MWANANCHI
Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) limekubaliana na ombi la klabu za Ligi Kuu la kusajili wachezaji saba wa kigeni badala ya watano wa sasa.Bodi ya Ligi iliwasilisha uamuzi wa
klabu zote za Ligi Kuu wa kuiomba TFF ibadilishe kanuni ili ziweze
kusajili wachezaji wengi zaidi wa kigeni kwa lengo la kuinua kiwango cha
ligi hiyo.
Jana, katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesiga alisema kikao hicho cha shirikisho hilo na sasa klabu zinaweza kusajili wachezaji zaidi wa kigeni.
Klabu hizo zimekuwa zikijikuta kwenye
wakati mgumu kuamua kukata jina la mchezaji wakati zinapokuwa na
wachezaji wengi wazuri kutoka nje, ikiwamo Yanga ambayo hadi sasa ina
wachezaji sita wageni na ilikuwa ikisubiri uamuzi huo ili ikamilishe
usajili wa wachezaji wageni.
Wakati hayo yakiendelea, Yanga imemruhusu kipa wake Juma Kaseja kusajiliwa na klabu yoyote inayomhitaji.
Mwanasheria wa Yanga, Frank Chacha
aliliambia gazeti hili jana kuwa Yanga haiwezi kumzuia kipa huyo
kujiunga na klabu nyingine yoyote kwa kuwa tayari ilishavunja mkataba
wake, hivyo siyo mwajiriwa tena wa klabu hiyo yenye makao yake makuu
makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.
Timu mbalimbali za Ligi Kuu zilielezwa
kuwa zimekuwa zikihitaji huduma ya kipa huyo aliyejipatia sifa kwa
umahiri langoni, kiasi cha kujipatia jina la Tanzania One, lakini
zilikuwa zikihofia kesi yake ya kimkataba dhidi ya Yanga iliyopo Tume ya
Usuluhishi ya Mahakama ya Kazi.
Kaseja alisaini Yanga mkataba wa miaka miwili na alitumikia mwaka mmoja na kubakisha mkataba wa mwaka mmoja uliozua mgogoro.
Chacha alisema anashangazwa na watu wanaodaia kuwa klabu hiyo imemzuia Kaseja kujiunga na timu yoyote wakati si kweli.
“Sisi
hatumzuii Kaseja kujiunga na timu yoyote na hata mwanasheria wake
tulimwambia hivyo kuwa anaweza kutafuta timu wakati kesi yake
inaendelea.
“Ndiyo
ana kesi na Yanga, lakini kumbuka yeye ndiye alivunja mkataba na Yanga
ikamshtaki hivyo haitapendeza kuwa hukumu inatoka halafu Kaseja hana
timu yoyote inayomwingizia kipato, atailipa nini Yanga.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu jambo hilo, Kaseja alijibu kuwa hawezi kulizungumzia kwa sasa.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewashangaa makada wanaojinadi kuwa ni wasafi na waadilifu, akisema sifa hizo zinatakiwa zitolewe na jamii.
Jaji Warioba, mmoja wa watu ambao
wamekuwa wakikemea masuala ya ukiukwaji wa maadili, pia amesema
hatamuunga mkono mgombea ambaye anakiuka maadili ya uongozi.
Tayari makada 37 wamejitokeza kuomba
ridhaa ya wana-CCM kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na
wengi wao wamekuwa wakijinadi kuwa ni wasafi na waadilifu na kuwataka
wanachama kutowapitisha watu wenye harufu ya ufisadi na wasio waadilifu.
Lakini Jaji Warioba alisema anaona wanakwenda kinyume na inavyotakiwa kufanyika.
“Viongozi
wa sasa wanaonekana hawajali misingi ya maadili kwa sababu jamii yetu
yenyewe imeonyesha kutochukizwa na suala hili la mmomonyoko wa maadili
na wala jamii haijalipa uzito unaostahili,” alisema Jaji Warioba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Vuguvugu la uhuishaji wa Maadili kwa Jamii (Moral Rivival Movement).
“Viongozi
wengi waliochukua fomu za kugombea urais wanaonekana kujitangaza kuwa
wao ni waadilifu. Jamii ndiyo ilipaswa kusema kuwa viongozi hao ni
waadilifu au sio waadilifu na sio wao kujinadi,” alisema Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu.
Mkutano huo ulioandaliwa na viongozi wa
dini kwa kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Wakikristo (CPT)
ulijadili ujenzi mpya wa maadili katika jamii utasadia kupata kiongozi
mwenye misingi ya maadili ili kuepuka mitafaruku baina ya siasa za
madaraka na siasa za maslahi.
Warioba, ambaye alieleza kuwa ameamua
kukaa kimya kuhofia kila anachosema kuhusishwa na masuala ya uchaguzi,
alisema viongozi ambao hawana maadili wamechangia kwa kiasi kikubwa
kuwapo kwa mianya ya rushwa.
“Lakini
kama tunataka kuwa na viongozi wenye misingi ya maadili, ni lazima
tujenge upya maadili kwa sababu tusipofanya hivyo yatazidi kuporomoka,”
alisema waziri mkuu huyo wa zamani.
“Tumeona
sasa ukabili umeanza kurudi, ubaguzi wa kidini umeanza kurudi, ubaguzi
wa kikanda umeanza kurudi, ubaguzi wa namna hii umeanza kurudi kutokana
na kukosekana kwa maadili,” alisema Jaji Warioba ambaye alitumia muda mwingi kuishauri jamii kufuata misingi ya maadili iliyoachwa na waasisi.
MWANANCHI
Serikali imesema kuanzia Julai mosi
mwaka huu, ajira za utumishi wa umma zitakuwa zikiombwa kwa njia ya
mtandao, ili kuongeza ufanisi wa mchakato wa kuwapata watumishi wenye
sifa na kupunguza malalamiko ya kupotea kwa barua za maombi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani
alisema mtandao huo umezinduliwa na waombaji watapaswa kuingia katika
tovuti maalumu ya ajira na kutuma maombi yaliyoambatanishwa na vyeti vya
taaluma walizosomea.
“Maombi
kwa njia ya mtandao yatapunguza kazi ya kuchambua maelfu ya barua za
maombi ya kazi zilizokuwa zinatumwa, itapunguza pia manung’uniko kwamba
barua zimetumwa kisha zimekaliwa tu,” Kombani.
Waziri huyo, alisema kwa kutumia
utaratibu huo mpya, wananchi wanaotaka ajira serikalini watakuwa na
uhakika kuwa barua zao zimefika na kupokewa na wahusika. Pia, wanaweza
kupata mrejesho kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu zao za mkononi.
Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi alisema baada ya kuona
mchakato wa kuajiri unachangamoto nyingi, waliamua kubuni mfumo wa
kuomba ajira kupitia mtandaoni.
“Utaratibu
huu utatupunguzia gharama, wanafunzi wanaohitimu kila mwaka vyuoni ni
maelfu kwa maelfu na nafasi tunazopata serikalini kupitia sekretarieti
ya ajira hazizidi 12,000 kila mwaka,” Daudi.
Hata hivyo, katibu huyo alisema wamekuwa
wakipata changamoto kubwa kutokana na baadhi ya waombaji kutumia vyeti
vya kughushi na hivyo kulazimika kwenda kwenye vyuo husika
kuvithibitisha.
MWANANCHI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kinazindua operesheni mpya ya kuwaandaa wanawake kufanya “maamuzi magumu” kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Kwa sasa, chama hicho kikuu cha upinzani, kinaendelea na kampeni ya “Amsha Amsha”, ambayo inalenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura.
Jana, Chadema ilitoa taarifa inayoeleza
kuwa sambamba na kampeni hiyo ya Amsha, Amsha”, chama hicho kinaanza
operesheni mpya itakayozinduliwa na katibu wake mkuu, Dk Willibrod Slaa
huku wanamuziki nyota, Christian Bella, Profesa Jay na Flora Mbasha
wakipamba uzinduzi huo.
Mratibu wa operesheni hiyo, Lilian
Wasira alisema jana kuwa shughuli hiyo itafanyika kwenye viwanja vya
Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
“Maandalizi
yamekamilika, wanawake Dar es Salaam na Pwani waje wajengeke kifikra
ili kufanya maamuzi magumu katika uchaguzi unaokuja,” Wasira.
Alisema operesheni hiyo itafanyika nchi
nzima kuhamasisha wanawake kujiandikisha kwenye Daftari ya Wapigakura na
kuwapa elimu ili watambue nafasi yao katika jamii na uwezo wao kuleta
maendeleo ya kweli,” alisema Wasira.
Kada huyo, aliyewania uenyekiti wa
Baraza la Wanawake wa Chadema bila mafanikio, alisema: “Zama za wanawake
kupewa khanga, vitenge, vilemba na kofia wakati wa uchaguzi zimepitwa
na wakati, lazima wajithamini, ndiyo maana tumeanzisha hii operesheni
ili tuwajenge kiuwezo.”
Alisema ni wakati mwafaka kuachana na
fikra za kurubuniwa na kuuza haki zao za msingi kwa rushwa za aina
mbalimbali kama “chumvi”, akishauri watambue kuwa njia pekee ya kuiondoa
CCM madarakani ni kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura na
kugombea uongozi.
“Hatutaki
kuona hali ikiendelea. Saa ya ukombozi imefika, mwanamke amekuwa ni
mwathirika wa matatizo mbalimbali kwenye jamii, hivyo asiache kuja kesho
(leo) ili Tanzania izaliwe upya Oktoba,” Wasira.
Mbali na Dk Slaa, hafla hiyo itahudhuriwa na mbunge wa Kawe, Halima Mdee
na wasanii wa muziki, wote wakiwa na lengo la kutoa hamasa kwa wanawake
nchini kushiriki katika siasa. Ikiwa ni miezi minne imesalia kabla ya
uchaguzi wa Oktoba, Chadema imesambaza makada wake walio kwenye mabaraza
ya wanawake na vijana kwenda maeneo mbalimbali kuhamasisha uandikishaji
wapiga kura.
Juzi gazeti hili lilimkariri mkurugenzi
wa mafunzo na uchaguzi wa Chadema, Benson Kigaila akisema kwa sasa
wanaelekeza nguvu katika uandikishaji wa wapigakura ili kutengeneza
mazingira mazuri ya ushindi.
Hamasa hiyo inakwenda sambamba na
mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu, ikiwa ni siku saba kabla ya siku
ya mwisho ya hatua hiyo kwa watiania wa ubunge na udiwani katika maeneo
yasiyo na uwakilishi wa madiwani na wabunge.
MTANZANIA
Mbunge wa Sengerema Willium Ngeleja
amesema iwapo CCM kitamteua kuwa mgombea wa Urais katika uchaguzi mkuu
utakaofantyika Oktoba na kuibuka mshindi Serikali atakayiiunda
haitakumbatia ushoga wala ndoa za jinsia moja.
Ngeleja aliyasema hayo wakati
akiwashukuru wananchi wa Nyamagana kwa kumdhamini ili kutimiza mat akwa
ya chama chake ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa Urais.
“Nikibahatika
kuingia ikulu, sitakuwa naanza upya, tayari Serikali yetu chini ya Rais
Kikwete imeweka msimamo juu ya suala hilo, na mimi nikiwa rais
mwadilifu ninayeheshimu mila zetu njema, masuala ya ushoga hauyatakuwa
nan a nafasi kabisa”Ngeleja.
Alisema ili kulinda utamaduni na heshima
ya Kitanzania na Afrika ni muhimu kwa Taifa kuanza kuchukua hatua
kupunguza utegemezi ili kuepukana na masharti ya kufedhehesha kama hayo.
MTANZANIA
Wakati idadi ya makada wa CCM waliochukua fomu ikifikia 38 jana, UKAWA wanajipanga kumkabili LOWASSA .
Ukawa inamuona Lowassa kama ndiye
mgombea kutoka CCM ambaye ndiye wanaweza kukabiliana naye katika
uchaguzi mkuu ujao kutokana na jina lake kuvuma sana hasa wakati huu
mwana siasa huyo pamoja na makada wengine wa CCM wakizungumza Mikoani
kuomba udhamini.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe alisema wanamsubiri kwa hamu Lowassa katika kinyang’anyiro cha Urais katika uchaguzi wa mwaka huu.
Katika mkutano uliofanyika kwenye
viwanja wa njoro, Moshi, Mbowe aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha katika daftari la wapigakura pamoja na kufanya mabadiliko
katika uchaguzi mkuu ujao.
Amesema ameona watu wengi wakimpamba
Lowassa ambaye ametangaza nia ya kugombea Urais kupitia CCM, hivyo
wanansubiri amalize michakato yote kwenye chama chake aje kukutana na
Ukawa.
NIPASHE
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe,
amesema utitiri wa wagombea urais kupitia CCM kunaonyesha dalili ya wao
wenyewe kutoaminiana, kutothaminiana na kimepoteza hazina ya viongozi.
Aidha, alisema kazi ya urais ingekuwa
inachukuliwa kwa uzito wagombea wa CCM wasingefikia 10 badala yake
imeonekana ni kazi nyepesi na imerahisishwa na CCM. Kabwe alisema sifa
13 pekee za wagombea wa CCM ni nyepesi ndio maana kila mmoja anajiona
anaweza kuwa kiongozi wa nchi.
Kabwe alisema moja ya sifa ya chama cha
ACT-Wazalendo ni wagombea kufuata masharti kwa kutangaza mali na madeni
ikiwamo kufuata miiko ya viongozi iliyotangazwa na Azimio la Tabora.
Kabwe aliwataja viongozi hao kuwa ni wa kitaifa wa chama, rais, mawaziri, wabunge na madiwani watakaotokana na chama hicho.
Aliongeza kuwa ili kubomoa mfumo wa
kinyonyaji na kifisadi miongoni mwa viongozi, chama hicho kimeamua
kurejesha miiko ya uongozi na kuishia ambayo imehusishwa kutokana na
Azimio la Arusha.
“Chama
kinamtaka kiongozi katika uongozi wa umma asiwe mkurugenzi katika
kampuni au shirika la umma, awe wazi na vyanzo vyake vya mapato, mali
alizonazo kwa kuzingatia utaratibu wa sheria ya nchi na kanuni za
mwenendo na maadili ya viongozi,” Kabwe.
Pia, alisema kiongozi anatakiwa asiwe mfanyabiashara wa aina yoyote katika chama na serikali anapokuwa kwenye nafasi ya uongozi.
Alisema tangu wagombea hao waanze
kutangaza nia hakuna mgombea urais aliyetamka neno miiko isipokuwa
Samuel Sitta pekee, licha ya kuahidi kupambana na rushwa pamoja na
ufisadi.
“Nitolee
mfano nchi ya Canada, Uingereza, Marekani wana miiko lakini Tanzania
tunageuza uongozi kuwa kichaka cha wezi kwa kutupa miiko pembeni,”Kabwe.
NIPASHE
Balozi Patrick Chokala,
amekuwa mwandishi wa habari wa pili kati ya makada 38, waliojitosa
katika kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Mwandishi wa habari wa kwanza kujitosa katika kinyang’anyiro hicho ni
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe.Hii ni mara ya pili kwa Chokala kuwania nafasi hiyo, baada ya kujitosa mwaka 2005 akiwa Balozi wa Tanzania nchini Moscow na kushindwa kupenya, huku akija na kaulimbiu ya ‘Kiatu kwanza Benzi baadaye’, akiwa na maana ya watu wa chini kuwezeshwa kwanza matajiri baadaye.
Chokala alisema pamoja na Ilani ya CCM, ataweka mkazo wa usafiri wa reli huku akiitaja reli ya kati kuwa ya kwanza kutumia umeme.
Balozi Chokala ambaye alitumia muda mwingi kueleza nchi alizowahi kuishi na kufanya kazi ikiwamo Urusi, alisema Tanzania inahitaji rais safi katika suala la rushwa, ambaye hana tamaa, mwenye haki, msimamo, ambaye hataangalia ndugu yake akifika Ikulu kufanya mambo yasiyofaa kwani atamfukuza.
“Hatuishi duniani miaka 100, unapokuwa Ikulu, uwe na msimamo wa kusaidia Ikulu…mimi simzungumzii yoyote bali nazungumzia principle,(kanuni, maadili) mimi ni mwanafunzi wa Political Science, uongozi na tabia ya nchi inategemea na kiongozi aliye juu ni kama nyumba ya msonge inategemea nani yupo juu,” alibainisha.
Aidha, alitoa mfano wa rais anaagiza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kumpa Sh. bilioni 2, lakini naye atachota nyingi zaidi, Waziri wa Fedha na wengine watachukua zaidi, ikiwamo kutumia mbinu mbalimbali.
Balozi huyo ambaye amekuwa Mwandishi wa Rais, Ali Hassan Mwinyi, kwa miaka kumi na Rais Benjamini kwa miaka mitatu, alisema anaamini kuwa anaweza kuwa rais wa nchi kwa kuwa ana uzoefu wa kutosha ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment