21 May, 2016

Ladha ya Muziki wa Dance Tanzania Inazidi kupotea.

 

Ni wazi kwamba miaka ya nyuma MUZIKII huu ulitamba sana na kila mahali ulipokua ukikatiza basi sikio lako haikosi kusikia muziki huu ila miaka hii yakizazi kipya MUZIKI WA DANCE umeonekana ukipotea licha ya BENDI tofauti tofauti kuendelea kurudishia uhai muziki huu.


    MARA nyingi nimekuwa nikijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu pale ninapowasikia watu ambao naamini hasa ni mashabiki wa muziki wa dansi wakilalamika juu ya kupotea kwa muziki huo, licha ya kuwepo kwa bendi ambazo zinajinadi kupiga aina hiyo ya muziki hivi sasa.

   Pengine wafuatialiji hasa wa muziki huu wanaweza kutambua ukweli wa jambo hili hasa kwa kulinganisha zama hizi na zile za Dar International, Moro Jazz, Cuban Marimba Bend ,Kimulimuli JKT, Tabora Jazz, Nyanyembe Jazz na nyingine nyingi ambapo wanamuziki mahiri kama Marijani Rajabu, Mbaraka Mwinshehe, Juma Ubao,Salum Abdalah, walitamba na kuufanya muziki wa Tanzania kujulikana kimataifa.

Za Kale Ni Dhahabu by Msondo Ngoma Music Band
   Jambo la kujiuliza hapa ni kwa nini muziki wetu wakati huo ulikuwa unakubalika na jamii yote licha ya kuwa kulikuwa na upinzani mkali kutoka kwa muziki wa Zaire (sasa DRC Congo) ambayo nayo wakati huo ilikuwa na wanamuziki vigogo kama Tabu Ley, Luambo Lwanzo Makiadi (Franco) , Abeti Maskini, Mbilia Mbel, Mpongo Love, n.k.

 Ukweli wa hili utaujua ukigundua kuwa wanamuziki wa Tanzania kipindi hicho walikuwa hawapendi kuiga kutoka kwa wageni badala yake walisimama imara kupiga na kuulinda muziki wao, ndiyo maana ilikuwa vigumu kutekwa kimuziki na wageni.

 Ukirudi nyuma kidogo miaka ya 80 na 90 kulikuwa na msururu wa bendi za muziki huo hapa nchini ambapo licha ya wingi wake, zilisimama imara na kuendelea kutangaza muziki huu kimataifa zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.


   Hakuna asiyefahamu ubora wa Bendi za Vijana Jazz wakati huo ikiwa na Hemed Maneti , Super Matimila chini ya gwiji la muziki Dk Remmy Ongara, DDC Mlimani Park ya Cosmas Chidumule, Juwata Jazz ya TX Moshi William, Tancut Almasi ya Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Bima Lee ya kina Jerry Nashon ‘Dudumizi’ n.k, bendi ambazo kila moja ilipiga muziki wa dansi wa Tanzania kwa mtindo wa wake lakini bado ukawa juu kuliko ule wa kutoka nje.




Lengo letu hapa si kuzitaja bendi hizo lakini kiukweli nyingi kati ya hizo zilikuwa hazifanyi hata matangazo ya barabarani, lakini wapenzi wake walikuwa wanajua mahali ambapo zilikuwa zinafanya maonyesho na kwenda kufurahia burudani ya muziki halisi wa dansi ambao leo haupo tena.

Iko wapi leo Njata Njata , au ni wapi iliko Mwenge Jazz ‘Paselepaa’, Bantu Group ‘Kasimbagu’, Tancut Almas ‘Kinyekinye kisonzo’ ni wazi ukikumbuka haya kama ulikuwa mpenzi wa kweli wa burudani wakati huo lazima chozi litakutoka hasa ukiiona Sikinde ya sasa iliyobaki jina tu, huku ikishuhudiwa muziki wake kumezwa na aina ya muziki kutoka Congo DRC.

Kwa sasa asilimia kubwa muziki wa Tanzania imemezwa na muziki wa Kikongo, kwani kila bendi hivi sasa baada ya wimbo kuisha kinachofuata ni rap ambazo zinachukua nafasi kubwa huku zikiwa hazina ujumbe wowote zaidi ya kusifia watu

Hii ni tofauti na siku za nyuma ambapo mbali na kupata wimbo wenye mashairi mazuri yenye mafunzo kilichokuwa kinafuta baada ya wimbo kumalizika ni kuachia ufundi wa wapiga vyombo kumalizia burudani na kuwafanya mashabiki walioshiba ujumbe vichwani mwao kujimwaga ukumbini kuserebuka.

Hakika hii ilikuwa maana halisi ya dansi. Hebu tuambizane ukweli ni nani ama ni bendi ipi leo inafanya haya niende ukumbi gani ambapo sitakutana na makelele ya rapu za kumsifia mfanyabiashara fulani wa magari ambaye hana anachokijua katika muziki zaidi ya kumwaga hela ukumbini ah ah! Kazi kwli kweli!


Hakika miaka hiyo ilikuwa ya ukweli kwa dansi la Tanzania kwani mbali na ubora wa bendi na wanamuziki waliokuwa hodari wa utunzi na upigaji vyombo wakati huo pia kulikuwa na Mashindano ya kutafuta bendi bora Tanzania yaliyojulikana kama (MASHIBBOTA), mashindano ambayo kwa kiasi fulani yalikuwa nguzo ya muziki huo ambayo kwa sasa yamebaki historia.



No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...