01 May, 2015

MAGAZETINI LEO MAY 1

Image result for fridayMTANZANIA
Vyama vinavyoundwa na Umoja wa katiba ya Watanzania UKAWA vimeibua madai mapya ya kuwepo njema za Serikali za kutaka kusogeza uchaguzi mkuu hadi 2017.
Kwa mujibu wa Umoja huo Serikali ipo katika maandalizi ya kupeleka muswada wa sheria Bungeni ili kumwongezea miaka miwili Rais Jakaya Kikwete abaki madarakani.

Viongozi wa UKAWA walisema njama hizo za Serikali zitaungwa mkono na  na wabunge wote wakiwemo baadhi wapinzani kwa maslahi yao wenyewe.
“Wanaona wakifanya uchaguzi huu mwaka huu wataanguka kwa sababu dalili zinaonyesha hata mgombea wao wa Urais ataanguka, wanaona wasogeze kidogo ili iwe rahisi kwao”
“Wanafikiri kwa vile wabunge wanasema wana njaa, tukisema tuwaongezee miaka miwili watapigiwa makofi wawe wa upinzani au wa CCM…hayo ndiyo matumaini yao.
Mwenyekiti wa NEC Damian Lubuva alikanusha taarifa hizo na kusema ni hisia za viongozi hao na hakuna mpango wa aina hiyo.
NIPASHE
Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kujikaanga kwa mafuta yake, iwapo kitachelewa kutangaza mgombea urais katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Sumaye alisema hayo baada ya kuombwa na waandishi wa habari mjini hapa, wakimtaka azungumzie hali ya kisasa nchini, uchaguzi mkuu ndani ya CCM na hali ya utekelezaji wa adhabu ya kifo dhidi ya watu waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Alisema wengi wana shauku ya kufahamu atakayepeperusha bendera ya CCM kugombea urais, hiyo ikiwa ni kutokana na kupewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo, na kwamba katika hali isiyo ya kawaida kimechelewa kumtaja.
“Anapotangazwa mapema watu wanatafiti, kufahamu ubora wake na kuwa na msimamo wa kumchagua, hata mgombea anapata muda wa kutosha kufikiri na kufanya kampeni za kutosha,” alieleza.
Alisema pia hiyo itasaidia wapinzani kukosa muda wa kutosha kumshambulia mgombea anapotangazwa kwa kuchelewa, hata yeye mgombea anaathiriwa kwa kutopata muda wa kutosha kufanya kampeni.
Wananchi nao hawapati muda wa kutosha kutafiti ili kufahamu ubora wake, ikiwa ni pamoja na kumhoji maswali, ili wasifanye uchaguzi kwa kufuata mkumbo.
“Hata mimi hali hii sijaielewa, katika hali ya kawaida sasa hivi wenye nia ya kugombea wangeshachukua fomu na kuingia mikoani kutafuta wadhamini, kwa mfano, uchaguzi wa mwaka 2005, mgombea alitangazwa Mei 05,Sumaye,
Sumaye alisema anaamini siku siyo nyingi ratiba ya wenye nia ya kuwakilisha chama katika kugombea urais, ubunge na udiwani itatolewa na chama hicho.
NIPASHE
Siku tatu baada ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (TABOA), kuendelea na msimamo wa kugoma nchi nzima kupinga nauli mpya, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imenywea na kufuta agizo lake la awali la kupunguza nauli hizo.
Badala yake, Sumatra imetangaza kusitishwa utekelezaji wa viwango vipya vya nauli vilivyotangazwa hivi karibuni na kutaka vya zamani viendelee.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sumatra kwa vyombo vya habari, jana jijini Dar es Salaam, na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Gilliard Ngewe, utekelezaji utasitishwa hadi marejeo yatakapofanyika tena.
“Sumatra imepokea kutoka kwa msafirishaji ABC Trans na Afritrans Limited maombi ya kupitia upya maamuzi yake ya kushusha viwango vya nauli za mabasi ya masafa marefu yalitolewa Aprili 15, mwaka huu.  Maombi ya Kampuni mbili yalipokelewa Sumatra Aprili 29, mwaka huu, ,” alisema.
Alisema kwa sasa viwango vya nauli vya zamani vitaendelea kutumika hadi hapo umma utakapotaarifiwa vinginevyo.
Afisa Uhusiano wa Sumatra, David Mziray, alisema sheria inatoa haki kwa wahusika kukata rufaa ndani ya siku 14 na kwamba kwa sasa wanapitia hoja zao kuona kama zina mashiko ndipo watatoa maamuzi ambayo yatawekwa wazi.
Alisema viwango vipya vya nauli vilitolewa baada ya kukokotoa na kwamba kwa mujibu wa kanuni na kwamba mambo yatawekwa wazi ndani ya siku 14.
MWANANCHI
Mwanasiasa mkongwe aliyevuliwa uanachama wa CCM, Hassan Nassor Moyo  amesema yeye ndiye aliyefanya kazi kubwa, usiku kucha, kumshawishi Maalim Seif Sharrif Hamad, aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, akubaliane na matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 kabla ya hata kutangazwa.
 Moyo alisema alitumwa na Rais Amani Abeid Karume kufanya kazi hiyo kwa bidii, utiifu na uadilifu hadi akafanikiwa.
Moyo alifanya kazi mbalimbali akiwa waziri kwenye Baraza la Mapinduzi Zanzibar na akiwa waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika maisha yake ya utumishi wa kisiasa, lakini akajikuta akipata tuzo ya kuvuliwa uanachama wa CCM akiwa ameshastaafu siasa kwa madai ya kuhudhuria mikutano ya hadhara ya CUF.
Moyo alisema kuwa Mohamed Riyami, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, alikwenda nyumbani kwake na kumpa ujumbe huo kutoka kwa Rais Karume, na baada ya majadiliano naye, alikubali.
“…Ni kweli Mohamed Riyami alikuja kuniamsha saa 10:00 alfajiri hivi akisema ametumwa na Rais Karume aje aniambie nikamwombe Maalim Seif aridhie matokeo ya uchaguzi mkuu yatakayotangazwa,”  Moyo.
Alipoulizwa kama ni kweli maneno hayo tu ndiyo yalimlainisha Maalim Seif aridhie matokeo hayo, Moyo alijibu; “Hapana, nilizungumza naye kwa kina historia ya mabadiliko, tulikotoka, kufikia kuundwa kwa kamati za miafaka mpaka sasa, naye alikubali.”
MWANANCHI
Ndege iliyokuwa imembeba rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton na mwanaye Chelsea, juzi ilipata hitilafu katika moja ya injini zake na kulazimika kutua Dodoma kwa ajili ya matengenezo kabla ya kuendelea na safari.
Ndege hiyo aina ya DHC 7 yenye namba za usajili 5Y-CDK, iliyokuwa ikitokea mkoani Iringa kuelekea Ziwa Manyara, ilitua saa 10.15 jioni juzi  na kuondoka saa 10.24 jioni.
Chanzo cha habari kutoka uwanja huo wa ndege, kilisema ndege hiyo ilikuwa na tatizo dogo na lilirekebishwa wakati Clinton na abiria wengine wakiwa ndani ya ndege.
“Tulimuuliza rubani wa ndege hiyo kama angehitaji msaada wowote kutoka kwetu, lakini alisema kuwa ni tatizo dogo tu na angeweza kutua mwenye bila msaada na akafanya hivyo,” .
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, (TCAA),  Ludovic Ndumbaro alikataa kulizungumzia kwa madai yeye si msemaji wa mamlaka hiyo.
Mtafute mkurugenzi ndiyo msemaji wa mambo yote yanayohusu mambo ya anga,”
Clinton na binti yake Chelsea walifika Tanzania kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na mfuko wa familia ya Clinton.
Clinton ataendelea na ziara yake ya siku tisa katika nchi za Kenya, Liberia na Morocco. Miradi inayosimamiwa na mfuko wa Clinton ni ya kilimo cha kibiashara.
MWANANCHI
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa amemtaka Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha za Mfuko wa Barabara katika mkoa wa Dar es Salaam ili kujihakikishia kura ikiwa atagombea Urais kama anavyotajwa.
Silaa alitoa kauli hiyo juzi wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Uhuru iliyopo katika Manispaa ya Ilala.
Alisema mkoa wa Dar es Salaam una wapigakura wengi wanaoweza kuamua kupita au kushindwa kwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Meya huyo kijana alibainisha kuwa Manispaa ya Ilala na zile za Temeke na Kinondoni, zimekuwa zikipata fedha kidogo kutoka Mfuko wa Barabara, licha ya kuchangia fedha nyingi kwenye mfuko huo.
Nakuomba  katika bajeti yako ya 2015/16 iangalie Dar es Salaam kwa jicho la huruma. Nikuhakikishie katika takwimu za makadirio ya Sensa za Watu na Makazi za mwaka 2012, jiji hili lina wapigakura 2.3 milioni sasa mzee kama yanayosemwa semwa na yenyewe yamo, hebu iangalie Dar es Salaam kwa jicho la huruma,”  Silaa
Silaa alisema manispaa yake inapata Sh 4.1 bilioni kwa mwaka, lakini barabara ya kilomita moja inajengwa kwa Sh2.95 bilioni, hivyo uwezo wa halmashauri hiyo kuzihudumia barabara zote ni mdogo mno.
MWANANCHI
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) Maynard Swai, ametangaza kuwania ubunge katika Jimbo la Hai kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa tangazo hilo, Swai sasa atakuwa na kibarua kizito cha kukabili upinzani kutoka kwa mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Freeman Mbowe (CHADEMA) ambaye tayari ametangaza nia ya kutetea nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hata hivyo, wakati kurudi kwa Mbowe kwenye kinyang’anyiro cha ubunge jimboni humo kutategemea uamuzi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao utalazimika kumkubali au kumkataa kupitia vikao vyake vya kupanga wagombea.
Swai anatakiwa kupita kwenye kura ya maoni ndani ya CCM, kabla hajawa mgombea rasmi.
Swai ambaye ni kada wa kwanza wa CCM kufungua pazia la kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Hai, alisema jana kuwa dhamira yake ni kufanya kazi na wananchi ndani ya jimbo hilo, tofauti na sasa ambapo wawakilishi wengi wanaomba kura na wakipata wanahamia Dar es Salam.
Nimeamua kuingia kwenye siasa niendelee kuwatumikia wananchi. Ifike mahali kiongozi anayechaguliwa aishi na wananchi ili ajue shida zao, matatizo yao na changamoto walizonazo na siyo unapewa heshima na wananchi, lakini ukipata huonekani ukiwatumiakia,” Swai.
Alisema iwapo chama kitampa ridhaa ya kugombea, atahakikisha anawaweka vijana pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili likiwemo suala la ajira.
HABARILEO
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema ajali za barabarani zinachangiwa na uzembe wa taasisi inayosimamia sekta ya usafiri jambo linalogharimu maisha ya watu wasio na hatia, na kuitaka taasisi hiyo kuchukua hatua na kuhakikisha nidhamu inarejea kwenye sekta hiyo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ndiyo yenye dhamana ya kusimamia na udhibiti wa sekta ya usafiri katika nchi kavu na majini.
Sitta aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari wakati Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilipokuwa ikizungumza na viongozi wa wizara hiyo.
Sitta alisema “Hakuna kitu kinachoniuma kama ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na uzembe, ubovu wa magari na matairi ya mtumba, halafu baya zaidi ni kwamba Mamlaka husika ya kudhibiti vyombo hivyo ipo, inaona na kuwasamehe makosa,” Sitta.
Aliongeza, mamlaka husika zina wajibu wa kusimamia vyombo hivyo na kuhakikisha vile vinavyofanya makosa vinachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuvifutia leseni, kwani matukio mengi ya ajali yanatokana na uzembe na kuanzia sasa masuala ya msamaha yasiwepo.
Sitta aliongeza, wamiliki wa vyombo vya moto na madereva, wanapaswa kufuata sheria za barabarani na kuhakikisha wanazitii na kwamba vyombo hivyo vinapaswa kuwa na vipuri vyenye viwango na kuhakikisha mabasi yanayokwenda umbali zaidi ya kilometa 700, yawe na madereva wawili.
“Ipo sheria inayozungumzia umbali unaotakiwa dereva mmoja aendeshe gari, lakini pia nilizungumza na daktari kuhusu umbali unaokubalika kwa madereva kuendesha chombo cha moto, aliniambia dereva mmoja hatakiwi kuendesha gari kwa umbali wa zaidi ya kilometa 700, zaidi ya hapo inabidi wawe madereva wawili,” Sitta.
Alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba kwa umbali huo, wa kilometa 700 dereva huwa amechoka na akienda zaidi ya hapo anaweza kusababisha ajali kwa kuwa akili na mwili vimechoka hivyo hawezi kuwa makini barabarani.
Akizungumzia ubovu wa mabasi ya abiria na daladala, Sitta alisema magari yote mabovu, yanapaswa yasiwepo barabarani, kwani kuwepo kunachangia ajali kwa njia moja au nyingine.
Kuhusu mgomo, Sitta alisema nchi inaongozwa kwa sheria na kwamba sio kila kitu kinachofanywa na serikali ni masuala ya siasa, hivyo sio sahihi madereva na wamiliki wa mabasi kugoma kutoa huduma kwa abiria.
HABARILEO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuamuru Mbunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar, Abdallah Sharia Ameir (CCM) kutoa Sh 200,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto wake wa kiume, mwenye umri wa miaka mitatu na nusu, anayedaiwa kumtelekeza.
Pamoja na amri hiyo, Hakimu Mkazi, Hellen Liwa alisema mbunge huyo atatoa kiasi hicho cha fedha kuanzia siku alipokoma kutoa matunzo na matibabu kwa mtoto huyo, anayetajwa kuwa ni mlemavu.
Pia, aliamuru mtoto huyo kulelewa na wazazi wake na siyo bibi yake, kama alivyokuwa akitaka mbunge huyo. Hivyo ataendelea kukaa na mama yake.
Kwa upande wake, Wakili Gideon Mandes aliyekuwa akimtetea Hawa Deus aliyekuwa mke wa mbunge huyo, alisema kupitia hukumu hiyo Mahakama imetoa uamuzi wa haki.
“Kupitia hukumu hii nimebaini wazazi wanawajibu wa kumtunza mtoto wanayemzaa bila ya kujali hali yake hata kama ni ya ulemavu asitelekezwe na imedhihirisha hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba sheria ipo sawa kwa kila mtu,”.
Wakili huyo aliwashauri Watanzania wenye matatizo na changamoto kama hizo, kuweka bidii ya kuijua sheria na taratibu zake ili waweze kuitumia kupata haki na suluhisho kupitia Mahakama.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...