Rais
alipomteua Dkt. Abdallah Possi kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu -
Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na walemavu wengi walifurahi kuona
Mtanzania wa kwanza mwenye ualbino anaingia katika Baraza la Mawaziri
Furaha
hiyo ilizidi alipowateua Mhe. Amon Anastaz Mpanju mlemavu wa kuona kuwa
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria na Profesa James James
Epiphan Mdoe kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, ambaye
ni mlemavu wa miguu.
Mhe
Mpanju, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na ambaye pia alikuwa mmoja wa
wajumbe wa Bunge la Katiba, alishangaza kila mtu wakati alipokula kiapo
mbele ya Rais bila kusoma mahali kama ilivyo desturi.
“Huyu bwana pamoja na ulemavu wake hakika ni mtu wa kazi” alisikika mmoja wa wageni waliohudhuria hafla ya kuapishwa Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu wakuu Ikulu siku ya Mwaka mpya.
Akiwa
amesindikizwa na mke wake, Mhe. Mpanju alipokea Biblia Takatifu na
kuinyanyua juu na kuanza kula kiapo, ingawa mkewe alikuwa ameshika
karatasi ya maandiko ya vitone ambayo ilikuwa aitumie. Hata Rais
alitabasamu kwa hilo.
Huko
mitaani, ambako tukio hilo la kuapishwa Makatibu wakuu lilikuwa
likirushwa ‘live’ na vituo kadhaa vya TV na Redio na mitandao, wengi
walishikwa na butwaa, huku wakimsifia Rais Magufuli kwa kuwakumbuka watu
wenye ulemavu.
Waliendelea
kufurahi walipomuona Profesa James James Epiphan Mdoe, ambaye ni msomi
aliyebobea katika Kemia, akisogea mbele kwa mikongojo miwili na kula
kiapo cha kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini.
Dkt. Abdallah Possi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na walemavu - siku alipoapishwa rasmi Ikulu jijini Dar es salaam Desemba 13, 2015
Profesa
James James Epiphan Mdoe akila kiapo kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini mbele ya Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli Ikulu
jijini Dar es salaam jana January 1, 2016
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Amon Anastaz Mpanju
akiongozwa na msaidizi wake kujiunga na viongozi wenzie ili kutia saini
Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma mbele ya Rais Dkt John Pombe
Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam jana January 1, 2016
No comments:
Post a Comment