MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Anna Mgwira
amesema chama hicho hakina matatizo na Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) na hata sasa kinasubiri majibu ya barua yao waliyoituma kwa
umoja huo kuomba kuunganishwa. Mgwira alitoa kauli hiyo wakati chama
hicho kilipofanya
ziara ya kutembelea hospitali ya mkoa ya Mt Meru
kugawa zawadi mbalimbali katika wodi ya kinamama ikiwa ni njia ya
kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.
Alisema ACT-Wazalendo wanaunga mkono muungano wowote wa vyama vya upinzani nchini ulio halali.
“Hatuna matatizo na Ukawa tunaunga mkono muungano wowote wa upinzani ulio halali,” alisema kiongozi huyo
Alisema tangu waandike barua ya kuomba mwongozo wa namna ya kujiunga na Ukawa, bado hawajapata mrejesho.
“Tunatamani
kuunganisha nguvu katika siasa za vyama vya upinzani na sasa tunasubiri
majibu ya barua yetu ya kuomba kuingia Ukawa,” .
Alisema kuwa chama hicho kimepokewa
vizuri na wananchi wa mikoa mbalimbali nchini na katika ziara ya awamu
ya kwanza walifanikiwa kuingiza jumla ya wanachama wapya 700.
“Tumepokewa vizuri mikoani tumefanikiwa kuingiza wanachama wapya na hoja ya umoja na uzalendo watu wameipokea vizuri,” Mgwira.
Akipokea misaada katika hospitali hiyo
Muuguzi Mfawidhi, Sifael Masawe alisema kwamba misaada hiyo itasaidia
kupunguza shida za wagonjwa.
MWANANCHI
Makada watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ambao ni miongoni mwa wanaotajwa kutaka kuwania nafasi ya urais,
wamefanya uamuzi mgumu wa kutangaza kutogombea tena ubunge kwenye
majimbo yao.
Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa .
Wengine ambao wanatajwa kuutaka urais na tayari wametangaza kutogombea tena ubunge ni Spika wa Bunge, Anna Makinda , na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wakati wabunge hao wakitangaza kuachana na kiti hicho cha uwakilishi, wengine; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira , Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu wamesema watarudi tena kwenye ubunge kama watashindwa urais.
Mei 26 mwaka 2013, Sitta alikaririwa na
vyombo vya habari akisema anafikiria kustaafu ubunge, na tayari
ameshawaambia wapigakura wa Urambo Mashariki juu ya azima yake hiyo.
“Viongozi wenzangu msipende kung’ang’ania madaraka. Nawaombeni mjifunze kusema yatosha…staafuni kama ninavyotaka kufanya mimi,”
alisema Sitta katika Kongamamo la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali
la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St.
Augustine (Saut), Mwanza.
Kwa upande wake, Membe alitoa kauli ya kustaafu ubunge Januari Mosi 2013 kwenye sherehe za Mwaka Mpya nyumbani kwake. Alisema, “Unajua nimekuwa mbunge wenu kwa kipindi cha tatu. Hivi leo ninawaaga rasmi kuwa sitagombea tena nafsi hii ya ubunge.”
Lowassa, amekuwa Mbunge wa Monduli kwa
zaidi miaka 20 na kutokana na azma yake ya kutaka kugombea urais,,
makada kadhaa wa CCM wameanza kupigana vikumbo kumrithi.
Baadhi ya makada wanaoanza safari ya
kumrithi Lowassa Monduli ni aliyewahi kuwa Katibu Uenezi wa CCM Mkoa wa
Arusha na Diwani wa Monduli Mjini, Loata Sanare na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Namelok Sokoine, ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani marehemu Edward Moringe Sokoine.
Pinda ambaye tayari ameshatangaza nia ya
kugombea urais alieleza Agosti 17, 2010 kuwa hatagombea tena ubunge
katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Pinda aliirudia kauli hiyo katika
mkutano wa hadhara jimboni kwake akisema muda wa kuwa mbunge umetosha na
sasa anatafuta kitu kingine cha kufanya.
TANZANIADAIMA
Mtoto mchanga wa kiume wa siku tatu
katika mtaa wa Masanga Wilaya ya Igunga ameokotwa akiwa amekatwa viungo
vyake na watu wasiojulikana.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Masanga Julius Kitundu alisema mtoto huyo aliokotwa na wasamaria wema pembezoni mwa barabara ya lami.
“Kwa
kweli kitendo kama hiki kimetusikitisha na watu waliofanya kitendo hicho
wanapaswa kusakwa kwa nguvu zote na kufikishwa kwenye vyombo husika” Kitundu.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wananchi
kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kuwaomba watoe
ushirikiano kwa jeshi la Polisi katika kuwasaka wahusika.
Baadhi ya wananchi wamelaani kitendo
hicho cha kinyama na kusema wataanzisha msako mkali ili kuhakikisha
waliohusika wanakamatwa na mama aliyejifungua anashikiliwa.
NIPASHE
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mwendokasi jijini Dar es Salaam (Dart), Dk. Asteria Mlambo, amewataka waathirika waliojihifadhi kwenye makalavati ya barabara hizo eneo la Jangwani kuondoka mara moja.
Pia amewaagiza watendaji wa Dart
kuwaelimisha na kuwashauri waondoke kwa hiyari kwenye maeneo hayo hadi
leo jioni kwani si mahali sahihi pa makazi.
Dk. Mlambo alisema jana kuwa eneo ambalo
wakazi hao wamejihifadhi ni kwa ajili ya matumizi ya barabara na siyo
makazi hivyo waondoke.
Alisema, watu hao wanaweza kuiharibu
miondombinu kwa kuwa haikujengwa kwa ajili ya hifadhi ya watu bali kwa
atumizi ya barabara, hivyo shughuli zisizofaa zinazoendelea zitaharibu
miundombinu.
“Tayari
nimeshawaagiza wafanyakazi wa Dart, waende kuzungumza nao ili waondoke
wenyewe kwa hiyari na ifikapo kesho jioni (leo), asionekane mtu yeyote
kwenye eneo lile la kituo cha mabasi ya mwendokasi,”Dk. Mlambo.
Alisema wamebaini kuwa wakazi hao ni
wale ambao walipewa viwanja eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni,
lakini hawakutaka kwenda huko na pia wengi wao siyo wenye nyumba bali ni
wapangaji.
“Wakazi
wa mabondeni serikali inawajali, lakini wenyewe hawajijali, wamepewa
maeneo rasmi hawataki kwenda, wamembiwa wahame, lakini hawataki, sasa
sijui wanataka nini,” .
Katika eneo hilo, Wafanyakazi wa Kampuni
ya Ujenzi wa Barabara hiyo Strabag, wakiendelea na shughuli za
kusafisha eneo hilo huku mvua ikiendelea kunyesha.
Rais Jakaya Kikwete, juzi alifika eneo
hilo kujionea hali ya mafuriko na kuwaagiza Wakala wa Barabara Tanzania
(Tanroads, kusafisha eneo hilo la daraja kwa kuzoa taka pamoja na
mchanga.
Rais Kikwete alisema taka pamoja na
mchanga uliojaa katika eneo hilo la daraja ndio unasababisha maji kujaa
na kusababisha kupita juu ya daraja badala ya chini ya daraja.
NIPASHE
Serikali imekanusha kuuza eneo la Polisi
Oysterbay, jijini Dar es Salaam, bali imeingia ubia na mwekezaji
binafsi ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kupunguza tatizo la nyumba kwa
askari.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali, bungeni jana.
Machali alitaka kujua kauli ya serikali
kuhusiana na eneo hilo ambalo linadaiwa kuuzwa kupitia Mpango wa
Ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi (PPP), ili yajengwe maduka
makubwa.
“Serikali ina kauli gani kuhusiana na jambo hilo wakati inasema kuwa ina mpango wa kujenga nyumba kwa polisi,” alihoji mbunge huyo.
Silama alisema mbia huyo atajenga nyumba za polisi 350 nchini na ameanza kufanya hivyo.
Naye Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema katika wilaya ya Rombo nyumba za polisi zimejengwa kwa mabanzi na zina wadudu aina ya kunguni na sungusungu.
Akijibu, Silima alimpiga kijembe
Selasini kuwa ameuliza swali hilo kwa sababu amechangia Sh. milioni 5
kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi.
NIPASHE
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba,
ameishangaa serikali kumsafisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,
Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliyesimamishwa
kazi, Eliakim Maswi, dhidi ya tuhuma za kuhusika katika kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku watuhumiwa wengine wakiachwa kusafishwa.
Alisema hayo alipokuwa akichangia hotuba
ya mwelekeo wa kazi za serikali, makadirio ya matumizi ya fedha ya
Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2015/16 iliyowasilishwa na
Mizengo Pinda, bungeni juzi.
Serukamba alisema inashangaza kusikia kamati iliyochunguza tuhuma dhidi ya Maswi na Prof. Muhongo kwamba, imebaini kuwa ni wasafi na muamala uliofanywa katika akaunti hiyo ulikuwa safi.
Alisema hakubaliani jinsi suala hilo
lilivyoshughulikiwa na kutoa taarifa kuwa licha ya suala la Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) kusimamiwa na wizara hiyo, viongozi wake
wanasafishwa kuwa hawana hatia. Alihoji inakuwaje watu wengine
wafikishwe mahakamani, waondolewe kwenye nyadhifa na wengine wakiwa bado
maofisini.
“…hao ni wachafu? Maswi na Muhongo ndiyo wasafi?”Serukamba.
Aliongeza: “Kama
wao ni wasafi na muamala wa Escrow ulikuwa safi, kwanini Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, Mbunge wa
Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, nao wasisafishwe? au ni wachafu?”
Alimtaka Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kutangaza kuwa wengine waliotuhumiwa kuwa ni wachafu kama Prof. Tibaijuka, Chenge, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kuwa nao pia hawana hatia.
“Nashangaa
wengine wamesafishwa. Mbona William Ngeleja na Victor Mwambalaswa,
waliondolewa kwenye nafasi za uenyeviti? Nao wasafishwe,” Serukamba.
Ngeleja alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala wakati Mwambalaswa alikuwa anaongoza
Kamati ya Nishati na Madini. Ngeleja alitajwa kupokea Sh. milioni 40
kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James
Rugemalira, wakati Mwambalaswa alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Tanesco
iliyotajwa kuhusika katika kashfa ya akaunti hiyo.
Serukamba alitaka Bunge liambiwe kama kuna wasafi, wachafu ni wepi na Katibu Mkuu Kiongozi aeleze usafi wao ni nini?
HABARILEO
Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamelaani jaribio la mapinduzi ya kumng’oa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi na kutaka Katiba ya nchi hiyo ifuatwe ili kudumisha amani na utulivu nchini humo.
Aidha, wameagiza mamlaka husika nchini
Burundi kutangaza kusimamisha kwa muda uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike
Juni 26 mwaka huu ili kurejesha hali ya amani katika nchi hiyo.
Akizungumza jana katika kikao cha ndani
kilichofanyika kwa takribani saa nne kutokana na mkutano wa dharura wa
wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, Mwenyeikiti wa Mkutano huo, Rais
Jakaya Kikwete alisema hatua ya kufanya jaribio la mapinduzi
halitasaidia kuleta amani katika nchi hiyo.
“Tumekuwa na vikao kwa muda wote tangu
asubuhi mpaka muda huu tukijadili suala la Burundi. Tukiwa tunaendelea
na vikao kukawa na mambo yanaendelea Bujumbura.
Kama Jumuiya tunalaani mapinduzi ya
Burundi na jumuiya inaona kuwa hatua hiyo hataisaidia kumaliza hali ya
sasa, hivyo tunataka kuheshimiwa kwa Katiba.
Aliongeza: “Kwa hali iliyopo sasa nchini
Burundi, Jumuiya inaona sio mwafaka kufanyika uchaguzi, hivyo
tunaziagiza mamlaka husika nchini Burundi kutangaza kuahirishwa kwa
uchaguzi huo na ufanyike ndani ya kipindi cha utawala wa uongozi wa sasa
kwa muda usiozidi muda wa utawala wa sasa.
Aidha, Kikwete alisema jumuiya
itaendelea kuzungumza na wadau wote katika kuhakikisha hali ya amani
inarejea ili uchaguzi uweze kufanyika kwa uhuru na haki kwa kuzingatia
katiba ya Burundi, sheria ya uchaguzi na kuzingatia maazimio ya Arusha.
“Pia
tunalaani vurugu zinazoendelea, hivyo tunavitaka vyama vyote kuhakikisha
wanazuia na kuacha vurugu. Jumuiya haitakubali kuona vurugu
zinaendelea,” .
Kikwete alisema wakuu wa nchi ya jumuiya
hiyo, watakutana baada ya wiki mbili kufuatilia suala hilo na kuchukua
hatua stahiki. Hata hivyo, pamoja na Rais Nkurunziza kuwapo nchini jana,
hakuweza kufika katika ukumbi wa mkutano Ikulu.
Baadaye jioni ilielezwa Rais Nkurunziza
anayeiongoza Burundi tangu Agosti 26, 2005 aliondoka kurejea nchini
mwake, lakini habari ambazo zilitufikia wakati tunakwenda mitamboni
zinasema rais huyo alishindwa kutua jijini Bujumbura, Burundi na hivyo
kurejea tena jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, mawaziri wa mambo ya
nje na Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera
walikuwa wa kwanza kuingia katika mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini
Dar es Salaam.
Rais Kikwete aliingia ukumbini hapo
majira ya saa 7.00 mchana ambako alifanya kikao cha ndani na mawaziri wa
mambo ya nje wa EAC kwa saa moja kabla ya kuanza kuingia wakuu wa nchi
za jumuiya hiyo.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliwasili
ukumbuni hapo saa 8:12 mchana na kufuatiwa na Makamu wa Rais wa Afrika
Kusini, Cyril Ramaphosa, na baadaye Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais
wa Uganda, Yoweri Museveni ambao walifanya mkutano wa ndani kupitia na
kujadili ripoti ya timu ya mawaziri wa mambo ya nje.
Wengine waliokuwamo kwenye kikao hicho, mbali ya Ramaphosa aliyemwakilisha Rais Jacob Zuma, mpatanishi wa mgogoro wa Burundi aliyeachiwa jukumu hilo na aliyekuwa Rais wa Kwanza, Nelson Mandela ambaye naye aliachwa jukumu hilo na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,
pia alikuwepo Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) na Waziri
wa Mambo ya Nje wa Angola ambao ni mwenyekiti Maziwa Makuu.
HABARILEO
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
imetangaza bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016 huku
ikiimarisha na kuongeza kodi katika vyanzo vya mapato kutokana na
washiriki wa maendeleo kupunguza misaada yao ya kibajeti.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Omar Yussuf Mzee
alisema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2015/2016 ambapo Serikali inatarajiwa kutumia jumla ya Sh bilioni 830.4.
Alisema fedha zinazotokana na washirika
wa maendeleo zimepungua na hivyo kudhoofisha mipango ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo na Serikali imeweka zaidi mikakati yake ya kubuni
vyanzo vipya pamoja na kuziba mianya yote iliyokuwa ikivujisha mapato.
Aliziita, baadhi ya mikakati ya vyanzo
vya mapato ambavyo vitaimarishwa kuanzia sasa na wananchi kutozwa kodi
ni pamoja na ada ya usajili wa ardhi na upimaji.
Alisema maeneo mengi Zanzibar
hayajapimwa pamoja na kufanyiwa usajili na hivyo kulikosesha taifa fedha
nyingi ambapo katika kuweka mikakati ya usajili wa ardhi kwa mwaka
zaidi ya Sh bilioni 262 zinatarajiwa kupatikana.
Katika bajeti hiyo, Waziri wa Fedha
ametangaza kuwepo kwa ongezeko la kodi katika viwanja vya ndege pamoja
na bandari za Unguja na Pemba kwa kiwango cha ongezeko la ada Sh 2,000.
Kwa upande wa abiria wanaofanya safari
za kwenda Tanzania Bara watalazimika kulipa ada ya bandari Sh 2,000
pamoja na ada kwa upande wa viwanja vya ndege ambapo maeneo yote hayo
yataiwezesha Serikali kujipatia jumla ya Sh bilioni 280.
Alisema bodi ya mapato (ZRB) inatarajiwa
kukusanya jumla ya Sh bilioni 225.7, wakati TRA inatarajiwa kukusanya
jumla ya Sh bilioni 175.
Aidha alisema Serikali ya Mapinduzi
inatarajiwa kuingiza jumla ya Sh bilioni 21, ikiwa ni fedha
zinazokusanywa kutoka kwa watumishi wa Serikali ya Muungano waliopo
Zanzibar kutokana na makato yanayotokana na makusanyo ya mishahara.
Mzee alisema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika mwaka 2015/2016 imeweka kipaumbele utekelezaji wa bajeti
katika sekta ya miundombinu na ujenzi wa viwanja vya ndege pamoja na
maji safi na salama kwa asilimia 53.2.
Alisema katika eneo hilo la mawasiliano
serikali inatazamiwa kutumia jumla ya Sh bilioni 212 kwa ajili ya kazi
hizo ambazo zitakapotekelezwa kwa kiasi kikubwa zitasaidia kupiga hatua
kubwa ya maendeleo.
Aidha, sekta ya elimu alisema imetengewa
jumla ya Sh bilioni 120.7 na huku kipaumbele, ikiwa ni kuhakikisha
kwamba sekta ya elimu inapata mafanikio ambapo Serikali imefuta michango
yote iliyokuwa wakitozwa wazazi kutoka kwa wanafunzi.
“Kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016
tunafuta malipo yote ya ada waliyokuwa wakitozwa wazazi na sasa michango
yote inafutwa na Serikali inabeba jukumu hilo,” alisema.
RAIA TANZANIA
Jeshi la Polisi Mkoani Simiyu
linamshikilia Mwenyekiti wa kijiji cha Bukigi kupitia chama cha
Mapinduzi CCM kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu likiwemo fuvu
la kichwa na mifupa.
Mtuhumiwa huyo ambaye pia ni mganga wa
jadi alikamatwa nyumbani kwake baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa
amewahifadhi majambazi wakisubiri kupangwa waendelee na uhalifu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu Gemin Mushy alisema tukio hilo lilitokea Mei 9 na walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema kuwa upepelezi unaendelea kubaini iwapo kweli viungo hivyo ni vya binadamu na kama kuna watu wengine wanahusika.
UHURU
Ikulu ya Tanzania sio mahali pa kuishi
wagonjwa na watu waliochoka, bali ni kwa ajili ya viongozi makini na
shupavu na wenye uwezo wa kuliongoza Taifa.
Imeelezwa kuwa viongozi waliochoka kama katibu wa Chadema Wilbroad Slaa ambaye amekuwa akipigiwa chapuo kuwania Urais hana sifa za kuishi ikulu.
Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde
alisema viongozi wa Chadema akiwemo muhasisi wake Edwin Mtei wamechoka
na licha ya kuchoka pia wamekuwa tegemeo ndani ya CHADEMA na ndio
sababu wamekuwa wakipigiwa upatu kuingia ikulu.
Lusinde alikiri kuwa Serikali ya CCM
imechoka kutokana na kufanya kazi nyingi za kuwatumikia wananchi wake
kwa kutumia akili nyingi,maarifa na nguvu kwa lengo la kuhakikisha
wanaishi katika maisha mazuri.
Alisema Serikali imekuwa ikitekeleza
mambo menfi ya maendeleo kwa wananchi wake huku ikitimiza ahadi zote
ilizoahidi katika ilani ya Uchaguzi tofauti na wapinzani.
No comments:
Post a Comment