12 April, 2015

MAGAZETINI APRIL 12 JUMA PILI

Image result for sunday newsMWANANCHI
Kuanzia Julai mwaka huu Watanzania wataanza kupata umeme wa uhakika na usiyo kuwa na gharama baada ya kuanza kazi kwa mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi, utakaoingiza kwenye gridi ya Taifa megawati 150.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Injinia Felchesmi Mramba wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kinyerezi na vituo vya kupokea na kusambaza umeme vya Gongolamboto, Kipawa na Ilala City Center, vyote vya Dar es Salaam.
Alisema kuna uwezekano mkubwa wa bei za umeme kushuka, iwapo wataafikiana vizuri na wazalishaji wa umeme wa gesi.
Ni vigumu kusema zitashuka kwa kiasi gani, lakini haziwezi kupanda,Mramba .
Mramba akiwa ameongozana na Meneja Miradi wa Tanesco, Injinia Simon Jilima, kuanza kuzalishwa kwa umeme wa gesi, tafsiri yake ni kwamba nchi haitakuwa na mgawo wa umeme, bei hazitapanda, lakini kuna uwezekano zikashuka kama gharama za uzalishaji hazitakuwa kubwa.
Alisema kukamilika kwa mtambo huo kumeenda sambamba na ujengaji wa mtandao wa vituo vya kupokea na kusambaza umeme, ambapo kwa Dar es Salaam vituo vinavyosambaza umeme wa hadi megawati 180 kwa wakati mmoja viko vine, Ubungo, Kipawa, Ilala City Center na IPTL.
Kuhusu vituo hivyo vinne na vingine vidogo, Injia Jilima alisema shirika limejenga mtandao wa kisasa wa kupokea na kusambaza umeme, ambapo kama eneo moja, mfano kituo cha Tandika kitapa hitilafu na kushindwa kusambaza umeme, wakazi wa eneo hilo wataendelea kupata umeme kutoka kituo kingine chochote, hata kilichopo Mikocheni.
Akizungumzia kupungua kwa gharama, Mramba alisema mtambo wa Kinyerezi utakapoanza wataachana na kampuni za Symbion na Aggreko, ambapo kwa kampuni ya IPTL wako kwenye mchakato wa kuanza kufua umeme kwa kutumia gesi.
Mramba alisema mtambo wa Kinyerezi utasaidia kuokoa Dola za Marekani milioni 70, ambazo Tanesco wamekuwa wakitumia kila mwezi kuzilipa kampuni hizo.
Kuhusu kuunganishia wateja wapya umeme, Mramba alisema wameanzisha program ya kuwaunganishia umeme wateja wa mijini ambapo kwa mujibu wa utafiti wao wa nchi nzima kwa maeneo ya mijini kuna wateja wapya 500,000.
Alisema program hiyo maalumun utatumia wakandarasi kuunganisha umeme kwa wateja na kwamba ndani ya miaka mitatu wateja hao watakuwa wameunganishiwa umeme, na kuanzia hapo Tanesco itakuwa na uwezo wa kuunganisha umeme kwa haraka kwa kila mteja anayeomba.
MWANANCHI
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema atalazimika kuachia wadhifa huo kwa mtu mwingine atakayeteuliwa na chama hicho kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho mwanachama anayeruhusiwa kugombea urais ni lazima awe kiongozi wa chama, wadhifa ambao unashikiliwa na Zitto ambaye hajafikisha umri wa kikatiba wa kugombea urais ambao ni kuanzia miaka 40. Kwa sasa ana miaka 39.
Zitto alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari wa Mwananchi katika ofisi za gazeti hili Dar es Salaam juzi.
“Ikitokea hivyo (ACT ikapata mgombea urais, kutoka ndani au nje ya chama hicho), mimi natoka namwachia mtu mwingine na tumeshaamua hivyo, kwetu sisi tatizo siyo cheo. Tukipata mgombea urais leo nitampisha, sitakuwa kiongozi wa chama nitabaki kuwa mwanachama wa kawaida na mjumbe wa Kamati Kuu.” Zitto
Hata hivyo, alisema ili mtu huyo apate nafasi hiyo ni lazima aelewe malengo ya chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana.
“Tunataka mtu ambaye hata tukipata mabadiliko asiwe kikwazo cha hayo mabadiliko. Nasema hivi kwa sababu mnaweza kupata mtu mwingine kuwa kiongozi wa chama lakini baadaye anang’ang’ania na hataki kutoka,” .
Alifafanua kuwa yeye bado ni kijana ana muda mrefu katika siasa na anaungwa mkono sehemu nyingi, hivyo hana haja ya kuharakisha katika kila jambo.
Hata hivyo, akizungumzia watu wa vyama vingine watakaojiunga na chama hicho alisema, “Kati ya watu watakaojiunga ACT au walioonyesha nia kutoka CCM au Ukawa hadi sasa hakuna ambaye ni mgombea urais.”
Alifafanua, “Sisi (ACT) tutasimamisha mgombea wetu wenyewe katika nafasi ya urais au tunaweza kumuunga mkono mgombea wa upinzani.”
Alisema watafanya hivyo kwa sababu hawataki kuua matumaini ya nchi kupata Serikali inayotokana na vyama vya upinzani, “Pale ambapo tutaona ni lazima kuunga mkono wenzetu kuing’oa CCM madarakani tutafanya hivyo. Si kama tunajiunga Ukawa, hapana ni kwa sababu bado hatujawa na mazungumzo nao na kujua nini kitakachotuunganisha.”
Zitto aliziponda sera na ilani za vyama vya siasa nchini kwamba hazina tofauti, zote zina mfumo wa kiitikadi na mwelekeo uleule, isipokuwa kwa ACT Wazalendo.
MWANANCHI
Watu watano wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mikoa ya Dodoma na Iringa ikiwa ni muda usiozidi saa 24, baada ya kumalizika mgomo wa madereva wa mabasi na malori.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, jana alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo ya Dodoma, saa 3:45 usiku, katika eneo la Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea Mwanza kwenda Morogoro liligongana na gari ndogo aina ya Toyota Mark II iliyokuwa likiingia barabara kuu kutokea Nzuguni.
“Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari dogo kuingia barabarani bila kuwa makini na kusababusha kushindwa kumpa kipaumbele aliyekuwa barabara kuu kupita kwanza.
“Lakini pamoja na makosa ya gari ndogo, suala la mwendo kasi wa dereva wa basi umesababisha madhara kuwa makubwa,”  Misime.
Aliwataja waliopoteza maisha ambao wote ni waliokuwa katika gari ndogo kuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Monduli mkoani Arusha, Jackson Lazaro aliyekuwa dereva wa gari dogo.
Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni  Mkazi wa Makole, Helena Chiuyo (36), Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya City ya mjini hapa, Fatuma Mtauga (17) na Mkazi wa Kisasa Stella Giseon (36).
“Dereva wa gari dogo alikuwa akitokea kijiji Nzuguni kuingia barabara kuu ya Dodoma kuelekea Morogoro kugongana basi ambalo lilipoteza mwelekeo na kuingia porini umbali usiopungua mita 300 na kugonga mti na kisha kusimama,”Misime.
Alisema dereva wa basi ambaye ni Mkazi wa Kirumba Mwanza, Leonard Magesa (51) anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.
Naye Ofisa Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Cecilia Sanya,  alisema alipokea majeruhi huyo saa 6.20 Fatuma Patrick kutoka eneo la ajali akiwa majeraha sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani .
“Waliongoza na wauguzi wa zamu kwenda katika eneo la tukio wakiwa na gari la wagonjwa, walivyofika pale walikuta watu hao wamefariki dunia,”  Cecilia.
Naye mmoja wa mashuhuda,  Christian Kihonda, alisema dereva wa basi alikuwa katika mwendo kasi baada ya mgomo kumalizika juzi mchana.
NIPASHE
Wakazi wa Kibamba nje kidogo ya jiji la Dar es salaam jana walifurika nyumbani kwa Emmanuel Joseph kushuhudia maajabu ya tukio la kufufuka kwa mtoto anayedaiwa kufariki dunia mwezi Agosti mwaka jana.
Mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja inadaiwa alizikwa katika makaburi ya Mlongazila na alifariki Agosti 7 baada ya kuugua gafla na kuishiwa damu.
Mtoto huyo anadaiwa kurudishwa akiwa hai na Juma Nakochinya (33) maarufu kwa jina la Bino, mkazi wa eneo la Pandambili mkoani Dodoma ambaye hutibu kwa njia ya maombi.
Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto  huyo, Hellena Mtoro, alisema ilikuwa siku ya Jumamosi majira ya saa 11:00 jioni ambapo mwanawe akiwa na umri wa miezi tisa alizidiwa ghafla na kumkimbiza hospitali ya Mbezi kwa matibabu.
Alisema baada ya kufika hospitalini hapo, vipimo vilionyesha ameishiwa damu hivyo alihamishiwa hospitali ya Tumbi, iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Madaktari walijitahidi kadiri ya uwezo wao kutafuta mishipa ya damu maeneo tofauti ya mwili ikiwamo kichwani, cha ajabu mishipa ilikuwa ikionekana lakini ilikuwa inavimba, wakati madaktari wakihangaika, ilipofika saa 6:00 usiku alifariki dunia,” Mtoro,
Alisema baada ya kuzika siku tatu baadaye walielekea Dodoma kwa ajili ya kumaliza msiba na kurudi Dar es Salaam.
“Ukweli ni kwamba kifo cha mtoto wangu kilikuwa sio cha kawaida, hivyo tulianza maombi na mume wangu, tulikuwa tunasali kwa Nabii Flora Peter, ambaye baada ya kumweleza mazingira ya kifo hiki, alimuweka kwenye maombi na kututaka tumpelekee picha yake,”
“Baada ya maombi alitueleza kuwa anamuona mtoto wetu yupo hai na anaamini atarudi siku moja. Tuliendelea na maombi na siku moja nilikutana na mama Mariamu ambaye baada ya kumwelezea kifo cha mtoto wangu, aliniambia kuna kijana anaitwa Bino ambaye anaweza kumrudisha kama alikufa kichawi,”
Alisema mama huyo alimpa namba ya mtu huyo na alipowasiliana naye, Bino alimtaka ashike Sh. 100.
“Nilifanya hivyo na baada ya dakika tano tukiwa bado hewani, alinijulisha kuwa mtoto wangu anamuona yupo hai hivyo akanitaka niende kesho yake Dodoma kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ya kumrudisha,”
Hellena alisema siku iliyofuata alisafiri kuelekea Dodoma na aliwasili saa 10:00 jioni ambapo alienda moja kwa moja kwa mganga huyo.
“Saa 1:00 jioni Bino alichukua mwiko, ungo na kinu, vifaa anavyovitumia kwenye kazi yake. Ungo aliuweka chini na akaanza kusoma dua kisha nikamuona mtoto amekaa ndani ya ungo ule, nilishtuka sana baada ya kumwona akiwa hana hata nguo, amechafuka na aliyechoka,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, mtoto alibaki kwa mganga huyo kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.
Alisema alikaa kwa mganga huyo kwa muda wa siku mbili na kurudi Dar es Salaam na kumuacha mtoto huko kama alivyotakiwa.
“Jana aliletwa na Bino ili aje kutusalimia kwa kweli nashukuru Mungu kwa sababu hali ya mwanangu inaendelea vizuri, afya yake ipo vizuri, ” alisema.
Baba wa mtoto huyo, Joseph, alisema kuwa tukio hilo ni la kwanza na la aina yake kwenye ukoo wao na kwamba lilipotokea hakuna aliyeamini hadi walipomuona mtoto.
Alisema baada ya mtoto wake kuletwa, majirani ambao walishiriki kwenye msiba wake, walishtuka na kujaa nyumbani kwake kitendo ambacho kiliwalazimu kwenda polisi kutoa taarifa ya kile kilichotokea.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Suhunyi (CCM), Wilaya Siha, mkoani Kilimanjaro, Moses Kileo , amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Mjini Moshi akiwa mahututi baada ya kuvamiwa na kutekwa na kundi la watu wasiojulikana na kukata sehemu ya uume wake na kutokomea.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Godfrey Kamwela, alisema Mwenyekiti huyo alinusurika kifo baada ya watu hao kutaka kipande cha juu cha uume wake, kwa kile alichoeleza huenda kinatokana na imani za kishirikina.
“Bado tunawasaka waliohusika kumteka na kisha kumkata Moses kiungo chake kutokana na imani za kishirikina. Nimeagiza polisi kuhakikisha watu hao wanapatikana mara moja na kuchukuliwa hatua za kisheria,”  Kamwela.
Alisema Mwenyekiti huyo kwa sasa hawezi kuzungumza kutokana na hali mbaya aliyokutwa nayo na kwamba Polisi wameshindwa kumhoji.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Kileo alikumbwa na mkasa huo, Aprili 10, katika Kijiji cha Kashashi, Wilaya ya Siha.
Alidai kuwa baada ya watu hao kukamilisha zoezi hilo, walimtelekeza kando ya barabara ya Kashashi-Suhunyi, akiwa anavuja damu nyingi na baadae kutokomea na kipande hicho cha uume wake.
NIPASHE
Baadhi ya majengo ya jijini Dar es salaalam yakiwemo ya Halmashauri za Wilaya na shule za kata yapo hatarini kuporomoka na kuleta maafa kutokana na kujengwa chini ya kiwango.
Mchumi wa majengo na mwangalizi wa ubora Lello Didas alisema majengo yatakayopona endapo kutatokea tetemeko,radi au mvua kubwa za mfululizo ni majengo ya umma kwa kuwa yamejengwa kwa ubora unaokubalika.
Alifafanua kuwa tatizo la majengo kutokidhi ubora kunatokana na kutengewa bajeti finyu isiyokidhi viwango hali inayochangia kutafuta mafundi wa mitaani wasio na ujuzi wa kina.
“Kujenga jengo la ofisi ni gharama,halmashauri haina fungu la kutosha na ili ziweze lengo linalotakiwa na uhitaji wa shule za kata ikiwa ni pamoja na maabara wanatumia mafundi wa mitaani ambao ni wa bei rahisi” Didas.
Alisema mfuko mmoja wa saruji unapswa utoe matofali 30 tu na yakizidi idadi ni chini ya kiwango.
MTANZANIA
Chama cha Mapnduzi kimesema kipo tayari kuyaweka kapuni majina ya makada wake sita walioadhibiwa kwa kosa la kuanza kapeni  za kuwania Urais katika uchaguzi mkuu ujao kabla ya muda.
Kimesema hatua hiyo itakuja kama haitapokea ripoti ya kamati ndogo ya nidhamu inayoongozwa na makamu Mwenyekiti wa chama hicho Philip Mangula kabla ya kumalizka kwa muda wa uteuzi.
Tamko hilo la CCM limetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye katika mahojiano kuhusu hatma ya kifungo cha makada hao pamoja na msimamo wa chama kuhusu makada wake wengine wanaodaiwa kutenda kosa kama hilo.
Nape alisema kwa sasa kifungo cha makada hao hakifahamiki kitaisha lini na endapo watatupwa nje ya mbio za kuwnaia urais wanapaswa kijilaumu wenyewe kwa makosa yao ya kukiuka taratibu za chama.
Makada walio katika kifungo ni pamoja na Waziri mkuu wa zaman Edward Lowassa,Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe,Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Stephen Wasira,Naibu Waziri wa Mawasiliano na teknolojia January Makamba na Mbunge wa Sengerema Willium Ngeleja.
HABARILEO
Hatua ya mawakili wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kutengeneza ubishi wa kisheria katika agizo la Polisi la kuwasilisha nyaraka za mali za Askofu huyo, imeelezwa kuwa ni ukaidi ambao hautamsaidia kisheria.
Badala yake, kwa hatua hiyo ya mawakili hao, Jeshi la Polisi limewekewa mazingira mazuri ya kuchukua hatua ya pili ya matumizi ya nguvu katika kutekeleza agizo lao, baada ya hatua ya hiyari kushindikana.
Wakizungumza jana, wanasheria mbalimbali walishangazwa na ubishi wa juzi, uliotokana na barua ya mawakili wa Askofu Gwajima kwenda kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Katika barua hiyo, mawakili hao walitaka Polisi itoe agizo la maandishi la kuwasilisha nyaraka hizo, litakaloeleza vifungu vya sheria vinavyomtaka mteja wao kuwasilisha nyaraka hizo.
Ukaidi wa Gwajima Barua hiyo iliyosainiwa na Wakili Peter Kibatala, iliwasilishwa juzi mchana katika jeshi hilo ikiwa ni siku moja baada ya Askofu Gwajima kutakiwa kuwasilisha nyaraka 10 zinazohusu umiliki wa mali zake, Aprili 16 mwaka huu watakapoendelea na mahojiano.
Mawakili hao kwa niaba ya mteja wao wameliomba Jeshi la Polisi kumwandikia barua rasmi Gwajima, wakiainisha nyaraka wanazozihitaji, pamoja na vifungu vya sheria vinavyotumiwa na jeshi hilo kutaka nyaraka hizo.
Mawakili hao wanasema watashukuru kupata hati hiyo ambayo wamedai hawaijui jina, lakini wanaamini Jeshi la Polisi litafahamu jina la kisheria la nyaraka husika inayotumika kumtaka Gwajima, awasilishe nyaraka wanazozihitaji.
Aidha wanasema askofu Gwajima atakapopata nyaraka anayoihitaji, atatimiza mwito na kuchukua hatua stahiki za kisheria.
Nyaraka 10 Nyaraka hizo ni Hati ya Usajili wa Kanisa, Namba ya Usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya Kanisa na muundo wa uongozi wa Kanisa.
Nyingine ni Waraka wa Maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za Kanisa na nyaraka zinazoonesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari.
HABARILEO
Mitambo ya kukodi inayotumia mafuta kufua umeme nchini, imemaliza mikataba yake na kuanza kuondolewa nchini na kubaki mmoja wa Aggreko uliopo Ubungo unaozalisha Megawati 50 pekee ambao nao utaondoka miezi mitatu ijayo.
Mitambo iliyoondoka nchini ambayo mikataba yake imeisha, ni pamoja na ile ya Symbion iliyokuwa mkoani Dodoma na Arusha iliyoondoka Juni mwaka jana na wa Dar es Salaam ulioondoka Septemba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Felchesmi Mramba, alisema hayo jana wakati wa ziara ya waandishi wa habari kutembelea vituo vipya vya kuzalisha umeme, ambavyo mpaka kufikia Septemba vitakuwa vikizalisha Megawati 296.
Alisema baada ya kuondoka kwa mitambo hiyo ya kuzalisha umeme, kwa sasa kunazalishwa megawati za umeme 1,226 huku mahitaji yakiwa 940.
Hivyo alisema umeme unaozalishwa ni mwingi, lakini changamoto ni miundombinu ambayo kwa vituo hivyo vipya tatizo la umeme kukatika na nyinginezo zitafikia kikomo.
“Inashauriwa kuwa si vyema kuondoa mitambo yote ya umeme wa mafuta hivyo tutabaki na megawati 60 zilizopo mkoani Mwanza pamoja na ile ya IPTL, ambayo baadaye itazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, “.
Katika ziara hiyo ilianzia katika mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi asili ya Kinyerezi One ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 84, ifikapo Juni umeme wa megawati 150 utaingia kwenye Gridi ya taifa.
Meneja Miradi wa Tanesco, Saimon Jilima, alisema ifikapo Mei mwaka huu, wataanza kutayarisha mitambo hiyo iliyojengwa kwa fedha za ndani kwa asilimia 95, kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa.
HABARILEO
Abiria waliolazimika kuanza safari juzi mchana badala ya alfajiri kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mikoani, hasa wa mikoa ya mbali wamejikuta wakikabiliana na adha na taabu ya kuchelewa kutoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo, kutokana na mgomo wa madereva.
Taarifa zilizofikia gazeti hili, zilieleza kuwa baadhi ya abiria hao walijikuta wakidamkia katika kituo hicho, wakashinda katika mabasi, wakalala katika mabasi hayo na katika vituo vya mabasi na kuiona asubuhi ya jana wakiwa ndani ya mabasi hayo, huku wengine wakiwasili jana mchana.
Kaskazini Abiria waliokuwa wakienda mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha, walitaabika na usafiri na wengine walijikuta wakipoteza mizigo baada ya kufika usiku.
Baadhi ya mawakala wa mabasi ya mkoani Kilimanjaro, walisema kuna abiria walilazimika kulala katika Kituo Kikuu cha Mabasi mjini Moshi, baada ya kukosa usafiri wa kwenda katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.
“Unafahamu abiria hujipangia nauli ya kwenda wilayani mfano Rombo, Siha maeneo kama Kibosho na Mwika, lakini kuna muda maalum wa kupata usafiri na abiria akichelewa, ina maana hana njia nyingine zaidi ya kulala katika nyumba za wageni, wale wasio na uwezo walilala stendi,” alisema Wakala wa Mabasi ya Capricorn, Juma Ibrahim.
Ilielezwa kuwa abiria wengine walipoteza mizigo ama kwa kuibiwa au kuchukuliwa na abiria wasio waaminifu, kutokana na muda waliofika na uchovu.
Mawakala hao walisema mabasi ya Dar es Salaam yalianza kuingia mjini Moshi kuanzia saa 3.30 usiku na mengine yalifika saa 6 usiku jambo ambalo lilileta changamoto kwa abiria.
Pamoja na adha hiyo, mawakala hao walidai safari za usiku zina faida na hasara zake, mfano walidai kuwa basi linaposafiri usiku, madereva huwa makini zaidi ambapo mwanga wa taa ya gari humlazimu kwenda taratibu na magurudumu hayapati moto kama mchana wakati wa jua.
Wakala wa mabasi ya Stamil, Omary Mpemba, alidai kuwa kutokana na hali hiyo ya kusafiri usiku, ikiwemo uwepo wa magari machache, ajali hupungua ingawa pia hasara zake ni kubwa kukitokea utekaji wa mabasi au ajali kwa kuwa abiria hukosa msaada wa haraka.
Kanda ya Ziwa Mabasi yaliyokuwa yakitokea Dar es Salaam yaliwasili jijini Mwanza kuanzia jana saa 5.30 asubuhi hadi saa 7.30 mchana.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...