Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano
ambalo uhai wake unaisha Julai 9, linaonekana dhahiri kwenda mrama baada
ya wabunge 23 kumlazimisha Spika kuwatimua kikaoni wakipinga
kuwasilishwa kwa miswada mitatu kwa hati ya dharura.
Kwa siku tatu mfululizo, Spika Anne Makinda
amekuwa akipata shida kuendesha chombo hicho cha kutunga sheria
kutokana na mbinu waliyogundua wapinzani ya kupiga kelele kukwamisha
shughuli za Bunge.
Juzi, kiongozi huyo wa Bunge aliamua
kuwapeleka wabunge 11 mbele ya Kamati ya Maadili kwa makosa ya kudharau
kiti chake na chombo hicho kikaibuka na adhabu ya kuwafungia wabunge
wanne kutohudhuria vikao vyote vilivyosalia, wengine wawili kufungiwa
vikao viwili.
Jana, hali iliendelea kuwa ya mapambano
baada ya wabunge hao kuhoji uhalali wa adhabu hiyo, huku wakihoji sababu
ya miswada hiyo kuwasilishwa kwa dharura.
Ezekia Wenje, mbunge wa
Nyamagana, aliendelea kubishana na Spika na kusababisha atangaze
kumzuia kushiriki vikao vitano, uamuzi uliosababisha wabunge wengine wa
upinzani kusimama na kupiga kelele wakitaka nao waadhibiwe.
Spika Makinda alisema kuwa ametumia kanuni ya 74(i) kuwatimua wabunge hao kwa kushindwa kuheshimu kiti kwa kupiga kelele.
Wakati wabunge waliopewa adhabu
wakiongezeka, wenzao ambao hawakuwapo sasa wamehamasishwa kwenda mjini
Dodoma kuendelea na walichokiita mapambano, hali inayoweza kusababisha
Bunge hilo likavunjwa likiwa limepukutika wabunge wa upinzani.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba
amesema CCM inakabiliwa na kazi ngumu ya kupata mgombea wa urais
atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka huu,
akionya kuwa makundi ya urais yasipomalizwa yanaweza kufika hadi ngazi
ya kata.
Makada 38 wamejitokeza kuomba ridhaa ya
chama hicho tawala ya kugombea urais katika kipindi ambacho kuna
ongezeko kubwa la nguvu ya vyama vya upinzani, huku vyama vinne vikiwa
vimeamua kusimamisha mgombea mmoja.
Tayari vikao vya kujadili jinsi ya
kumpata mteule wa kupeperusha bendera ya chama hicho vimeshaanza kwa
wenyekiti na makamu wao kukutana na jana Kamati Kuu ilikuwa inakutana
mjini Dodoma.
Akiangalia hali hiyo, Jaji Warioba
aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho tawala kinatakiwa kuwa makini
katika mchakato huo, kwa maelezo kuwa unaweza kuacha majeraha makubwa
kutokana na makundi yaliyoibuka.
“CCM
inakabiliwa na wakati mgumu wa kupitisha jina la mgombea urais kutokana
na waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 38, na mpaka sasa imekuwa
ni vigumu kutabiri atakayepitishwa, jambo ambalo halikujitokeza wakati
wa upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995 na 2005,” Jaji Warioba
Alisema kila unapofika Uchaguzi Mkuu
kunakuwa na changamoto zake, lakini mwaka huu CCM inakabiliwa na
changamoto kubwa zaidi kwa sababu uchaguzi huo utamleta rais mpya na
mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Alisema jambo la kwanza lililotokea
katika mchakato wa kumpata mgombea urais litakalokifanya chama hicho
kuwa na wakati mgumu ni kitendo cha baadhi ya wagombea kueleza sera zao,
wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya
uchaguzi.
“Waliotangaza
nia wamekuwa wakieleza sera zao na ukiwasikiliza unaona kama walikuwa
wagombea binafsi hivi kwa sababu CCM ina sera, wanayo ilani ambayo ipo
tayari na yeyote atakayepeperusha bendera ya CCM lazima ajikite kwenye
ilani ya chama,” alisema jaji Warioba.
“Kama
mtu ametangaza sera na vipaumbele vyake na havifanani na vipaumbele vya
ilani ya chama unafanyaje? Ni mtihani mwingine huo.”
Alisema jambo la pili ni kukiukwa kwa
utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote anayehusika kwenye
ngazi ya maamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais, huku akiwatolea
mfano wajumbe wote wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao ndio humchagua
mgombea urais wa chama hicho.
“Nimeambiwa kwamba wajumbe wa mkutano
mkuu walikatazwa kudhamini wagombea, lakini tulivyoona ni kwamba
viongozi wengi wameonyesha waziwazi wapo kundi gani, wapo waliojitokeza
na kusema na wengine hawakusema lakini wanajulikana wanamuunga mkono
mgombea gani,” alisema.
“Hawa
ndio watakwenda kuchuja, sasa hapa itakuwa kazi ngumu na inawezekana
kukawa na mgongano wa maslahi na hilo lisipoangaliwa linaweza kufanya
mchujo ukaonekana kuwa haukuwa wa haki. Jambo hili linatakiwa kuangaliwa
na hasa kwa kuwa kuna makundi.”
MWANANCHI
Wakati watu watano wakijeruhiwa, wawili
kwa kupigwa risasi, kwenye uandikishaji wa wapigakura eneo la
Makunduchi, mkutano baina ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wadau
umevunjika kutokana na mzozo wa mgwanyo wa majimbo.
Vurugu hizo zimetokea baada ya watu
waliokuwa wamekusanyika katika Msikiti wa Kubini kwa madhumuni ya
kupinga kazi hiyo ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura wakituhumu
kuwapo kwa mamluki waliokuwa wakiandikishwa, lakini wakajikuta
wakivamiwa na kundi la askari wasiokuwa na sare ambao walikuwa na silaha
za moto.
Waliojeruhiwa kwa risasi ni Kheri Makame Hassan na Ramadhani Hija Hassan wote wakazi wa Makunduchi wakati Ali Seif Issa, Ali Hassa Hassan kutoka Paje akiwa amepigwa kwa magongo na nondo na kuumia vibaya miguuni, na Hassan Ali Ameir.
Majeruhi wao walisema walikuwa katika kituo cha Nganani, Shehia ya Nganani Kusini Unguja ndipo walipokuja watu waliovaa vinyago na kuwaamuru waondoke eneo hilo wakati uandikishaji ukiendelea.
“Ilikuja
gari na watu waliojifunika nyuso zao wakatuambia tuondoke na sisi
tukakataa kwa sababu tulikuwa tunazuia kuandikishwa mamluki katika eneo
letu. Baada ya kubishana pale wakaenda kuchukua gari nyingine wakaanza
kutupiga,” alisema Kheri ambaye amepigwa risasi ya pajani.
“Watu
waliojifunika nyuso walikuja mara mbili na kuondoka kabla ya kufanya
shambulio na kufanikiwa kuondoka katika eneo la tukio la Nganani kwa
kutumia magari mawili,’ alisema Faki huku akilalamika kusikia maumivu.
Shuhuda wa tukio hilo, Ameir Mussa,
mkazi wa Makunduchi, alisema kwamba waliamua kukusanyika eneo la msikiti
wakitafakari jinsi ya kuzuia uandikishaji wa wapigakura mamluki, ambao
ni pamoja na walio na umri mdogo.
“Lilikuja
kundi la watu mara mbili na kuondoka. Walikiwa wamefunika nyuso zao na
waliporudi kwa mara ya mwisho walitushambulia kwa kutumia silaha za
kienyeji na baadaye kufyatua risasi za moto na kujeruhi watu wawili,”Mzee Ameir.
Daktari wa zamu wa Hospitali ya Al Rahma, Seif Suleiman alithibitisha kupokea majeruhi na kusema kwamba katika hatua za awali wanazuia damu kuvuja kutoka kwenye majeraha.
Alisema wanaendelea na vipimo ili kujua majeraha hayo yamesababishwa na nini.
“Tumewafanyia x-ray ili kujua majeraha yao yanatokana na nini lakini
yanaonesha wazi kuwa ni majeraha kama ya risasi kwa kuwa risasi jeraha
lake linakuwa ni kitobo kidogo inapoingia lakini kitobo kikubwa
inapotokea risasi.” Dk Suleiman alisema majeruhi hao wanaendelea vizuri baada ya kutibiwa na wengine wataruhusiwa watakapopata nafuu.
“Wapo
walioumia sana hao wataendelea kuwepo hospitali kwa sababu wametokwa
damu nyingi sana na kutoka Makunduchi hadi Mjini ni mbali kwa hivyo
wanahitaji kupumzishwa kwanza hadi hapo watakapopata nafuu,” Dk Suleiman.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saadi alisema
kuwa katika mkoa wake kuna uandikishaji wananchi kuwaingiza kwenye
Daftari la Wapigakura, lakini hana taarifa za watu kupigwa risasi na
kwamba anachojua ni risasi hizo kupigwa hewani na hivyo hazijajeruhi
mtu.
MWANANCHI
Kiongozi mkuu wa chama chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe
jana alianika orodha ya majina ya watu wanaotuhumiwa kuhodhi akaunti
zenye mabilioni ya fedha nje ya nchi, lakini akasita kuyataja kutokana
na sababu za kisheria.
Zitto aliwapa waandishi wa habari orodha hiyo akisema waende kufanyia kazi kwa kuwahoji wahusika kulingana na taaluma yao.
Orodha hiyo ina majina yenye asili ya kiasia isipokuwa wachache ambao wanaonekana wana majina ya kibantu.
Zitto alisema: “Majina ninayo haya hapa niwataje nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki kampuni kubwa.”|
Alisema Zitto alisema wamejaribu
kuishinikiza Serikali ichukue hatua, lakini inaonekana kutotaka kufanya
hivyo na kwamba anaamini waandishi wa habari kwa kutumia taaluma yao
wataweza kuwaanika wahusika.
Wakati maofisa wa ACT wakigawa orodha ya
majina hayo, wananchi walionekana kuwa na shauku ya kupata nakala ya
karatasi hiyo yenye majina 99 ya wafanyabiashara hao maarufu ndani na
nje ya nchi, lakini kiongozi huyo hakuwa tayari kuwapatia na badala yake
akiwaambia wasome magazeti ya kesho (leo).
Zitto alisema kwamba kati ya majina ya
raia hao wenye mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kuna wengine wanamiliki
kihalali lakini wengine wamejirundikia isivyo halali.
‘’Nimeamua
leo kuiweka orodha hii wazi kama shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa
ya uchunguzi kabla ya Bunge kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa
habari aliyepo kwenye mkutano huu nimempatia nakala yenye majina 99 ya
Watanzania au watu wenye uhusiano na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya
Uswisi. Jumla ya akiba katika akaunti benki hii pekee ni Dola 114
milioni za Marekani,’’
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa
ametawawa kuwa chifu wa mkoa na wazee wa Dar es Salaam na kuitaka
serikali kuhakikisha inawarudishia wananchi chenji zinazotokana na
ufisadi wa Escrow , EPA na Richmond.
Dk Slaa alisema ingawa wazee waliungana na Hayati Mwalimu Nyerere kupambana na maadui wa tatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini kwa sasa ameongezeka adui wa nne ambaye ni ufisadi.
“Ujinga alioupinga Mwalimu na wazee umeondoka? Lakini ujinga, umaskini na maradhi na kuna adui wa nne ambaye ni ufisadi,” alisema.
Alisema hakuna Mtanzania ambaye
atakwenda dukani na Sh10,000 kununua chumvi na kibiriti halafu akaacha
chenji yake dukani kwa makusudi na hivyo Watanzania bado wanadai fedha
zao zilizopotea kutokana na ufisadi.
Kadhalika Dk Slaa alisema kitendo cha
wazee hao kukutana katika kongamano hilo kinaashiria kuwa wana kiu, njaa
na matumaini ya kutaka mabadiliko.
HABARILEO
Jitihada za Serikali kuhakikisha
rasilimali adimu ya gesi yenye fursa ya kutokomeza umasikini kwa
Watanzania wote inanufaisha umma zaidi, zimeendelea kupingwa ili
rasilimali hiyo inufaishe sehemu ndogo ya jamii.
Katika kuhakikisha gesi inakuwa fursa ya
kuondoa umasikini kwa umma wa Watanzania na kutimiza ndoto za Rais
Jakaya Kikwete kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania masikini, mwishoni mwa
wiki hii Serikali iliwasilisha bungeni miswada mitatu ya sheria ukiwemo
Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015.
Mingine ni Muswada wa Sheria ya
Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria
ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka
2015.
Hata hivyo, kazi ya kuzuia manufaa hayo
kwa umma iliyoanza tangu kuvumbuliwa kwa gesi nyingi baharini inayozidi
futi za ujazo trilioni 55, iliendelea na kuvuruga vikao vya Bunge,
ambavyo vimelazimika kuendelea leo na kesho kutwa, siku ya Sikukuu ya
Sabasaba.
Sehemu ya kazi hiyo ilihusisha baadhi ya
wabunge walioamua kuzuia jitihada hizo za Serikali, huku baadhi yao
wakitamka wazi bungeni kwamba, wenzao wameshawishiwa na kampuni na
wafanyabiashara wanaonyemelea kunufaika zaidi na rasilimali hiyo.
Gesi hiyo inayozidi futi za ujazo
trilioni 55, pekee ni mtaji katika kuanzisha na kuendeleza miradi yoyote
ya umma, katika sekta zote zinazogusa maisha ya Watanzania.
Profesa Sospeter Muhongo,
amesema kiasi hicho ni sawa na mapipa bilioni 10 ya gesi na kwa bei ya
chini ya dola za Marekani 50 kwa pipa, ni sawa na mtaji wa zaidi ya Dola
za Marekani bilioni 500.
Mtaji huo ni sawa na karibu nusu ya
bajeti ya nchi kubwa ya Uingereza ya mwaka 2014, ambayo ilikuwa Dola za
Marekani trilioni 1.1. Uwazi, elimu.
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM) alisema miswada hiyo ikipitishwa na kuwa sheria, itaweka uwazi katika leseni na mikataba ya madini, gesi na mafuta.
Naye Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene,
alisema miswada hiyo isipopitishwa kuwa sheria, itakuwa hasara kubwa
kwa Watanzania, ikisubiri Bunge lijalo Serikali italazimika kuanza
kuwajengea upya uwezo wabunge hao katika jambo hilo, wakati wabunge wa
sasa walishapata elimu hiyo.
“Wabunge
hawa wamejengewa uwezo, wameenda nchi mbalimbali kujifunza masuala ya
gesi na mafuta na tangu mwaka 2010 tumeanza mchakato wa jambo hili,
ndiyo sababu tunataka itungwe sasa vinginevyo itakuwa matatizo mbele,”Simbachawene.
Hasara uchelewaji Simbachawene alisema
masuala ya kujadili mikataba na kampuni za gesi, inachukua kati ya mwaka
mmoja hadi mwaka mmoja na nusu, hivyo kama sheria haitakuwa tayari,
uzalishaji uliopangwa uwe kati ya mwaka 2018 na 2019, utalazimika
kucheleweshwa, maana yake muda utazidi kusonga mbele na itakuwa hasara
kwa Watanzania.
“Suala
la majadiliano ya mkataba si la wiki moja au mwezi, ni kati ya mwaka
mmoja na zaidi, sasa unasema Bunge lijalo ndiyo lifanye kazi hiyo unajua
litakuwaje?” Alihoji.
Alisisitiza kuwa Muswada wa Sheria ya
Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji ukipitishwa, utafanya
mikataba yote ya madini na gesi iwe wazi na halitakuwa jambo la siri
kama ilivyo sasa.
HABARILEO
Hatimaye baada ya hujuma ya wabunge wa
Kambi Rasmi ya Upinzani kushindwa, Serikali imewasilisha bungeni miswada
ya sheria kuhusu masuala ya mafuta na gesi, huku matumizi ya mapato ya
gesi yakiwekewa vizingiti.
Akisoma hotuba ya Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 bungeni jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba,
alisema muswada unaweka masharti kuhusu uanzishwaji wa Mfuko wa Mafuta
na Gesi, ambao utakuwa na akaunti mbili zitakazotunzwa na kusimamiwa na
Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alizitaja akaunti hizo ni Akaunti ya
Kupokea Mapato na Akaunti ya Kutunza Mapato na kwamba mfuko wa mapato
yatokanayo na mafuta na gesi, unapendekezwa kuanzishwa kwa madhumuni ya
kupokea na kugawa mapato yatokanayo na mafuta na gesi kwa kuzingatia
malengo makubwa matatu.
Malengo hayo ni kuhakikisha uimara wa
kifedha na kiuchumi, kugharamia uwekezaji katika sekta ya mafuta na
gesi, kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kulinda rasilimali
kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Katika muswada huo, Nchemba pia alitaja
vyanzo vya mapato vya mfuko huo kuwa ni mirabaha, gawio na faida ya
Serikali katika shughuli za mafuta na gesi.
Vingine ni kodi za mapato ya makampuni,
ambayo hukatwa baada ya kupata faida ghafi na gawio litokanalo na tasnia
ya mafuta na gesi pamoja na faida itakayopatikana kutokana na uwekezaji
wa fedha za mfuko.
Nchemba alisema inapendekezwa katika muswada kwamba mapato yote ya mfuko yawekwe kwenye Akaunti ya Kupokea Mapato.
Baadaye, Akaunti ya Kutunza Mapato
itapokea kiasi cha asilimia ya mapato kutoka kwenye Akaunti ya Kupokea
Mapato kwa kuzingatia miongozo ya kibajeti.
NIPASHE
Kamati Kuu Maalum (CC) ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imekutana kwa dharura mjini
Dodoma kupokea, kuchambua na kutoa baraka kwa vipaumbele na ahadi za
Rais ajaye vilivyoainishwa katika ilani mpya ya uchaguzi ya mwaka 2015.
Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete; iliwaita Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira,
ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam ya Kuandaa Rasimu ya Ilani
ya Uchaguzi, pamoja na wajumbe wake kwa ajili ya kuikabidhi na kutoa
ufafanuzi wa baadhi ya mambo.Kamati hiyo ilikuwa na kibarua kizito cha kutoa ufafanuzi kuhusu Rasimu za awali ambazo zilikuwa zimefanyiwa maboresho na kisha kupatikana kwa ilani mpya itakayotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kabla ya Rais Kikwete kuwasili mjini hapa saa, 8:37 mchana na kuendesha kikao hicho kwa zaidi ya saa nne; wapambe wa makundi ya baadhi ya wagombea wa kiti cha urais, walionekana wakirandaranda Makao Makuu ya CCM kwa lengo la kutaka kujua kinachoendelea baada ya kuitishwa ghafla kwa kikao hicho.
Wajumbe wa Kamati ya Wassira ni Anamringi Macha (Katibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali-Zanzibar, Ali Juma Shamhuna.
Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Anthony Mavunde, Mbunge wa Manyoni Mashariki, Kapt. John Chiligati, na Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Aboud; ndio walioitwa ili kukabidhi ilani hiyo.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya CC hiyo, vilieleza kuwa ajenda nyingine ilikuwa ni kuwajadili wenyeviti 18 wa mikoa wa CCM ambao wanadaiwa kujilipua kwa kumuunga mkono mmoja wa wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, kupitia chama hicho.
Ajenda ya tatu ilikuwa ni kupata mrejesho wa hali halisi ya mwenendo wa bunge; kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo inaundwa na vyama vinne vya Ukawa kuchafua hali ya hewa kwa siku mbili na kulazimika kuahirishwa ili kupata utulivu.
Awali, akifungua kikao hicho, Rais Jakaya Kikwete alisema, kikao hicho ni maalum kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
NIPASHE
Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wamempa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, majukumu ya kuikomboa nchi kwa mara ya pili kama alivyofanya mwalimu Julius Nyerere wakati akiitoa mikononi mwa wakoloni.
Jukumu hilo alipewa jana na wazee hao baada ya kumvisha vazi la
uchifu na kumkabidhi vitu mbalimbali vikiwamo kisu, panga, shoka, jembe,
nundu na usinga ikiwa ni ishara ya kumtawadha kushika madaraka hayo kwa
Mkoa wa Dar es Salaam ambapo sasa atatambuliwa kama Chifu Mwinyikambi.Mzee Ally Mwinyikambi, ambaye alimkabidhi Dk. Slaa uchifu huo kwa niaba ya wazee wa mkoa huo, alisema wanamtaka ahakikishe anakiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
Katika hotuba yake, Dk. Slaa alisema kuwa, kilichotokea kimekumbusha enzi za Nyerere wakati akiwa anatoka masomoni.
Alisema kitendo hicho kimekihakikishia chama hicho ushindi wa kuelekea Ikulu katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Aliwahakikishia wazee hao na Watanzania kwa ujumla kuwa, uchaguzi huu lazima washinde kwa kishindo.
Alisema licha ya Mwalimu Nyerere kuwataja maadui wa nchi kuwa ni umaskini, ujinga, maradhi lakini CCM katika utawala wake wote imeshindwa kuyaondoa hayo.
“CCM imekuwa ikikusanya wazee wa chama chao pekee kwenye ukumbi na kuwapa Sh. 5,000 bila kuangalia matatizo yao, sisi hatuna ubaguzi na tunawatambua wazee wote wa nchi hii,” alisema.
Alisema licha ya CCM kutawala muda mrefu lakini huduma za jamii kama barabara, afya, elimu utekelezaji wake bado ni hafifu wakati wananchi wamekuwa wakitozwa kodi.
“Tunadai chenji zetu kwenye Richmond, Epa, Escrow kwa sababu hizi ni fedha za watanzania ambao ndio walipakodi,” alisema.
Dk. Slaa alisema watakapoingia madarakani miaka kumi watahakikisha nyumba zilizojengwa kwa nyasi zinatoweka huku huduma za afya zilipungua gharama zake kulingana na kipato cha Mtanzania.
Kuhusu mashine za kuandikisha wapiga kura za Kieletroniki Biometrick Voters Registration, katibu huyo aliwataka wazee kutumia muda wao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji na kuhakikisha hawatoki vituoni hadi vinafungwa.
Akiongelea migogoro ndani ya nchi ukiwemo ule wa madereva ambao waligoma hivi karibuni, alisema kuwa serikali haipaswi kutafuta mchawi bali itafute muafaka.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, wakili mashuhuri, Mabere Marandu, alisema kuwa Chadema haina tamaa ya madaraka na kwamba wakiingia madarakani muda wake ukiisha na wananchi wakiona hawajafanya kitu, wapo radhi kuondoka.
Naye, mwenyekiti wa Wazee Tanzania, Hashimu Issa Juma, alisema kuwa Chadema ikiingia madarakani itatoa pensheni ambao haitapungua 100,000.
Pia alisema watatoa matibabu bure na huwahakikishia usafiri wa daladala utakuwa bure.
Usisumbuke Mawerenewz.blogspot.com ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO, SIASA, na HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>mawere_mtoka_mbali,
No comments:
Post a Comment