16 April, 2015

KAMA ULIKOSA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI 16 CHUKUA TIME YAKO KUJUA NN KIMETOKEA MAGAZETINI LEO.

topp
NIPASHE
Serikali imepunguza idadi ya masomo kutoka saba hadi matatu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la pili lengo likiwa ni kuboresha mfumo wa elimu nchini.
Masomo ambayo wanafunzi hao watatakiwa kuyasoma ni Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Naibu Waziri wa elimu Kassim Majaliwa alisema alisema hayo wakayi akifungua mafunzo ya mtaala mpya ya walimu wa darasa la kwanza na la pili mjini Dodoma.
Alisema mabadiliko hayo ni kutokana na sera mpya ya elimu iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais Kikwete.
“Zamani wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili walikuwa wanasoma masomo saba, lakini katika sera hii mpya yamepungua na kubaki matatu” MAJALIWA.
Alisema katika sera hiyo mpya mwanafunzi atakayeshindwa kufaulu katika masomo hayo matatu hataruhusiwa kuendelea na darala la tatu.
Alisema vitabuvoye vitakavyotumika kufundishia shule za msingi na Sekondari vitakuwa vya aina moja kila darasa.
NIPASHE
Serikali imetangaza viwango vipya vya nauli za mabasi zitakazoanza kutumika kuanzia Aprili 30, mwaka huu, huku nauli za magari hayo yanayokwenda mikoani zikishushwa na zile za daladala zinazotoa huduma maeneo ya mijini zikiendelea kubaki kama zilivyo.
Nauli hizo mpya zilitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Nchini (SUMATRA), Gilliard Ngewe.
Alisema punguzo la nauli hizo ni asilimia 7.8 kwa daraja la kawaida la chini na asilimia 5.81 daraja la kati.
Ngewe alisema viwango hivyo vimebadilika kutokana na kushuka kwa kwa bei ya mafuta mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, Sumatra imekuwa ikipokea wito wa kupitia upya viwango vya juu vya nauli vilivyowekwa na mamlaka hiyo Aprili, 2013.
Pia alisema wamefanya mabadiliko hayo baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau na wamiliki wa usafirishaji katika mikutano mbalimbali iliyofanyika jijini Mwanza, Dar es Salaam na Arusha.
Alisema Machi 9, mwaka huu, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma Zinazodhibitiwa na Sumatra (SCCC) liliwasilisha kwa Sumatra maombi ya kushusha nauli za mabasi ya masafa marefu na mijini.
Ngewe alisema katika maombi hayo baraza liliainisha sababu za kuomba punguzo hilo kuwa ni kushuka kwa bei za mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi mapya kutoka asilimia 25 hadi 10.
NIPASHE
Wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi katika maeneo mengi nchini, wamepinga vikali tishio la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, la kuzifuta taasisi za kijamii na kidini na kueleza kuwa amekurupuka, hakushauriwa na kushindwa kufuata misingi ya demokrasia na Katiba ya nchi.
Wakizungumza katika maeneo mbalimbali nchini jana, wadau hao walidai kuwa, kufanya hivyo ni kusababisha vurugu na udikteta mkubwa kwa nchi inayoendeshwa kwa misingi ya utawala bora na demokrasia.
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo la Rulenge, mkoani Kagera, Severin  Niwemugizi, alisema amelipokea tamko hilo kama matamshi ya watu ambao hawajakomaa kisiasa, wasio tayari kupokea maoni ya wengine tofauti na yao na kwamba halina haki bali limejaa woga.
“Katika nchi ya demokrasia yenye viongozi wa namna hii hawana tofauti na madikteta, ukianza kutishia wenzako kuwa ukisema maneno nisiyoyapenda nakufuta huo ni udikteta,” alisema na kuongeza:
“Sheria ya kura ya maoni inasema kutakuwa na makundi ya ndiyo na hapana, najiuliza ni kundi lipi la pande hizo, kwanini wawepo wanaozuiwa wasihamasishe watu kusema hapana kama taasisi za serikali zinazoruhusiwa kuhamasisha ndiyo?” alihoji.
Baadhi ya asasi za kijamii na watu binafsi mkoani Arusha, walisema tishio hilo ni udikteta ambao ni aibu kutolewa na viongozi katika nchi inayothamini demokrasia na kwamba inapaswa kukemewa kwa vile ina lengo la kupora uhuru wa kujieleza ambao upo kikatiba.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Utetezi wa Haki za Wafugaji, Warina Asali na Waokota Matunda (Pingo’s Forum), Edward Porokwa, alisema kauli ya Waziri Chikawe ni tishio kubwa linalowanyima uhuru wa kujieleza.
Mkurugenzi wa asasi ya Grassroot Youth Development Organisation (GYDO), Henry Cigwasi, alishauri matamko mengine ya viongozi wa serikali yatolewe baada ya kufanyiwa utafiti.
Alisema maisha yote ya binadamu ni siasa, kila kitu anachofanya ni siasa, hivyo hawawezi kuacha kuzungumzia au kutoa elimu ya uraia bila kuzungumzia masuala muhimu yanayohusu maisha yao.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema inaonyesha waziri alikurupuka bila kushauriana na kwamba siyo kauli inayopaswa kutolewa kwa umma katika zama hizi za demokrasia na siasa huria.
Amekosea, ninachojua serikali haiwezi kufuta Katoliki au KKKT, utajiridhisha umewafutia, lakini dini itaendelea kuwapo, askofu hawezi kufuta ukatoliki wangu, hayo yanatokea kwenye mataifa yenye udikteta pekee,” .
Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar  es Salaam, Bashiru Ally, alisema: “Jukumu kubwa la serikali yoyote ni katika ‘law and order’ na ‘stability’, lakini serikali ya kidemokrasia haitumii mabavu bali unaweza kujenga amani na utulivu kwenye nchi kwa kujadiliana,” .
MWANANCHI
Hoja za kisheria alizowasilisha Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu kutakiwa kuwasilisha nyaraka 10 za utajiri na usajili wa kanisa lake polisi zimezaa matunda.
Sasa, agizo la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam la kumtaka Askofu Gwajima kuwasilisha nyaraka hizo leo limesitishwa kusubiri utatuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
Wakili John Mallya anayemtetea Askofu Gwajima alilieleza gazeti hili jana usiku kuwa baada ya makubaliano na polisi mteja wake leo hatafika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama ilivyokuwa imepangwa mpaka hoja hizo za kisheria zitakapotolewa uamuzi.
Alhamisi iliyopita, polisi ilimtaka Gwajima kuwasilisha vielelezo hivyo, lakini hatua hiyo ilipingwa na kiongozi huyo akieleza kuwa hatapeleka nyaraka yoyote iwapo jeshi hilo halitajibu barua aliyoliandikia kutaka liombe vitu hivyo kwa maandishi.
Nyaraka zilizotakiwa kuwasilishwa polisi ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini, idadi ya makanisa anayohudumia na nyaraka za helikopta ya kanisa.
Nyaraka nyingine ni; muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
Katika barua yake kwa polisi, Wakili Mallya alisema: “Tunaiomba Polisi kumwandikia rasmi mteja wetu kimaandishi nyaraka mnazozihitaji na vifungu vya sheria vinavyotumika na polisi kutaka nyaraka hizo… tutashukuru kupata hati hiyo.”
Mapema alipoulizwa kuhusu kitakachotokea leo, Kamanda Kova alisema: “Suala la Mchungaji Gwajima kwenda na vielelezo alivyoagizwa na Polisi siwezi kulizungumzia hadi hapo itakapotokea hakuja navyo ndipo nitakapotoa tamko langu la mwisho.
MWANANCHI
Mbunge wa Moshi mjini, Philemon Ndesamburo, juzi alifanya tukio la aina yake pale alipomtangaza Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael kuwa ndiye atakayerithi mikoba yake.
Tangazo hilo sasa linavunja minong’ono iliyokuwa imezagaa kwamba Ndesamburo hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya kuliwakilisha jimbo hilo kwa miaka 15 kuanzia 2000.
Ndesamburo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro alimtangaza Michael katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Manyema kuwa ndiye anatamani awe mrithi wake.
“Niwatafutieni mbunge nisiwatafutie? Niwatafutieni mrithi wangu niache? Nimtaje nisimtaje?”, hayo ndiyo maneno aliyoyatumia Ndesamburo kuwauliza wananchi kama amtaje mrithi wake au la.
Mtaniunga mkono kwamba nitakayemtaja ndiye mtakayemsaidia? Jaffar njoo hapa bwana (akimwita Meya). Sasa nawaambia wakati ukifika ndio huyu nitakayemfanyia kampeni,”  Ndesamburo.
Huku akiwa amemnyanyua mkono, Ndesamburo alisema muda ukifika atamleta Michael mbele ya wananchi ili wamfanyie kampeni.
Nimefanya hivi kwa ajili ya kuondoa majungu, kwa ajili ya kuondoa makundi na kwa ajili ya kujenga umoja wa chama chetu,” alisema huku akimsifia kuwa ni mtu msafi na anayewajibika kwa wananchi.
Hata hivyo, katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alipoulizwa jana kuhusu uamuzi huo wa Ndesamburo alisema haikuwa sahihi kumtangaza mrithi akisema ni kinyume cha Katiba yao.
“Ninakubali maoni yake binafsi kama binadamu, lakini kama mwenyekiti wa mkoa haikuwa sahihi kwa sababu hiyo ni kinyume cha Katiba. Akifanya hivyo anaminya demokrasia ndani ya chama,”.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, linawashikilia watu 10 waliokamatwa msikitini wakiwa na vifaa mbalimbali, ikiwamo milipuko 30, sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na bendera nyeusi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonald Paul alisema tukio hilo lilitokea Aprili 14, mwaka huu saa 3.30 usiku katika Kitongoji cha Nyandero, Tarafa ya Kidadu wilayani Kilombero.
Kamanda Paul alisema watu hao walikamatwa katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu, ambapo mmoja kati ya watu hao ambaye anadaiwa kuwa mwenyeji wa kundi hilo, aliuawa na wananchi kwa kuchomwa moto.
Kamanda Paul alimtaja mtu huyo kuwa ni Hamad Makwendo Mkazi wa Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Alisema siku ya tukio, polisi walipata taarifa za watu wanaojihusisha na uhalifu na kuanza kufuatilia tukio hilo na kwamba baada ya kufika eneo la tukio walikuta watu hao wameondoka.
“Askari wetu walipofika pale walikuta watuhumiwa wote wameondoka kwa kutumia usafiri wa bajaji mbili,” Kamanda Paul.
Alisema wakati wakiendelea na ufutiliaji, walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria mmoja ambapo walilazimika kuisimamisha.
Alisema baada ya kuisimamisha bajaji hiyo, mtu mmoja aliruka na kuanza kukimbia ndipo askari mwenye namba F.3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa jambia na kumkata askari huyo shingoni.
Alisema askari mwingine mwenye namba E9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma, alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu mtuhumiwa huyo na kuanguka chini.
Alisema baada ya kuanguka, wananchi wa eneo hilo tayari walikuwa wamefika na kuanza kumshambulia na baadae kumchoma moto.
Hata hivyo, Kamanda Paul alisema iliwalazimu kuongeza askari wengine ili kuwasaka watu wengine ambapo walipata taarifa za uwepo wa watu msikitini humo.
Alisema polisi walipofika katika msikiti huo, waliomba viongozi wa msikiti kuwatoa watu wote waliokuwamo msikitini ili kuwabaini wahalifu kwa sababu wanatiliwa shaka.
Alisema waumini wote walitakiwa kutoka nje ya msikiti wakiwa na mabegi yao, ambapo polisi waliendesha ukaguzi na kufanikiwa kuwakamata watu kumi.
Kwa mujibu wa Kamanda Paul, vitu vilivyokutwa katika mabegi hayo ni pamoja na milipuko 30 na bendera nyeusi iliyoandikwa maneno ya Kiarabu na Kiswahili yenye maana ya Mungu Mmoja.
Vifaa vingine walivyokutwa navyo ni nyaya za umeme, majambia , bisibisi, vifaa vya kujikinga puani (maski), sare moja ya Jeshi la Wananchi na nyingine ambazo hazikujulikana kutoka nchi gani.
Vifaa vingine walivyokutwa navyo ni misumeno, spana ya kufungulia mabomba, madaftari na vitabu mbalimbali vikiwemo vya risiti.
Alisema mbali na vitu hivyo, marehemu alikutwa na risasi sita, kati ya hizo tano ni za Sub Machine Gun (SMG) na moja ni ya bunduki ya Mark IV.
MTANZANIA
Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), kimesema kuwa kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa lengo la kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kubomoa mfumo unaowanyonya wananchi.
Kutokana na hali hiyo, kimewahakikishia Watanzania kuwa ujio wa chama hicho ni wa kuleta mageuzi ya kweli kwa taifa badala ya porojo kama vyama vingine vinavyofanya.
Akihutubia wananchi jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Ukombozi, mjini hapa, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kuwa hivi sasa Taifa limekuwa na shauku ya ACT kushirikiana na vyama vingine kama njia ya kufanikisha malengo ya kukitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), madarakani.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni lazima Taifa lijengwe upya kwa matumaini, ikiwamo kuhakikisha vyama vinakuwa na ushirikiano wa dhati utakaoleta mageuzi ya kimfumo na uchumi kwa Watanzania wote.
“ACT- Wazalendo tunaunga mkono juhudi zozote za kushirikiana kwa vyama na hili linathibitishwa na jina letu, Alliance na msimamo wetu kuhusu mabadiliko ya Katiba.
Kubwa tunataka ushirikiano utakaonufaisha wananchi na si ushirikiano wa kugawana nafasi za uongozi,” Zitto.
MTANZANIA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema kumekuwapo na mafanikio katika vita dhidi ya majangili kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, majangili walivamia kwa kasi na kuwaua wanyamapori wakiwamo tembo na faru, hatua ambayo iliibua tishio la kutoweka kwa baadhi ya wanyamapori.
Juzi Waziri Nyalandu alitangaza kukamatwa kwa silaha za kivita zikiwamo bunduki za AK 47 na SMG katika Pori la Akiba la Rungwa lililopo katika wilaya za Manyoni na Chunya.
Silaha hizo zimekamatwa kutoka mikononi mwa majangili, ambapo katika msako huo, majangili 10 yalikamatwa kabla ya kukamilisha mipango ya kuua tembo.
Akizungumza baada ya kukagua silaha zilizokamatwa, Waziri Nyalandu alisema Serikali kamwe haitarudi nyuma hadi majangili wasalimu amri.
Alisema kukamatwa kwa shehena ya silaha hizo zikiwamo na kivita ni salamu kwa majangili.
Nyalandu alisema hakuna jangili ambaye atakuwa salama iwapo hataweka silaha chini na kuwa Serikali lazima ishinde.
Kaimu Meneja wa Pori la Rungwa, Kwaslema Male, alisema silaha hizo zimekamatwa katika kipindi cha kuanzia Januari 2012 hadi Aprili, mwaka huu, huku idadi kubwa zikiwa zimekamatwa mwanzoni mwa mwaka huu.
HABARILEO
Serikali ya Tanzania inatarajia kufungua ubalozi nchini Kuwait kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha wa 2014/2015.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alipokutana na Shehe Sabah Al-Khalid Al-Sabah, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait, juzi jijini Kuwait City, Kuwait.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili walisifu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili, ambao ni wa kindugu na unalenga kuwanufaisha wananchi wa nchi hizi.
Kwa kufungua ofisi za Ubalozi, Kuwait ushirikiano huu wa kidugu utaongezeka kwenye nyanja zote muhimu na utazaa matunda yatakayo wanufaisha watu wetu, kwa nchi hizi mbili,” Membe.
Kwa upande wa Kuwait, Serikali yao ilifungua ubalozi nchini Tanzania Februari mwaka huu na Jassem Ibrahim Al Najem ndiye Balozi wake wa kwanza nchini Tanzania, mwenye makazi yake Jijini Dar es salaam.
Kwa sasa Tanzania inawakilishwa nchini Kuwait kupitia Ubalozi wake uliopo Riyadh, Saudi Arabia.
Katika mkutano huo, Sabah Al- Khalid Al Sabah alisifu jitihada za Tanzania za kulinda na kuleta amani barani Afrika hususan kwenye maeneo yenye migogoro.
Alisema Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania, sio tu kwenye maeneo muhimu ya maendeleo, lakini pia hata kwenye ulinzi wa amani, kwani ndio changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa.
Kuhusu misaada barani Afrika, viongozi hao walijadili suala la uratibu wa misaada mbalimbali ya Serikali ya Kuwait, ambapo waliangalia uwezekano wa kuanzisha kituo maalum nchini Tanzania kwa ajili ya kusimamia shughuli za uratibu wa misaada hiyo.
JAMBOLEO
Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma imewahukumu mume na mke kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin.
Watuhumiwa hao ni Halid na Marium Mwanzalima wakazi wa eneo la Hazina Wilani humo.
Watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Juni mwaka jana eneo la Hazina kinyume cha sheria.
Kabla ya kutolewa hukumu watuhumiwa hao walipewa muda wa kujitetea ndipo mume akaomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa yeye ni mlemavu wa miguu hivyo hawezi kufanya kazi nzito.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...