Rais wa Uchina Xi Jinping amesema taifa lake litatoa ufadhili wa dola bilioni 60 kwa nchi za Afrika.
Tangazo
hilo amelitoa kwenye mkutano mkuu wa ushirikiano kati ya Uchina na nchi
za bara Afrika, ambao umeanza leo jijini Johannesburg. Viongozi kadha
wa mataifa ya Afrika wanahudhuria.Tangazo la fedha hizo za mabilioni ya dola ambazo zitatolewa kupitia ruzuku, mikopo na ufadhili wa miradi ya maendeleo lilisubiriwa, lakini kiasi cha fedha kilichoahidiwa kimezidi matarajio, mwandishi wa BBC aliyeko Afrika Kusini Karen Allen anasema.
Sehemu kubwa ya usaidizi huu wa kifedha sana utatolewa kupitia miradi ya miundo mbinu, kusaidia kusisimua ukuaji wa kiuchumi, lakini maelezo zaidi hayajatolewa.
Kiongozi mwenza wa mkutano huo Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesifu ushirikiano kati ya Uchina na nchi za Afrika.
Amesema watu wanaoishi Uchina na Afrika ni theluthi moja ya watu wote duniani, na kwamba hilo ni soko kubwa la bidhaa.
Uchina, nchi yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, imetoa msururu wa mikopo kwa nchi za Afrika, ambazo nazo huuzia taifa hilo mafuta na bidhaa nyingine muhimu.
Hata hivyo, idadi ya bidhaa ambazo mataifa hayo huuzia Uchina imekuwa ikipungua.
Uwekezaji wa Uchina Afrika ulishuka asilimia 40 nusu ya kwanza ya mwaka huu, kwa mujibu wa wizara ya uchumi ya Uchina.
Ziara ya Bw Xi barani Afrika imetazamwa na wengi kama hatua ya kuyahakikishia mataifa ya Afrika kwamba Uchina itaendelea kuwekeza katika bara hilo licha ya kupungua kasi kwa ukuaji wa uchumi wa Uchina.
Mapema wiki hii Uchina na Afrika Kusini zilitia saini mikataba na mikopo ya thamani ya $6.5bn (£4.3bn), inayoangazia zaidi miundo mbinu.
Jumla ya mikataba 26 ilitiwa saini Jumatano, $2.5bn zikienda kwa shirika la reli la serikali.Kabla ya kutua Afrika Kusini, Bw Xi alizuru Zimbabwe Jumanne, ambako pia aliahidi taifa hilo mikopo ya kusaidia kuinua uchumi wake uliodorora.
No comments:
Post a Comment