Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.Kuvuja kwa ujumbe huo na nambari ya simu
iliyotuma, kumeibua hisia tofauti kuhusu usiri wa ofisi ya Rais katika
kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
Mhumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (TUGHE) Tawi la KCMC anadaiwa na Menejimenti ya KCMC kuwa ndiye aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi
umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa Mei
mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” .
KCMC imedai katika barua hiyo, taarifa
hiyo ya sms ilibeba ujumbe unaohusiana na matumizi mabaya ya fedha za
hospitali hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi na Shirika la Msamaria
Mwema (GSF).
Mbali na tuhuma hizo, lakini pia KCMC
inadai taarifa hiyo ilimweleza Rais kuwa KCMC na GSF linalomiliki
hospitali hiyo, zinajitosheleza kwa mapato, hivyo hakuna haja kwa
Serikali kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia, menejimenti imedai taarifa hiyo
ilidai wafanyakazi wa KCMC wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi
yao (watumishi) Serikali ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na
Serikali.
MWANANCHI
Chama cha NCCR-Mageuzi kimeponda kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu
kwamba Katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk Willibrod Slaa
ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa
Chadema mjini Moshi, hivi karibuni, Lissu alikaririwa akieleza kuwa Dk
Slaa, ndiye atakayepitishwa na Ukawa kugombea nafasi hiyo.
Lakini Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura
aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa ni makosa kudhani kwamba
Chadema ndicho chenye nafasi ya kusimamisha mgombea urais kupitia Ukawa,
wakati bado mchakato wa kumpata mgombea haujafanyika.
Sungura ambaye pia ni miongoni mwa
waasisi na mwanzilishi wa mageuzi nchini, alisema kati ya vyama vinne
vilivyounda Ukawa, tayari Chadema imepewa majimbo mengi ya ubunge. “Fursa hiyo pekee imeshawapa uwezekano wa kutoa waziri mkuu kama upinzani utashinda”, alisema.
“Kwa
kawaida chama chenye wabunge wengi ndicho kinachotoa waziri mkuu, sasa
kwa namna yoyote Chadema ndiyo itakayotoa waziri mkuu, hivyo haiwezekani
watoe na mgombea urais. Nawashauri wachague nafasi mojawapo,” Sungura.
Sungura alisema kauli hiyo ya Lissu siyo
sahihi na hailengi kujenga Ukawa, bali kuubomoa kwa kuwa haiwezekani
chama kimoja kitoe rais, makamu wake na waziri mkuu. “Ni
vizuri ikaeleweka mapema kwamba, haiwezekani chama kimoja kati ya vyama
vinne washirika wa Ukawa, kikatoa mgombea urais, makamu na waziri
mkuu,” alisema Sungura na kuongeza:
“Kwa
kuwa CUF kina nafasi kubwa ya kumtoa mgombea urais wa Zanzibar, vyama
vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, kimoja kati ya vyama hivyo kitamtoa
ama rais au waziri mkuu au spika wa Bunge, kinyume chake ni tamaa
inayoweza kuua Ukawa.”
MWANANCHI
Wakati uandikishaji wapigakura
ukiendelea kulalamikiwa katika Mkoa wa Lindi kutokana na kasoro
mbalimbali, madudu zaidi yamebainika, huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka hadharani idadi ya watu wanaoandikishwa katika kila kata.
Miongoni mwa kasoro zinazolalamikiwa ni pamoja na vituo vya kujiandikisha kuwa tofauti na vile vya kupigia kura na mashine za Biometric Voter Registration (BVR) kuondolewa kabla ya watu kujiandikisha.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba
alisema jana kuwa idadi ya watu waliondikishwa katika kila kata
ikiwekwa wazi na NEC itawasaidia kulinganisha na makadirio ya Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) ili kufahamu idadi ya watu wasioandikishwa.
Alisema viongozi wa chama hicho walifanya ziara mikoa Ruvuma, Lindi na Mtwara na kushuhudia kasoro nyingi katika uandikishaji.
Akitoa mfano, alisema katika Kata ya
Matemanga wilayani Tunduru, asilimia 60 ya watu wenye haki ya kupiga
kura hawajaandikishwa, lakini mashine zimehamishwa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema kila aliyefika kwenye kituo cha kuandikisha aliandikishwa.
“Niko
Mtwara kutembelea vituo, ninachoweza kusema ni kwamba tume haimfuati mtu
nyumbani kwake kwenda kumwandikisha, kila aliyefika kituoni
aliandikishwa, sehemu zote tunazopita hakuna malalamiko, sijui akina
Lipumba wanapata wapi taarifa hizo, mambo mengine siwezi kuyazungumza
kwa sasa,” alisema.
NIPASHE
Baadhi ya wabunge wamemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwa mkweli kuhusu kuwasafisha viongozi watuhumiwa wa Escrow na Operesheni Tokomeza, badala ya ‘kuhadaa’ kuwa wanaendelea kuchunguzwa.
Waziri Mkuu akihitimisha mjadala wa
bajeti yake juzi mjini Dodoma, alisema Ikulu haijawasafisha viongozi hao
kwa vile wanaendelea kuchunguzwa.
Akichambua maelezo ya Pinda, Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema Watanzania wanatakiwa kumshangaa kiongozi huyo kwa kutolieleza taifa ukweli.
Waliosafishwa na Ikulu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Prof. Sospeter Muhongo.
Wengine ni mawaziri waliowajibika kutokana na kashfa ya Tokomeza, Dk. Emmanuel Nchimbi, Balozi Khamis Kagasheki na Shamsi Vuai Nahodha .
Wabunge hao waliwajibishwa na Bunge kwa
kushindwa kusimamia operesheni hiyo na kutaka wawajibike kwani
ilisababisha vifo, udhalilishaji, mateso kwa watu na uharibifu wa mali.
Mwingine aliyelazimika kujiuzulu katika sakata hilo ni Dk. David Mathayo David, ingawa Bunge halikumuwajibisha.
Mkosamali alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, vyote viko chini ya Ofisi ya Rais, haviwezi kufanya kazi kwa kupingana.
Alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
alitoa taarifa ya kamati ya uchunguzi kwa niaba ya Rais, hivyo kusema
kuwa kuna taasisi nyingine ndani ya Ikulu zinaendelea na uchunguzi, ni
jambo la kushangaza.
“Tungeelezwa
na Ikulu maoni na mapendekezo ya Sekretarieti ya Maadili, kwa vile
hatujaambiwa kilichoko kwenye ripoti yake. Lakini Sefue pia awafahamishe
wananchi, hicho alisema ni cha Kamati ya Rais na ya Makatibu Wakuu,
mapendekezo ya sekretarieti hiyo yako wapi?”
Mkosamali alishauri kuwa kwa vile hizi
ni zama za uwazi, sheria zifanyiwe marekebisho ili zitoe muda maalum kwa
Rais kutangaza ripoti na mapendekezo ya sekreterieti ili kuongeza
uwazi.
Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, alisema wamesafishwa kwa vile anachosema Sefue ndizo taarifa za Ikulu.
“Ukisema
hajawasafisha unategemea nani mwingine azungumzie habari na ripoti za
tume hizo zilizoteuliwa na Rais na kupeleka mapendekezo Ikulu. “Ni Sefue
ndiye Ikulu na Ikulu ndiyo yeye,” alisema.
Alisema Maswi amesafishwa kwa kuwa ndiye
aliyeandika barua fedha zitolewe kutoka Benki Kuu (BoT), ukisema
anachunguzwa zaidi na nani mbona kila kitu alichofanya kinafahamika?
Ikulu inawafahamu wote waliochota fedha kwenye Benki ya Stanbic na
kwingineko mbona hawajatajwa?” alihoji na kuendelea:
“Kusema wanaendelea kuchunguzwa ni mchezo wa kisiasa na kufunika kombe mwanaharamu apite au kumaliza mambo kimya kimya.”
HABARILEO
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
inatarajia kusambaza vijana wa kazi katika majimbo yote nchini,
kuwashughulikia wote walioonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali za
uchaguzi, ambao wanatoa rushwa ili kupata wafuasi.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea, alisema hayo jana alipokuwa akijibu agizo alilopewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, George Mkuchika katika semina ya wabunge wa Mtandao wa Wabunge wa Afrika wa Kupambana na Rushwa (APNAC), tawi la Tanzania.
Mkuchika alimtaka Dk Hosea asisubiri
kipenga cha kampeni kuanza, bali asambaze vijana wake kwenye majimbo ya
uchaguzi kwani viashiria vya rushwa vimeshaanza.
“Kazi imeanza, waambie vijana wako wasisubiri Oktoba, waanze kazi sasa maana kuna viashiria vya rushwa, waingie wafanye kazi,”Mkuchika.
Alisema semina hiyo imekuja wakati mzuri
wanapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, hivyo ni vyema
wabunge wakumbuke wana wajibu wa kulinda maadili na kuepuka vitendo vya
rushwa.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge baada
ya kuwasilisha mada ya rushwa na uchaguzi, Dk Hosea alizungumzia hatua
zitakazochukuliwa na Takukuru kwa watoa rushwa kupitia njia ya mtandao,
ambapo alisema kwa uchaguzi huu ni vyema watoa rushwa kwa njia hiyo
waache.
Katika swali lake, Mbunge wa Nkasi, Ali Keissy (CCM),
alihoji njia zitakazotumika kubaini wanaotumia njia ya mtandao kutoa
rushwa, ambapo Dk Hosea alisema wanajua hilo na watalifuatilia kwa kuwa
wana uwezo wa kufanya hivyo.
Dk Hosea alisema miamala yote
inayofanywa na wagombea itafuatiliwa na kutoa rai kwa wagombea kuacha
kutoa rushwa, kwani watakaobainika sheria itachukua mkondo wake.
“Nyie
mnaotumia mitandao ya simu kutoa rushwa, mwaka huu mtaumia vibaya
acheni, tuna uwezo wa kudhibiti vitendo hivyo, tumesomesha vijana wetu
na tuna vifaa vya kufuatilia,”Dk Hosea.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa
tofauti na wa mwaka 2010, kwani wamejipanga vizuri kuhakikisha vitendo
vya rushwa vinadhibitiwa.
Moja ya mbinu zitakazotumika kwa mujibu
wa Dk Hosea, ni kubadilisha magari yao yanayotumika kwenye uchunguzi kwa
kuwa yaliyopo yameshazoeleka.
“Niwaambie
tu tutatumia magari mengine maana haya ya sasa mmeyazoea, mnayajua na
wengine walinunua yanayofanana ili iwe rahisi kwao kutoa rushwa wakiwa
ndani…sasa watu hawatayatambua kama ni ya kwetu au la,” Dk Hosea.
Akijibu swali la Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka
(CCM), aliyehoji kusafishwa kwa baadhi ya watuhumiwa wa sakata la
Akaunti ya Tegeta Escrow kama hakuharibu uchunguzi wa Takukuru, Dk Hosea
alisema hakuna kilichoharibika.
“Sisi
hatusafishi mtu na mafaili yetu hatujayafunga na wala hatuna mpango wa
kuyafunga, tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kazi yetu ya
kuwachunguza inaendelea na tukimaliza tutakabidhi kwa mamlaka nyingine,” Dk Hosea.
Alisema kusafishwa kwa baadhi ya
watuhumiwa wa tukio hilo hakujaharibu uchunguzi wao na kwamba wao
wanaendelea na kazi yao na hakuna aliyewaingilia kwenye kazi yao, hivyo
watahakikisha wanaikamilisha.
HABARILEO
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa ameonesha ujasiri wa kipekee kwa kumwokoa mama yake mzazi, Magreth Ibrahim (50) kuuawa na mamba baada ya kupambana na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.
Mama huyo mkazi wa kijiji cha Karema,
mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda, kwa sasa amelazwa katika
Hospitali ya wilaya ya Mpanda mjini Mpanda kwa matibabu baada ya mkono
wake kunyofolewa na mamba aliyemshambulia wakati akifua kando ya Mto
Ikola.
Akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima
aliyemtembelea hospitalini hapo masaibu yaliyomsibu, alisema
anamshukuru sana binti yake mwenye umri wa miaka tisa aliyeweza kuokoa
maisha yake licha ya kuwa amenyofolewa mkono na mamba huyo.
Akisimulia mkasa huo, Magreth alieleza
kuwa juzi akiwa anafua kando ya mto Ikola ghafla mnyama huyo aliibuka
majini na kumpiga usoni na mkia wake.
“Mamba
huyo aliibuka ghafla mtoni na kunichapa usoni na mkia wake nami
nikaangukia majini ndipo aliponidaka mkono wangu na kunivutia mtoni
….binti yangu aliyekuwa jirani yangu alipoona niko karibu kuliwa na
mamba kwa ujasiri aliweza kukabiliana naye … Alinishika mkono mwingine
na kunivutia nje huku akipiga kelele kumtisha mnyama huyo ili aniachie
hatimaye akaunyofoa mkono wangu na kutokomea nao mtoni ….” alieleza.
Aliongeza kuwa watu waliokuwa wakifua
mtoni hapo wengi wao wakiwa wanawake walifika eneo la tukio ambapo
wakiwa na binti yangu walimvuta na kumtoa nje na baadae wakamkimbiza
hospitalini mjini Mpanda kwa matibabu.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa amethibitisha kuwa hali ya mama huyo inaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu.
HABARILEO
Raia wa Tanzania na Msumbiji watakaotaka
kuingia katika nchi hizo na kukaa wa miezi isiyozidi mitatu,
hawatalipia viza kama ilivyokuwa awali, imeelezwa.
Aidha, imetangazwa pia kuwa, wanafunzi
kutoka katika nchi hizo kuanzia sasa wanaruhusiwa kusoma kokote ndani ya
Msumbiji na Tanzania wakitumia pasipoti zao zitakazogongwa viza bure,
kwa kipindi chote cha masomo yao, hata kama ni miaka mingi.
Hatua hizo zimefikiwa Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya Marais Jakaya Kikwete na Filipe Nyussi
wa Msumbiji kukubaliana kufanyia marekebisho mkataba wa masuala ya
uhamiaji kati ya nchi hizo mbili kudumisha udugu, urafiki na uhusiano wa
kirafiki.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya
viongozi hao wakuu wa nchi hizo kufanya mazungumzo ya faragha kwa saa
kadhaa Ikulu, na kisha Mawaziri Jaime Basilio Monteiro, wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, aliyemwakilisha Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Mathias Chikawe, kusaini hati ya makubaliano hayo.
Mkataba huo wa sasa wenye marekebisho
katika maeneo matatu makuu, umeeleza pia kuwa muda wa siku 30 uliokuwa
ukitolewa na Msumbiji kwa watanzania, kukaa nchini humo bila kulipia
viza sasa umeongezwa na kuwa siku 90.
Kutokana na matakwa mapya ya mkataba huo
wa sasa, Membe alisema umeweka usawa wa siku za kuishi kwenye nchi hizo
mbili kwa raia wa Tanzania na Msumbiji, tofauti na ilivyokuwa awali
kwamba watanzania walipewa siku hizo kuwepo bure kwenye nchi hiyo wakati
raia wa Msumbiji waliweza kuishi kwa siku 90 bila kutozwa ada ya viza.
“Makubaliano
ya Marais hawa yameleta ahueni kubwa kwa raia wa nchi hizi mbili katika
masuala ya uhamiaji. Wanafunzi nao wamepata nafuu kubwa kwa sababu
hawataulizwa ada ya viza tena hadi wamalize masomo,” Membe.
Aliongeza kuwa, mabadiliko hayo yanahusu
hati za kidiplomasia, za kiserikali na za kawaida ambapo, mtumiaji
atagongewa viza bure kwa siku atakazo kaa, ilimradi zisizidi 90.
Membe alieleza kuwa kabla ya makubaliano
hayo, raia wa Msumbiji alipaswa kulipa ada ya viza ya Sh 10,000 tu, ili
kukaa nchini kwa siku zisizo zidi 90, wakati raia wa Tanzania
aliyekwenda Msumbiji na kukaa kwa zaidi ya siku 30, alipaswa kulipa Dola
za Marekani 900 ikiwa ni ada ya viza.
Pia,Mtanzania aliyekwenda nchini humo
kwa shughuli za biashara alipaswa kulipa ada ya viza ya Dola za Marekani
700, wakati mfanyabiashara wa Msumbiji aliyekuja nchini kwa shughuli
kama hizo alitozwa ada ya viza ya Dola za Marekani 200 tu.
Mawerenewz.blogspot.com
ndio mtandao wako wakipekee unaokupa habari za BURUDANI,MICHEZO, SIASA, na
HABARI MBALIMBALI ZA KIMATAIFA pamoja na KITAIFA Endelea kutembelea MTOKA MBALI
pia nifuate twitter>>>@mawere3, facebook>>>Mawere Mtoka Mbali, Instagram>>>mawere_mtoka_mbali,SuScribe Youtube>>>MAWERE TV
No comments:
Post a Comment