWERE
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliamua kuanzisha mfumo wa kiuchumi wa Ujamaa na Kujitegemea miaka michache baada ya Tanganyika kujipatia uhuru wake.
  Kwa kufanya hivyo alikuwa ameamua kufuata mawazo ya akina Adam Smith, David Ricardo, Milton Friedman, Fredrich Hayek, Ayn Rand Robert Owen, Pierre Leroux na Karl Marx kwa kuwataja kwa uchache; ambao wanatajwa kama waasisi na watetezi wa Ujamaa.
Hii ni kwamba aliamua kusimama kinyume na mawazo ya ubepari ya akina  Stuart Mill, Albert Einstein, George Bernard Shaw, Leo Tolstoy na Emma Goldman ambao katika anga za uchumi wanaheshimika kuwa waasisi na watetezi wa ubepari.
Mwalimu Nyerere alitumia muda, akili na nguvu nyingi sana kuwasilisha na kuwashawishi Watanzania kuupokea na kuukubali Ujamaa na Kujitegemea.
Mambo hayakwenda vizuri katika pande mbili. Mosi, kutokana na hali ya uchumi wa kidunia na nafasi ya Ujamaa kwa wakati huo duniani; utekelezaji wa sera za Kijamaa ulikuwa ni wa kutoa jasho mno. Pili, Watanzania wengi waliupokea Ujamaa na Kujitegemea kwa shingo upande na wale walioupokea kwa moyo mweupe inaonekana hawakumuelewa vizuri Mwalimu Nyerere.
 Upande wa kwanza ni nafasi ya Ujamaa duniani wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa anauleta Ujamaa uliokolezwa mapambo (Ujamaa na Kujitegemea) hapa Tanzania. Ukweli ni kwamba hadi kufika miaka ya 1950 tayari Ujamaa ulishakuwa kwenye hali mbaya ya kumalizikia kuanguka. Hii ina maana Mwalimu Nyerere alikuwa anajaribu “bahati” ya kuijenga Tanzania imara kiuchumi kwa kutumia mfumo wa uchumi ambao ulishakuwa katikati ya changamoto kali sana za kushindwa.

 Ushahidi wa kushindwa kwa Ujamaa katika miaka hiyo, tunaupata kutoka kwa mataifa ambayo tunaweza kuyaita waasisi na miamba wa Ujamaa duniani. Gazeti la Urusi liitwalo Pravda, Mei 1988 liliandika habari ya kitafiti kuhusu hali tete ya uchumi wa Umoja wa Nchi za Urusi (USSR) kutokana na kufuata sera za Ujamaa.
 Katika habari hiyo, Pravda ilithibitisha kuwa matarajio ya Wajamaa yanazidi kuyeyuka kutokana na matokeo mabaya kwenye uchumi. Kwa mfumo, ilielezwa kuwa kati ya sekta 170 zilizoainishwa kuboreshwa na Ujamaa wao hakukuwa hata na moja iliyofanikisha malengo walau kiasi cha kuridhisha. Gazeti hilo lilihitimisha kwa kusema kuwa mfumo wa Ujamaa ni sawa na machafuko yaliyokusudiwa.

 Si hivyo tu, bali nyuma kabisa hapo mwaka 1920 wakati wa utawala wa Lenins Bolsheviks kule Urusi, tayari wanauchumi wengi akiwamo mwanauchumi wa Kiaustralia, Ludwig von Mises, walieleza kwa kina kuwa Ujamaa ulishakuwa umeanguka.
 Kwenye machapisho yake mawili maarufu sana, Economic Calculation in the Socialist Commonwealth  na Socialism, An Economic and Sociological Analysis, Mises anasema kuwa kutokana na tabia, tamaduni, mazoea na asili ya mwanadamu; kufanikisha Ujamaa ni sawa na kutengeneza sanamu kisha kutaka uipe uhai.

 Tunafahamu kuwa vita kubwa ya wafuasi wa Ujamaa na wale wa ubepari chimbuko lake kubwa ni mgawanyo wa rasilimali zilizopo katikati ya wanajamii. Ubapari wenyewe unasifa ya kuruhusu watu binafsi kuendesha uchumi kwa watu binafsi kumiliki njia kuu za uzalishaji.
 Kwenye ubepari, serikali inatakiwa kubaki kama mwangalizi tu na inapaswa kuliacha soko kuamua. Wakati Ujamaa wenyewe unasisitiza kuwa njia kuu za uchumi ni lazima zimilikiwe kwa pamoja na serikali iwe na mamlaka kamili ya kuingilia chochote katika mwenendo wa kiuchumi.
 Hapa ndipo penye kasheshe kubwa. Wale wapinzani wa Ujamaa huwa wanaenda mbali na kumnanga Karl Marx na kusema kuwa hakuwa na sababu za kiuchumi kuasisi Ujamaa. Marx yeye aliona kuwa ubepari ulikuwa ukilinyonya tabaka la wafanyakazi hivyo alipofikiria Ujamaa alisema utakuwa ni mfumo ambao utamlipa kila mtu kwa kadiri ya anavyofanya kazi.

Pengine tuanzie hapa kuutazama Ujamaa wa Mwalimu Nyerere hasa tukiangalia ule upande wa pili wa namna ambavyo ulipokewa kwa shingo upande na namna ambavyo haukueleweka. Mwalimu Nyerere alipoibuka na mfumo wa Ujamaa aliuongezea viungo kwa kuuita “Ujamaa na Kujitegemea”, lengo lake lilikuwa ni kuona Tanzania kama taifa likisimama na kumudu mahitaji yake na ya watu wake pasipo kutegemea fadhila, kuombaomba ama misaada.

Yakafanyika mambo mengi lakini makubwa mawili ni kuanzishwa kwa Vijiji vya Ujamaa na kutaifishwa kwa mali binafsi kuwa za umma. Nia ilikuwa nzuri lakini matokeo ya hatua hizi mbili hayakuwa mazuri pengine kwa sababu wananchi hawakuuelewa vema huu Ujamaa na Kujitegemea.
Kutokana na hili, maelfu ya wananchi hasa wale waliohamishwa makazi, waliopoteza mifugo yao, waliotakiwa kuacha mashamba na mazao yao na kwenda kwenye vijiji vya ugenini waliuchukia Ujamaa na Kujitegemea katika hatua za awali kabisa. Hata ubinafsishaji wa mali binafsi zikiwamo hospitali, shule, viwanda, kampuni na mashirika ulileta kizaazaa kwa sababu wamiliki wake walikuwa na wafuasi wengi na kama hawakuridhika basi na wafuasi wao waliuchukia Ujamaa na Kujitegemea ungali unaanza.

Pamoja na hilo inaonekana wananchi walioupokea Ujamaa na Kujitegemea walielewa kipengele kimoja tu cha Ujamaa lakini hiki cha Kujitegemea inaonekana hakikueleweka kabisa. Ili useme taifa linajitegemea ina maana kuwa wananchi wanajitegemea. Kwenye Ujamaa na Kujitegemea serikali ilihodhi njia kuu za uchumi na miundombinu ya kijamii, huku wananchi wakibaki kufanya kazi “kijamaa”.
 Suala hili lilisababisha wananchi wengi kama si wote kuitegemea serikali kwa mambo mengi ikiwamo upatikanaji wa elimu, huduma za afya, miundombinu na mengineyo. Serikali iliendelea kufurukuta kuwapa wananchi bure huduma za kijamii hadi ikafika mahali ikajikuta haina ujanja tena. Ndipo pale mahali Mwalimu Nyerere alipoamua kung’atuka na ghafla bin vuu nchi ikawa haina ujanja zaidi ya kujisalimisha kwenye makucha ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika na Fedha (IMF).
 Ilikuwaje Taifa la Ujamaa na Kujitegemea likashindwa kujitegemea? Jibu ni rahisi. Ni kwa sababu wananchi wake katika ngazi ya mtu mmoja mmoja walikuwa hawajitegemei. Badala yake walikuwa wakiitegemea Serikali kwa kila kitu. Jambo hili halikutokea kwa bahati mbaya na wala halikutokana na ubovu wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, isipokuwa una chimbuko lake kutoka katika saikolojia na tabia za kibinadamu kama alivyosema mwanauchumi Mises.

Kosa kubwa lililofanyika katika mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea ilikuwa ni kutafuta usawa wa kijamii na kiuchumi kwa watu wote. Kiasili kila mwanadamu ameumbwa tofauti na kupewa upeo, vipawa, karama, uwezo, matarajio na maono yanayotofautiana. Tena kiasili mwanadamu hutafuta kuwa tofauti, kufanya lile alipendalo na kutambuliwa na kujulikana kwa yale ayafanyayo.
Hapa kwenye karama, maono, vipawa ndipo mahali ambapo humuwezesha mwanadamu kusoma mazingira yake, kuangalia matatizo yaliyopo na kuyatafutia ufumbuzi kwa kutumia karama, vipawa, maono na uwezo wake. Namna hii ya utatuzi wa matatizo na changamoto ndiyo msingi na chimbuko la ujasiriamali (Intrinsic Entrepreneurship).

 Mchumi na mwanasaikolojia wa kale, John Stuart Mill, katika kitabu chake cha Principles of Political Economy (1848) anasema, “Ukimlazimisha mwanadamu awe sawa na wengine, afanye kila kitu kwa kuamuliwa na mamlaka, basi atakuwa na hulka zifuatazo: Atakuwa mtu anayefanya mambo nusunusu (passive), hatafanya mambo makubwa zaidi ya yale wanayofanya wenzake hata kama ana uwezo na kubwa kabisa hataona umaana wa kujipambanua katika kazi kwa sababu iwe atafanya sana ama atafanya kidogo, maslahi anapata yale yale.”
Hapa ndipo mahali Ujamaa na Kujitegemea ulipoua vipawa vingi vya kijasiriamali. Wafanyakazi hawakuona umuhimu wa kufanya zaidi, wananchi hawakuwa na sababu ya kufanya zaidi kwa sababu Serikali ilitoa kila kitu na vile vile ilikuwa na utaratibu unaobana unapotaka kufanya biashara. Mathalani, ule mtindo wa kumbana mtu na kutaka ajieleze namna alivyofanikiwa hata akajenga nyumba ama kununua kitu cha thamani ulizalisha woga miongoni mwa Watanzania wengi.
 Kivuli cha woga ule kinatutafuna hadi sasa, ndiyo maana nchi hii mtu anapofanikiwa kiuchumi watu hawamuamini, wanamtilia shaka; eidha watasema ni fisadi ama ni mshirikina ama ni mwizi. Ujamaa na Kujitegemea ingawa haukuandika katika maandishi ya sera zake, lakini ulihesabu mtu kuwa na utajiri kama “dhambi na unyonyaji”.

 Kule Magharibi walianza kutumia msamiati wa ujasiriamali miaka ya 1700! Sisi Tanzania msamiati huu ndiyo kwanza unavuma miaka hii ya 2000. Dhana ya ujasiriamali iliasisiwa na ubepari. Tulipokuwa tunacheza ngoma ya Ujamaa na Kujitegemea tuliuita ubepari ni unyama. Kwa lugha nyepesi ni kuwa Ujamaa na Kujitegemea ulipenyeza imani vichwani mwa Watanzania; ya kuamini kuwa “ujasiriamali ni unyama”.
 Hili tunaweza kulithibitisha kwa kutazama kile ambacho Watanzania tunafahamu kuhusu ujasiriamali. Wengi wa Watanzania bado wanashangaa-shangaa, wanasikiasikia tu lakini wanahisi kuwa ujasiriamali si kitu kinachowahusu. Jirani zetu Wakenya ambao wamekuwa wabepari nyakati zote; hadi watoto wa shule za msingi wananunua hisa katika soko lao la hisa Nairobi. Sisi hapa Tanzania wasomi wetu wanahitimu vyuo vikuu hawajui hata ABC hisa achilia mbali uwezo wa kutumia maarifa waliyopata kujiajiri.

 Nihitimishe kwa kusema kuwa kushindwa kwa Ujamaa na Kujitegemea hakuwezi kuhesabiwa moja kwa moja kama ni kushindwa kwa Mwalimu Nyerere; kwa sababu Ujamaa ulishakuwa umeshindwa kabla hata Mwalimu Nyerere hajabuni Ujamaa na Kujitegemea.
Wachumi wanatuthibitishia kuwa miundombinu ya Ujamaa ndiyo chimbuko la kuanguka kwake. Na moja ya sababu za kudondoka kwa viwanda na mashirika mengi ya umma ilikuwa ni kushindwa kuzalisha kwa kuangalia mahitaji na matakwa ya watumiaji (soko).
Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi tunapoendelea kumuenzi Mwalimu

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...