WEZI
wa simu nchini watakuwa na wakati mgumu baada ya programu maalumu
kubuniwa. Programu hiyo inaweza kulinda taarifa zote za simu ya mteja
pamoja na simu yenyewe pindi ikiibwa, ambapo mwizi ataweza hadi kupigwa
picha bila mwenyewe kutambua.
Programu
hiyo iliyobuniwa na Mtafiti wa kitanzania, Godfrey Magila kupitia
Kampuni yake ya Magila Technologies, itakuwa ikitumiwa na kampuni ya
simu za mkononi ya Tigo Tanzania. “Programu hii ni maalumu kwa wateja wa
kampuni ya simu za mkononi ya Tigo na inajulikana kama ‘Tigo backup’.
Imeshaanza
kutumiwa na wateja wa kampuni hiyo,” alisema Magila. Magila alisema
kuwa wateja wa Tigo, wanaweza kujiunga na programu hiyo ya ulinzi wa
taarifa zao zote za simu, ikiwa ni pamoja na simu yenyewe, ambapo simu
ikiibwa pia inaweza kupatikana kwa haraka.
Alisema
mara nyingi watu wamekuwa wakipoteza simu zao na taarifa zote katika
simu hizo, ikiwa ni pamoja na namba za simu, picha zao za kumbukumbu na
vitu vingine muhimu na simu zenyewe, hivyo alibuni kwa lengo la
kuwasaidia watanzania kulinda simu zao.
Kupitia
programu hiyo ya ‘Tigo Backup’, mtu anaweza kupata taarifa zake na simu
ikipotea, unaweza kutumiwa taarifa zote mahali ilipo simu yako na picha
ya mtu anayeitumia simu hiyo pasipo mwizi kujijua.
Akizungumzia
programu hiyo, Meneja Biashara na Maendeleo wa Dar Development
Bussiness Incubator (DTBI), Collin Gumbu alisema ubunifu wa programu
hiyo ni wa hali ya juu na una uwezo mkubwa huku akizitaka kampuni za
mawasiliano nchini kuwaunga mkono vijana wa Tanzania wanaobuni programu
za aina hiyo.
“Vijana
wamekuwa wakifanya utafiti na ubunifu wa programu za aina mbalimbali za
simu, ambazo kama kampuni za simu nchini zingeweza kuzinunua
zingewasaidia sana vijana wetu na kuweza kujiajiri huku wakiitangaza
Tanzania kimataifa katika sekta ya sayansi na teknolojia,” alisema
Gumbu.
Gumbu
aliipongeza kampuni ya simu ya Tigo kwa kuchukua programu hiyo na
kuomba kampuni nyingine nchini kuiga mfano huo. Akiwasiliasha mada
katika se mina ya siku moja, iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi
na Teknolojia (COSTECH) kwa wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es
Salaam, Gumbu alisema vikwazo vilivyopo katika baadhi ya kampuni,
huwarudisha nyuma vijana walio na nia ya ubunifu.
Alitaja
baadhi ya bidhaa ambazo zilibuniwa na watanzania na sasa zinafanya kazi
vizuri na kutoa ajira mbalimbali kwa watanzania kuwa ni pamoja na
MaxMalipo. Mbali na programu hiyo ya simu za mkononi, pia Magila amebuni
programu ambayo inawawezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika
upigaji kura.
Pia
programu ya simu ambayo inawawezesha wananchi kusikiliza bunge na
kushiriki katika mijadala ya Bunge moja kwa moja na kutoa maoni yao
wakati bunge likiendelea.
No comments:
Post a Comment