Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe amesema iwapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anataka kugombea urais kupitia chama hicho afuate taratibu za chama ikiwamo kutangaza mali zake.
Akiwahutubia mamia ya
wakazi wa Jiji la
Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha juzi, Zitto alisema hawezi kumzuia
mtu anayetaka kujiunga ACT – Wazalendo ikiwa atafuata taratibu
zilizowekwa na chama hicho.
“Naomba
niwaambie Watanzania kwamba ACT siyo chama cha kumtengenezea mtu
mazingira ili agombee urais, lakini kama Lowassa anataka kugombea urais
kupitia huku lazima atangaze mali zake na kueleza wapi amezipata kama
taratibu za chama zinavyosema,” Zitto.
Zimekuwapo taarifa kwenye vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya wagombea akiwamo Lowassa
ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, wana mpango wa kutimkia ACT
iwapo watakatwa majina yao katika mchujo wa wagombea.
Kwa mujibu wa habari hizo, ACT –
Wazalendo imepewa fedha na Lowassa ambazo inatumia katika mikutano hiyo
kumwandalia nafasi ya kuwania urais, madai ambayo pande zote
zimeyakanusha.
Akizungumzia taarifa hizo kwenye mkutano
huo, Zitto alisema chama chake kinaongozwa kwa kufuata taratibu na
kitampokea yeyote atakayefuata taratibu hizo.
Kiongozi huyo ambaye hivi karibuni
alitangaza mali na madeni yake, alisema iwapo Lowassa atataka kujiunga
na chama hicho itambidi atangaze mali zake na kueleza jinsi
alivyozipata, kama yeye alivyofanya.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu kauli ya Zitto, msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alisema: “Hakipo kitu kama hicho na hakitakuwapo, hatujui habari hii inatoka wapi? Mzee (Lowassa)
amekuwa akitumikia CCM maisha yake yote tangu enzi za TANU … yupo na
anaendelea kutumikia kifungo chake. Maisha yake yote ni mtumishi wa
chama.”
Lowassa pamoja na makada wengine watano
wa chama hicho walipewa adhabu ya onyo kali baada ya Kamati Kuu ya CCM
kuwatia hatiani kwa kuanza kampeni za urais mapema na kukiuka maadili ya
chama.
MWANANCHI
Kamati Kuu ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), imempendekeza Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema kutetea kiti chake cha ubunge katika jimbo la Vunjo.
Kaimu Katibu Mkuu wa TLP Nancy Mrikaria,
alisema jana kuwa kamati hiyo pia imemthibitisha Mrema kuendelea na
nafasi yake ya uenyekiti wa chama hicho kwa kipindi kingine.
Alisema kamati imeridhia Mrema kuendelea
kugombea ubunge katika jumbo la Vunjo ikiwa na imani kuwa ana nafasi
kubwa ya kushinda, ikilinganishwa na wengine watakaojitokeza kupambana
nao.
“Kamati
imefikia hatua hiyo kwa kutambua uwezo alionao mwenyekiti katika
kukiendeleza chama, pia hadi sasa hakuna mwanachama mwingine
aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo na tulianza kutoa fomu tangu Aprili 9
hadi 17, wakati kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti Bara ndiyo kuna
ushindani wa watu wawili wanaoigombea,”Mrikaria
Alisema nafasi ya Makamu Mwenyekiti
upande wa Zanzibar pia haina mpinzani kwa kuwa hadi sasa aliyechukua
fomu ni Alhaji Hamad Mkadam ambaye ndiyo anashika nafasi hiyo.
“
Tunatarajia wajumbe wa mkutano watajitokeza kwa wingi ili kufanikisha
uchaguzi huo ambao ni muhimu kwa maendeleo ya chama, hasa katika kipindi
hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa kuwa ukikamilika tunapata
nafasi ya kujipanga,” Mrikaria.
Naye Mrema alisema kwamba anaamini
kwamba kamati hiyo imempendekeza kutokana na kuwa na imani naye kwamba
ana uwezo mzuri wa kukiendeleza chama hicho.
“ Siyo
kwamba nitakuwa nagombea kwa ubabe au ujeuri bali kamati yenyewe
imenibariki, naamini Vunjo nitashinda na kuendelea kukifanya chama
kistawi kwani nisipokitetea chama kitakuwa kama cha wacheza ngoma,” Mrema.
Hadi kufikia hatua hiyo ya kufanya
uchaguzi TLP ilibanwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kwa
kupewa siku 80 kwa uongozi kuhakikisha kinafanya uchaguzi wake wa ndani
ili kuwapata viongozi wapya.
MWANANCHI
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeshika nafasi ya kumi miongoni mwa vyuo vikuu 50 bora na vyenye umaarufu Afrika.
Kadhalika UDSM kimetajwa kuwa miongoni mwa chuo vikuu chenye idadi kubwa ya wanafunzi na walimu na wingi wa programu za masomo.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala alisema chuo hicho kina haki ya kushika nafasi hiyo kutokana na jitihada zinazofanywa na uongozi.
“Tulifanya
jitihada kuhakikisha tuna walimu wazuri wenye shahada za uzamili na
uzamivu, maabara nzuri na miundombinu rafiki ya kufundishia,” Mukandala.
Alisema UDSM ina mitaala bora inayoendana na wakati na inazalisha wataalamu wengi kwa mwaka.
Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Vyuo Vikuu na vya Kati (4ICU) ya Uingereza, chuo hicho kilishika nafasi ya 10 kati ya vyuo 50 vilivyopimwa kulingana na vigezo vya taasisi hiyo.
Hata hivyo, taasisi hiyo ilieleza kuwa
hawapimi ubora wa vyuo kwa kuangalia kiwango cha elimu inayotolewa au
huduma bali wanaangalia umaarufu wa chuo kimataifa.
Katika taarifa hiyo, Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini kilishika nafasi ya kwanza huku vingine vilivyoshika tano bora vikitoka nchini humo.
Nafasi ya pili ilishikwa na Chuo Kikuu cha Pretoria, ya tatu Chuo Kikuu cha Stellenbosch na nne ilikwenda kwa Chuo Kikuu cha Witwatersand na tano ikishikwa na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.
MWANANCHI
Kuna kila dalili kuwa wanasiasa nchini wamebuni mbinu mpya ya kuzitumia klabu za mbio za pole maarufu kama ‘jogging’ kutekeleza mikakati ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu, mwaka huu.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na
baadhi ya wananchi walisema kuwa matukio ya kijamii yanayoendelea hivi
sasa nchini na kuhusisha wanasiasa yanapaswa kutazamwa kwa jicho la
karibu.
Juzi kulikuwa na matukio makubwa mawili
katika maeneo tofauti jijini hapa yaliyohusisha matembezi ya kilomita
kadhaa yaliyokuwa yakifanya kampeni mbili tofauti na kuhusisha vigogo wa
ngazi ya juu wa CCM.
Katika tukio la kwanza, vijana wapatao 10,000 kutoka klabu mbalimbali za mbio za pole wakiongozwa na wenyeji wao Temeke Family, walimwalika Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kuongoza matembezi ya kulaani na kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Lowassa katika tukio hilo aliambatana na wabunge Idd Azzan, Mussa Zungu na Abbas Mtemvu aliyekuwa mwenyeji wa matembezi hayo yaliyoanzia Uwanja wa Taifa hadi Viwanja vya TCC Chang’ombe.
Katika upande mwingine, jimboni Segerea, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiongozana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye waliongoza klabu 100 za ‘jogging’ kuhamasisha vijana wajiandikishe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Wakati wa kuanza hotuba yake, Lowassa
alisema hawezi kuzungumza kwa kirefu kutokana na kifungo kinachomkabili
cha kutumikia adhabu ya kuanza kampeni za urais mapema alichopewa na
chama chake.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda
alisema kipindi kama hiki wanasiasa hutumia kila mbinu ya kuongeza
ushawishi kwa wapiga kura, hivyo matumizi ya klabu za mbio za pole ni
moja ya njia za kukuza umaarufu wao.
“Kitendo
cha mwanasiasa kushiriki kwenye klabu za ‘jogging’ kinatengeneza ngome
ya umaarufu, ataonekana na kuandikwa kwenye vyombo vya habari. Siasa ni
vita. Wapo wengine wanatumia hadi njia za kuandika vitabu ili jamii
iwakubali,” Mbunda.
Alisema matukio yoyote yanayoendelea na
kuhusisha wanasiasa yasipuuzwe licha ya mengine kugusa masuala ya
kijamii ambayo ni vigumu mtu kuyang’amua kuwa yanahusisha siasa.
NIPASHE
Wakati serikali ikitangaza kuwarejesha
Watanzania 21 kati ya 23 walioko kwenye moja ya makambi yanayowahifadhi
raia wa kigeni walioathirika na vurugu zilizohusisha mauaji, uporaji na
watu kukimbia makazi nchini Afrika Kusini, Mtanzania aliyeko nchini
humo, amesimulia jinsi raia wengi wa kigeni walivyoathirika.
Joseph Moses, anayeishi mjini Durban,
amesema pamoja na baadhi ya raia wa kigeni kuawa, lakini waliothirika
hadi sasa wengi wao hawajui watalipwaje mali zao zilizopotea katika
ghasia hizo.
Moses, alisema kuna Watanzania wengi mjini Durban wamepoteza mali zao katika vurugu hizo na hawajui watalipwaje.
Hata hivyo, alisema raia wa kigeni walioathirika zaidi na ghasia hizo ni wanaotoka katika nchi za China, Pakistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Nigeria na Somalia, baada ya maduka pamoja na nyumba wanazoishi kuvamiwa na watu wanaosaidikiwa kuwa ni raia wa Afrika Kusini na kuporwa.
“Kinacholeta utata ni kwamba, hata kama fidia itatolewa haijulikani itakuwaje,” Moses na kuongeza kuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi katika mji wa Durban ambao umeathiriwa zaidi na vurugu hizo.
Alisema jana ulifanyika mkutano uliomhusisha Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Chifu wa Wazulu, Goodwill Zweluthini anayetuhumiwa kuchochea vurugu hizo na viongozi wengine nchini humo katika kambi ya waathirika hao mjini Durban.
Moses alisema katika mkutano huo, Chifu
Zweluthini aliwapiga marufuku raia wa Afrika Kusini kuendelea
kuwashambulia raia wa kigeni.
Alisema sababu iliyotolewa na Chifu
Zweluthini ni kwamba, nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania,
ziliwasaidia weusi wa nchi hiyo kuondoa siasa ya ubaguzi wa rangi.
Wakati Moses akisema hayo, Watanzania 21
kati ya 23 walioko kwenye kambi hiyo wamekubali kurejea nchini baada ya
serikali kuwahakikishia kuwalipia gharama za safari, lakini wawili
wamekataa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa,
Watanzania wanaoishi Afrika Kusini wanakisiwa kuwa zaidi ya 10,000.
Alisema kati yao, 23 ndio waliobainika kuhifadhiwa katika kambi hiyo kufuatia kuibuka kwa ghasia hizo nchini humo.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali
imekubali kugharimia safari ya Watanzania hao 21 baada ya wenyewe
kukubali kurejea nchini.
Alisema Watanzania hao 21 ni miongoni
mwa raia wa kigeni ambao baadhi wanasadikiwa kupoteza kazi na wengine
shughuli zao za biashara kuharibiwa katika ghasia hizo.
NIPASHE
Naibu Katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amesema baada ya Rais Jakaya Kikwete
kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa uchotaji wa fedha za akaunti ya
Tegeta Escrow, achukue hatua ya kuwakamata na kuwafilisi watuhumiwa hao.
Aidha, alisema watuhumiwa hao baada ya
kukamatwa na kufilisiwa mali zao, wanatakiwa kufikishwa mahakamani
pamoja na kuamriwa kurejesha fedha zote walizoiba.
Akihutubia wananchi katika mkutano wa
hadhara kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo katika Manispaa ya
Musoma mkoani Mara, alisema iwapo hatua hizo hazitachukuliwa hadi Bunge
lijalo la bajeti, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) watawasha moto upya ili kupata majibu ya kina kabla ya kuelekea uchaguzi mkuu.
Mnyika alisema baada ya Rais kupokea ripoti ya Baraza la Mawaziri, taasisi ya kuzuia rushwa (TAKUKURU) na
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, ni wakati mwafaka ripoti hizo
zikawekwa hadharani ili watuhumiwa wote wafikishwe mahakamani baada
ya kufilisiwa mali zao.
“Katika
kikao chetu na sasa mkutano wetu huu tunatoa azimio la pamoja na
tunamtaka Rais Kikwete na tunataka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani
na mali zao kufilisiwa ili fedha za umma zirejeshwe,” Mnyika.
Mnyika alisema sakata la Tegeta Escrow mwaka
huu, halitafunikwa kama walivyofunika mikataba ‘hewa’, hakuna majibu ya
tofauti yatakayotolewa na kusukumiana mpira na viongozi wa sekta
zingine bila kujali wao ndiyo wasimamizi wakuu.
Alisema kamwe Chadema hawawezi kuwa
wasaliti wa Taifa hili kama bendera ya chama hicho yenye rangi ya
kuonyesha upendo, hivyo lazima kitapambana hadi tone la mwisho kuona
Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi zao.
MTANZANIA
Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani mstaafu, Mzee Nassor Moyo, amesema hajutii kufukuzwa uanachama ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hatarajii kukata rufaa.
Moyo alisema ataendelea kuwa muumini wa Serikali tatu na kudai mamlaka kamili ya Zanzibar hadi mwisho wa maisha yake.
Alisema anaamini kile anachosimamia
ndani ya moyo wake, hivyo hakuna chama wala taasisi yoyote yenye uwezo
wa kubadilisha kile anachokiamini kusimamia masilahi ya wananchi wa
visiwa vya Zanzibar.
“Naamini ninachofanya na kusimamia siyo dhambi wala usaliti kama baadhi
ya wanachama wa CCM wanavyoamini, bali napigania uhuru, usawa wa watu na
mapambano haya ni endelevu,” alisema.
Moyo ambaye amekuwa mtumishi wa umma
ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kwa muda mrefu, alisema anatambua mambo mengi ambayo
yamefanyika, lakini sasa anashangaa kuona vijana wengi wanajifanya
wanajua mambo ya CCM kuliko wazee.
Alipoulizwa kuhusu ukweli juu ya tuhuma
zinazomkabili, alisema safari ya kupigania haki na usawa katika maisha
ya wanadamu haiwezi kukosa vikwazo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi, Yussuf Mohamed Yussuf, alikiri Moyo kuvuliwa uanachama na Halmashauri Kuu ya Mkoa huo juzi.
Alisema CCM imetumia busara na hekima
nyingi kufuatilia mwenendo wa mwanachama huyo kwa miaka minne baada ya
kupokea tuhuma mbalimbali za kukiuka maadili ya chama.
Yussuf alisema miongozi mwa makosa
makubwa aliyofanya Moyo, ni kusimama katika majukwaa ya Chama cha
Wananchi (CUF) na kudai yeye ni muumini wa Serikali tatu, mfuasi wa
kudai mamlaka kamili ya Zanzibar na kujiita mjumbe wa CCM katika Kamati
ya Maridhiano ambayo chama chenyewe hakikuhusishwa.
MTANZANIA
Ni dhahiri sasa vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vimeanza kuumana jino kwa jino kutokana na kupishana kwenye mikutano ya kisiasa inayoendelea mikoani.
Wakati vyama hivyo vikiendelea kuchuana
na kujaza mamia ya wananchi kwenye mikutano yao, viongozi wake wamekuwa
wakituhumiana kwa mambo mbalimbali.
Vyama hivyo vimekuwa vikipishana katika
kanda tangu vilipoanza ziara za mikoani hivi karibuni. Wakati Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika akiwa mkoani Mtwara, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alikuwa mkoani Ruvuma na timu yake.
Baada ya Mnyika kumalizia ziara hiyo,
alirejea Dar es Salaam kabla ya kuanza mikutano yake Kanda ya Ziwa,
ambako ACT nao walikwenda.
Akiwa mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki,
Mnyika akihutubia mamia ya wananchi kwenye viwanja vya Furahisha,
alisema Chadema haiko tayari kuwakaribisha ACT-Wazalendo kwenye Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Lakini siku moja baada ya Mnyika kuondoka Mwanza, Zitto na msafara wake nao waliwasili mkoani humo.
Baada ya kuwasili, Zitto alifanya
mkutano wa hadhara kwenye viwanja hivyo hivyo na kusema ACT-Wazalendo
wamejipanga kurudisha uzalendo.
Baada ya mkutano huo, jana Zitto aliwasili mkoani Mara ambako alifanya mkutano mkubwa wa hadhara.
Alisema kamwe hatorudi nyuma kwa maneno ya watu, kwani safari ya mapambano imeanza.
Zitto alisema hivi sasa kuna kundi la
watu waliojivika upinzani dhidi ya ACT-Wazalendo, ambao wamekuwa
wakikesha ili waone chama hicho kinapotea katika siasa za nchi hii.
Akizungumza katika mkutano huo kwenye
Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo mjini Musoma, Zitto alisema ameamua
kuingia kwenye jahazi la ACT, huku akitambua namna ambavyo anapigwa kila
aina ya mishale na watu wasiomtakia mema kwenye siasa.
Alisema anashangazwa na madai ya watu
hao kueneza kila aina ya propaganda zenye lengo la kukiua chama cha
ACT-Wazalendo, ikiwamo kukihusisha na mipango ya kuwaandalia nafasi
baadhi ya makada kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili wagombee urais
katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, baada ya
kutemwa.
“Mimi
ndugu yenu nimepigwa mishale mingi kweli ndani na nje – huko
nilikotoka, ikafika mahali unajitahidi kueleza kile unachojua, wenzako
hawakutaki, mngekuwa ninyi mngefanyaje?
JAMBOLEO
Simanzi zimetawala katika familia ya mtoto Festo Filbert mwenye miaka 11 iliyopo Majohe kwa Ngosoma, Dar es salaam baada ya mtoto huyo kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali.
Tukio la kujinyonga kwa mtoto huyo
aliyekuwa akisoma darasa la nne katika shule ya Msingi Pugu limeacha
huzuni kwa majirani na ndugu zake ambao walikuwa karibu na mtoto huyo.
Mtoto huyo alifikia maamuzi hayo juzi
katika maeneo hayo ambapo alikutwa chumbani kwake akiwa amejinyonga na
mwili wake ukiwa umeng’inia kwenye mkanda alioufunga shingoni.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi
karibu na mtoto huyo walisema wameshtushwa na kifo chake kwani kabla ya
kufikia uamuzi huo alionekana akicheza na wenzake.
Walisema jumapili asubuhi alikwenda
kanisani, na aliporudi alikuwa akichezana wenzake lakini walishangazwa
na taarifa za kwamba amefariki baada ya kuamua kujinyonga.
Hata hivyo haikuwa rahisi kufahamu
sababu za kuamua kujinyonga na sasa maiti yake imehifadhiwa katika
hospitali ya Amana huku upelelezi wa Polisi ukiendelea
No comments:
Post a Comment