Beki wa kulia wa Barcelona Dani Alves, ametanabaisha kuwa Lionel Messi ni bora zaidi ya Cristiano Ronaldo kwa sababu ya hamasa yake kubwa katika timu. Alves amesema hayo kutokana na mjadala mkubwa uliopo ulimwenguni kwa sasa kuwa nani kati ya wawili hao ni bora zaidi ya mwenzake.
Hata hivyo, Alves amesema kuwa Messi ana ushawishi mkubwa hasa katika kuichezesha timu kuliko ambavyo Ronaldo hufanya akiwa Real Madrid, huku akidai kuwa Mreno huyo huwa hafanyi chochote kingine uwanjani zaidi ya kufunga magoli tu. “Messi ni bora zaidi ya Cristiano Ronaldo,” aliliambia Bola da Vez. “Messi ana ushawishi mkubwa uwanjani kitu ambacho Cristiano hana. Hebu angalia kama utaona ana kitu kingine zaidi ya kufunga na kujitokeza katika baadhi ya matukio tu”.
“Messi ana hamasa kubwa, anafunga na kutoa pasi za magoli. Messi ni kipaji kutoka kwa Mungu. Christiano anafanya mazoezi mno. Tuna mapambano yetu binafsi lakini mimi huwa namkubali sana. Ni mtu ambaye hujitolea lakini anayependa ushindani pia”.
“Ronaldo ana vitu ambavyo binafsi sivikubali kwa sababu mimi napenda kucheza kitimu. Nadhani timu ni muhimu zaidi yangu. Nadhani kwa kiasi kidogo sana yeye huweka timu mbele, baadhi ya watu walitukosoa sisi kusherehekea ubingwa wetu wakati Ronaldo alikuwa akishagilia kuwa mfungaji bora”, alimaliza Alves.
No comments:
Post a Comment