28 September, 2016

Simba v Yanga Jumamos Rekodi zitaongea


JUMAMOSI ya wiki hii, yaani Oktoba 1, 2016, nyota wa zamani wa soka ulimwenguni, Mliberia George Opong Weah, atakuwa akisherehekea miaka 50 tangu kuzaliwa kwake, lakini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kutakuwa na habari nyingine wakati mahasimu wakuu wa soka Tanzania, Yanga na Simba, watakapokuwa wakivaana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

George Weah ndiye mchezaji wa kwanza kutoka barani Afrika kutunukiwa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, yaani tuzo ambayo mpaka leo hii hakuna mchezaji yeyote wa Kiafrika aliyewahi kuipata.

Nakumbuka ilikuwa mwezi Desemba, mwaka 1995, ambapo FIFA iliitangazia dunia ya soka kuwa Weah amechaguliwa kwa kupigiwa kura kuwa mwanasoka bora wa dunia.

Ni katika mwaka huo, George Weah akawa Mwanasoka Bora wa Ulaya na haikuishia hapo, akatangazwa pia kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika! Ndani ya mwaka mmoja, akajikusanyia mataji matatu.

Hapana shaka haya ni mafanikio yasiyo na mifano katika historia ya soka barani Afrika. Weah ni alama ya soka ya Liberia. Aliwahi kutoa misaada kwa timu ya taifa ya Liberia iliyokuwa na hali duni ili iweze kucheza michuano ya Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika, hii ilichangia kumfanya aheshimiwe zaidi na wananchi wa nchini humo.

Nakumbuka mara baada ya kutunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa dunia, Weah aliwahi kuibeba timu yake ya Taifa akiwa ndiye nahodha wa kikosi hicho kwa gharama zake yeye mwenyewe, ambapo aliambatana na kikosi hicho kwa ajili ya mchezo wa kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania.

Watanzania wengi walikuwa wagumu sana kuamini kuwa yeye ndiye hasa alikuwa George Weah. Kila alichokuwa akikifanya pale Sheraton Hotel (sasa Serena Hotel), kilionekana kushuhudiwa na Watanzania wengi waliokuwa wakimshangaa.

Ukiachana na stori ya Weah ambaye Jumamosi anatimiza umri wa miaka 50, Simba na Yanga zitakutana siku hiyo ikiwa ni siku ya 275 ya mwaka kati ya siku 366, lakini ni baada ya siku 237 tangu zilipopambana mara ya mwisho Februari 20, 2016 katika mchezo wa marudiano msimu uliopita ambapo Simba ililala kwa mabao 2-0.

Kabla ya hapo, Septemba 26, 2015 kwenye uwanja huo huo, Yanga pia waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, wakilipa kisasi cha kufungwa ‘bao la kizembe’ na pekee Machi 8, mwaka huo, lililopachikwa kimiani na Emmanuel Okwi.

Kinachosubiriwa na mashabiki wa soka hapa nchini ni kuona ni timu ipi kati ya Yanga na Simba itakayosherehekea ushindi na kuungana na Weah kwenye ‘birthday’ yake Jumamosi hii, ni jambo lililo gumu kutokana na rekodi ya timu hizo mbili, ambazo kimsingi ndizo zilizoleta mwanga wa soka nchini.

Tangu Simba ilipozinduka kutoka katika kufanya vibaya kwenye ligi na hatimaye kukalia usukani mpaka sasa, kumekuwa na mhemko mkubwa baina ya timu hizo mbili, mashabiki na wanachama wake wakitambiana kwamba timu yao itaibuka na ushindi.

Lakini kelele hizo zitahitaji pia kuangalia matokeo ya uwanjani yakoje, vinginevyo upande mmoja unaweza kuzizima.

Matokeo baina ya mechi hizo daima huwa hayatabiriki na tangu Simba walipoibamiza Yanga kwa mabao 5-0 Mei 6, 2012, wamevuna ushindi mmoja tu wa Machi 8, 2015 wakati Okwi alipopachika bao la pekee, huku kipa wa Yanga, Ali Mustafa Barthez akiwa ametoka langoni.

Itakumbuka kwamba, baada ya kipigo kile cha aibu kwa Yanga, timu hizo zilikutana mara nane, Yanga ikishinda mara tatu na Simba mara moja, huku zikitoka sare mechi nne.

Zilipokutana Oktoba 3, 2012 zilitoka sare 1-1, mechi ya Mei 18, 2013 Yanga wakashinda 2-0, Oktoba 20, 2013 timu zikatoka sare ya 3-3, Aprili 19, 2014 sare ya 1-1 na Oktoba 18, 2014.

Machi 8, 2015 ndipo Simba iliposhinda, lakini Septemba 26, 2015, Yanga ikapata ushindi wa 2-0 kama ilivyofanya tena Februari 20, mwaka huu.

Simba inaingia uwanjani ikiwa na washambuliaji wapya ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali, akina Laudit Mavugo, Shiza Kichuya na Ibrahim Ajib, lakini Yanga inao wachezaji wake wote wawili walioipa ushindi Februari 20, ambao ni Donald Ngoma na Amis Tambwe.

Yanga, ambao ni mabingwa watetezi, ndio wana kibarua kigumu zaidi kwa sababu licha ya kupitwa mchezo mmoja na Simba, inahitaji kushinda mechi hiyo ili iweze kurejesha matumaini ya kuutetea ubingwa wao baada ya kupoteza mechi moja mwishoni mwa wiki, ilipofungwa na Stand United bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga.

Simba ina pointi 16, baada ya kushuka dimbani mara sita na kushinda mechi tano, huku ikitoka sare mechi moja wakati Yanga imecheza mechi tano, ikishinda mechi tatu, sare moja na kupoteza mechi moja.
Kupoteza mechi hiyo kuna maana moja kwa Yanga, itakuwa imejeruhiwa vibaya katika kampeni yake na kuwapa matumaini zaidi Simba, ambao hawajawahi kutwaa taji la ubingwa tangu mwaka 2012.

Matokeo ya sare bado hayatainufaisha Yanga, lakini itakuwa ni faida kwa Simba ambayo itakuwa na uhakika wa kufanya vizuri katika mechi zake zote ngumu msimu huu.

Mechi baina ya timu hizi mbili kongwe katika historia ya soka nchini huwa zinatawaliwa na vituko vingi mno. Kuvunja nazi, kuoga maji ya maiti, kuruka ukuta, kuingia uwanjani kinyumenyume na mengine kama hayo hutajwa kwamba ni sehemu ya kuhanikiza ushindani.

Hata hivyo, kwa sasa hawawezi kuruka ukuta kama ilivyokuwa miaka ile ya zamani, wala hawawezi kuoga maji ya kuoshea maiti au kuvunja nazi hadharani, kwa sababu sheria za soka haziruhusu ushirikina na timu hizo mbili zimekwishawahi kutozwa faini kwa vitendo hivyo.

Hii itakuwa mechi ya 82 kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Katika kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekea mechi hizi umekuwa mkubwa, bila kujali nani anawania kitu gani.

Hata hivyo, katika mechi 81 zilizopita, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala zaidi kwa kushinda mara 31, wakati Simba imeshinda mara 23.

Jumla ya magoli 168 yamefungwa tangu kuanza kwa Ligi Kuu mwaka 1965, Yanga ikiongoza kuifunga Simba magoli mengi zaidi.

Timu hiyo imeishindilia Simba magoli 91, huku Simba ikitumbukiza nyavuni kwa Yanga magoli 77.
Faraja pekee yaliyokuwa nayo wanachama na mashabiki wa Simba ni kwamba timu yao inaongoza kwa kuifunga Yanga tangu kuingia kwa karne ya 21.

Kwa mujibu wa rekodi, tangu kuingia mwaka 2000, Simba imeifunga Yanga mara 11, zikiwa zimetoka sare mara 15, huku Yanga ikishinda mechi nane kwenye mechi za Ligi Kuu tu.

Watani hao wamekutana mara 34 kwenye mechi za Ligi Kuu Bara. Katika mechi hizo zote, magoli 65 yamefungwa, Simba ikiwa imefunga magoli 35 dhidi ya 32 ya Yanga.

Yanga imeweza kuifunga Simba mara mbili kwa msimu mmoja kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1991.
Ikumbukwe kuwa kabla ya Ligi Kuu kubadilishwa na kuanza kuchezwa kwa mfumo wa msimu kama England, ilikuwa ikichezwa mwanzoni mwa mwaka hadi mwisho, hivyo timu zilikuwa zikikutana mwaka mmoja mara mbili, tofauti na sasa zinapokutana msimu mmoja, lakini miaka tofauti.

Mfano mechi ya kwanza Simba iliyofungwa mabao 2-0 msimu uliopita ilichezwa Septemba 26, mwaka jana.
Hii ni tofauti na mwaka 1991, Yanga ilipoifunga Simba mara mbili kwa msimu mmoja, lakini pia ilikuwa mwaka huohuo.

Ilikuwa ni Mei 18, Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Said Sued ‘Scud’ dakika ya saba na mechi ya marudiano mzunguko wa pili ikashinda tena bao 1-0, mechi iliyochezwa Agosti 31, mfungaji akiwa ni yuleyule Scud.

Katika mechi zote 81 zilizopita na kuzaa mabao hayo 168, winga machachari wa Yanga, Omar Hussein ‘Keegan’ wa Yanga ndiye anayeongoza kwa kufunga magoli mengi katika historia ya timu hizo, akiwa amezifumania nyavu mara sita, akifuatiwa na straika Abeid Mziba pia wa Yanga, aliyefunga magoli
matano kwenye mechi zinazoihusisha timu hizo.

Mastraika wengine wa Yanga, Idd Moshi na Jerry Tegete wa Yanga, pia wao wamepachika mabao manne kila mmoja.

Hata hivyo, Simba nayo imeingiza wachezaji waliofunga magoli manne kwenye mechi za watani ambao ni marehemu Edward Chumila na Musa Hassan ‘Mgosi’.

Rekodi zinasema kuwa tangu kuingia karne ya 21, yaani kuanzia mwaka 2000 wachezaji wanaoongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye mechi za watani ni Mgosi na Tegete, ambao kila mmoja amefunga magoli manne, idadi ambayo haijafikiwa na mchezaji yeyote yule karne hii.

Wachezaji waliopachika mabao matatu kwenye mechi za watani wa jadi kwa upande wa Yanga ni Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Said Mwamba na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na kwa upande wa Simba ni Abdallah Kibadeni na Emmanuel Okwi.

Orodha hiyo inaonyesha waliofunga mabao mawili kwa upande wa Yanga ni Salehe Zimbwe, Juma Mkambi, Rashid Hanzuruni, Said Sued ‘Scud’, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’, Issa Athumani, Idelfonce Amlima, Sekilojo Chambua, Ben Mwalala, Sunday Manara na Amis Tambwe.

Kwa upande wa Simba ni Jumanne Hassan ‘Masimenti’, John Makelele ‘Zig Zag’, Malota Soma ‘Ball Jugler’, Nicodemus Njohole, Dua Said, Steven Mapunda ‘Garincha’, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe na Athumani Machupa.

Moja ya tukio litakalobaki kumbukumbu kwa muda mrefu kwa wanachama na mashabiki wa Simba ni mwamuzi wa kike, Jonisiya Rukyaa kumtoa mapema beki Abdi Banda wa Simba dakika ya 20 na kuwafanya kucheza pungufu kwa muda mrefu, huku ikilazimika kubadilisha mbinu ilizokuwa nazo awali.
Tukio hili lilionekana kulalamikiwa sana na mashabiki wa Simba, ambao awali waliamini kuwa timu yao itaibuka kidedea.

Walidai kuwa rafu ya Banda ilikuwa nyepesi mno na mwamuzi hakupaswa kutoa kadi nyekundu, hasa ikizingatia mechi kubwa kama ya watani wa jadi.

Wakati Yanga wakitoka na nderemo na vifijo, Simba walitoka uwanjani wakilia na mwamuzi Rukyaa.
Hii inakumbusha miaka 42 iliyopita kwenye mechi ya Ligi Kuu (Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara wakati huo) iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, mjini Mwanza.

Ni mechi ambayo haitasahaulika kirahisi na kizazi cha soka kilichokuwa hai wakati huo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Agosti 10, Yanga iliifunga Simba mabao 2-1 kwenye pambano kali, tata na lililokuwa na matukio ya kukumbukwa.

Simba ilielekea kuwa bingwa na kushinda mechi hiyo kwa bao 1-0 lililofungwa na Adam Sabu dakika ya 16.
Dakika ya 87 marehemu Gibson Sembuli aliisawazishia Yanga bao. Dakika saba za nyongeza, Sunday Manara (baba yake mzazi Haji Manara, msemaji wa Simba) akaiandikia Yanga bao la pili na kutwaa ubingwa.

Simba ilimlalamikia sana mwamuzi, marehemu Manyoto Ndimbo kwa madai alikuwa amezidisha muda. Mchezaji Saad Ali wa Simba alianguka na kuzirai na mpaka sasa zipo simulizi kuwa eti sehemu ile aliyoangukiwa hapaoti tena majani hadi leo hii, na wengine wakidai kumeota kichuguu.

 SOURCE: DIMBA

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...