Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, anaweza kuingia katika vitabu vya kumbukumbu kutokana na staili yake ya kuuaga uwanja wa kisiasa kwa kutazama tatizo la ajira kwa vijana, ambalo ni tatizo sugu na limekuwa likizungumziwa kisiasa kama bomu linalosubiri kulipuka.Alipowaaga wananchi wake kwa kuwaachia kitega uchumi chenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.
Ndesamburo, amekuwa mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini
kwa vipindi vitatu mfululizo; yaani kuanzia mwaka 2000 hadi 2015 na
sasa ametangaza rasmi kutogombea ubunge.
Hoja hapa siyo kustaafu ubunge, ila ni staili
aliyoitumia kustaafu pale alipoamua kujenga soko la kisasa na kuliita
“Kiborlon Shopping Centre” na kuwapa hisa wafanyabiashara kadhaa wadogo,
maarufu kama Wamachinga.
Ndesamburo anasema amejenga soko hilo kubwa kuliko
yote katika mikoa ya Kaskazini, kama njia ya kutatua tatizo la muda
mrefu la wafanyabiashara wadogo na kati. Soko hilo lina runinga kubwa
katika mlango wake mkubwa ikiwa na stesheni mbalimbali za televisheni na
lina vibanda zaidi ya 200 vya maduka na eneo la kuchukua “Machinga” na
wauza mitumba 1,000.
Ujenzi wakwepa fitina za kisiasa
Ndesamburo anasema isingekuwa rahisi kwa
wafanyabiashara wadogo na wa kati kujikusanya na kuchanga fedha za
kujenga soko hilo la kisasa.
“Tatizo la maeneo ya kufanyia biashara kwa
Machinga na wafanyabiashara wa kati ni kubwa sana na nilipokuwa mbunge
kwa mara ya kwanza mwaka 2000 niliahidi kushughulikia tatizo hili,”
anasema.
Anasema alibaini Halmashauri ya Manispaa ya Moshi
wakati huo ikiongozwa na CCM, ilikuwa haina mpango wa kutenga eneo kwa
ajili ya Wamachinga na kwamba hata mikakati iliyowekwa ilikuwa ni ya
muda na haiwasaidii wengi.
“Hapo ndipo niliponunua eneo hili na kutoa wazo
kwa Serikali kwamba kwa kupitia mpango wa PPP (ubia serikali na sekta
binafsi) tujenge soko la kisasa la Mitumba na Machinga,” anasema
Ndesamburo.
Ndesamburo anasema wazo lake hilo lilikataliwa na
viongozi wa Serikali ya CCM kwa sababu za kisiasa kwamba kama
kungejengwa soko la wafanyabiashara hao, basi jina lake lingepanda
chati.
“Kwa sababu ya vita kubwa ya kisiasa ndani ya
Jimbo letu nikaamua nijenge mwenyewe lakini swali likawa je, hawa
madiwani wa CCM wangekubali kunipitishia michoro ya soko?” Anasema
akifafanua:
“Nikachora ramani na ikapitishwa kwa jina la mhindi. Sikutumia
jina langu kwa sababu kama ningelitumia wasingekubali,” anasema
Ndesamburo ambaye pia ni mfadhili wa Chadema.
“Nilipoanza kutaka kujenga, usalama wa Taifa, Gama
na Manispaa wote walikuja hapa kuzuia nisijenge lakini wakati huo
tayari nilishakuwa na vibali vyote vya ujenzi kwa jina la Mhindi.”
‘Vita vya panzi’
Ndesamburo alidai pamoja na soko kukamilika,
lakini wapo makada wa CCM ambao wameshika vyumba vya biashara lakini
hawavifungui ili dhana ya kuwapo kwa soko isiwepo.
“Nimesema yeyote asiyefungua tutawapa watu
wengine. Yeyote ambaye hata kama amelipa deposit (dhamana)
tunamnyang’anya na tutakata fedha yetu ya kukodisha,” anasema
Ndesamburo.
Mbunge huyo anasema ametoa ‘ofa’ kutoka sasa hadi
Julai Mosi, mwaka huu, wafanyabiashara waliochukua maeneo ya biashara
katika soko hilo wafanye biashara bure na baada ya hapo ndiyo wataanza
kulipa kodi.
Ndesamburo anasema wafanyabiashara wote
watakaomuunga mkono kwa kufungua biashara zao kuanzia jana, watakuwa
wana hisa wa soko hilo ili kuondoa propaganda chafu alizodai zinaenezwa
na CCM. “CCM wanapita huko na huko wanasema hiki ni kitega uchumi cha
mtu binafsi lakini mimi nasema hawa waliokodi vibanda hapa watakuwa
wanahisa. Tutaendesha pamoja hili soko,” anasema.
“Siyo hivyo, lakini nimeamua kuagiza mitumba moja
kwa moja kutoka Ulaya kwa wafanyabiashara watakaotumia soko hili. Bei
yake itakuwa chini ya wanaonunua hapa nchini.”
Kodi ni mzozo
Pamoja na ofa nyingi zilizotolewa na Ndesamburo
baadhi ya wafanyabiashara, wanaona kodi ya Sh100,000 kwa mwezi kwa
vibanda katika soko hilo ni kubwa na kutaka ipungue hadi Sh50,000 kwa
mwezi. Hamisi Shemdoe ni mfanyabiashara wa kutembeza viatu na anasema
anatamani kukodisha kibanda, lakini hawezi kumudu kodi ya Sh100,000 kwa
mwezi labda angepewa kwa Sh30,000 au 50,000.
Hata hivyo, Ndesamburo mwenyewe anasema milango ya
majadiliano haijafungwa, hivyo wale wenye maoni na michango ya namna ya
kuboresha huduma za soko hilo, wako huru kumuona.
Pamoja na mipango hiyo, watu wengi wana wasiwasi
kwamba chokochoko za kisiasa zinaweza zikakwamisha uzuri na shughuli za
kibiashara katika soko hilo.Hayo yanazungumzwa huku kukiwa na imani kwamba kwa kuwa soko hilo limejikita kwa faida ya jamii, siasa kamwe hazina nafasi.
No comments:
Post a Comment