15 May, 2015

Hakijaeleweka, Burundi bado tete


Image result for machafuko burundi leo may 15,2015 
Hali bado si shwari Burundi. Vituo vitano vya redio ikiwamo ya Taifa na ile ya African Public Radio (RPA) kilichokuwa kimefungwa na Serikali ya Burundi vilishambuliwa jana huku kukiwa kukiwa hakuna taarifa za uhakika za nani anayeitawala nchi hiyo kwa sasa Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya
Meja Jenerali Godefroid Niyombare kutangaza kumpindua Rais Pierre Nkurunziza wakati akiwa Tanzania katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa kikatiba wa Burundi.
RPA ilipigwa kombora la roketi ikielezwa kuwa askari wanaomtii Rais Nkurunziza ndiyo waliotekeleza shambulizi hilo.
Kituo hicho cha RPA kilifungwa na Serikali baada ya kuanza harakati za kumpinga Nkurunziza lakini kilianza kurusha matangazo yake juzi na usiku wa kuamkia jana kikapigwa kombora hilo.
Mbali na kituo hicho, vituo vya redio vilivyolipuliwa vinaelezwa kufanya harakati za kuipinga Serikali.
Vituo hivyo vilishambuliwa usiku wa kuamkia jana muda mfupi baada ya waandamanaji kuvamia kituo cha redio na televisheni ya Rema, vinavyohusishwa na chama tawala.
“Tunalaani mashambulizi kwa vyombo vya habari inatakiwa waandishi waachwe wafanye kazi zao,” alisema Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Habari Burundi, Alexandre Niyungeko.
Alisema hakufahamu hasa ni nani aliyeshambulia vituo hivyo na kwamba yamefanyika wakati jeshi liliahidi ulinzi katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, taarifa zilizochapishwa na Gazeti la Jeune Afrique zilisema vituo vya redio vilivyolipuliwa ni vitano, viwili vikilipuliwa na polisi, kimoja na waasi wanaomuunga mkono Jenerali Niyomare na viwili vikichomwa na waandamaji.
Nkurunziza atuma ujumbe
Rais Nkurunziza alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akiwataka wananchi wake kutulia kwa kuwa jeshi limezima majaribio yote ya mapinduzi.
Hata hivyo, Rais Nkurunziza ameendelea kubaki Dar es Salaam hasa baada ya kutangazwa kufungwa kwa mipaka ukiwamo Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Burundi, Leontine Nzeyimana alithibitisha kuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza yupo Tanzania.
Nzeyimana aliyasema hayo jana akiwa katika Hoteli ya Serena ambako wakuu wa nchi za Afrika Mashariki walikutana kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi.
“Bado yupo, lakini baadaye anaweza kuondoka,” alisema kwa kifupi waziri huyo bila kubainisha eneo alipo Rais huyo.
Baadaye Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Laurent Kavakure alisema jijini Dar es Salaam kwamba Rais Nkurunziza alitarajiwa kuondoka jana kurudi nyumbani na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salvatory Rweyemamu alisema jana kwamba kiongozi huyo alishaondoka nchini.
Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vikiwamo vya Burundi, vimekuwa vikihoji aliko Rais Nkurunziza ambaye alielezwa kuondoka baada ya mkutano wa usuluhishi juzi na kurejea Dar es Salaam baada kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Juzi, Meja Jenerali Niyombare alitangaza kuwa jeshi limemtimua Nkurunziza na kuunda Serikali ya mpito kuongoza nchi hiyo.
Mara baada ya taarifa hiyo, Nkurunziza hakuweza kuhudhuria mkutano Ikulu na baadaye ilielezwa kuwa anaondoka kurudi Burundi. Hata hivyo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa alilazimika kurejea nchini kutokana na sababu za kiusalama.
Alipoulizwa jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Tanzania, Bernard Membe alisema hajui alipo kiongozi huyo akisema hataki kuzungumzia suala la alipo kiongozi huyo na kwamba viongozi wa Afrika Mashariki watakutana tena Jumatatu ya wiki ijayo kujadili hali halisi ya Burundi.
Mapigano makali Bujumbura
Kumekuwa na mapigano makali ya kurushiana risasi Bujumbura kati ya majeshi na vikundi vinavyopingana nalo na wanajeshi takriban watano wameelezwa kuuawa.
Mwandishi wa BBC, Maud Jullien alisema mapigano hayo yalikuwa yanalenga kuiteka Televisheni ya Taifa.
Wakazi wa Burundi wameamka huku wakiwa na sintofahamu kuhusu nini kinaendelea baada ya kuelezwa kuwepo kwa mapinduzi.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...