25 December, 2015

Mwalimu jela kwa ‘kufuga’ wanafunzi watoro

post-feature-imageMahakama ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imemhukumu mwalimu wa Shule ya Msingi Nonwe, Raphael Matima kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh600,000 ili afiche wanafunzi watoro.


Hakimu Mkazi Mfawidhi, Robert Oguda alitoa hukumu hiyo jana baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewana upande wa mashtaka.
Alisema mshtakiwa huyo aliomba fedha hizo kwa wazazi wa wanafunzi watatu wa shule hiyo iliyopo katika Halmashauri ya Ushetu.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Kahama, Kelvin Murusulu alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha Sheria ya Elimu.
Murusulu alimuomba hakimu wa mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo kwa kuwa kuomba na kupokea rushwa kwa wazazi wa watoto hao ni kosa na anadidimiza elimu. Alidai licha ya taasisi yake kuweka mtego wa kumkamata, mshtakiwa huyo anapaswa kutumikia kifungo kikubwa.
Hakimu Oguda alimhukumu kifungo hicho cha miaka mitano ili iwe fundisho kwa walimu wengine wenye tabia kama hiyo.

Wakati huohuo, Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Ushetu, Focus Kahendaguza amekutwa na kesi ya kujibu kwenye tuhuma zinazomkabili za kutumia madaraka vibaya ikiwamo kugushi nyaraka na kujipatia fedha zaidi ya Sh4,000,000 kinyume cha sheria.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo na Takukuru wilayani Kahama. Murusulu alidai kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka vibaya akiwa mtumishi halali ya Serikali na kujipatia kesi hicho cha fedha.
Madai mengine yanayomkabili ni pamoja na kutosambaza viti kwa watendaji wa vijiji wakati huo ikiwa halmashauri ya wilaya ya Kahama kabla ya kugawanywa . Hakimu Oguda aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 19, mwakani mshtakiwa huyo atakapoanza kuwasilisha utetezi wake.
-Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...