18 July, 2015

Ubunge CCM Kama Urais

wabunge+pixWANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaowania kibali cha chama hicho ili wagombee ubunge, wamejitokeza kwa wingi katika baadhi ya majimbo na kufanya mchakato huo kuwa na mvuto wa aina yake, unaofanana na ule wa urais.

Jana ikiwa siku ya pili tu tangu kufunguliwa kwa pazia la uchukuaji fomu za kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali nchini, idadi ya wanachama waliochukua fomu katika baadhi ya majimbo, imekuwa kubwa na kuelekea kulingana na wawania urais katika chama hicho, ambao walifikia 42. Jimbo jipya la Mbagala ndilo lilitia fora kwa kuwa na wasaka ubunge 17, waliolipa Sh laki moja na kuchukua fomu ya kuomba wanaCCM wapendekeze mmoja wao kuwania nafasi hiyo katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa Katibu Muenezi wa Wilaya ya Temeke, Rutami Masunu, mpaka jana siku ya pili ya utoaji fomu, waliojitokeza katika Jimbo hilo jipya ni wanachama hao 17.
Alitaja baadhi ya aliowakumbuka kuwa ni pamoja na Peter Nyalali, Richard Tambwe Hiza, Lucas Malegeli, Issa Mangungu, Mindi Dominck Haule, Ally Makwilo, Kivuma Msangi na wengine.
Katika Jimbo la Temeke waliojitokeza kuchukua fomu ni Mbunge wa jimbo hilo anayemaliza muda wake, Abbas Mtemvu, Hamis Salim maarufu kama Chicago, Maimuna Chicago pamoja na Joseph Mhoha.
Masunu alisema kwa upande wa Jimbo la Kigamboni waliojitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Dk Faustine Ndugulile anayetetea nafasi yake pamoja na wanachama wengine watatu.
Kwa Wilaya ya Ilala, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Ernest Charles aliliambia gazeti hili kuwa jumla ya waliojitokeza katika wilaya hiyo ni wanachama 26.
Aliwataja baadhi ya wanachama hao na majimbo yao kwenye mabano kuwa ni Mussa Azzan Zungu, Mrisho Gambo, Waziri Kindamba (Ilala), Zahoro Lyasuka, Bona Kalua, Apruna Jaka, Siasa Chuma na Nicholaus, Baraka Omary, Christopher Japhet, Scholastica Kevela, Simon Kambe na Tunza Kanabe (Segerea).
Kwa jimbo la Ukonga ni Meya Jerry Slaa, Anthony Kalokola, Jacob Kasema, Hamza Mshindo, Fredrick Rwegasira, Ramesh Patel, Peter Kaseleko, John Machuta, Magesa Magesa, Amos Hangaya, Thomas Masegese, Edwin Moses na Ammo Mkuno.
Taarifa kutoka majimbo mengine ya Dar es Salaam, zilieleza kuwa katika Jimbo la Kinondoni walijitokeza wagombea tisa, Ubungo sita na jimbo jipya la Kibamba 10.
*Morogoro Kusini
Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, lililopo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini nalo lilijikuta likipata wasaka ubunge 12, akiwemo mbunge anayemaliza muda wake, Dk Lucy Nkya.
Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro Vijijini, Shaibu Mtawa, alitaja baadhi yao aliowakumbuka kuwa ni Upendo Konyaki, Abdallah Mohammed, Athuman Maneno, Issa Dilunga na Semeni Mwinyimvua Kingalu.
Chilonwa, Morogoro
Mkoa mwingine ambao umepata wasaka ubunge wengi katika jimbo moja ni Dodoma, katika Jimbo la Chilonwa, lililokuwa likiongozwa na Hezekiah Chibulunje, ambaye alitangaza kutogombea tena ubunge. Waliochukua fomu mpaka jana mchana walifikia wagombea 12.
Miongoni mwa waliojitokeza kuwania jimbo hilo ni Godrick Ngoli, Paschal Ndolosi, Charles Ulanga, Peter Mlugu, Amos Kusakula na Chiuti Masagasi Jimbo la Mtera, mbunge anayemaliza muda wake, Livingstone Lusinde, naye amejikuta akikabiliwa na ushindani wa makada sita, akiwemo Charles Ulanga, Essau Mzuri na Dk Charles Msendekwa.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...