18 October, 2016

Azam vs Mtibwa kupigwa usiku Chamazi kesho

MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar ya Morogoro utapigwa kesho usiku katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga, aliliambia Nipashe jana kuwa wameomba mchezo huo ufanyike usiku na wanashukuru ombi lao limekubaliwa na Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 

“Wenzetu wa Azam TV kwa sababu za kuweza kuonyesha moja kwa moja mechi nyingi za Jumatano, wakaomba mchezo wetu tuusogeze Saa 1:00 usiku, nasi tumekubali,”alisema Maganga. 

Azam iliyo chini ya benchi la Ufundi la wataalamu kutoka Hispania linaloongozwa na Zeben Hernandez Rodriguez, itaingia katika mchezo wa kesho ikitoka kutoa sare ya 0-0 na Yanga juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Azam FC imefikisha pointi 12 baada ya kucheza mechi tisa, ikitoa sare tatu baada ya kufungwa mechi tatu na kushinda tatu – wakati Simba SC yenye pointi 23 za mechi tisa kutokana na kushinda mara saba na sare
mbili, inagonoza Ligi Kuu. 


Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Jumatano na mbali na Azam na Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Ndanda FC wataikaribisha Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Prisons watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Mechi nyingine za Jumatano, Toto Africans watawakaribisha baba zao, Yanga Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, African Lyon wataikaribisha Majimaji Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Alhamisi Simba watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Uhuru na JKT Ruvu wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mabatini.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...