NIPASHE
Utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Dunia
kwa robo ya kwanza ya mwaka kuhusu hali ya kiuchumi barani Afrika,
umeonyesha kuwa Tanzania ni kati ya nchi barani humo ambazo bado zipo
imara kiuchumi ndani ya kipindi hicho.
Hata hivyo,
baadhi ya nchi zikiwamo
zinazozalisha na kusafirisha kwa wingi nje bidhaa ya mafuta, zinatarajia
kuonja makali ya mdodoro wa uchumi ndani ya mataifa hayo tangu kipindi
hiki hadi mwaka ujao.
Matokeo ya utafiti huo kwa kipindi cha
robo ya kwanza ya mwaka 2015, yaliyotolewa jana na taasisi hiyo ya fedha
duniani kwa kurushwa moja kwa moja kwa nchi zote zilizopo kusini mwa
Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo , kutoka Washington DC, Marekani.
Akitoa taarifa hiyo, Mchumi kiongozi wa Benki ya Dunia (WB), kwa upande wa Bara la Afrika, Punan Chuhan, alitaja nchi ambazo zinajimudu kiuchumi mpaka sasa kuwa ni Ivory Coast, Tanzania na Msumbiji.
Alitaja baadhi ya sababu kwa nchi hizo
hasa Tanzania kubaki katika hali nzuri wakati nyingine zikiteseka, kuwa
ni miundombinu imara na utengemavu katika shuguli za uchimbaji wa
madini.
Hata hivyo, huo wa kwanza kutolewa na
benki hiyo ya dunia barani humo kwa mwaka huu kulingana na utaratibu
wake, inaonyesha kuwa hali ya uchumi kwa ujumla barani humo imeshuka
kutoka asilimia 4.5 mwaka uliopita hadi asilimia 4 mwaka huu.
NIPASHE
Zaidi ya akinamama wajawazito 70 katika
kituo cha Afya cha Chikande, Manispaa ya Dodoma wameandamana hadi
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kulalamikia mambo mbalimbali.
Malalamiko yao ni pamoja na kujifungulia
njiani kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda hospitali hiyo na
baadhi yao kukataliwa kufunguliwa geti na walinzi wa hospitali
wanapojisikia uchungu.
Martha Masine, alisema wameamua kuandamana ili kuwasilisha kilio chao kwa uongozi wa hospitali hiyo ili matatizo yao yatafutiwe ufumbuzi.
“Walinzi
wa hospitali ya mkoa wamekuwa wakikataa kuwafungulia geti akina mama
wanaofika hospitalini hapo usiku wakitokea Chikande na kusababisha
baadhi ya wenzetu kujifungulia njiani na kuhatarisha maisha ya mama na
mtoto anayezaliwa,” Masine.
Alisema wamekuwa wakipata shida sana kufika hospitali hapo usiku, ingawa kituo hicho kipo nyuma ya hospitali.
Aidha, alisema wamekuwa wakisindikizana
mmoja wao anaposhikwa na uchungu, lakini wanapofika hospitalini walinzi
wanagoma kufungua mageti na kuwalazimu kurudi kituoni.
Alibainisha kwa nyakati mbili tofauti
akiwa bado katika kituo hicho ameshuhudia akina mama wawili kujifungulia
njiani kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma na mwingine kukataliwa
na walinzi.
“Bado
nipo katika kituo hiki nasubiria kujifungua, muda bado haujafika, lakini
jamani sisi tunapata shida walinzi wa General wanapotukatalia kufungua
mageti, huwa inatulazimu kuanza safari ya kurudi kituoni na kuna siku
tukiwa njiani mwenzetu akajifungua tukamsaidia sisi tuliopo,” Masine.
Rose Atanas ambaye yupo
katika kituo hicho akisubiria kujifungua, alisema changamoto nyingine
ni kituo hicho kuzidiwa uwezo kutokana na kupokea akina mama wengi
kutoka vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Dodoma.
“Kituoni
kuna kinamama wengi kuzidi uwezo wake, kituo kina vitanda 15 na hadi
sasa kuna akinamama zaidi ya mia moja hali inayotulazimu kulala wawili
wawili au watatu na wengine kulala chini na pia kuna wadudu watambaao
kama vile kunguni na papasi,”Atanas.
Alisema mbali na mrundikano huo pia unahatarisha afya zao na unatishia kuambulizwa na magonjwa ya kuambukiza.
“Pia
tuna vyakula vyetu na kujipikia wenyewe kutokana na chakula tulichokuwa
tukikipata kutoka hospitali ya mkoa kusitishwa bila ya kuambiwa sababu
ya kufanya hivyo.
“Hapa
tupo zaidi ya 100 kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma wengine
tunalazimika kulala chini vitanda havitoshi, vyoo vyevyewe matundu yapo
mawili na mabafu mawili yaani tukianza kuoga ni foleni na kwenda msalani
ni foleni,” Rose.
Akijibu malalamiko hayo, Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Sista Cesilia Sanya, aliwaahidi akinamama hao kuwa suala la walinzi kutofungua geti halitajirudia.
Hata hivyo, alisema hospitali imepokea
malalamiko ya akina mama hao na walinzi waliobainika kufanya vitendo
hivyo watachukuliwa hatua.
MWANANCHI
Maiti 13 kati ya 19 za watu waliopoteza maisha katika ajali ya Basi la Nganga Express na lori iliyotokea juzi eneo la Iyovi, Milima ya Udzungwa mkoani Morogoro wamezikwa jana katika kaburi la pamoja eneo la Msamvu mkoani hapa.
Simanzi na vilio vilitawala katika eneo
hilo wakati miili ya watu hao ilipofikishwa hapo saa saba mchana kabla
ya mazishi hayo kuanza ya saa 8.30 mchana.
Viongozi wa dini zote walifanya misa za
kuwaombea marehemu hao waliopoteza maisha katika ajali hiyo ambayo baada
ya kutokea, basi na lori hilo aina ya Fuso yaliteketea kwa moto na
abiria waliokuwamo.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele alisema tukio hilo ni la kusikitisha na la tofauti ambalo limeitia simanzi nchi nzima.
“Ni tukio la nadra sana, lakini pia naweza kusema ni la kizembe kwa sababu tayari tumejua chanzo cha ajali hiyo,” .
Henjewele alisema wamepata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu madereva wanaoendesha magari ovyo.
“Nawapongeza vijana wa eneo hili kwa kusaidia kutoa miili kwenye magari licha ya kuwa moto ulikuwa unawaka,” alisema Henjewele katika mazishi hayo yaliyohudhuriwa pia na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe.
Miili ya abiria wengine sita,
imetambuliwa na ndugu zao ilikohifadhiwa katika Hospitali ya Mtakatifu
Kizito, Mikumi Wilaya ya Kilosa.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam limekiri kupokea barua iliyotolewa na mawakili wa Askofu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ya kulitaka kuonyesha kifungu cha sheria kinachomtaka mtu kutoa hati ya mali anazozimiliki.
Hata hivyo, jeshi hilo limekataa
kuzungumzia chochote kuhusu barua hiyo, lakini limeahidi kuijibu baada
ya kuwasiliana na mpelelezi wa kesi hiyo na mwanasheria wa Serikali.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema barua imeshapokewa, lakini hawezi kuijibu kwa haraka.
“Siwezi kujibu barua hiyo kwa sasa, tutakapokaa na kujadili ndipo tutakapopata jibu la kutoa juu ya barua hiyo.
“Haya
mambo yote yanaenda kisheria, hivyo tunatakiwa tukutane na mpelelezi wa
kanda pamoja na mwanasheria wa Serikali muda wowote kuanzia sasa ili
tuijadili barua hiyo na kuweza kuipatia majibu,” Kova.
Aprili 16, mwaka huu, Jeshi la Polisi
lilimtaka Askofu Gwajima kupeleka nyaraka 10 za mali anazomiliki ikiwamo
helkopta baada ya kumaliza mahojiano yao yaliyofanyika Aprili 9.
Nyaraka hizo ni pamoja na hati ya
usajili wa kanisa, bodi ya baraza la wadhamini wa kanisa, idadi ya
makanisa anayomiliki pamoja na matawi yake.
Nyingine ni za muundo wa utawala wa
kanisa, waraka wa maaskofu, hati za kanisa, nyumba na mali za kanisa
pamoja na mpigapicha za video za kanisa.
Machi 26, mwaka huu, Askofu Gwajima
alijisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam baada
ya kutakiwa na jeshi hilo kufanya hivyo kwa tuhuma za kumkashifu Askofu
wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
MTANZANIA
Serikali imeshindwa kuweka wazi kufungwa kwa shule zake za sekondari kutokana na ukosefu wa chakula unaozikabili.
Badala yake imewatupia lawama wakuu wa shule zilizoamua kuwarudisha wanafunzi makwao kutokana na kukosa chakula cha kuwalisha.
Baadhi ya shule za sekondari nchini hivi
karibuni zilifungwa kutokana na kukabiliwa na uhaba wa chakula baada ya
wazabuni kugoma kuwasambazia chakula kwa sababu hawajalipwa fedha zao
kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumannne Sagini alisema mkuu wa shule mwenye mamlaka ya kufunga shule hizo ni Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Alisema Serikali hutoa huduma ya chakula
kwa shule za sekondari za bweni na shule za msingi elimu maalum za
bweni kwa kuzingatia fedha zilizotengwa na upatikanaji wake katika mwaka
husika.
Alisema fedha za chakula hutolewa kwa awamu na kukamilishwa katika kipindi cha mwaka wa fedha unaotekelezwa.
“Kati
ya Julai 2014 hadi Machi 2015, Serikali imetoa Sh bilioni 28.1 kwa ajili
ya chakula cha wanafunzi ambazo ni sawa na asilimia 66.7 ya Sh bilioni
42.1 zilizotengwa kwa mwaka 2014/15,Kiasi kilichobaki ni Sh bilioni 13.9
sawa na asilimia 33.23 ya fedha zilizotengwa,”alisema.
Sagini alisema kiasi hicho cha fedha
hupelekwa katika hamashauri na baadaye wazabuni hulipwa kwa kuzingatia
huduma waliyotoa kwa kila shule.
“Shule
nyingi zilikuwa katika kipindi cha mapumziko mafupi kati ya Machi 28,
hadi Aprili 14, mwaka huu… katika kipindi hiki wanafunzi walitakiwa
kwenda nyumbani kwa ajili ya mapumziko na shule nyingi zimefungua April
8, mwaka huu na nyingine April 12, hivyo wanafunzi walikuwa nyumbani
katika mapumziko mafupi ya kawaida,” alisema.
MTANZANIA
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe,
amesema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, aliugeuza Mkoa wa Morogoro kuwa
wa viwanda lakini kushindwa kusimamiwa kwa sera zake na viongozi wa
Serikali iliyoko madarakani kumesababisha wananchi wake kubaki maskini.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Ndege mjini hapa.
Alisema ndiyo maana ACT- Wazalendo
inaamini katika misingi ya Nyerere inayoleta usawa wa kidemokrasia na
kuimarisha uchumi wa kila Mtanzania.
“Mwalimu
Nyerere aliipenda Morogoro kwa kuigeuza kuwa mkoa wa viwanda lakini leo
hii viwanda vya sukari asilimia 50 hapa na hakuna kiwanda kipya cha
sukari tofauti na alivyovijenga Mwalimu.
“Mtibwa,
Kilombero, Kagera na TPC Moshi vyote vilijengwa enzi za mwalimu, lakini
leo hii viwanda vinapata ushindani mkubwa kutokana na uagizaji wa
sukari kutoka nje ya nchi na hata kuzuiwa viwanda vipya kujengwa,” Zitto.
Alisema pamoja na kujengwa viwanda hivyo
bado vimekuwa vikiwanyonya wakulima wa miwa na hivyo kusababisha kilimo
chao kutofaidisha wakulima wa miwa kama inavyofanyika kwenye bei na
hawana haki ya kujua thamani ya miwa yao.
Kutokana na hali hiyo alisema chama cha
ACT-Wazalendo kinataka kupiga marufuku uagizaji wa sukari bila kodi,
huku akishauri kuanzishwa kwa viwanda vidogo vya miwa na wananchi
wanaolima miwa wote kuwa na hifadhi ya jamii kuweza kuboresha maisha yao
ya sasa na baadaye.
Zitto ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema Mkoa wa Morogoro unazalisha nusu ya sukari nchini.
“Hata
hivyo sukari nchini haitoshi kwani uwezo wetu ni kuzalisha tani 300,000
wakati mahitaji ni tani 500,000. Ili kuhakikisha bei ya sukari inakuwa
himilivu ACT inapendekeza viwanda vya sukari kupewa bei nafuu ya umeme
kama ruzuku,” alisema.
Akizungumzia jinsi Mkoa wa Morogoro unavyochangia katika Pato la Taifa (GDP), Zitto alisema unashika nafasi ya sita kati ya mikoa 21 ya Tanzania Bara lakini bado upo chini kwa maendeleo.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete
amesema hajaletewa majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo kutokana na
mauaji ya maalbino nchini kwa sababu safari ya kisheria ya majina hayo
kufikishwa kwake ni ndefu.
Aliyasema hayo juzi wakati alipozungumza
katika ibada maalumu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Liberatus
Sangu kuwa Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Shinyanga.
Akizungumza katika ibada hiyo
iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini
Shinyanga na mbele ya viongozi wengi wa Kanisa hilo wakiwemo maaskofu
wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, Rais Kikwete alitumia nafasi
hiyo kujibu madai kuwa Serikali yake haichukui hatua za kutosha
kukabiliana na mauaji ya albino.
Pia kufafanua juu ya shinikizo ambalo
linatolewa na baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya serikali yakimtaka Rais
kutia saini ya kuruhusu watu hao wanyongwe.
“Naomba
mtusaidie kuielimisha jamii ili iachane na imani za kishirikina,
Vikongwe wanauawa kwa sababu tu ya kuwa na macho mekundu na ujinga
uliokithiri unaosababisha Watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi
(albino) kusakwa na kuuawa kikatili kabisa.”
“Nawaombeni
sana viongozi wa dini tusaidiane katika kukomesha ujinga huu mkubwa kwa
kutoa elimu kwa waumini wenu, ili wajue kuwa vikongwe wana macho
mekundu kwa sababu ya kutumia samadi ya ng’ombe kupikia kwa muda mrefu
na kuwa kiungo cha albino hakiweza kuleta utajiri wowote,” Rais aliwaambia viongozi hao wa dini.
Kuhusu madai kuwa Serikali yake
haichukui hatua za kutosha kukabiliana na mauaji ya albino, Rais Kikwete
aliwaambia viongozi hao:
Watu 16 tayari wamehukumiwa kifo na
wengine wanasubiri…kesi zao zinaendelea kusikilizwa. Yapo maneno maneno,
lakini binafsi kama Rais sijaletewa majina ya watu hao.” Aliongeza:
“Ni lazima tuelewe jinsi mfumo wetu wa kutoa haki unavyofanya kazi hasa katika eneo hilo la kunyonga ama kutokunyonga.
Ni mlolongo mrefu. Katika kesi za watu
kuhukumiwa kifo, kwanza kukata rufani ni lazima na wala siyo jambo la
hiari ama matakwa ya aliyehukumiwa.
HABARILEO
Serikali imesema ajira za walimu wapya
zitaanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu huku ikiweka wazi kuwa walimu hao
wasitegemee kupangiwa katika maeneo ya majiji, manispaa na miji.
Walimu hao wametakiwa kutotegemea
kupangiwa katika maeneo hayo kutokana na idadi ya walimu waliopo ni
kubwa na inakidhi mahitaji, huku maeneo yaliyopewa kipaumbele ni
vijijini na halmashauri ambazo zina mahitaji na upungufu mkubwa wa
walimu.
Idadi ya walimu wapya watakaoanza ajira
zao mwezi ujao ni 31,056 ambapo kwa walimu wa ngazi ya Cheti ni 11,795,
Stashahada (Diploma) 6,596 na wenye Shahada (Degree) 12,665.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne
Sagini wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajira mpya za
walimu kwa mwaka 2014/2015.
Alisema kwa mwaka huu ajira hizo
zimechelewa kutokana na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kufanya ufuatiliaji wa kina hadi katika ngazi ya shule ili
kubaini kwa uhakika mahitaji halisi ya walimu kwa kila halmahauri na
shule.
“Ufuatiliaji
huo umebaini kuwepo kwa halmashauri na shule hasa za mjini zenye walimu
wa ziada na zingine hasa za vijijini zina upungufu mkubwa wa walimu,” Sagini.
Alisema taarifa hizo zimesaidia
kuwapanga walimu wapya kwa usawa ili kuondoa uwiano usioridhisha kwenye
maeneo mengi ya vijijini.
Alisema kwa sasa wanakamilisha taratibu
za kupata kibali kwa ajili ya ajira za walimu na fedha za kuwalipa
stahili zao ili waanze ajira zao rasmi mwezi ujao.
Aidha, alisema orodha ya walimu na vituo
watakavyopangiwa vitawekwa katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
TAMISEMI ambayo ni www.pmoralg.com na ya Wizara ya Elimu www.moe. go.tz
ifikapo Aprili 24, mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Zuberi Samataba
alisema, pia ufuatiliaji huo ulikuwa ni kuhakikisha wanakuwa na taarifa
sahihi za walimu wanaoajiri wote ni wapya ambao hawajawahi kuajiriwa
ili kuepuka usumbufu kwa walimu ambao hawatoi taarifa.
Alisema baadhi ya walimu ambao
wameshaajiriwa wanapoenda kusoma, hupangiwa upya vituo na hawatoi
taarifa hivyo kuleta usumbufu wa kuchelewa kutopata mishahara yao.
HABARILEO
Kutokana na mgomo wa madereva wa mabasi
ya abiria nchi nzima uliofanyika Ijumaa iliyopita, Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilikuwa limeshaandaa mabasi 300 ambayo yangetumika kusafirisha abiria, imebainika.
Chanzo cha habari kutoka serikalini
kimebainisha kuwa JWTZ ilikuwa imeweka tayari mabasi hayo na kuwa
walikuwa wakisubiri taratibu za kufanya kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na
kujua safari za mabasi hayo na nauli ambayo wangewatoza wananchi.
Taarifa za ndani zinabainisha kuwa mgomo
wa madereva wa abiria ulipangwa kufanyika kwa zaidi ya siku mbili,
jambo ambalo lilifanya serikali kuliandaa jeshi kuwa tayari kutoa huduma
kwa wananchi.
Ijumaa iliyopita, mamia ya abiria katika
maeneo mengi ya nchi walipata madhila na mahangaiko baada ya madereva
wa mabasi ya abiria nchi nzima kugoma, wakishinikiza serikali kubadili
masharti ya kutakiwa kusoma kila wanaposajili leseni zao za udereva kila
baada ya miaka mitatu, na matumizi ya tochi barabarani unaofanywa na
askari wa usalama barabarani.
“Mbali
na kulinda mipaka ya nchi kutoka kwa maadui wa nje, jeshi pia lina
wajibu wa kuimarisha amani na usalama, na pia kufanya shughuli za
kijamii kama vile kuingilia na kutoa huduma fulani muda wowote
wanapotakiwa kufanya hivyo na serikali,” ilibainika.
Huu ni ushahidi kwani JWTZ imekuwa
ikishiriki kusaidia jamii katika masuala mbalimbali wanapohitajika,
ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vyao kujenga madaraja ya dharura,
kuokoa maisha ya watu na kutolea mfano wa mafuriko ya Jangwani mwaka
2011 ambapo Jeshi lilishiriki katika kuwaokoa watu waliokuwa wamekwamba
kwenye nyumba zilizokuwa zimezingirwa na maji.
Chanzo cha habari kimebainisha kuwa Jeshi lina mabasi mengi, na kutoa mfano tukio la hivi karibuni nchini Malawi wakati Rais Peter Mutharika alipotangaza hali ya hatari, JWTZ ilitoa malori 46 yaliyotumika kusafirisha msaada wa mahindi na dawa kwenda Malawi.
Kwa mujibu wa Nyasa Times,
Serikali ya Tanzania ilichangia tani 1,200 za mahindi na dawa za
binadamu katika kuisaidia serikali ya Malawi kupunguza uhaba wa chakula
na magonjwa miongoni mwa maelfu ya Wamalawi kutokana na mafuriko ambayo
yaliikumba nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment