Mjumbe maalum wa Marekani katika
eneo la maziwa makuu amezitaka pande husika nchini Burundi kuafikiana
ili kulinusuru taifa hilo ambalo linaelekea kuangamia na vita.
Thomas Perrielo alikuwa akizungumza na BBC baada ya wapiganaji kuvamia kambi moja ya kijeshi katika mji mkuu wa Bujumbura.Amesema kuwa Burundi inaelekea kuwa taifa lililofeli .Amesema kuwa Marekani inaunga mkono vikosi vya kuleta amani kutoka mataifa jirani badala ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.
Serikali imesema kuwa jeshi limewauwa wapiganaji 12 ambao walivamia kambi hiyo.Milio ya risasi pamoja na milipuko imekuwa ikisikika katika mji huo kwa saa kadhaa.
Wakati huohuo mashirika ya ndege ya Kenya Airways na RwandAir yamesitisha safari zake za kuelekea mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, kufuatia makabiliano ya risasi mjini humo.
Kwa mujibu wa afisa mkuu wa mawasiliano wa shirika la ndege la Kenya, KQ, Wanjiku Mugo, safari hizo zimesitishwa kutokana na ukosefu wa wafanyakazi katika uwanja wa ndege wa Bujumbura.
Serikali ya Burundi imesema uwanja huo haujafungwa ila tu shughuli zimetatizika kwa sababu wafanyakazi hawakuweza kufika katika uwanja huo, kutokana na makabiliano makali ya risasi kati ya wapinzani wa serikali walioakuwa wamejaribu kuvamia kambi kadhaa za kijeshi mjini humo.
Shirika la kimataifa ya Msalaba mwekundu ICRC nalo kwenye Twitter limesema kuwa halikufanikiwa kuingia katikati mwa mji mkuu Bujumbura kutokana na vizuizi vilivyowekwa na maafisa wa jeshi ambao wanaendelea na msako dhidi ya watu wanaomiliki silaha.
Ripoti zinasema kuwa watu wanane wameuawa kwenye makabiliano hayo huku wengine wengi nao wakiwa wamejeruhiwa.
Mitaa ya Mutakula na Musaga ndiyo iliyoathirika zaidi huku wakaazi wa mitaa hiyo wakirpoti milio ya risasi kuanzia saa kumi alfajiri.
Huku hayo yakijiri Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza ameongoza mkutano wa baraza lake la mawaziriMsemaji wa rais Willy Nyamitwe amesema lengo la mkutano huo limekuwa kujadili bajeti ya serikali ya mwaka ujao.
Kuhusu makabiliano ya asubuhi, Bw Nyamitwe amesema kuwa watu wenye silaha walijaribu kuvamia kambi kadhaa za kijeshi, katika kile alichokitaja kama jaribio la kutaka kuwaachilia huru wafungwa.
Nyamitwe amesema kuwa juhudi hizo zimezimwa na Jeshi na kuwa hali ya utulivu imeanza kurejea.
Machafuko yalianza nchini Burundi Aprili mwaka huu, wakati rais Nkurunziza alipotangaza kuwa atawania muhula wa tatu kinyume na mkataba wa Arusha uliosainiwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa zaidi ya watu 200 wameuawa tangu machafuko hayo kuanza huku maelfu ya wengine nao wakikimbia nchi jirani.
No comments:
Post a Comment