04 January, 2016

Waziri Mbarawa Atoa Siku Tatu Ukarabati Reli Ya Kati Iliyosombwa na Mafuriko


Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka watendaji wa Shirika la Reli nchini (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (RAHCO) kuhakikisha sehemu ya reli iliyosombwa na mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro inaunganishwa ndani ya siku tatu na huduma za treni kurejea. 
 
Prof. Mbarawa amesema hayo baada ya kukagua sehemu ya reli hiyo kutoka Kilosa hadi Magulu- Kidete kuona athari zilizosababishwa na mafuriko yaliotokana na mvua zilizonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma. 
 
“ Fanyeni kazi usiku na mchana ili ikifika alhamisi mawasiliano ya reli kati ya mkoa wa Morogoro na Dodoma yawe yamerejea na abiria waendelee kupata huduma ya treni ,” amesema Waziri Prof. Mbarawa. 
 
Amewahakikishia wananchi wa vijiji vya Munisagara, Mkadage, Mzaganza, Magulu na Kidete ambao usafiri wao pekee wa uhakiki ni wa kutumia reli watoe ushirikiano kwa serikali ili ukarabati na ujenzi wa reli hiyo ukamilike kwa haraka. 
 
Amewataka wananchi waishio pembezoni mwa reli katika wilaya ya Kilosa kupanda miti ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaosababisha mafuriko kwa urahisi wakati wa mvua na kubomoa reli kila wakati.
 
“Pandeni miti, lindeni miundombinu ya reli na acheni vitendo vya uharibifu wa mazingira ili ujenzi wa mwaka huu uwe wa kudumu na reli isiathiriwe kirahisi na kuwasababishia kero wananchi,” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa. 
 
Naye Diwani wa kata ya Kidete Bw. Mohamed Seleman Mbunda amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wananchi wake watashirikiana na serikali kulinda mazingira ili kudhibiti mafuriko yanayoharibu miundombinu ya reli kila wakati wilayani humo. 
 
Mafuriko wilayani Kilosa ni matokeo ya mvua zinazonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma ambayo husababisha maji ya mto mkondoa kuacha mkondo wake na kubomoa tuta la reli katika eneo la Msagali hadi Kilosa kila wakati. 

Mvua za hivi karibuni zilizonyesha mkoani Iringa na Dodoma zimesomba reli katika eneo la Magulu-Kidete kilomita 315 kutoka Dar es Salaam na kukata mawasiliano ya reli kwa siku tatu sasa. 
 
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa TRL na RAHCO kutafuta suluhisho  la kudumu katika madaraja 32 yaliyo katika mtandao wa reli ya kati ili yasiathiriwe na mvua wakati wote.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...