HABARILEO
Makatibu wakuu na Naibu Makatibu Wakuu walioteuliwa na kuapishwa juzi
wamekutana katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es Salaam kwa
ajili ya semina elekezi iliyoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mada zilizoandaliwa katika semina
hiyo jana, Katibu Mkuu Kiongozi Sefue, alisema semina hiyo ni ya kikazi
zaidi na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha viongozi hao waandamizi
wanatekeleza wajibu wa kusimamia utendaji kazi wa serikali vizuri.
Balozi Sefue alisema kila Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu anapaswa
kutambua kuwa nafasi yake ni ya maamuzi, hivyo serikali inatarajia kuona
wanafanya maamuzi kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu zinazomuongoza kila mmoja katika majukumu yake.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inawatarajia viongozi hao kuwa
wasimamizi wazuri wa fedha za umma na kwamba haitarajii kuwepo kwa hati
za ukaguzi wa mahesabu zenye kasoro.
Balozi Sefue aliongeza kuwa Makatibu Wakuu hao na Naibu Makatibu
Wakuu ni mamlaka ya nidhamu katika wizara zao, hivyo serikali haitarajii
kuona wanakuwa na kigugumizi katika kuchukua hatua dhidi ya watumishi
watakaokuwa na makosa.
Aliwakumbusha pia kwamba haikubaliki kwa mtumishi aliyefanya makosa
katika sehemu moja ya kazi, kuhamishiwa katika sehemu nyingine badala ya
kuchukuliwa hatua palepale alipo.
HABARILEO
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba amesema hakutakuwa na msamaha na huruma kwa watakaobainika kuhujumu sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini.
Nchemba alisema hayo baada ya kubaini kuwepo kwa utafunwaji wa mapato
ya serikali ya vibali vya mifugo, yanayokusanywa katika Mnada wa Pugu,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Alibaini kuwepo kwa hujuma hizo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza
ya kukagua mnada huo na machinjio ya Vingunguti yaliyopo Manispaa ya
Ilala juzi usiku.
Baadaye alitangaza hatua kadhaa, ikiwemo Mkuu wa Mnada huo wa Pugu na
watumishi waliokuwa zamu Desemba 24 mwaka jana na Januari Mosi mwaka
huu, kesho Jumatatu wafike ofisi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Pili, Mwigulu alisema kuanzia sasa amesitisha ukusanyaji wa ushuru
kwenye eneo la Mnada wa Pugu, badala yake makusanyo yote ya fedha za
Serikali, yatafanyika kwenye Machinjio la Vingunguti kwa kutumia mashine
za kielektroniki za Mamlaka ya Mapato Tanzania (EFDs).
Alisema mnada wa Pugu sasa utakuwa unatumika kutoa vibali tu vya
mifugo ili kudhibiti ubora wa mifugo inayotakiwa kuchinjwa. “ Sitakuwa
na huruma na hatua stahiki zichukuliwe kwa mtu yeyote mwenye dhamana ya
kusimamia sekta hiyo atakayebainika kutowajibika kwa mujibu wa Sheria,”
alisema.
Akizungumza katika machinjio hayo, Nchemba alisema ubadhirifu uliopo
ni wa uandikaji wa vibali kwa mifugo wachache kwa ajili ya kwenda
machinjioni, tofauti na idadi ya mifugo inayoingizwa machinjioni hapo.
Alisema mifugo mingi inaingizwa machinjioni bila kibali.
Katika ukaguzi huo, Mwigulu alibaini uwepo wa utafunwaji wa kodi ya
mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa ushuru,
kwa ajili ya kupelekwa katika machinjio hayo kutoka Mnada wa Pugu.
“Kwa hatua za awali nimekutana na ubadhirifu wa kutafunwa kwa
kodi ya mifugo zaidi ya 1,107 kwa siku, kati ya mifugo 1450 iliyolipiwa
ushuru kwa ajili ya kuja kwenye machinjio ya Vingunguti kutoka Mnada wa
Pugu Desemba 26,2015,” alisema.
Aidha, Nchemba alisema alisikiliza kero na maoni ya wananchi
wanaotumia machinjio hayo pamoja baadhi ya viongozi wenye dhamana na
kusimamia juu ya uendeshwaji wa machinjio hayo.
Nchemba aliagiza uongozi wa machinjio hayo, kukutana kwa ajili ya
kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kukiuka taratibu na sheria.
Uchinjaji wa ng’ombe na mbuzi katika machinjio hayo, hufanyika nyakati
za usiku kuanzia saa 4 hadi 10 alfajiri.
HABARILEO
Watu sita wamekufa papo hapo na wengine 25 kujeruhiwa na kulazwa
hospitalini kutokana na ajali mbili tofauti. Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema
mjini hapa jana kuwa ajali ya kwanza, ilihusisha basi la abiria
lililokuwa na abiria 42, ambalo liligonga kingo za daraja, likaparamia
miti miwili kisha kutumbukia ndani ya mto Lukosi, Iyovi eneo la Msosa
huko Mikumi wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, katika barabara kuu ya
Iringa – Morogoro.
Alisema tukio hilo ni la Januari Mosi mwaka huu majira ya saa 8
mchana. Basi hilo lilitokea Dar es Salaam, lilikuwa linakwenda Mbeya.
Kamanda Paulo alisema dereva wa basi hilo aliendesha gari kushoto zaidi,
akaenda kugonga kingo za daraja hilo, akaenda kuparamia miti miwili
kisha alilitumbukiza ndani ya mto huo.
Kamanda huyo alisema katika ajali hiyo, watu watatu walikufa akiwemo
dereva wa basi hilo na kujeruhi wengine 16, ambapo majeruhi 14 walilazwa
katika Kituo cha Afya cha Tandika kilichopo eneo la wilaya ya Kilolo,
mkoani Iringa. Majeruhi wengine sita walisafirishwa hadi Hospitali ya
Mkoa wa Iringa na kulazwa.
Kamanda alisema basi hilo lilibeba abiria 42 na chanzo za ajali hiyo
kilielezwa na mashuhuda kuwa ni uzembe wa dereva wa basi, aliyeshindwa
kufuata sheria za usalama barabarani katika eneo hilo la safu ya milima
ya Iyovi, lenye kona nyingi na mito yenye madaraja. Alisema maiti mmoja
ametambulika na ni dereva wa basi hilo.
Maiti wawili, mmoja mwanamume na mwingine mwanamke, bado
hawajatambuliwa na wamehifadhiwa katika chumba za maiti cha Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Alitoa mwito kwa watu kufika kuwatambua.
Kamanda huyo wa Mkoa alisema ajali ya pili ilitokea Januari Mosi
mwaka huu, ambapo watu watatu walifariki papo hapo na wengine watano
kujeruhiwa na kulazwa katika Kituo cha Afya cha Gairo wilayani Gairo
mkoani Morogoro.
Alisema ajali hiyo ilihusisha gari ndogo, lenye namba za usajili T
252 CGV aina ya Toyota Vitz, lililokuwa likiendeshwa na Bundala Charles
Mahimbo, mkazi wa Dar es Salaam. Gari hilo liligongana uso kwa uso na
lori, lenye namba za usajili T531 CFE lenye tela namba T 509 AFY aina ya
Scania, lililokuwa likiendeshwa na dereva, Ally Said Magimbi (33),
mkazi wa Mtongani , Dar es Salaam.
Alisema ajali hiyo ilitokea jioni eneo la Ngiroli wilayani Gairo
barabara kuu ya Morogoro- Dodoma. Gari ndogo lilikuwa likitokea Mkoa wa
Tanga kwenda Mwanza wakati lori kubwa lilitokea Kagera kwenda Dar es
Salaam.
Kamanda Paulo alisema watu watatu waliokuwa katika gari ndogo,
walikufa papo hapo na wengine watano walijeruhiwa, miongoni mwao mmoja
ni abiria wa lori. Kamanda huyo wa Polisi aliwataja waliokufa katika
ajali hiyo ni Bundala Mahimbo ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, Flora
Mugabo na Emmanuel Mahimbo, wote wakazi wa Nyakato mkoani Mwanza.
Majeruhi waliolazwa Kituo cha Afya Gairo ni dereva wa lori, Ally
Magimbi, mkazi wa Mtongani Dar es Salaam, Peter Mahinda ambaye ni mkazi
wa Nyakato na Hassan Mwera. Walioruhusiwa ni Judith Joseph na Scolastica
Fransis aliyekuwa abiria kwenye gari kubwa.
HABARILEO
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) wiki ijayo
inakutana na wadau kujadili nauli zitakazotumika kwa mabasi yaendayo
kasi.
Kwa sasa kampuni ya UDA-RT inapendekeza nauli ya chini kuwa Sh 700 na wanafunzi kulipa nusu yake.
Aidha, katika mapendekezo yake, UDA-RT inataka nauli ya safari kwenye
njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh
1400 na wanafunzi nusu ya nauli hizo.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra
ilisema maombi hayo kwa ajili ya kutoa huduma za mpito za usafiri wa
mabasi yaendayo haraka katika awamu ya kwanza ya mradi wa DART
yatajadiliwa na wadau ili kuona uhalali wake.
Ilisema kwa mujibu wa sheria, Sumatra inapaswa kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kuridhia viwango vya nauli.
“Katika kutekeleza hilo, mamlaka imeandaa mkutano ili kupokea maoni
ya wadau ikiwa ni pamoja na watoa huduma, watumiaji wa huduma na
wananchi kwa ujumla,” ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo wa wadau utafanyika Januari
5, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuanzia saa
tatu asubuhi ambapo wadau wote wa usafiri wanaalikwa.
MWANANCHI
Kasi ya Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano jana ilichukua sura ya
aina yake wakati mawaziri watatu walipoibuka kwenye machinjio ya
Vingunguti, na kutoa maamuzi magumu kutokana na kukithiri kwa uchafu,
ubadhilifu wa makusanyo ya fedha za ushuru.
Wakiwa katika eneo la machinjio hayo mawaziri hao, Mwigulu Nchemba
(Kilimo, Mifugo na Uvuvi), Dk Hamisi Kigwangalla (Afya), na George
Simbachawene (Ofisi ya RaisTamisemi), walishuhudia hali ya uchafu wa
eneo hilo na baadaye kubaini ubadhilifu mkubwa.
Baada ya kufanya ziara hiyo iliyoanza saa 4:47 asubuhi na kumalizika
saa 5:32, mawaziri hao hawakuridhishwa na hali ya usafi kwenye maeneo ya
kuwekea nyama.
Mbali na hayo walisikiliza kero za wadau ambao ni wachinjaji na
wauzaji wa mifugo, waliodai wanatozwa ushuru mkubwa kama malipo ya
Sh11,000 kwa ng’ombe mmoja, fedha ambazo hulipwa mnada wa Pungu
(sh6,000) na Vingunguti (Sh5,000).
Catherine Severine, ambaye ni mchuuzi aliyekuwa zamu usiku wa Desemba
24 mwaka jana, aliwaambia mawaziri hao kuwa kumekuwepo udanganyifu wa
utoaji wa vibali kwenye mnada wa Pugu.
Alidai kuwa siku hiyo walifikishwa mbuzi 1,407 huku wenye vibali
wakiwa 300 , ng’ombe 700 lakini wenye vibali halali 492, hivyo kwa
hesabu za haraka, zaidi ya Sh3.4 milioni zilipotea.
Alisema kwa ujumla wanatakiwa wakusanye kiasi cha Sh75 milioni kwa
mwezi, lakini walikuwa wanakusanya Sh18 milioni huku Sh55 milioni
zikiingia mifukoni mwa wajanja. Simbachawene alimpa siku tatu mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala kuwaondoa wale wote waliokaa muda mrefu katika
eneo hilo na kujimilikisha kila kitu.
“Kigwangalla naomba usitufungie, Jumanne nitataka kupata maelezo ya
waliohusika na haya mabanda. Si kweli kwamba yamegharimu Sh100 milioni.
Hadi Jumatatu umeme uwe umerudishwa kwenye hayo mabanda, yatumike ili
kupunguza mbanano,” aliagiza Simbachawene.
Mwigulu aliwataka wote waliokuwepo mnadani Desemba 24, kufika kwa
katibu mkuu wa Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Jumatatu na kuanzia leo
waanze kutafuta kazi ya kufanya kwa sababu ya kujumlisha ng’ombe na
mbuzi imewashinda.
Mwigulu alisema hayo baada ya juzi usiku kukuta machinjio ya
Vingunguti kuna vibali 300 vya mbuzi, lakini kukiwa na mbuzi zaidi 1,000
na ng’ombe zaidi ya 200 hawakuwa na vibali, kitu alichosema kinaashiria
wanafanya makusudi siyo kwamba hawajui kujumlisha.
“Kuanzia sasa vibali vyote vya wanyama wanaotakiwa kuchinjwa hapa,
vitolewe kwenye mnada wa Pugu, huku wakusanya ushuru wa Serikali Kuu na
Halmashauri watakusanya hapa katika machinjio ya Vingunguti.
Mnaolipia ushuru hakikisheni mnaondoka na risiti, lango la kuingizia
ng’ombe lijengwe mara moja hata matatu, manne tena kwa fedha
inayopatikana hapa hapa machinjioni,” alisema Mwigulu huku
akishangiliwa.
Kigwangalla alisema anakubali ombi la Simbachawene la kutaka
wasifungiwe kwa muda na watavamia wakati wowote kukagua maagizo
waliyotoa kama yanafanyiwa kazi. Alisema mambo aliyoyaona akiwa katika
Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa miaka miwili
iliyopita ndiyo aliyoyakuta jana , hivyo hatawavumilia wanaohusika.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi limemkamata raia wa Nigeria kwenye Uwanja wa Ndege wa
Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya
ambazo thamani yake ni kubwa ingawa haijajulikana.
Kamanda wa polisi wa JNIA, Martin Ottieno alisema mtuhumiwa huyo, Ejiofor Ohagwu,
alikamatwa na kilo nne za dawa hizo ambazo alisema licha ya kutofahamu
thamani yake kwa sasa, inaweza kuwa kubwa kwa sababu hawajawahi kukamata
dawa za kiwango hicho.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, kilo moja ya heroin kwa bei ya
mitaani ni kuanzia Sh90 milioni. Ottieno alisema mtuhumiwa huyo
alikamatwa saa 8:00 usiku wa kuamkia jana kwenye sehemu ya ukaguzi ya
eneo la wasafiri wanaoondoka.
Alisema awali polisi walipata taarifa za kiintelijensia kuhusu Ohagwu
na alipopekuliwa alikutwa na dawa alizodai kuwa ni heroin zilizofungwa
katika pakiti sita za plastiki.
“Mtuhumiwa huyo alikuwa anasafiri kuelekea mji wa Lagos, Nigeria,
akitumia Shirika la Ndege la Ethiopia,” alisema. “Dawa hizi alizificha
kitaalamu kwa kushonea pakiti zote pembeni mwa mabegi yake mawili ya
nguo ili asibainike haraka na vyombo vya dola.” Alisema polisi bado
inamshikilia mtuhumiwa huyo na upelelezi utakapokamilika, atafikishwa
mahakamani kujibu mashtaka.
Pia, alisisitiza kuwa kwa sasa viwanja vya ndege si vichochoro vya
kupitisha dawa hizo, kwa kuwa polisi ikishirikiana na wadau wengine,
imejipanga kupambana na aina hiyo ya uhalifu.
“Mbali na kuwakamata hawa, pia tumelenga kuwakamata mapapa wanaoagiza dawa hizi, ”
alisema Kamanda Ottieno. Desemba 17 mwaka jana, Waziri wa Mambo ya
Ndani, Charles Kitwanga alikutana na maofisa wa polisi wa Kanda ya Dar
es Salaam na kutaka wamueleze mipango ya kukabiliana na dawa za kulevya.
MWANANCHI
Wakati watu mbalimbali wakimminia sifa Rais John Magufuli kwa kubana matumizi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga amesema uwingi wa makatibu wakuu unakinzana na dhana ya yake ya kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri.
Lakini naibu waziri huyo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne amesifu
hatua mbalimbali za kupambana na ufisadi anazochukua Rais Magufuli
akisema amefanikiwa kutumbua majibu, lakini sasa anatakiwa awe na
ubunifu katika kutatua matatizo ya wananchi.
Dk Mahanga alikuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira tangu mwaka 2008 na
hakuwahi kuhamishwa wala kupandishwa hadi ngazi ya uwaziri hadi Serikali
ya Rais Jakaya Kikwete ilipomaliza muda wake na baadaye kujiunga na
Chadema.
Akizungumza na Mwananchi jana, mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la
Segerea (CCM) alisifu kazi inayofanywa na Rais Magufuli akisema
inaonekana wazi. “Kweli ametumbua majipu ambayo hakika yalikuwa
yameiva,” alisema Dk Mahanga. “Naweza kusema alikuta nyumba chafu na
inanuka, ameisafisha.
Sasa tunapenda kuona baada ya kusafisha ataiweka katika hali gani?
Atabuni nini ili kuwasaidia vijana dhidi ya tatizo la ajira ili wengi
waweze kumudu gharama za maisha.
” Lakini katika waraka wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Dk
Mahanga alimkosoa Rais Magufuli akisema ameongeza ukubwa wa Baraza la
Mawaziri baada ya kuteua makatibu wakuu 27 wakati anawaaminisha wananchi
kwamba wizara ni 15 tu.
Dk Magufuli ameunda baraza lenye mawaziri 15, na manaibu waziri 19 na
hivyo kufanya baraza lake kuwa na jumla ya mawaziri 34, tofauti na
baraza lililopita lililokuwa na mawaziri 55. Uamuzi wa kupunguza idadi
ya wizara ulikumbana na changamoto ya nafasi za makatibu, ambao hata
hivyo baadhi amewarudisha wizarani ambako watapangiwa kazi na kubakiwa
na makatibu 27.
“Si kweli kwamba kapunguza ukubwa wa Serikali, bali kaongeza
ukubwa wake. Sina hakika kama wasaidizi wa Rais wamemshauri na kumweleza
kwamba wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu,” alisema Dk Mahanga akifafanua kuwa katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu wa wizara na afisa masuhuli.
Alisema katibu mkuu ndiye mwenye dhamana ya utendaji na ndiyo maana
hata katika ngazi ya kata, ofisi inaitwa ofisi ya ofisa mtendaji wa kata
na si ofisi ya diwani.
Kwa maana hiyo, Dk Mahanga, ambaye kitaaluma ni mhasibu, alisema Rais
alipounda Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambazo awali zilikuwa
mbili tofauti na kuteua makatibu wakuu watatu, kiuhalisia hakuunganisha
wizara mbili kuwa moja bali ameunda wizara tatu kutoka mbili za awali.
“Ongezeko la gharama kwa kuongeza waziri mmoja ni ndogo sana
kulinganisha na kuongeza katibu mkuu mmoja.
Waziri anapoteuliwa tayari anakuwa ni mbunge mwenye mshahara wake wa
ubunge na kinachoongezeka ni kama laki tano tu juu ya ule mshahara wa
ubunge na gharama nyingine ndogo za gari, pia mishahara na gharama za
katibu muhtasi, msaidizi na dereva,” alisema Dk Mahanga.
Alisema kwa ujumla ahadi ya Rais Magufuli aliyotoa kwenye kampeni
kwamba ataunda Serikali ndogo, hakuitimiza badala yake ameongeza ukubwa
wa Serikali.
Wakati wa kampeni na alipoapishwa, Rais Magufuli alisema ataunda
baraza dogo la mawaziri, hiyo ilijenga shauku kwa wananchi kufahamu
kiwango cha ukubwa au udogo wa baraza hilo ikilinganishwa na mabaraza
yaliyoundwa na watangulizi wake, tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.
Dk Magufuli pia alitoa ahadi hiyo alipozindua Bunge Novemba mwaka jana
mjini Dodoma.
MWANANCHI
Wingu zito linaendelea kutanda kwenye anga za siasa visiwani hapa
baada ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kusema mchakato wa
kupanga bajeti kwa ajili ya marudio ya uchaguzi umekamilika, huku CUF
ikishangazwa na kupinga tamko hilo.
Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein na katibu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad
wako kwenye mazungumzo ya kujadili kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa
Rais, wawakilishi na madiwani na hadi sasa hawajatoa tamko la maendeleo
ya mazungumzo yao.
Lakini viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa taarifa za kuwataka wafuasi
wao wajiandae kwa marudio ya uchaguzi, huku CUf ikisema inachosubiri ni
kutangazwa kwa mshindi wa uchaguzi wa Rais na haiku tayari kurudia
uchaguzi.
Kauli nyingine ya namna hiyo ilitolewa jana na juzi na Balozi Seif
alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya sherehe za
kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, akisema kwa kuwa matokeo ya
uchaguzi yalifutwa basi ni wazi kuwa hakuna utaratibu ambao
utakaofanyika wa kuyamaliza matokeo yaliobaki isipokuwa kurudia uchaguzi
upya.
“Tuache kusikiliza maneno ya porojo bali nawaambia suala la
kurudia uchaguzi lipo kama kawaida na kilichobaki sasa ni kusubiri amri
ya Tume (ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)) kutangaza siku ya uchaguzi huo,” alisema Balozi. “Kwa upande wetu CCM tupo tayari kushiriki uchaguzi huo.
Hata kama CUF hawatashiriki, sisi hawatubabaishi.” Kwa upande wa
mazungumzo yanayofanyika Ikulu kwa kuwashirikisha viongozi wa wakuu wa
Serikali, Balozi alisema kuwa hajui nini kinaendelea hadi sasa, lakini
akawataka wananchi wasubiri taarifa rasmi mazungumzo hayo
yatakapomalizika.
“Kikubwa zaidi nilichokisikia mimi katika mazungumzo hayo ni suala la
kudumisha amani na utulivu ila kwa upana zaidi tusubiri mazungumzo hayo
yatakapomalizika taarifa itatolewa kwa wananchi wote,” alisema.
Lakini kwa mara nyingine, CUF walipinga vikali kauli hiyo wakisema
hawako tayari kurudia uchaguzi. Kaimu mkurugenzi wa habari, uenezi na
mawasiliano ya umma wa CUF, Ismail Jussa alisema matamko hayo
yanashangaza wakati bado mazungumzo yanaendelea.
Jussa alidai kuwa kuna timu imejifungia mahali inafanya hujuma na
inampotosha Dk Shein. Kuhusu sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar,
Balozi Seif alisema kutoshiriki kwa viongozi wa CUF hakutaathiri sherehe
hizo.
Alisema kamati ya maadalizi ya sherehe na mapambo tayari
imeshajipanga vya kutosha na kilichobaki ni ufanikishaji wa maadhimisho
hayo ambayo shamrashamra zake zilitarajiwa kuanza jana.
Alisema madhimisho hayo yapo kama kawaida na mwaka huu wamepanga siku
ya kwanza ya shamrashamra zake kuitumia kufanya usafi wa mazingira ya
mji wa Zanzibar.
Alisema kuwa shamrashamra nyingine za maadhimisho hayo zitaendelea kama kawaida kwa kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7
KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...
-
C9 Records presents STAR by Foby!. Click DOWNLOAD button bellow to download this song.
-
John ana mke ambaye haoni uzuri wa kitu chochote anachofanya, akifika tu nyumbani mke wake huanza kumlalamika kuwa hela anayoacha nyumba...
-
Mboga za majani na matunda zimekuwa zikisisitizwa kwa sana na wataalamu wa afya hasa kwa wanawake wajawaziti kwani zimekuwa zikiongeza Damu...
No comments:
Post a Comment