Majambazi yamemuua polisi wa upelelezi,
William Mtika (29) wa jijini hapa wakati wa mapambano kwenye tukio la
kutaka kupora fedha za Kampuni ya Export And Trading eneo la Iwambi.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:00
alasiri na
katika mapigano hayo, jambazi mmoja alipigwa risasi mguuni na
baadaye kufariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa
marehemu huyo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema Mtika
akiwa na askari wenzake walipata taarifa za watu waliotiliwa shaka
nyendo zao eneo hilo ndipo wakaelekea kwenye tukio.
“Askari wakiwa eneo la tukio
walifanikiwa kuwakamata majambazi waliokuwa kwenye pikipiki baada ya
kugonga gari la Polisi kabla ya nyingine kutokea na kuwapiga risasi
ambazo moja ilimpata askari wetu Mtika,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Mnasa
aliwataka polisi kutorudi nyuma katika mapambano, huku akiwasisitiza
wananchi kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.
Mwili wa marehemu Mtika uliagwa jana
mchana nyumbani kwake eneo la Ghana Mbeya na kusafirishwa kwenda mkoani
Mara kwa ajili ya mazishi.Alisema polisi pia walifanikiwa kukamata
bastola moja iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shotgun na
pikipiki mbili.
Akifafanua chanzo cha tukio alisema,
awali majambazi walimvamia mfanyakazi wa kampuni aitwaye Madhu
Basavaranjappa lakini alipiga risasi juu ambazo ziliwafanya nao wajibu
na hatimaye kuamua kukimbia na ndipo walipokutana na polisi.
Kamanda Msangi alisema wanaendelea na
msako mkali wa kuwatia nguvuni majambazi hao huku akisisitiza kwamba
kifo cha polisi wake katu hakitawavunja moyo polisi bali kitaongeza
morali kuhakikisha wanapambana na aina yoyote ya uhalifu.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba, Jumapili atachukua fomu ya kugombea
urais ndani ya chama hicho na atawaeleza Watanzania sababu ya kuwania
nafasi hiyo.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Mipango
na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo alisema, Profesa Lipumba ndiye
mgombea pekee wa urais aliyetangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.
Alisema muda wa kutangaza nia kwa wagombea urais kupitia chama hicho ulianza Mei 10 hadi Juni 10, mwaka huu.
“Kalenda yetu inaonyesha muda wa mwisho
wa kutangaza nia ilikuwa juzi na aliyefanya hivyo ni Profesa Lipumba
pekee yake,” alisema.
Alisema muda wa kuchukua fomu kwa nafasi ya urais kupitia chama hicho ulianza jana na utakamika Juni 14, mwaka huu.
“Mkutano huo utakaoonyeshwa moja kwa moja kupitia runinga,” alisema.
Mketo alisema vikao vya Baraza Kuu la
Uongozi la chama hicho vitaanza Julai 11 hadi Julai 12, mwaka huu ili
kumpitisha mgombea urais, wabunge na madiwani.
“Wagombea watakaopitishwa na Baraza
watasubiri vikao vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakavyotoa
mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani,” alisema.
Kama Ukawa itamteua Profesa Lipumba ambaye kitaalamu ni mchumi itakuwa ni mara ya tano kuwania nafasi ya urais.
Akizungumzia nafasi za ubunge, Mketo alisema kati ya majimbo 189 ya Tanzania Bara, wamepata wagombea kwenye majimbo 133.
Alisema majimbo 56 bado hayajapata
wagombea na kuwataka wafuasi wa chama hicho wenye sifa kuwania.
Mkurugenzi huyo alisema, bado mchakato wa kura za maoni kwa nafasi za
ubunge na udiwani zinaendelea katika kanda mbalimbali.
MWANANCHI
Mkazi wa Kijiji cha Mpandapanda Kata ya
Kiwira wilayani Rungwe, anahojiwa na vyombo vya usalama kwa tuhuma za
kujiandikisha mara mbili katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Rungwe, Veronica Kessy alisema jana kuwa tayari suala hilo limefikishwa
katika vyombo vya sheria.
“Suala hilo kweli lipo lakini siwezi
kuzungumza chochote kwani tulishalifikisha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) na linafanyiwa kazi,” alisema Kessy.
Kwa mujibu wa mitandao, mtuhumiwa
alikamatwa akiwa na vitambulisho viwili vilivyotolewa kwenye vituo
viwili tofauti katika Kijiji cha Mpandapanda.
Kitambulisho cha kwanza kinataja jina la
Veklene B. Mwankenja kikionyesha alizaliwa Aprili 26, 1993 alichokipata
katika Kituo cha Shule ya Msingi Kiwira A, akiwa amevalia shati la
mistari. Lakini kitambulisho cha pili kina jina la Vekline B. Mwankenja
akiwa amezaliwa Julai 26, 1996 akiwa amevaa shati na sweta, alichokipata
katika Kituo cha Shule ya Msingi Kiwira B.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed
Msangi alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kijana huyo alikamatwa na
kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
“Alishakamatwa na amefikishwa mahakamani kwa kosa hilo,” alisema Kamanda Msangi.
Baadhi ya wakazi wa Kiwira walipoulizwa
kuhusu kijana huyo alipo kwa sasa, walidai kuwa hawajamuona licha ya
kusikia taarifa za kukamatwa kwake.
“Huyu mtu hatujamuona tangu atuhumiwe kwa kosa hilo,” alisema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Kijalo.
MWANANCHI
Polisi Mkoa wa Morogoro inawashikilia
madereva 15 wa bodaboda kwa tuhuma za kufanya vurugu katika eneo la Fire
zilizosababishwa na mmoja wao kumdhalilisha askari mmoja wa kike.
Ofisa Habari wa Kikosi cha Zimamoto na
Uokoaji katika Kituo cha Fire, Issa Isandekeku alisema jana kuwa tukio
hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi.
Alisema kabla ya vurugu hizo, dereva wa pikipiki alifanya kitendo hicho kwa askari aliyekuwa akielekea kazini muda huo.
Isandekeku ambaye pia ni Mkaguzi
Msaidizi wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, alisema baada ya dereva
kufanya kitendo hicho alikimbia, lakini alikamatwa.
Alisema muda mfupi baadaye kulizuka
vurugu zilizoanzishwa na waendesha pikipiki wakipinga mwenzao kukamatwa,
huku wakirundika mawe na taka katika Barabara ya Mindu, Kata ya Kingo.
Isendekeku alisema hali hiyo
ilisababisha shughuli mbalimbali za wananchi kusimama kwa zaidi ya saa
moja kutokana na kuhofiwa kujeruhiwa katika tukio hilo.
“Hizi vurugu zimesababishwa na waendesha
pikipiki ambao waliweka vizuizi barabarani ili raia wasipite. Lakini
muda huo mwenzao alikuwa ameshakamatwa. Tena alimdhalilisha askari akiwa
na sare za kazi, hali ambayo ni kinyume cha sheria,” alisema
Isendekeku.
Alisema baada ya askari wa zimamoto
kuzidiwa nguvu, walitoa taarifa polisi ambao walidhibiti vurugu eneo
hilo na kurejea utulivu.
Alisema katika vurugu hizo, polisi Rajabu Seleman alijeruhiwa kichwani kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mussa Maramba
alisema mbali na watu hao kukamatwa pia wanazishikilia pikipiki tano
zilizotelekezwa katika vurugu hizo.
Kamanda Maramba alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya uchunguzi kukamilika.
“Vurugu hizi ukiangalia hazikuwa na
sababu ya msingi… sasa sijui hao madereva walifanya fujo kwa masilahi ya
nani ?” alihoji Kamanda Maramba.
MTANZANIA
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Mazingira), Steven Masele, ametangaza kumuunga mkono Waziri Mkuu
wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kuwania urais kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Masele aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kabla ya Baraza
la Mawaziri kuvunjwa, jana aliibukia katika mkutano wa kutafuta
wadhamini wa Lowassa uliofanyika mjini Shinyanga na kusema sasa kada
huyo wa CCM anasubiri kupitishwa na vikao vya chama.
Akizungumza katika mkutano huo, Masele ambaye pia ni mbunge wa Shinyanga
Mjini, alisema yeye pamoja na wana CCM wenzake wanasubiri Kamati Kuu ya
CCM ifanye kazi yake kisha wamalizie kumpitisha Lowassa.
“Tanzania yote inajua,” alisema Masele na kuuliza “inajua haijui…?” huku akijibiwa na wana CCM, “Inajuaaa…”
“Tanzania inajua na dunia nzima inajua kwamba Lowassa yuko hapa. Mimi ni
mjumbe wa Mkutano Mkuu, wa NEC wetu wamesema hapa, sisi tumekaa mkao wa
kula tunasubiri wafanye kazi yao na sisi tunamalizia kupiga bao tu,”
alisema Masele.
Mbali na Masele, mawaziri wengine walioonyesha kumuunga mkono Lowassa
kwa nyakati tofauti ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
watoto, Sophia Simba na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro
Nyerere aliyemsindikiza kuchukua fomu mjini Dodoma.
Katika mkutano huo, alikuwapo pia Mbunge wa Msalala ambaye pia aliwahi
kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye alimsifia
Lowassa kwa utendaji bora alipokuwa Waziri Mkuu na hasa kuwaletea maji
wakazi wa Mkoa wa Shinyanga.
“Sisi wananchi wa Mkoa wa Shinyanga tuna imani na wewe kwa jambo moja
ulilotufanyia. Ulileta maji kutoka Ziwa Victoria. Shinyanga ilikuwa
jangwa, lakini ulileta maji, sisi watu wazima tuliona kwa macho,”
alisema Maige.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, alisema
Lowassa ni miongoni mwa viongozi walioandaliwa tangu enzi za Mwalimu
Nyerere.
“Kuna wakati chama kiliwaandaa vijana wake kwa kuwapeleka chuo kikuu ili
wawe viongozi wa baadaye, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, Lowassa na
wengineo nawahifadhi. Sasa umefika wakati wa Lowassa…,” alisema
Guninita.
Katika mkutano huo, Lowassa alivunja rekodi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kupata wanachama 7,014 waliojitokeza kumdhamini.
Katika mkutano huo, Lowassa alivunja rekodi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kupata wanachama 7,014 waliojitokeza kumdhamini.
Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Charles Sangula, alisema kati ya
wanachama hao, 3,221 walitoka katika wilaya yake, 2,610 Kishapu na 1,183
Kahama.
Naye Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Kanali Maulid aliwataka makada wa
chama hicho kutochafuana kwa kashfa wakati huu wa uchaguzi, na kuchagua
mtu anayekubalika ndani na nje ya chama.
“Tumchague mtu anayekubalika ndani na nje ya chama chetu. Lowassa
anakubalika. Lakini wako baadhi ya makada wanaochukua fomu na kuanza
kuwachafua wenzao. Nashukuru Lowassa hakufanya hivyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja,
alisema kulingana na matokeo ya utafiti uliofanywa na asasi yake ya
Tanzana Mzalendo Foundation, Lowassa amekidhi vigezo vyote 10 vya
uongozi bora.
“Tuna taasisi yetu ya Tanzania Mzalendo Foundation, tumeweka vigezo 10
na vyote Lowassa amepata asilimia 100. Baadhi ya vigezo hivyo ni
uzalendo, uvumilivu na kuwa na uamuzi mgumu,” alisema Mgeja.
Akizungumza na wana CCM waliokusanyika katika ukumbi huo, Lowassa aliwashukuru na kurudia sababu yake ya kugombea urais.
“Nimerudi nyumbani kuwaambia kuwa nimeanza safari ya matumaini. Nilikuwa hapa mwaka 1977 hadi 78, mlinilea vizuri.
“Nimegombea kwa sababu nimechoshwa na umasikini. Mwaka 1962, Mwalimu
Nyerere alitaja maadui watatu wa Tanzania kuwa ni ujinga, umasikini na
maradhi. Lakini hadi leo kuna viongozi wa Tanzania wanajivunia
umasikini. Kazi ya kiongozi ni kuwatoa watu kwenye umasikini na
kuwapeleka kwenye utajiri,” alisema Lowassa.
Aliwataka pia wana CCM kujiandikisha ili wawe na sifa ya kupiga kura.
Lowassa aliingia Shinyanga saa sita mchana kwa ndege akiwa na msafara
wake kisha wakaelekea kwenye ofisi ya CCM mkoa na baadaye ofisi ya
wilaya.
NIPASHE
Wabunge wameikosoa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, wakisema haina jipya na haitekelezeki.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania
bungeni, Freeman Mbowe, amesema bajeti ya serikali ya mwaka 2015/16
haina unafuu wowote kwa Mtanzania wa kawaida, bali bajeti iliyojaa
maneno matamu ya kuhadaa umma.
“Ukipitia baadhi ya vifungu utabaini
kuwa vina lengo la kutoa kauli nzuri za matumaini na ahadi
zisizotekelezeka, ni bajeti ya kikampeni kwa ajili ya uchaguzi,” alisema
na kuongeza:
“Wamedandia hoja ya Kambi ya Upinzani ya
kutoa pensheni kwa wazee tangu bajeti 2012/13 na serikali ikasema jambo
hili halitekelezeki, leo wanazungumza wataanzisha na hakuna sheria ya
utekelezaji na haiko katika sheria zitakazoletwa bungeni, hakuna mzee
atakayelipwa pensheni katika mwaka ujao wa fedha,” alisema.
Mbowe alisema ongezeko la kodi ya mafuta
ni tishio kwa Mtanzania wa kawaida, kwani kila kitu kitapanda gharama
kwa Sh. 100 kwa dizeli na petroli, huku mafuta ya taa ikiongezeka kwa
Sh. 150, yataathiri wananchi na kuongeza gharama za maisha
Mbowe alisema katika soko la dunia bei ya mafuta inashuka kila siku, huku Tanzania ikiongeza badala ya kupungua.
Alisema Watanzania wanadanganywa tena
kwa fedha za kodi ya mafuta zitakwenda kwenye mfuko wa Umeme Vijijini
(Rea), kwani mwaka uliopita fedha zilizoingizwa kwenye mifuko maalum ni
fedha zilizotakiwa zisitumike, lakini imezichomoa na kutumia kwa mambo
mengine, hivyo siyo kweli kuwa zitatumika kwa umeme.
“Bajeti inaweza ikasomwa ikaonekana ni
tamu, tatizo kubwa ni utekelezaji wa bajeti, Chama hiki (CCM) na
serikali hii zimeshachoka, hakina uwezo wa kutekeleza bajeti, wamebakiza
miezi minne waondoke Ikulu, watuachie sisi tuingie,” alisema na
kuongeza:
“Inashangaza kuona bajeti inasomwa leo,
lakini nusu ya mawaziri hawapo katika bajeti ya serikali yao, Naibu
Waziri wa fedha anaingia wakati waziri anahitimisha bajeti…wabunge wa
upinzani hususan wa Chadema wote wameacha majukumu yao kuja kusikiliza
bajeti.”
Naye, Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu, alisema haoni kipya ndani ya bajeti hiyo kwa
sababu kila kitu ni kile kile.
“Kwa kweli nilishindwa kufatilia kwa
sababu ni maneno yale yale, ya watu wale wale ya siku zote na ya miaka
yote…wakitaka fedha ni mafuta na bia, lakini safari hii hawakwenda
kwenye maji ila yale yale tu,” alisema.
Kuhusu kupandisha kodi ya mafuta, alisema serikali haijawahi kufikiria vyanzo vipya vya mapato.
Alisema hakuna mji uliojengwa na kuwa chanzo kikubwa cha mapato kama Dar es Salaam kutokana na majengo makubwa yaliyojengwa.
“Hayo majengo ni chanzo kikubwa cha mapato nchi nyingi zinaingiza mapato kwa kutumia majengo makubwa yaliyojengwa,” alisema.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema,
alisema bajeti ya mwaka huu haina tofauti na mwaka jana kwani kila kitu
ni kile kile hakuna jipya.
“Ni bora wangekaa wenyewe wakaipitisha,
sisi (wabunge) tukabaki nyumbani, kwa sababu kila tunachopitisha
hakitekelezeki,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther
Bulaya, alisema bajeti ya serikali haiwezi kumsaidia mwananchi wa kipato
cha chini kutokana na kupandisha bei ya mafuta.
“Kwa kawaida mafuta yakipanda ni lazima
kila kitu kitapanda bei, hivyo kuwepo kwa ongezeko la mafuta ni
kuwafanya wananchi kuendelea kuwa maskini tofauti na ilivyokuwa
ikikusudiwa kuwa uenda bajeti ingekuwa ya kuwasaidia wananchi wenye
kipato cha chini,” alisema
Aidha, alisema inashangaza kuona kuwa fedha za matumizi zimekuwa nyingi huku fedha kwa ajili ya maendeleo zikipunguzwa.
Naye, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luaga
Mpina, ameibeza bajeti na kudai kuwa haina jambo lolote ambalo ni jipya
kwani kila jambo linaonekana kuwa ni la kawaida.
Alisema serikali haikuwa na sababu ya
kuongeza ongezeko katika mafuta kuwa ilikuwa na uwezo wa kutafuta vyanzo
vingine vya mapato tofauti na kujielekeza katika mafuta.
Mpina alisema pamoja na serikali kudai
kwamba wataweza kupeleka fedha za miradi katika wakala wa Umeme vijini,
lakini kimsingi pesa hizo hazipelekwi.
Waziri Kivuli wa Fedha wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, James Mbatia, alisema:
“Ni bajeti ya kufurahisha wapiga kura
katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa sababu upungufu huo unatokana na
ongezeko la thamani ya Dola ya Marekani kuchupa kutoka Shilingi 1,650
kwa mwaka jana hadi Shilingi 2,054 kwa viwango vya wiki hii…Bajeti kwa
ajili ya matumizi ya serikali ni kubwa kuliko Bajeti ya Maendeleo.”
Mbatia alisema bajeti ya mwaka huu,
itawaumiza Watanzania kwa kuwa serikali imepandisha kwa kiwango cha juu
mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa huku ikilenga kukopa zaidi ya
shilingi trilioni sita na kuongeza kasi ya ukuaji wa deni la Taifa.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema),
Mchungaji, Peter Msigwa, alisema bajeti hiyo ni ya kiini macho na
haiwezi kutekelezeka kwa kuwa hata bajeti inayoishia Juni 30, mwaka huu
imetekelezwa kwa asilimia 28 tu kutokana na wahisani wanaochangia bajeti
ya Taifa kugoma.
“Tunasikitika bajeti hii itaiacha nchi
ikiwa kapu tupu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika. Wamekuja na bajeti ya
makusudi kwa sababu wanafahamu wako kwenye kupindi cha mpito cha
kukabidhi nchi kwa Ukawa…Hakuna muujiza utakaotokea na kuifanya bajeti
iliyoletwa bungeni itekelezeke,”alisisitiza Msigwa.
FELIX MKOSAMALI
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix
Mkosamali, alisema bajeti iliyowasilishwa inalenga kuwafurahisha
wasanii na si wananchi kwa kuwa ni bajeti ya maigizo kutokana na hofu ya
kuanguka kwa chama tawala na si kupanua wigo wa maendeleo ya
Watanzania.
NIPASHE
Serikali imetakiwa kupunguza vizuizi mipakani ili kurahisisha biashara na kuongeza kipato kwa wananchi waishio humo.
Wito huo ulitolewa na Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi(CCM), Abdulrahman Kinana (pichani), wakati
akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Misenyi ikiwa ni mwendelezo wa
ziara yake ya siku 10 mkoani Kagera.
Kinana ambaye alipokea malalamiko kutoka
kwa wananchi wa kijiji cha Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda ya
kutozwa kodi nyingi, alisema kuweka kodi nyingi mipakani ni kuongeza
uingizaji na utoaji wa bidhaa kwa njia ya panya.
“Serikali itambue kuwa wananchi wa
mipakani wanategemea kipato kutokana na biashara zinazoingia na kutoka
nchini sasa kama wanaweka vizuizi zaidi ya vitano, kuna biashara
itafanyika na mwananchi wa mipakani atafaidika vipi? Na ndiyo maana watu
wanaamua kupitisha biashara zao kwa njia za panya,” alisema Kinana.
Alieleza kuwa Tanzania ni nchi pekee
miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki inayopakana na nchi nane, hivyo ni
vyema fursa hiyo ikatumika kuwanufaisha wananchi wa mipakani.
Kinana aliongeza kuwa asilimia 30 ya
Watanzania wanaishi mipakani, hivyo wanapaswa kurahisishiwa mfumo wa
biashara kwa kuwapunguzia kodi.
“Lazima serikali itambue namna nzuri ya
kulinda mipaka yake, haiwezi ikalinda mipaka kwa kukusanya kodi nyingi
ambazo zinageuka kuwa kero, watumie akili ya kukusanya na siyo mabavu na
uonevu,” alisema Kinana.
Pia aliahidi kulifikisha suala hilo kwa
ngazi husika kuanzia kwa waziri mwenye dhamana ili mipaka hiyo igeuke
kuwa yenye manufaa kwa wananchi.
Kinana pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, John Mongela, kukaa na kamati ya ulinzi na usalama, kuona namna
ya kupunguza kodi hizo kwa sababu ziko ndani ya uwezo wao.
NIPASHE
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, ambaye anawania uteuzi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kugombea urais, ameahidi kuwa asipoteuliwa hatakuwa na
kinyongo na atarejea kukijenga chama.
Aidha, ameahidi kuwa atalirudisha Jimbo la Iringa Mjini mikononi mwa CCM.
Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kadhalika, Makamba amemwaga ahadi lukuki
kwa wakazi wa mji wa Iringa ikiwamo kuwasaidia vijana wa bodaboda,
kupanua uwanja wa ndege mkoani humo, kujenga barabara ya lami kuelekea
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na kufufua viwanda.
Ahadi nyingine ni pamoja na kuhakikisha
vijana wanaojiunga na vyuo vikuu, wanapata mikopo bila usumbufu wowote
kwa kuwa kupata elimu ni haki yao.
Aliyasema hayo jana alipozungumza na
makada wa CCM, kutoka wilaya zote za mkoa wa Iringa, alipokuwa akitafuta
wanachama wa kumdhamini.
Makamba alipata zaidi ya wadhamini 600 ambao ni zaidi ya idadi inayotakiwa na chama ambayo ni wanachama 30 kwa kila mkoa.
Aliongeza kuwa mchakato wa kumpata
mgombea, hauna uhasama na kwamba hata kama kushinda ama kushindwa
atakuwa mtu wa kwanza kuanza kukijenga chama upya ili kurudisha
mshikamano.
“Mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuanza
kukijenga chama baada ya uchaguzi mkuu, wanachama wote wanatakiwa kukaa
kama familia moja ili kujenga mshikamo pamoja na kujadili makovu ya
uchaguzi,” alisema.
Makamba alisema ana imani kwamba CCM
kitapitisha mgombea kwa kujiamini bila kuogopa kusambaratika na wala
wanachama wasisikilize watu wanaojipitisha mitaani na kusema kwamba
chama kitasambaratika baada ya uchaguzi.
Kabla ya kukutana na wanachama wa CCM
katika ofisi za wilaya, Makamba alisema Iringa ni kama nyumbani kwao kwa
kuwa aliwahi kuishi hapo wakati baba yake akifanya kazi mkoani humo.
Wakati wa mapokezi yake, vijana
waendesha bodaboada waliongoza msafara wake, huku wakiimba nyimbo hadi
katika ofisi za wilaya ambako alikabidhiwa majina ya makada
waliomdhamini.
No comments:
Post a Comment