MWANANCHI
Kamati Kuu ya Chadema imepanga Agosti 4
kuwa siku ya kumpata mgombea wake wa urais ambaye ataingia kwenye
kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Vyama vinne vilivyounda Ukawa, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD,
vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais,
lakini kila chama kitateua mgombea wake kabla ya kukubaliana mtu
atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Ratiba iliyotolewa jana na Chadema
inaonyesha kuwa chama hicho kitatumia siku 76, kuanzia Mei 18,
kumaliza mchakato wa kuwapata wagombea wake wa nafasi za udiwani, ubunge
na urais kwa kuhitimisha na Mkutano Mkuu.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Chadema itampata mgombea wake wa urais takriban siku 14 zaidi kulinganisha na mwaka 2010 wakati Dk Willibrod Slaa alipoteuliwa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
aliwaambia wanahabari jana kuwa kamati hiyo imeridhia mchakato wa
uchukuaji na urejeshaji fomu uanze ili watia nia katika maeneo
mbalimbali waanze kuchukua fomu za udiwani, uwakilishi na ubunge.
Katika ratiba hiyo , chama hicho
kimeyapa kipaumbele maeneo yanayoonekana kutokuwa na madiwani na
wabunge, kuanza kuchukua fomu siku ya kwanza ya kazi hiyo na kuzirudisha
Juni 25.
Aidha ratiba hiyo inaonyesha kuwa makada
waliopo kwenye maeneo yenye madiwani watachukua na kurejesha fomu
ndani ya siku 10 kuanzia Julai Mosi.
MTANZANIA
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda
na maofisa wa Jeshi la Polisi jana walijikuta katika wakati mgumu baada
ya kunusurika kupigwa mawe na vijana waliokuwa wamejazana katika Kituo
Kikuu cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.
Makonda na maofisa hao, walifika eneo
hilo kwa nia ya kuwaomba madereva wa mabasi yaendayo mikoani kusitisha
mgomo waliouanza juzi.
Maofisa wa polisi walionusurika kupigwa mawe ni Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura.
Tukio hilo lilitokea kituoni hapo saa
4:00 asubuhi, wakati Makonda alipokwenda kuzungumza na viongozi wa Chama
cha Madereva kuhusu namna ya kumaliza mgomo uliodumu tangu juzi.
Makonda alipofika kituoni hapo,
alikwenda moja kwa moja kufanya mazungumzo na uongozi wa madereva, huku
akilindwa na askari polisi na wengine waliovaa kiraia.
Askari walianza kutumia mbwa kuwatishia
madereva pamoja na umati mkubwa wa watu uliotaka kusikiliza kilichokuwa
kikizungumzwa na baadaye mbwa alimrukia kijana mmoja na kumjeruhi mkono
wa kulia.
Tukio hilo liliamsha hasira kwa baadhi
ya madereva ambapo walianza kuzomea na kurusha mawe mfululizo katika
eneo ambalo Makonda alisimama pamoja na maofisa wa polisi.
Hali hiyo iliwafanya viongozi wa polisi,
wakiwamo Kamanda Mpinga, Wambura na wengine kujikusanya na kumkinga
Makonda kwa kutumia mikono.
Kisha walifanikiwa kumweka chini Makonda ili mawe yaliyokuwa yakirushwa ovyo yasimfikie.
Vurugu hizo ziliwalazimu askari wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufyatua mabomu ya machozi na risasi za
moto hewani ili kutawanya kundi kubwa la vijana.
Katika hali ya kushangaza, Makonda alisema anaunga mkono mgomo huo kwa sababu ni haki ya raia kudai haki yao.
“Mimi naunga mkono mgomo huu, kwa sababu
ni haki ya kila raia na huu ndiyo msingi wa kupata haki yako kwa
mtendaji asiyefanya kazi yake sawa sawa.
Mbowe aliwasili akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa, Patrobas Katambi, Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob na makada wengine.
Idadi kubwa ya madereva na umati mkubwa
wa vijana waliukimbilia msafara huo, na kuanza kushangilia huku
wakionyesha alama ya vidole viwili hewani.
MTANZANIA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya itakayoanza kutumika leo ambapo mafuta ya petroli na dizeli yamepanda huku mafuta ya taa yakishuka.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo, alisema bei ya jumla na rejareja ya mafuta aina zote imebadilika ikilinganishwa na bei elekezi iliyotolewa Aprili, mwaka huu.
Alisema bei ya rejareja kwa mafuta ya
petroli imeongezeka kwa Sh 111 kwa lita sawa na asilimia 6.32 huku
dizeli ikiongezeka kwa Sh 23 kwa lita sawa na asilimia 1.37.
“Kuanzia
leo lita moja ya petroli itauzwa kwa shilingi 1,866 kwa Jiji la Dar es
Salaam na shilingi 2,097 kwa mikoa ya pembezoni ikiwamo Kigoma ambapo
bei ya zamani ilikuwa ni shilingi 1,755 Dar es Salaam na shilingi 1,986
kwa Mkoa wa Kigoma,” alisema Kaguo.
Alisema mafuta ya dizeli yatauzwa kwa Sh 1,695 Dar es Salaam na Sh 1,938 kwa mikoani ambapo bei ya awali ilikuwa ni Sh 1,672.
Kaguo alisema mafuta ya taa yameshuka
kwa Sh 31 kwa lita sawa na asilimia 1.86 ambapo yatauzwa kwa Sh 1,624
Dar es Salaam na Sh 1, 867 kwa mikoani.
Alisema mabadiliko hayo yametokana na
kupanda kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia pamoja na kushuka
kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
“Wananchi
wategemee mafuta kupanda zaidi ifikapo Julai, mwaka huu kwani madhara
ya kupanda kwa dola ya Marekani na kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania
yataonekana,” Kaguo.
Akizungumza suala la uhaba wa mafuta
katika baadhi ya vituo vya mafuta nchini, alisema inatokana na kushindwa
kupakiwa kwa wakati.
Alisema tangu Mei Mosi mwaka huu
kulikuwa na mfululizo wa mapumziko ambayo yalikumbana na Jumatatu ya
mgomo wa madereva wa mabasi na malori ambayo ndiyo wasafirishaji wa
mafuta ndani na nje ya nchi.
MTANZANIA
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda amekabidhiwa tuzo ya kuwa meya bora barani Afrika.
Tuzo hiyo alikabidhiwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TANZANIA), Hawa Ghasia.
Meya Mwenda amefanikiwa kupata tuzo hiyo
katika kundi la mamlaka za miji ya kati ambayo ina majiji yenye idadi
ya watu isiyozidi milioni moja.
Akitaja sifa za tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty,
alisema vigezo hivyo ni pamoja na uongozi na dira katika utoaji wa
huduma kuchochea maendeleo, uadilifu, ubunifu na usimamizi bora wa
shughuli za halmashauri.
Natty alisema sifa nyingine ni
uhamasishaji wa jamii katika kushiriki masuala ya halmashauri, uwezo wa
kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, uwezo wa kusimamia ulinzi na
usalama wa wananchi ikiwamo kujenga mahusiano mazuri katika jamii.
Zawadi alizokabidhiwa Mwenda ni kikombe, cheti na fedha taslim kiasi cha dola za Marekani 100,000 sawa na Sh milioni 200.
Waziri Ghasia aliipongeza halmashauri
hiyo ikiwamo na kuishauri kutumia zawadi ya fedha walizopata kuzalisha
ajira kwa na akina mama wa Kinondoni.
NIPASHE
Mahakama ya katiba ya Burundi imemuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza
wa nchi hiyo, kuwania tena nafasi hiyo kwa awamu nyingine ya tatu na
kwenda kinyume cha katiba ya taifa hilo kumtaka kumaliza uongozi wake
kwa awamu mbili.
Wakati huo huo, makamu wa rais wa mahakama hiyo, Jaji Sylvere Nimpagaritse,
ameripotiwa kuondoka nchini humo kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo
ambao hauonyeshi uhalali wa rais wa taifa hilo kugombea tena nafasi hiyo
baada ya kumaliza vipindi vyake viwili vya uongozi.
Hata hivyo, uamuzi wa Mahakama hiyo
umeelezwa kuwakasirisha zaidi waandamanaji nchini humo wanaopinga
Nkurunzinza kugombea tena wadhifa huo na kusababisha vurugu kubwa.
Vurugu hizo zimesababisha maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbilia Tanzania na wengine Rwanda ili kunusuru maisha yao.
Jaji Nimpagaritse aliliambia Shirika la
Habari la Ufaransa kuwa mahakama hiyo ilikuwa inakabiliwa na vitisho vya
kuuawa majaji saba akiwamo yeye, iwapo isingemuidhinisha Rais
Nkurunzia kuwania tena nafasi hiyo na kuendelea kubaki madarakani.
Mahakama hiyo iliidhinisha uamuzi huo
kupitia taarifa iliyotolewa jana nchini humo huku maelfu ya waandamanaji
wakimiminika katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo wa Bujumbura,
wakipinga uamuzi huku wakisema umeenda kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa Chama tawala cha CNDD-FDD, Pascal Nyabenda, aliliambia Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) nchini humo kupitia ujumbe mfupi wa simu kuhusiana na maamuzi ya mahakama hiyo .
Tangu kuanza kutokea kwa vurugu hizo, polisi wanadaiwa kuua waandamanaji 13 mjini Bujumbura hadi jana.
Pia gazeti la serikali ya Rwanda la New Times, liliripoti kuwa, makamu huyo wa rais wa mahakama hiyo amekimbilia nchini Rwanda juzi.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ametuma ujumbe wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya hiyo, kwenda Burundi kuchunguza hali ya kisiasa ilivyo nchini humo.
Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa
suluhisho la kisiasa la matatizo ya sasa ya Burundi yatapatikana kwa
wananchi wa Burundi kuheshimimu Katiba na Sheria ya Uchaguzi na kuwa ni
jukumu la jumuia ya kimataifa kuisaidia nchi hiyo kuvuka katika
changamoto za sasa.
NIPASHE
Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii
iko hatarini kutopitishwa, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira kukataa kwa mara pili kuijadili.
Wabunge wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake, James Lembeli, walifikia uamuzi wa kutoijadili tena na kuwaamuru viongozi wa Wizara hiyo wakiongozwa na Waziri Lazaro Nyalandu, kurudi tena baada ya wiki moja wakiwa wametekeleza maagizo yaliyotolewa na kamati.
Maagizo hayo ni pamoja na kukaidi amri
ya Mahakama Kuu ya kukataa kuanza mara moja utekelezaji wa tozo mpya
kwenye Hifadhi za Taifa.
Lingine ni utaratibu wa kiingilio kwenye
hifadhi na kwamba tozo iliyotakiwa ni kila mtalii anapoingia anapoingia
anatozwa kiingilio na akitoka na kutaka kuingia tena ni lazima alipe.
Agizo lingine ni mgogoro wa mipaka
kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani. Kamati iliagiza kuwa mipaka ya
hifadhi hiyo ibaki kama ilivyokuwa tangu awali, lakini kinyume chake,
wizara imemega sehemu ya ardhi na kuitafutia hati miliki.
Kutokana na maagizo hayo, Kamati hiyo
juzi iliwaagiza viongozi hao wa Wizara ya Maliasili na Utalii kufika
katika kamati hiyo jana wakiwa na maelezo yote.
NIPASHE
Wabunge wameitaka serikali kushughulikia
kwa haraka msongamano wa magari jijini Dar es Slaam ikiwa ni pamoja na
kutaka viongozi wakuu wa serikali kutumia helkopta katika ziara zao
badala ya magari.
Walisema lengo ni kupunguza adha hiyo katika jiji hilo ambalo linachangia kwa asilimia kubwa uchumi wananchi.
waliitaka serikali kuruhusu barabara zinazojengwa na mradi wa magari yaendayo haraka jijini humo (DART), ikiwamo ya Morogoro, kuanza kutumiwa na daladala za kawaida na zile zinazomilikiwa na Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), wakati wakisubiri mabasi yanayotarajiwa kuletwa na mradi huo, ili kupunguza adha ya usafiri inayolikabili jiji hilo kwa sasa.
Wabunge hao walitoa kauli hizo katika
kikao cha kujadili rasimu ya mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka
2015/2016 kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jana jijini humo
kati ya Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Tume ya Taifa
ya Mipango na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Dk. Mary Nagu.
Mansoor Hirani, alisema
msongamano wa magari jijini humo ni janga la kitaifa na kwamba misafara
ya viongozi wakuu kutumia ‘vimulimuli’ ni moja ya chanzo, hivyo kutaka
viongozi hao kutumia helkopta kwa ziara zao.
Kadhalika, aliitaka serikali kuanza
kuruhusu daladala za kawaida na zinazomilikiwa na Uda, kuanza kutumia
barabara inayojengwa na mradi wa Dart wakati ikisubiri magari
yanayoelezwa kuletwa na mradi huo ili kuwapunguzia wananchi adha ya
usafiri.
Mjumbe mwingine, James Mbatia, aliitaka serikali kuwekeza kwa haraka katika jiji hilo kutokana na mchango wake mkubwa katika kuinua uchumi wa Taifa.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk. Philip Mpango,
alitaja baadhi ya changamoto ambazo walikumbana nazo wakati wa kupanga
bajeti ya mwaka huu kuwa ni ufinyu wa rasilimali fedha, kashfa ya Escrow
kwani iligusa hata wale ambao serikali ilitarajia kwenda kuwakopa na
malimbikizo ya madeni kwa wakandarasi na wazabuni.
NIPASHE
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
amezindua timu ya wataalamu 25 ambao wamechaguliwa kwa ajili ya
kuwakilisha serikali katika mazungumzo yote ya mikataba na kampuni za
gesi asilia.
Lengo la kuundwa kwa timu hiyo ni kuleta
mikataba yenye manufaa makubwa kijamii na kiuchumi kwa ajili ya
Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Timu hiyo ambayo lengo lake pia ni
kutatua masuala ya uchumi endelevu wa gesi inajumuisha wataalamu kutoka
ofisi na taasisi mbalimbali kama Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya
Fedha, Wizara ya Kazi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TANESCO.
Nyingine ni TPDC, Tume ya Mipango,
STAMICO, Ofisi ya Waziri Mkuu, Benki Kuu, TRA, Wizara ya Viwanda na
Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, TAMISEMI na NEMC.
Akizindua timu hiyo, Balozi Sefue
alisema kwamba mpango huo utawawezesha kuwapatia wataalam wa kufanya
mazungumzo yenye ueledi na mafanikio kwa Taifa.
Pia aliishauri timu hiyo kujitolea
kujifunza, kuelewa, kufikiria kimkakati, kusimamia, kutafiti, kuchunguza
na muhimu zaidi kufanya mazungumzo vizuri kwa niaba ya serikali kwa
ajili ya maslahi ya Tanzania kwa sasa na hata baadaye.
“Kufanya
mazungumzo ya mikataba ya mafuta na gesi asilia na kampuni za kimataifa
ya mafuta ni changamoto kubwa kwa serikali za nchi zilizobarikiwa na
rasilimali nyingi kutoka Afrika, changamoto ambayo lazima itatuliwe,”.
Balozi Sefue alisema kampuni za
kimataifa za mafuta zina uwezo mkubwa wa kuleta wataalamu wao waliobobea
katika fani za uhandisi, kiuchumi na kisheria kutoka duniani kote na
wenye uzoefu wa muda mrefu.
HABARILEO
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon amesema dunia ina imani kubwa na Rais Jakaya Kikwete
na wajumbe wengine wa Jopo la Watu Maarufu Duniani waliopewa jukumu la
kutafuta jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na magonjwa ya milipuko,
kama vile ebola, katika siku zijazo.
Aidha, Ki-moon amewaambia wajumbe hao
kuwa uteuzi wao uliofanywa na yeye mwenyewe mwezi uliopita umefanyika
baada ya majina yao kuwa yamependekezwa na taasisi nyingine za
kimataifa, mbali na Umoja wa Mataifa na ni matarajio yake kwamba jopo
hilo litakuja na mapendekezo yanayolenga kuifanya dunia mahali bora
zaidi pa kuishi.
Aliyasema hayo juzi wakati alipokutana
na kuzungumza na wajumbe wa jopo hilo ofisini kwake katika Makao Makuu
ya UN mjini New York, muda mfupi kabla ya wajumbe hao kufanya kikao chao
cha kwanza chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete.
“Nawashukuru
sana kwa kukubali uteuzi wangu. Dunia ina imani kubwa na uwezo wenu
katika kutuwezesha sote kukabiliana kwa kujiamini zaidi na magonjwa ya
milipuko katika siku zijazo,” Ki Moon aliwaambia wajumbe hao
sita ambao wamepewa hadi Desemba mwaka huu kuwasilisha Ripoti kuhusu
namna gani dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya
milipuko.
Mbali na Rais Kikwete ,ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo hilo, wajumbe wengine ni Celso Amorim wa Brazil, Micheline Calmy-Rey wa Uswisi, Marty Natalegwa wa Indonesia, Joy Phumaphi wa Botswana na Rajiv Shah wa Marekani.
Rais Kikwete amemshukuru Ki -moon kwa
uteuzi wa jopo hilo akisisitiza kuwa uteuzi huo unaonyesha ni kiasi gani
UN ina imani katika uwezo wa wajumbe wa Jopo kuifanya kazi hiyo vizuri.
No comments:
Post a Comment