07 July, 2015

Jina la mchezaji David Beckham, pengine ndio maarufu zaidi katika sio tu soka bali michezo kwa ujumla

beckmam
Jina la mchezaji David Beckham, pengine ndio maarufu zaidi katika sio tu soka bali michezo kwa ujumla. Becham ambaye hajawahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya wala dunia, lakini ndiye mchezaji ambaye amekua tajiri na maarufu zaidi kushinda hao waliwahi kushinda tuzo hizo. Na hilo linaitimiliza kauli isemayo ’mpira ni zaidi ya kuucheza’. David Robert Joseph Beckham alizaliwa mei2, 1975 huko Leytonstone, London. Beckham ni mtoto wa msusi wa nywele bi Sandra Georgina na bwana David Edward Alan Beckham. Wazazi wake Beckham walikua ni mashabiki wa kutupwa wa mashetani wekundu, Manchester United. Huku wakiwa wanaishi London walikua mara kwa mara wakisafiri hadi Old Trafford kuishuhudia Manchester United ikicheza. Maji hufuata mkondo, Beckham naye akarithi upenzi huo wa Manchester kwa wazazi wake.
MAISHA YAKE YA SOKA
Manchester United;
Alijiunga Manchester United baada ya kufanya vizuri katika majaribio kwenye mazoezi ya timu hiyo julai8, 1991 na kuwa sehemu ya vijana wenzake akina Paul Scholes, Ryan Giggs na Gary Neville chini ya kocha Eric Harrison na kuisaidia klabu kushinda kombe la vijana la chama cha soka cha England, FA mnamo mei 1992. Alifanya vizuri katika timu ya vijana hadi kupelekea kuingizwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo septemba 1992, huku akisajiliwa kama mchezaji wa kulipwa mwaka 1993. Alipelekwa kwa mkopo Preston North End msimu wa 1994/95 ili akapate uzoefu wa kucheza kikosi cha kwanza. Akiwa Preston alifunga mara mbili katika michezo mitano aliyocheza, huku akifunga moja kwa moja kwa mpira wa kona. Mwisho wa msimu alirudi tena Manchester na juhudi zake uwanjani zilimfanya awe moja kati ya figa muhimu katika kikosi cha Sir Alex Ferguson akicheza kama kiungo wa kulia. Alifanikiwa kucheza kwa mafanikio zaidi huku akiwa na wenzake akina Nick Butt, Neville brothers, Ryan Giggs, Paul Scholes walishinda kikombe cha ligi pamoja na Fa Cup mara mbili na kufanikiwa kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kwenye michuano ya Euro 1996.

“Ilibadilisha maisha yangu, mpira ulionekana kama unaenda juu, lakini ukatulia na ukazama nyavuni. Nilijihisi niko juu mawinguni, na kutamani kumshika mkono kila mtu pale uwanjani” Becham akielezea goli lake mwaka huo huo wa 1996 alilolifunga dhidi ya Wimbledon nyuma ya mstari wa katikati, goli lililofanya awe Beckham huyu kila mtu anamjua.  Msimu wa 1996/97 David alikabidhiwa jezi namba 10 aliyokuwa akiivaa Mark Hughes lakini baadae mwaka 1997 Eric Cantona alistafu soka na kuiacha jezi maarufu Old Trafford, jezi namba7 na kumfanya Beckham amuachie jezi namba 10 Teddy Sheringham  aliyesajiliwa kutokea Tottenham Hotspurs na kisha yeye kuvaa namba 7.
Msimu wa 1998/99 Beckham alikua miongoni mwa wachezaji muhimu walioshinda mataji matatu ‘treble’ baada ya kushinda Fa cup, ligi kuu na klabu bingwa ulaya. Katika fainali ya Uefa dhidi ya Bayern Munich Beckham alicheza kama kiungo wa kati baada ya nahodha Roy Keane na Paul Scholes kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano. Katika usiku usiosahaulika mjini Barcellona katika dimba la Camp Nou, ikiwa imefungwa goli moja kwa bila hadi dakika ya tisini, kona mbili zilizopigwa na kijana huyo baba wa watoto wanne hadi sasa ndio zilizaa mabao kupitia kwa Teddy Sherigham na Ole gunna Solkjear.  Huku akiwa nyuma ya Rivaldo katika tuzo ya mchezaji bora wa dunia na Ulaya msimu huo wa 1999.
Agombana na kocha Ferguson
Kuanzia miaka ya 2000 uhusiano kati ya Beckham na kocha wake Sir Alex Ferguson ulianza kupungua. Hilo lilitokana na Beckham kuchagua umaarufu zaidi ya mpira amekaririwa Sir Alex akiyasema hayo katika kitabu chake cha hivi karibuni. Kwani mwaka huo wa 2000 Beckham aliruhusiwa kutofanya mazoezi ili akamuone mwanae Brooklyn aliyekua anaumwa, lakini Ferguson alikasirika baada ya kuona picha za Victoria Beckham ‘Posh’ mke wake Beckham akifanya manunuzi ‘shopping’ usiku huo huo Beckham alioruhusiwa. Fergie alimkata mshahara wa wiki mbili Beckham kama faini kwa madai kua Posh angeweza kuwa na mtoto na yeye kuzingatia mazoezi. “hakua ni tatizo, ila hadi alipofunga ndoa. Alikua akifanya mazoezi kwa bidii na makocha wa academy hapa. Alikua ni kijana mzuri sana. Kuoa kulikua ni kitu kigumu sana kuanzia wakati huo. Hakua Beckham tuliye mfahamu. Alikua ni staa mkubwa, na kufanya mpira sehemu ndogo ya maisha yake” Ferguson akizungumzia ugomvi wake na Beckham mwaka 2007. Pamoja na kufanya vizuri uwanjani na kuipa mafanikio timu yake lakin hali bado ilikua tete kati yake na kocha Ferguson. Uhusiano wao ulipotea kabisa mapema mwaka 2003 katika chumba cha kubadilishia nguo baada ya kufungwa goli mbili na Arsenal katika mchezo wa FA cup na kusababisha Ferguson ampige na kiatu chake katika paji la uso kwa hasira na kumuumiza vibaya jichoni. Hali hiyo ilipelekea kuondoka kwa Beckham na kuuzwa Real Madrid.
Atua Real Madrid, Hispania
“Ni mchezaji mkubwa ambaye ataingia katika historia ya klabu na kufanya vizuri. Ni mchezaji mwenye njaa ya mafanikio na kipaji cha ajabu, ni moja kati ya wachezaji bora kabisa wa kiingereza wa muda wote.” Alikaririwa raisi wa Real Madrid Florentino Perez katika utambulisho wa Beckham. Julai1 mwaka 2003 Beckham akatua Madrid kwa uhamisho wa dola za kimarekani 35m. kutokana na nahodha Raul kuvaa jezi namba7, Beckham alichagua jezi namba 23 akionesha kumkubali mkongwe wa mpira wa kikapu Michael Jordan. Akiwa sambamba na nyota kibao wakati huo kama Zinedine Zidane, Raul, Iker Casilus, Carlos, Figo na wengine walitwaa vikombe muhimu kama Spanish super Cup  dhidi ya Mallorca mwishoni mwa 2003 kwa ushindi wa 3-0 Beckham akifunga goli la tatu. Akiwa Hispania Beckham alioneshwa kadi nyekundu mara3 kwa kipindi cha miaka4. Real Madrid hawakufanikiwa kufanya vizuri katika michuano ya klabu bingwa Ulaya kwani mara nyingi walitolewa hatua ya robo fainali. Beckham alifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Hispania katika msimu wake wa mwisho na Real Madrid, 2007 chini ya kocha Fabio Capello. Kutokana na kuwekwa benchi muda mwingi na muitaliano Fabio Capello, Beckham alijiunga na ligi kuu ya soka ya Marekani. Mwezi mmoja baada ya Beckham kumaliza maisha yake ya soka na Madrid, gazeti la Fobres liliripoti kwamba Beckham alikua ni mchango mkubwa sana kibiashara Real Madrid kwa kuisaidia kuongeza mapato hadi kufikia dola 600m kwa kipindi cha miaka minne aliyokaa na Madrid.
LA Galaxy, Marekani
“siji huko kuwa supa staa, siji huko kuigiza filamu, nakuja huko kuwa sehemu ya timu, kufanya kazi kwa bidii na ikiwezekana kushinda mataji. Kwangu mimi soka ndio kipau mbele. Nakuja kuonesha tofauti, nakuja kucheza mpira. Sisemi ujio wangu huko utafanya soka kuwa mchezo maarufu zaidi huko, ni kitu kigumu. Kikapu na michezo mingine ipo huko kwa muda sasa.” Maneno ya Beckham katika safari yake ya kwenda Marekani. Taarifa za kujiunga na LA Galaxy zilianza tangu akiwa na Real Madrid, January 2007. Utambulisho wa Beckham Marekani ulikuwa ni wa kihistoria baada ya kutikisa vyombo vyote vya habari duniani. Mkataba wa Beckham LA Galaxy uliineemesha LA Galaxy kwa kuingiza pesa nyingi kutokana na makampuni kibao kufanya nayo biashara kutokana na uwepo wa Beckham. Mkewe Victoria, Posh alinunua nyumba ya gharama ya thamani ya dola 18.2m ili aishi na familia yake. Beckham akasaini mkataba mnono wa miaka 5 wenye thamani ya us$32.5m sambamba na mikataba yake binafsi iliyokuwa inamuingizia pesa kote duniani. Akiwa nchini Marekani alichezea kwa mkopo mara mbili Ac Milan katika miezi ambayo ligi ilikua imesimama. Na hatimaye akaisaidia LA Galaxy kumaliza katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu ya Marekani, MLS. Katika msimu wake wa mwisho na LA Galaxy aliisaidia kushinda taji la ligi, MLS Cup huku akifanyiwa mabadiliko katika dakika ya 89 kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Houston na kushinda 3-1 huku akitokwa machozi baada ya uwanja mzima kusimama na kumshangilia. Mwaka huo huo 2012 yeye na timu yake ya LA Galaxy walialikwa ikulu ya White house na rais Barack Obama.
Paris Saint Germain na kustaafu soka
January 31, 2013 mwisho wa siku ya usajili Beckham aliripotiwa kufanya vipimo vya afya na kujiunga na Paris Saint Germain ya Ufaransa kwa mkataba wa miezi mitano huku akikataa kuchukua mshahara wake hata kidogo na kuchangia katika mfuko wa watoto yatima na wasiojiweza. Alicheza mechi yake ya kwanza na Paris dhidi ya Olympique Marseille akiingia kutokea benchi dakika ya 76 ya mchezo. Alifanikiwa kucheza michezo mingi na timu yake hiyo chini ya kocha Carlo Ancelloti dhidi ya Barcellona katika michuano ya klabu bingwa ulaya. Hatimaye akawa muingereza wa kwanza kushinda vikombe katika ligi nne tofauti baada ya mei12, 2013 kushinda taji la ligi kuu ya Ufaransa katika ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Lyon. Akatangaza kustaafu soka meiu 16, 2013 na PSG wakamtengenezea viatu vya aina yake avae katika mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Brest. Alivaa kitambaa cha unahodha katika ushindi wa 3-1 na kufanyiwa mabadiliko dakika ya 80 ya mchezo na kuagwa na mashabiki wote uwanjani huku akibubujikwa na machozi kwa hisia.
Anunua timu, Miami nchini Marekani
Tarehe 5 February 2014, ligi kuu soka Marekani ilitangaza kwamba David Beckham amenunua timu kwa dau la dola 25m za marekani ikiwa ni sehemu ya mkataba aliosaini akiwa na LA Galaxy 2007. Timu hiyo itakua mjini Miami na itaanza 2016 au 2017 kutokana nan kukamilika kwa ujenzi wa uwanja.
Umaarufu wa Beckham
Umaarufu wa Beckham nje ya uwanja ulikuwa kama moto wa shamba. Mikataba mikubwa na Coca_Cola company na IBM ndiyo sababu nyingine kubwa ya umarufu wake na utajiri. Ndoa yake na Victoria mwanamitindo mwenye pesa nyingi pia kumekua ni sababu ya yeye kuwa imara kiuchumi na umaarufu. Beckham amekua katika mitindo kwa uda huku akifanya matangazo lukuki. Beckham amekua akihusudiwa sio tu nchini China ambako watu walimtengenezea sanamu, bali dunianin kote.

Usisumbuke Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO, SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>mawere_mtoka_mbali,

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...