05 August, 2015

Kwenye StoriKubwa >>> Ya MAGUFULI, Rais JK.. Lowassa? mastaa waliokatwa YANGA …

222222MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan jana walichukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku Rais Jakaya Kikwete akisema wapinzani wataisoma namba.
Ofisi ndogo za makao makuu ya CCM zilizoko Lumumba na za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilifurika mashabiki waliovalia nguo za rangi ya njano na kijani, ambazo hutumiwa na chama hicho, huku wakazi wengine wanaofanya kazi au kuishi maeneo jirani na barabara za Morogoro, Bibi Titi na Ohio, wakilazimika kusimamisha shughuli zao kwa muda kushuhudia msafara wa wagombea hao ukipita.
Walinzi  wa ofisi za NEC walilazimika kufanya kazi ya ziada kudhibiti wafuasi wa CCM waliosindikiza wagombea hao kutoka ofisi ndogo za CCM kabla ya msafara huo kuondoka baada ya wawili hao kuchukua fomu, kurejea Lumumba, ambako mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete aliupokea.
“Wakwere wanasema chihendo na mwene mwana, yaani shughuli na mwenye mtoto,” alisema Rais Kikwete mara baada ya msafara kuwasili akieleza sababu za yeye kuwapo eneo hilo kwa kutumia maneno ya shughuli za kitamaduni za jandoni, unyagoni na mkoleni za kabila la Wakwere.
“Nimekuja hapa kujiridhisha kama kweli fomu zimechukuliwa. Na kweli nimeziona. Baada ya hatua hii wale wanaodhani kuwa CCM ni chama cha mchezo mchezo, wataisoma namba.”
Huku akikatiza hotuba yake kwa kuitaka bendi ya TOT ya chama hicho kuimba wimbo wa “Shangilia Ushindi Unakuja”, Rais Kikwete alisema kwa kuwa yeye ni baba alilazimika kuja kuangalia kama mwanaye ametekeleza alichotuma.
Kikwete, ambaye alitumia mifano iliyovunja mbavu wafuasi hao, alirusha kijembe kwa wanachama walioihama CCM akisema ni tamaa na kuahidi kufanya mkutano mkubwa wa uzinduzi wa kampeni.
CCM shangilia ushindi unakuja, tena ushindi wa uhakika na si wa wasiwasi. Baada ya hapa kitakachofuata ni uzinduzi hapo Agosti 22 kwenye mkutano utakaotisha. Hatumwi mtoto siku hiyo, unakuja mwenyewe,” alisema.
“Watu wanasumbuliwa na tamaa na wakati mwingine ni tamaa iliyopitiliza kutaka madaraka.”
Magufuli alitoka ofisi ya CCM Lumumba akiwa amepanda gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa wazi juu akiwa na msafara wa magari yapatayo 10 kuelekea ofisi za NEC. Baada ya kufika eneo la makutano ya Barabara ya Ohio na Bibi Titi, alishuka na kupanda gari nyingine iliyokuwa wazi nyuma na kuamsha kelele za shangwe.
Aliwasili ofisi hizo saa 5.22 asubuhi na baada ya kuchukua fomu za kuwania urais, msafara wa kurejea ofisi za chama hicho zilizoko Lumumba ulianza tena na kufika ofisi hizo ndogo za CCM, ambako ulipokelewa na Rais Kikwete.
“Matatizo ya Watanzania nayajua na  ninaahidi kuwa nitakuwa mtumishi wenu mtiifu,” alisema Dk Magufuli baada ya Rais Kikwete kumuomba aketi ili azungumze na wafuasi wa chama hicho.
“Nafahamu kuwa Watanzania wanahitaji ajira na hawataki usumbufu kwenye biashara zao kama mamantilie, wana kero kwenye huduma mbalimbali. Ninawaahidi kuwa nitazishughulikia.
Napenda nimhakikishie mwenyekiti na wananchi mliokusanyika hapa kuwa CCM itashinda na wala simuoni mtu wa kutushinda. Nashukuru kwa moyo mliouonyesha wa kunisindikiza mimi pamoja na Samia. Mmetoa jasho na mmepoteza muda wenu. Napenda kuwahakikishia kuwa muda wenu hautapotea bure.”
Alirudia wito wake wa kuwataka wananchi kuendeleza mshikamano uliopo bila kujali itikadi zao wala makabila ili kuliletea Taifa maendeleo kwa kuondoa kero zinazowakabili.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ilikuwa kazi kubwa kumshawishi Juma Duni Haji kukiacha chama hicho na kujiunga Chadema ili awe mgombea mwenza wa Edward Lowassa.
Duni, ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF, alitangazwa kujiunga na Chadema jana, ikiwa ni makubaliano ya mkakati maalumu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wa kukabiliana na kikwazo cha kisheria cha kupata mgombea mwenza kutoka chama tofauti na kilichosimamisha mgombea urais.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka Makamu wa Rais kutoka chama kilichoshinda kiti cha urais na hivyo Duni amejiunga na Chadema akiwa mwakilishi wa Ukawa kwenye Serikali iwapo umoja huo, unaoundwa na CHADEMA, CUF, NLD na NCCR – Mageuzi utashinda Uchaguzi Mkuu.
Lakini kabla ya Duni kukubali ushauri huo, Maalim Seif alisema walikuwa na kibarua kigumu.
“Tulimwita Babu Duni, tukamwambia azma hii, akasema; ‘hivi kweli niende Chadema mie?’” alisema Maalim Seif akimnukuu Duni wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chadema jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Nikamwambia kwa hili tunalotaka la mabadiliko, lazima uende Chadema.”
Maalim Seif, ambaye alikuwa mmoja wa wageni waalikwa waliopewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo ambao ni chombo cha juu cha uamuzi cha Chadema, alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu kuhakikisha kuwa upinzani unatwaa Dola katika uchaguzi ujao wa Rais, wabunge na madiwani.
Maalim Seif, ambaye alijitangazia ushindi wa kiti cha urais wa Zanzibar, pia alimtangaza Lowassa, ambaye pia aliondoka CCM na kujiunga na Chadema wiki iliyopita, kuwa ameshashinda mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mgombea mwenza na wanachosubiri sasa ni kuapishwa tu.
“Huu ni wakati wa kujiamini na kuamini kuwa tunaweza kuchukua dola,” alisema Maalim Seif ambaye pamoja na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba waliiongoza CUF katika kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK).
Wakati Maalim Seif akitangaza ushindi kwa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alionya kuwa kazi ya kuiondoa CCM si rahisi na kwamba nguvu ya Watanzania inahitajika kufanikisha azma hiyo.
HABARILEO
Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Ujambazi Mkoa wa Morogoro, Elibariki Pallangyo , amepigwa risasi na kufa papo hapo nyumbani kwake eneo la Yombo jiji Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alisema kuwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa tisa usiku, kundi la watu zaidi ya kumi lilivamia nyumbani kwa Pallagyo eneo la Yombo kwa kuruka ukuta, kisha kuvunja mlango na kuingia ndani walikopora fedha na simu za mabinti wanne waliokuwa ndani kabla ya kufanya mauaji.
“Hili tukio ni la kusikitisha kwani watu hawa wanaonesha walikuwa na lengo la kumuua tu na si kupora mali, kwani wamechukua fedha Sh 130,000 pamoja na simu za mkononi 4 ambazo walikuwa nazo hawa wasichana waliowakuta sebuleni,Satta.
Alisema baada ya watu hao kupora simu na fedha kutoka kwa mabinti, waliekea kwenye chumba cha Pallangyo, wakampiga risasi moja kifuani na kumuua.
Wauaji hao walitokomea kusikojulikana huku wakisahau kifaa kinachotumika katika milipuko. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Temeke na utapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi kabla ya maziko.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kufanya kampeni za kistaarabu, kwakuwa nchi ya Tanzania inayo sifa ya kuendesha mambo yake kwa njia ya amani na utulivu.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akihutubia mamia ya wakazi kwenye hafla maalumu ya kuwaaga wananchi wa mkoa wa Tanga, iliyofanyika katika uwanja wa Mkwakwani jijini hapa.
Katika hafla hiyo, ambayo Rais Kikwete aliongozana na Mama Salma Kikwete alipata fursa ya kupokea zawadi za aina mbalimbali kutoka kwa wawakilishi wa wananchi kutoka wilaya za Tanga, Mkinga, Pangani, Muheza, Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi ambazo zinaunda mkoa huo.
Alisema kwa kuwa kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi wa Oktoba zitaanza rasmi Agosti 21 mwaka huu ni vyema wananchi kila mmoja kwa nafasi yake, wahakikishe zinafanyika kwa ustaarabu na utulivu ili kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
“Tanzania ina sifa ya kuendesha vitu kwa amani na utulivu …naomba kampeni zitakazofanyika za kuwanadi wagombea wa udiwani, ubunge na urais ziwe za kistaarabu hakuna sababu ya kufanya vurugu bali kila mtu apewe nafasi ya kumwaga sera zake, asikilizwe kwa utulivu”, alisema.
Aidha, Rais Kikwete aliwashukuru wakazi wa Tanga kwa kuiunga mkono CCM sambamba na kumuunga mkono kwa kiwango kikubwa kwenye chaguzi zote, zilizomuweka madarakani mwaka 2005 na 2010, ikilinganishwa na baadhi ya mikoa mingine nchini.
“Wito wangu kwenu ichagueni CCM tu katika serikali inayokuja, chama hiki kitawajengea Chuo Kikuu cha Serikali kwa sababu hapa Tanga hamna… naomba wananchi tujiandae vizuri kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo mkuu,” alisema.
Awali, akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Saidi Magalula alisema “Wananchi wa mkoa huu wameniagiza niwasilishe kwako maombi ya vitu vifuatavyo ujenzi wa daraja la Mligazi linalounganisha wilaya ya Handeni na Miono, pia ujenzi wa barabara ya Tanga- Pangani–Bagamoyo kwa kiwango cha lami, Bandari ya Tanga, kufufuliwa kwa viwanda mbalimbali vya uzalishaji na kufufuliwa kwa reli ya Tanga – Moshi hadi Musoma”.
HABARILEO
Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Chiku Abwao ndiye atakayepeperusha bendera ya ACT kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa mjini katika uchaguzi mkuu ujao, huku akitamba kwamba atambwaga mbunge anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Mbali na Abwao aliyejiunga na ACT Wazalendo hivi karibuni, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chadema, Abuu Changawa naye ameiacha Chadema na kujiunga ACT Wazalendo, huku akitangaza kuwania udiwani katika Kata ya Mivinjeni, mjini hapa.
Abwao aliyewahi kuwa mbunge wa NCCRMageuzi, alisema; “Nimeondoka Chadema baada ya kubanwa kila kona na Mchungaji Msigwa akidhani kwamba mimi nilikuwa Chadema kwa sababu ya kutaka cheo.”
Alisema pamoja na kunusurika maisha yake wakati akipigania ushindi wa Mchungaji Msigwa 2010, mahusiano yao kisiasa yamekuwa mabaya kwa kipindi chote kwani kila alilokuwa akijaribu kulifanya kwa niaba ya chama hicho alitafsiriwa analenga kugombea ubunge jimbo la Iringa Mjini.
Alisema ili kumuonesha nguvu yake kisiasa na kwamba yeye sio mwanasiasa anayetaka tu uongozi lakini mwenye dhamira na maono ya dhati ya kusaidia kuleta mabadiliko nchini atagombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini kupitia ACT Wazalendo.
JAMBOLEO
Siku mbili baada ya mawaziri watano kushindwa katika kura za maoni ya ubunge ndani ya CCM, waziri mwingine, Gaudentia Kabaka anayeshughulikia Kazi na Ajira, naye amedondoshwa katika jimbo la Tarime Mjini.
Kabaka, kabla ya kujitosa katika siasa za majimbo, alikuwa mbunge wa muda mrefu wa viti maalumu. Aidha, katika kura hizo zilizofanyika kote nchini, zimewaacha katika hali mbaya wabunge wanne, baada ya kushindwa katika kura za maoni majimboni mwao.
Hao ni Nyambari Nyangwine, Gaudence Kayombo, John Lwanji na Salome Mwambu.
Matokeo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini ambako Nyangwine ameanguka, yamethibitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu Wazazi Wilaya ya Tarime, Mathias Lugola aliyetangaza rasmi matokeo ya majimbo hayo.
Awali, matokeo hayo ya kura za maoni yaliahirishwa kutangazwa kutokana na kuwepo kwa tuhuma za kuwapo kwa wizi wa kura. Kwa jimbo la Tarime Mjini, Lugola alifafanua kuwa Michael Kembaki ndiye aliyeibuka mshindi kwa kura 3,908 akifuatiwa na Kabaka aliyepata kura 2,411.
Katika Jimbo la Tarime Vijijini, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Christopher Kangoye ambaye amejaribu zaidi ya mara tatu kuusaka ubunge, lakini bila mafanikio aliibuka mshindi akivuna kura 15,928 dhidi ya 12,205 za John Gimunta ambaye ni Mweka Hazina wa CCM wilayani Tarime.
Nyangwine na Gimunta, baadaye walilalamikia matokeo hayo wakisema mchakato wa kura za maoni ulitawaliwa na hujuma.
Kayombo azidiwa Mbinga Katika Jimbo la Mbinga Vijijini, matokeo yaliyotangazwa saa 5:45 usiku baada ya mvutano wa kutangaza matokeo unaodaiwa kudumu kwa takribani saa 12, yameonesha kuwa mbunge wa jimbo hilo aliyekuwa amejitokeza kutetea kiti chake, Gaudence Kayombo ameshindwa katika kura za maoni ndani ya CCM.
Aliyeibuka mshindi ni Martin Msuha, aliyepata kura 13,354 dhidi ya 12,068 za Kayombo, ambaye pia kwa mwaka mmoja na nusu kati ya Januari 12, 2007 na Agosti 2, 2008 alikuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.
Wengine walioshiriki katika mchakato wa ubunge jimboni humo na kura zao kwenye mabano ni Humphrey Kisika (545), Dk Silverius Komba (1,289), Edesius Kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga (3,941) na Deodatus Ndunguru.
Wabunge Singida hoi MCHUANO wa makada mbalimbali wa CCM kuwania nafasi za ubunge katika mkoa wa Singida umekamilika, huku wabunge waliokuwa wakitetea nafasi zao na baadhi ya vigogo kwenye chama hicho wakiwa wamebwaga vibaya.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Singida, Mary Maziku, wabunge wawili waliokuwa wakitetea nafasi zao hawakuweza kupata kura za kutosha kwenye kura za maoni. Nao ni Salome Mwambu wa Jimbo la Mkalama na John Lwanji wa Manyoni Magharibi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai ambaye aligombea jimbo la Mkalama alifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kupata kura 3,908 nyuma ya Allan Kiula aliyezoa kura 5,823. Jimbo hilo lilikuwa na wagombea 16.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, amesaini miswada mitano ya sheria, iliyopitishwa na Bunge la 10 Julai, mwaka huu.
Imo iliyozua tafrani na kusababisha wabunge 45 wa Ukawa kutimuliwa bungeni na wengine kususia mkutano wa 20.
Katika tukio la kihistoria lililofanyika Ikulu, jana na kuhudhuriwa na mawaziri, watumishi wa wizara na wadau wa mafuta na gesi, Rais alisaini miswada hiyo baada ya mawaziri husika kuwasilisha maelezo ya miswada hiyo.
Miswada hiyo ni wa sheria ya mafuta, sheria uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia, muswada wa sheria ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi pamoja na muswada wa sheria ya Tume ya walimu.
Vile vile muswada wa sheria ya usimamizi wa masoko ya bidhaa yote ya mwaka 2015.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema tukio hilo ni la kihistoria kwa Tanzania kwa miswada mitano kusainiwa katika hadhara kubwa ya watu.
Alisema miswada ya sheria ya gesi na mafuta inaweka utaratibu mzuri wa kimfumo, kisheria na udhibiti mzuri wa kusimamia uchumi wa gesi na mafuta, kujibu kilio cha Watanzania kuwa rasilimali ziwanufaishe na kizazi kijacho.
Balozi Sefue alisema pia watanzania wataunganishwa na ulimwengu wa gesi kwa biashara watakazoanzisha na kutekeleza katika uchumi huo, ikiwa ni pamoja na kuwa na uchumi nyumbulifu katika kulinda mahitaji ya vizazi vijavyo na cha sasa.“Tunafanya walichofanya wengine duniani na kuepuka yaliyoleta matatizo katika nchi nyingine,” alisema Balozi Sefue.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema muswada wa sheria ya mafuta unalenga kuleta sheria mpya ya kusimamia sekta ndogo ya mafuta nchini kwenye masuala ya utafutaji; uendelezaji; uzalishaji; usafirishaji; uagizaji; uchakataji; uhifadhi na biashara ya mafuta na gesi asilia nchini.
“Malengo ya muswada wa sheria ni kuimarisha usimamizi wa sekta ili kuhakikisha maslahi ya nchi katika tasnia ya mafuta yanalindwa kikamilifu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, kuweka mfumo madhubuti wa kisheria utakaoimarisha usimamizi wa shughuli za mafuta katika mkondo wa juu, wa kati na wa chini kupitia sheria moja,” alisema  na kuongeza:
“Masuala muhimu ni kuweka utaratibu ambao serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar zitashirikiana katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uendelezaji wa vitalu vya mafuta na gesi katika yaliyo kwenye maeneo yanayugusa pande zote mbili,” alibainisha.
Simbachawene alisema sheria hiyo itawezesha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Pura) ambayo itasimamia shughuli zote za udhibiti katika masuala ya kiufundi na kibiashara katika mkondo wa juu.
NIPASHE
Mbunge wa Mkuranga mkoani Pwani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,  Adam Malima, amesema kuwa kura za maoni zilizopigwa jimboni humo hazikuwa huru na haki kwa madai kwamba waliopiga kura walikuwa wachache lakini kura za matokeo zikawa nyingi.
Malima ambaye alisema kuwa hakuridhishwa na mwenendo mzima wa kura za maoni kwa vile umechukua siku tatu bila mawakala kusaini fomu za matokeo.
Matokeo ya kura za maoni katika jimbo hilo yalitangazwa juzi usiku, huku Malima akiwaambia wananchi na wapambe wake wasifanye fujo na kuwataka warudi nyumbani na kwamba vikao vya juu vya maamuzi vitatoa jina la nani apeperushe bendera ya chama.
“Mchakato uligubikwa na udanganyifu mkubwa, kura haziendani na uhalisia, pia mawakala hawakutia saini baada ya kumalizwa kwa upigaji kura katika vituo vyao, lakini ninaviachia vikao vya maamuzi vifanye kazi yake,” Malima.
Alisema kuwa ana nafasi nyingi ndani ya chama na miongoni mwa watu walioaminiwa na Rais Jakaya Kikwete kuandaa ilani ya uchaguzi, na kuwa anashangaa kusikia kuwa hawezi kuwaletea wananchi maendeleo katika jimbo hilo.
“Watu kama hao ni timu za wenzangu ambazo zinatumika kusema eti wataenda upinzani, siwezi kuzuia kambi zisiongee kitu chochote, lakini mimi sihami CCM ingawa kura hizi zina walakini,’” alisema.
Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi wa  Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, Hadija Kusaga, alisema kuwa waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 46,904, kura zilizopigwa ni 26,949 na kwamba kura 904 ziliharibika.
Alisema kuwa katika matokeo ya kura hizo, mkuu wa wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Abdallah Ulega, aliibuka na ushindi kwa kupata kura 16, 294 huku Malima akipata kura 8, 212.
NIPASHE
Mgombe urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli jana alichukua fomu za kuwania nafasi hiyo huku Mwenyeti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiwaasa wanachama wa chama hicho wasimpuuze adui yeyote katika uchaguzi mkuu mwaka huu na kutamba watafunga magori uwanjani huku wapinzani wakiwatazama.
Magufuli alichukua fomu hizo katika ofisi za Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (Nec) kwa mbwembwe akiwa kwenye msafara wa magari, pikipiki, matarumbeta na muziki.
Akizungumza na wanachama wa CCM jana mchana katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete aliwasihi wanachama wa chama hicho kutodharau adui yeyote watayepambana naye katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Licha ya Rais Kikwete kutofafanua kauli yake hiyo, katika uchaguzi mkuu ujao CCM inatarajia kupambana vikali na mgombea urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa aliyehama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hivi karibuni.
Lowassa alikihama CCM huku akisema kwamba ameamua kufanya hivyo kutokana na kubakwa kwa demokrasia ndani ya chama hicho kikongwe nchini.
Kikwete alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, chama hicho kitafunga magori uwanjani huku upinzani ukitazama na kwamba kitapata ushindi wa kishindo na hilo hana wasiwasi nalo.
Rais Kikwete jana alionekana mwenye furaha muda wote huku akiomba kikundi cha kwaya cha TOT, kimuwekea wimbo wa ‘acha waseme CCM kina wenyewe, shangilia ushindi unakuja’.
Wakati wimbo huo ukipigwa, Kikwete aliamua kuucheza akiwa jukwaani huku akishangiliwa na wananchi waliokusanyika katika ofisi za CCM.
Hata hivyo, Rais Kikwete hakuzungumzia juu ya kuondoka  Lowassa ndani ya CCM, na kwenda kujiunga na Chadema kisha kuteuliwa kugombea urais kupitia umoja huo.
Alisema dunia nzima inajua maendeleo mazuri yaliyofikiwa kupitia utawala wake na kwamba katika kampeni watakwenda kuwaeleza wananchi mambo mazuri yaliyofanywa.
Alijivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika utawala wake na kusisitiza kuwa anaondoka madarakani huku akiiacha nchi ikiwa na amani, umoja na mshikamano.
Wakati wa kwenda kuchukua fomu ya kugombea urais, Dk. Magufuli jana aliambatana na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), huku wakisindikizwa na viongozi mbalimbali waandamizi wa CCM.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...