WAKATI zimebaki saa chache kabla ya Ruvu Shooting Stars kuivaa Yanga SC, imebainika kuwa
baadhi ya wachezaji wa timu hiyo jeshi wataikosa mechi hiyo muhimu kutokana na matatizo mbalimbali.
Masau Bwire, msemaji wa Ruvu Shooting Stars, ameuambia mtandao huu kwa simu kuwa kikosi chao kimefanya mazoezi ya mwisho Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani leo asubuhi na katika mechi ya kesho kitamkosa Betram Mwombeki anayesumbuliwa na majeraha ya enka.
Wachezaji wengine wa Ruvu Shooting Stars ambao hawatakuwamo katika kikosi cha Mkenya Tom Alex Olaba ni Seif Kijiko (matatizo ya kifamilia) na Juma Abdul mwenye majeraha ya goti.
Aidha, Bwire amesema wamejiandaa kufuatilia nyendo za mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga, ambaye amedai amekuwa na tabia sizizo za kiungwana uwanjani kwa kupiga mateke na kuwabinya sehemu za siri wachezaji wa timu pinzani.
“Tambwe alimnyanyasa mchezaji wetu George Michael wakati wa mechi yetu ya kwanza dhidi ya Yanga msimu huu, alimpiga mateke, lakini mchezaji wetu ndiye akaadhibiwa na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) baada ya kuamua kumjibu. Tambwe ana tabia za kuwabinya sehemu za siri na kuwapunguzia nguvu wapinzani,” Bwire amesema na kuongeza:
“Tunaomba marefa wachezeshe kwa kufuata misingi ya Sheria 17 za Soka na taaluma ya uamuzi. Tunajua ligi iko ukingoni na kuna timu zinajipanga kupata ushindi wa lazima hata pale zinapokuwa zimezidiwa.”
Mechi hiyo itachezwa kesho badala ya Jumamosi kutokana na maandalizi ya sherehe za Muungano Jumapili.
No comments:
Post a Comment