18 October, 2016

Mil. 130/- Simba, Yanga zashikiliwa

JUMLA ya Sh. milioni 130 ambazo ni mapato wanayostahili kupata klabu za Simba na Yanga kutokana na mechi yao ya Oktoba Mosi, mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa, zinaendelea kushikiliwa
na Kampuni ya Selcom Tanzania.
Kias hicho ni baada ya kuondolewa kwa makato mengine yote muhimu kwenye mapato ya jumla ya mchezo huo ulioingiza Sh. milioni 320 wakati timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1.

Habari za ndani zinaeleza kuwa fedha hizo  zimezuiwa kwa maelekezo ya serikali kufuatia uharibifu uliojitokeza katika mchezo huo kwa mashabiki wanaodaiwa kuwa wa  Simba kuvunja viti. 

Taarifa zinaeleza kuwa serikali imezuia fedha hizo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika juu ya hasara iliyojitokeza, ambayo kimsingi Simba wamekubalikulipa.Habari zinaeleza kuwa uharibifu uliofanywa na Simba unakaribia kuwa wa Sh. milioni 400.

Makato ambayo yamekwishaondolewa kwenye mapato hayo ni pamoja na asilimia18 ya VAT, asilimia 15 ya gharama za uwanja, asilima 9 ya Bodi ya Ligi, asilimia 5 ya TFF, asilimia 3 ya DRFA na asilimia 8 ya gharama za mchezo.

 Wenyeji Yanga wanastahili kupewa asilimia 40 ya mapato hayo wakati asilimia 20 ni za waliokuwa wageni, Simba. Tayari Simba wameandika barua TFF kuomba wapatiwe mgawo wao wa mchezo huo kwa kuwa wanahitaji fedha za kujiendesha kwa wakati huu na deni hilo watalipa taratibu.

Uharibifu huo ulitokana na mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba kukerwa na bao la kuongoza la dakika ya 26 lililofungwa na mshambuliaji Mrundi Amissi, ambaye aliumiliki mpira kwa mkono kabla ya kuuzamisha nyavuni, lakini mwamuzi akalikubali.

Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu nahodha wa Simba, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa madai ndiye aliyekuwa mstari wa mbele. Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba iliposawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.

Tayari TFF imeipiga Simba faini ya Sh. milioni tano huku Mkude akifutiwa kadi hiyo.

CHANZO: Nipashe

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...