21 October, 2016

Matumaini mapya 66,000 waliotoswa Bodi Mikopo

KUNA matumaini mapya kwa wanafunzi 66,500 waliokosa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo ulioanza mwezi huu.
Rais wa Daruso, Erasmi Leon, akizungumza na waandishi wa habari nje
 ya jengo la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
 jijini Dar es Salaam jana.
 Matumaini hayo yanakuja baada ya kupatikana kwa habari kwamba Kamati ya Bunge ya  Maendeleo na Huduma za Jamii imeweka kwenye ratiba yake ya shughuli za kamati, suala la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Maelezo ya mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Zitto Kabwe aliyotoa jana kupitia mtandao mmoja wa kijamii ilisema "kamati itashughulia suala hilo kuanzia Jumatatu, kwa mujibu wa ratiba niliyoona." 

"Natumai tutapata jawabu la wanafunzi walikosa mikopo."

 Bodi ya Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu (HESLB) ilitangaza juzi kuwa itatoa mikopo kwa wanafunzi 21,500 tu kwa mwaka 2017/2017 hivyo kuacha 'vilio' kwa maelfu ya wanafunzi wanaotakiwa kusomea shahada katika vyuo mbalimbali nchini.

 Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema juzi kuwa kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo hiyo, wanatarajia kutoa fedha hizo kwa 21,500 tu ambao "wamekidhi vigezo".

Kutokana na takwimu hizo, ni dhahiri wazazi ama walezi wa wanafunzi 66,500 watalazimika kuingia mifukoni kulipia gharama za elimu hiyo kwa watoto wao.

Aidha, mpaka sasa HESLB imetoa majina ya wanafunzi 3,966 ambao ni wanufaika wa kwanza wa mkopo kwa mwaka huu wa masomo.

Mwaka wa masomo uliopita bodi ilitoa Sh. bilioni 459 kwa wanafunzi 122,486, kati yao 53,618 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza na 68,916 ni waliokuwa wakiendelea na masomo yao.

Taarifa ya Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),
ilisema zaidi kuwa "wajibu wa serikali yoyote duniani ni kuhakikisha
kuwa watu wake wanapata elimu.


"Serikali inayoshindwa kusomesha watu wake haina haki ya kutawala." Kamati ya Bunge ya Maendeleo na Huduma za Jamii ipo chini ya uenyekiti wa Peter Serukamba ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM).

VIGEZO VIPYA
Akizungumza na gazeti hili juzi, Badru alisema wanafunzi watakaopata mikopo hiyo ni wale waliokizi matakwa ya vigezo vipya vya mikopo vilivyotangazwa na serikali hivi karibuni.

Alisema wameanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea tangu juzi.

Alisema HESLB inatoa mikopo hiyo kulingana na kalenda za vyuo husika, na kwamba kwa juzi walitoa kwa vyuo vikuu vilivyokwisha fungua kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema hali ya kifedha katika HESLB ni nzuri na wanafunzi wapatao 21,500 wanatarajia kunufaika na mikopo.

“Siyo kila mwanafunzi aliyedahiliwa anaweza kupata mkopo, wengine wamedahiliwa lakini wanauwezo wa kujisomesha, hivyo tutatumia vigezo mbalimbali katika kutoka mikopo,” alisema Badru.

Mbali na UDSM, Badru alisema vyuo vingine ambavyo kwa awamu ya kwanzavimepata fedha ni pamoja na Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), Chuo Kikuu ChaMtakatifu Agustino (Saut), Chuo Kikuu cha Mzumbe (Muse), Chuo Kikuu cha Ardhi, Taaisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Hata hivyo, Ofisa Mikopo wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino
Tanzania (SAUT), Mwanza, Wilfred Medadi alisema hadi kufikia juzi walikuwa hawajapokea fedha zozote kutoka HESLB.


Alisema Jumanne chuo kilipokea fedha za ada za wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu za mwaka jana, na kwamba taarifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo bado hazijarudishwa chuoni hapo kutoka HESLB.

CHANZO: Nipashe

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...