RAIS wa Simba, Evans Aveva,
amesema mshambuliaji aliyetemwa Yanga, Hamis Kiiza atawasili nchini
wakati wowote na kpimwa afya kabloa ya kusaini mkataba kuitumikia klabu
hiyo ya Msimbazi.
Aveva, aliyekuwa amefuatana na
makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ katika hafla ya uzinduzi wa kadi ya
watoto ya uanachama wa Simba jijini hapa leo mchana, amesema wamefikia
hatua nzuri na mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya URA ya Uganda.
“Mazungumzo yetu na Kiiza
yamekwenda vizuri, muda wowote kuanzia leo (jana) atawasili nchini kwa
ajili ya kupimwa afya. Akifuzu vipimo vya afya, tutamsajili kuwa
miongoni mwa wachezaji wetu,” amesema Aveva.
Ingawa kiongozi huyo wa juu wa
Simba hakutaja muda wa mkataba ambao Kiiza atasaini, Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope amesema leo kuwa
nyota huyo atatia saini ya kandarasi ya miaka miwili.
“Sisi na Kiiza kila kitu safi, anakuja kusaini miaka miwili hapa,” ametamba Hanspope.
Kiiza aliachwa na Yanga Desemba
mwaka jana ili kumpisha mshambuliaji Mliberia Kpah Sherman baada ya
kuitumikia klabu hiyo tangu 2011.
Tangu atemwe na mabingwa hao
mara 25 wa Tanzania Bara, Mganda huyo anayetisha kwa kupachika mabao,
amekaa bila timu baada ya mpango wake wa kwenda kucheza Fanja ya Oman
kushindikana Januari mwaka huu.
No comments:
Post a Comment