Je,Lazio watafuta uteja wa kutoifunga Juventus katika Serie A kwa miaka 12?
Lazio hawafanyi vizuri katika Ligi ya Italia kwa msimu huu kwani wanashika nafasi ya 10 katika Ligi wakiwa na pointi 19 katika michezo 14 waliyocheza mpaka sasa.
Kocha wa Lazio Stefano Pioli yupo katika wakati mgumu sana na inawezekana kufungwa na Juventus hii leo ikawa mechi yake ya mwisho kuiongoza Lazio msimu huu.
Juventus wanarudi katika mji wa Roma kwa mara ya pili kwani tayari wamekwishacheza katika mji huo dhidi ya AS Roma na Juventus kufungwa magoli 2-0 katika uwanja wa Olimpico.
Safari hii Juventus wataendaje katika mji wa Roma?
Mpaka sasa klabu ya Lazio imepoteza michezo saba ya Ligi kwa msimu huu ambayo ni mingi tofauti na msimu uliopita ambapo timu hiyo ilipoteza michezo 11 tu katika michezo 38 ya Ligi ya Italia.
Kukosekana kwa beki wake wa kati Stefan De Vrij kumeonekana kuwa pengo kwa Lazio kwani mabeki wawili wa kati wa sasa Santiago Gentiletti na Mauricio hawajaweza kutengeneza ushirikiano mzuri ’chemistry’ nzuri baina yao na hivyo Lazio kuruhusu magoli 22 katika michezo 14 mpaka sasa.
Ubora wa kiungo Lucas Biglia unaweza kuwa chachu ya Lazio kupata matokeo hii leo kwani anaonekana anaweza kupambana na wachezaji wa kariba ya Claudio Marchisio,Stefano Sturaro na Mario Lemina.
Lakini pia Biglia ndiye mchezaji aliyepiga pasi nyingi sahihi ‘complete pass’ kwa Lazio kutoka eneo moja la uwanja kwenda eneo lingine la uwanja akiwa na asilimia 81.6 ya kupia pasi sahihi.
Silaha nyingine ya Lazio itakuwa kwa mshambuliaji raia wa Brazil Felipe Anderson ambaye ameonekana kuwa muhimili kwa Lazio hasa katika ushambuliaji.
Felipe Anderson ana magoli 4 mpaka sasa katika Serie A ingawa tatizo lake kubwa ni kuwa hana muendelezo mzuri wa uchezaji wake na hii imekuwa ikiwapa Lazio wakati mgumu sana kupata matokeo kutokana na ubutu wa safu yao ya ushambuliaji.
Miloslav Klose hayupo katika fomu yake lakini pia nyota wengine wa Lazio kama Eddy Onazi ,Stefano Mauri na Senad Lulic wataendelea kukosekana hii leo kwa sababu ni majeruhi.
Jambo la kusikitisha kwa upande wa klabu ya Lazio ni kuwa klabu hiyo imepata ushindi wa Serie A mara ya mwisho tarehe 25/10/2015 katika mchezo dhidi ya Torino kwa ushindi wa magoli 3-0.
Baada ya hapo Lazio haijashinda mchezo wowote wa Ligi Kuu ya soka nchini Italia mpaka sasa.
Kwa upande wa Juventus hakuna shaka kuwa fomu ya Paulo Dybala mwenye magoli 6 na asisti 3 imeifanya safu ya ushambuliaji ya Juve kuwa na makali kwa siku za hivi karibuni.
Kwani Juventus imeshinda michezo minne iliyopita ya Ligi ya Italia ikifunga magoli 9 na kufungwa magoli 2 tu.
Hapo kabla kocha wa Juventus Allegri hakuonekana kumpa nafasi Dybala huku akijitetea kuwa mchezaji huyo bado hajakomaa kuweza kuanza kikosi cha kwanza.
Kutokuwepo kwa Paul Pogba katika mchezo wa kesho kunaweza kumpa nafasi kiungo Stefano Sturaro kucheza sambamba na Claudio Marchisio na Mario Lemina.
Kiungo Sami Khedira hajasafiri na timu na badala yake kiungo wa timu ya taifa ya Ghana Kwawdo Asamoah amejumuishwa katika kikosi kilichosafiri kwenda kucheza na Lazio leo.
Msimu uliopita Juventus walipata ushindi wa magoli 3-0 mbele ya Lazio katika uwanja wa Olimpico.Mara ya mwisho kwa Lazio kushinda mchezo wa Ligi kuu ya Italia dhidi ya Juventus ilikuwa tarehe 6 Desemba mwaka 2003 waliposhinda kwa magoli 2-0.
Magoli ya Lazio ya wakati huo yalifungwa na Bernardo Corradi na Stefano Fiore.
Naamini mashabiki wa soka wana kila sababu ya kuutazama mchezo huu na kujua kama Juventus imerudi katika makali yake au itakuwa ndio mwisho wa kocha wa Lazio Stefano Pioli.
No comments:
Post a Comment