Katika mchezo wa nusu fainali
uliofanyika juzi, Gor Mahia iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3- 1
dhidi ya Khartoum mabao yaliyofungwa na Michael Olunga, Innocent Wafula
na Kagere Medie na kukata tiketi ya kucheza fainali.
Gor Mahia chini ya kocha wake
Frank Nuttal mpaka kufikia hatua ya fainali imecheza jumla ya michezo
sita, ikiwemo michezo minne katika hatua ya makundi, robo fainali na
nusu fainali, ambapo imeweza kushinda michezo mitano na kutoka sare
mchezo mmoja.
Mshambuliaji wa Gor Mahia,
Michael Olunga ndie anaeongoza kwa ufungaji akiwa amepachika mabao
matano akifuatiwa na nahodha wa Khartoum Salehdin Osman na msadizi wake
Amin Ibrahim wote wenye mabao manne kila mmoja.
Kwa uapnde wa Azam chini ya kocha
wake Stewart Hall, imefanikiwa kufika hatua ya fainali bila ya kuruhusu
nyavu zake kutikisika, huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa imepachika
mabao kumi (10) katika michezo mitano iliyocheza kuanzia hatua ya
makundi.
Kuelekea mchezo wa fainali, Azam
FC iliziondosha Yanga SC kwa mikwaju ya penati (5-3) hatua ya robo
fainali, na kisha kuindoa KCCA hatua ya nusu fainali kwa kuifunga kwa
bao 1- 0 bao lililofungwa na mchezaji chipukizi Farid Mussa.
Mshambuliaji Kipre Tchetche ana
mabao matatu kwa upande wa washambuliaji wa Azam FC, akifuatiwa na
nahodha John Bocco na Farid Musa wenye mabao mawili kila mmoja.
Katika fainali hiyo ya leo,
inatarajiwa kuwa ya vuta ni kuvute kutokana na makocha wa timu hizo,
Frank Nuttal wa Gor Mahia kutaka kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza
baada ya miaka 30 tangu Gor Mahia kushinda kombe hilo mara ya mwisho
mwaka 1985 walipotwaa kwa mara ya tano (5).
Huku Stewart Hall akiwania kuweka
historia ya kwanza kwa klabu ya Azam FC kuweza kutwaa kombe hilo kwa
mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo miaka tisa iliyopita,
baada ya kusindwa kutwaa taji hilo ilipotinga fainali mwaka 2012 kwa
kufungwa na Yanga SC mabao 2-0.
Mchezo huo wa fainali unatarajiwa
kuanza saa 9:45 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, huku mchezo wa
kusaka mshindi wa tatu ukitarajiwa kuanza saa 7:30 mchana ukizikutanisha
timu za Khartoum ya Sudan dhidi ya KCCA kutoka nchini Uganda.
Bingwa wa michuano hiyo
atazawadiwa kitita cha dola za Kimarekani elfu thelathini (U$ 30,000),
mshindi wa pili dola za Kimarekani elfu ishirini (U$ 20,000) huku
mshindi wa tatu akizawadiwa dola za Kimarekani elfu kumi (U$ 10,000).
No comments:
Post a Comment