HABARILEO
Serikali imewasimamisha kazi katibu viongozi wote wakuu wa Kampuni ya Reli nchini(TRL), kwa kile kilichoelezwa kuwa hujuma ya mabilioni ya shilingi yaliyotumika kununua mabehewa chakavu.
Waliosimamishwa ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiraga na Meneja Mkuu wa Manunuzi wa kampuni hiyo,Ferdinand Soka.
Wakati hayo yakiwakuta hao, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA),Madeni Kipande aliyekuwa amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali, sasa amefukuzwa rasmi.
Hayo yaliwekwa hadharani jana na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta
alipokutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya uchunguzi kuhusu
ununuzi wa mabehewa machavu katika Kampuni ya Reli nchini.
Sitta, mmoja wa wanasiasa wakongwe
aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na uwaziri
tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius K.
Nyerere, alisema mbali ya madudu yaliyoonekana katika kamati iliyoundwa
na mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, waligundua mambo mengi Jumatatu wiki hii.
Yaliyogunduliwa ni pamoja na ukiukwaji
mkubwa wa masharti ya mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo, kwani mzabuni
alilipwa fedha zote, tofauti na taarifa za awali iliyoonesha malipo
yangefanyika kwa awamu.
“Hivyo
wizara ina maoni kwamba mazingira ya utekelezaji wa mkataba huu yana
dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo uzembe,”Sitta.
Akifafanua hilo alisema TRL iliagiza mabehewa ya mizigo 274 ambapo zabuni ilikwenda kwa Kampuni ya Hindustan & Industrial Engineering Limited
ya India, ambapo katika uagizwaji wa mabehewa hayo kulikuwa na uzembe
katika ufuatiliaji kiwandani, pamoja na uzembe katika kuyapokea yakiwa
mabovu.
Alisema mabehewa hayo yalipofikia 150 aliyazuiwa, hivyo 124 yakawa bado hayajafika nchini.
Sitta alisema kwa mujibu wa taarifa
alizonazo ilibidi mpaka sasa asilimia 50 ya gharama ya mabehewa hayo iwe
imeshalipwa, lakini kinyume chake nyaraka zinaonyesha mpaka sasa pamoja
na kuzuiwa kwa mabehewa 124 mzabuni huyo ameshalipwa asilimia 100.
MTANZANIA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vilivyotokea miaka ya nyuma nchini.
Kwa mujibu wa mtandao wa Chadema Diaspora, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa,
alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika mkutano na wanasheria
12 wakubwa nchini Marekani, uliofanyika Bloomington Jimbo la Indiana
kuhusu matukio makubwa ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyogusa
jumuiya ya kimataifa.
Dk. Slaa ambaye yuko ziarani nchini
humo, alisema watu wote watakaokutwa na hatia watapelekwa kwenye
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague nchini Uholanzi, lengo ikiwa kuifanya dunia iishi kwa amani.
“Haki nchini Tanzania iko kwa
watawala. Watu wa kawaida hawaipati, hali hii lazima ikomeshwe. Familia
ya mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa,
marehemu Daudi Mwangosi inahitaji haki. Waliomteka aliyekuwa Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Stephen Ulimboka lazima
wapatikane.
Walioua watu kwenye mkutano wa
Chadema uliofanyika Arusha lazima walipe kwa uhalifu wao. Nimeguswa na
moyo wenu kwa Tanzania. Hili ndilo lengo letu na kwa dunia nzima iishi
kwa amani,” Dk. Slaa.
Naye Dk. Richard Kruss wa Kituo cha Sheria cha Ahlers & Cressman PLLC alisema jinsi nchi inavyoelekea kwenye uchaguzi mkuu kunakuwa na uvunjifu wa haki za binadamu.
Dk. Kruss na taasisi yake, wameahidi
kuongoza timu ya wataalamu wa sheria na mashirika ya haki za binadamu
kuhakikisha wote waliohusika na uhalifu wanawajibishwa.
“Tutafanya
kazi kwa karibu na Taasisi ya Amnesty International, wanaharakati,
taasisi za haki za binadamu, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita
na wataalamu wa sheria wa Chadema kuorodhesha matukio ya uvunjifu wa
haki za binadamu nchini Tanzania,” Dk. Kruss.
Alisema timu yake pia inakusudia kutoa mafunzo ya sheria kwa wanasheria wa Chadema miezi michache ijayo.
MTANZANIA
Vipimo vya kimaabara alivyofanyiwa binti wa miaka 17 ambaye anadaiwa kubakwa na mfanyabiashara na mwimbaji wa muziki wa injili, Emmanuel Mbasha, havijaonyesha kama alifanyiwa kitendo hicho.
Ushahidi huo umetolewa jana na daktari
Migole Mtuka wa Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam katika Mahakama
ya Wilaya ya Ilala.
Mbele ya Hakimu Flora Mjaya, Dk. Mtuka alisema Mei 26, mwaka jana, binti huyo – ndugu wa mwimbaji wa nyimbo za injili, Flora Mbasha, mke wa Emmanuel Mbasha – alifikishwa katika hospitali hiyo na kudai amebakwa.
Dk. Mtuka alisema baada ya kufikishwa
hospitalini hapo, alimfanyia kipimo cha macho na kisha kutaka kumfanyia
kipimo cha kimaabara ambacho hutolewa bure hospitalini hapo.
Alisema hata hivyo binti huyo hakupima kipimo hicho badala yake alirudishwa nyumbani.
“Alirudishwa
hospitalini siku nane baadaye, yaani Juni 3, mwaka jana na
nilipomfanyia kipimo hicho sikuona chochote, nikawajazia katika PF3 kile
nilichokiona,” Dk. Mtuka.
Mara baada ya daktari huyo kumaliza
kutoa ushahidi wake, waliingia mashahidi wengine wawili ndani ya chumba
cha mahakama kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.
Hata hivyo, mahakama haikuweza
kusikiliza ushahidi huo baada ya kupata taarifa za msiba wa mmoja wa
mahakimu aliyewahi kufanya kazi katika mahakama hiyo kabla ya
kuhamishwa.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mjaya
alihairisha kesi hiyo hadi Aprili 20, mwaka huu ambapo itatajwa tena kwa
ajili ya kuwasikiliza mashahidi hao.
Mbasha anadaiwa kumbaka binti huyo
mwenye umri wa miaka 17, ambaye ni shemeji yake kati ya Mei 23 na 25
mwaka jana eneo la Tabata jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akiishi
naye.
Septemba 5 mwaka jana, binti huyo
aliieleza mahakama kwamba alibakwa na shemeji yake huyo kwa awamu mbili
tofauti kabla ya kufanikiwa kukimbia.
Kesi hiyo inasikilizwa mahakamani kwa
siri kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2003
sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu ili kulinda haki ya
binti huyo.
NIPASHE
Kashfa ya uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imemuweka katika wakati mgumu Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja,
baada ya wananchi wa jimbo lake kumuweka kiti moto wakimtaka atoe
maelezo ya kina kuhusu Sh. milioni 40 alizopewa na mmiliki wa Kampuni ya
VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira.
Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala, alikumbana na wakati mgumu wakati akizungumza na wananchi wa
jimbo lake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya
Shule ya Msingi Pambalu ambao walipata fursa ya kumuuliza kihusu fedha
za akaunti ya Escrow.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika
Jumanne wiki hii, mkazi wa Sengerema mjini, James John, alimuuliza
Ngeleja fedha alizopewa na Rugemalira zimesaidiaje katika miradi ya
Jimbo la Sengerema.
“Wakati
unahojiwa na Baraza la Maadili la Viongozi wa Umma, ulisema fedha hizo
baadhi uligawa katika makanisa na misikiti je, zilizobaki tueleze
zimesaidia katika mradi gani kwenye jimbo la Sengerema, tutajie hata
mradi mmoja,” John.
Ngeleja baada ya kuulizwa swali hilo,
alidai kuwa fedha alizopewa ulikuwa ni msaada kutoka kwa rafiki yake
Rugemalira, na kwamba alilipa kodi ya serikali Sh. 13,138,125 na kiasi
cha Sh. 27,286,875 kilichobaki alichangia harambee kwenye makanisa na
misikiti jijini Dar es Salaam.
Alisema fedha nyingine alichangia ofisi
za vyama vya siasa majimboni, vikundi vya wajasiriamali na shughuri za
maendeleo jimboni mwake huku akionyesha baadhi ya majina ya watu
walionufaika na misaada hiyo.
Ngeleja aliwataka wananchi hao kuacha
kusikiliza maneno ya wanasiasa ambao alidai walilenga kumchafua kutokana
na kashfa ya Escrow akidai wapo viongozi waliopata mgawo katika sakata
hilo na kumtaja aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe,
kwamba hajaguswa.
“Nina
vielelezo na ushahidi kuhusu Zitto Kabwe…mtakumbuka Mheshimiwa
Livingistone Lusinde (Mbunge wa Mtera (CCM) alimtuhumu Zitto kupokea
msaada wa zaidi ya Shilingi milioni 30 kutoka kampuni ya Pan African
Power Limited, maarufu kama PAP,” .
Wakati Ngeleja akijitetea baadhi ya wananchi walikuwa wakimzomea na kumweleza kuwa hawadanganyiki huku wengine wakimshangilia.
Licha ya Ngeleja kujitetea kwa takribani
saa moja, wananchi hao walionekana kuchachamaa kutokana na ahadi ya
upatikanaji wa maji safi na salama ambayo yamegeuka kuwa hadithi kwao.
“Naomba
mnisikilize kwa makini…huyu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) hakumtaja mtu yeyote kwamba alipata fedha kinyume cha
utaratibu…isipokuwa lilipofika kwenye kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), lilikuzwa…na mengine yalikuwa yakitolewa kwenye
magazeti,” Ngeleja.
NIPASHE
Tanzania itetangaza kuwarejesha nchini raia wake wanaoishi Yemen, kufutia mapigano yanayoendelea nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitangaza uamuzi huo wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Yemen, Ali Ahmed Saleh, jana.
Waziri Membe alisema ni jukumu la
Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi,
wanarejea nyumbani salama.
Awamu ya kwanza ya kurudisha Watanzania
ilianza siku chache zilizopita chini ya uratibu wa Ofisi za Ubalozi wa
Tanzania mjini Mascut, Oman.
Kwenye awamu hiyo Watanzania 25 walirudishwa nyumbani huku jitihada za kuandikisha wengine zikiendelea.
“Nimeruhusu
matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye
hatari na machafuko ya Yemen wanarejeshwa salama nyumbani mara moja,” Membe.
NIPASHE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paulo Makonda, kuwasilisha utetezi wake dhidi ya kesi ya madai iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti CCM mkoa Dar es Salaam, John Guninita.
Kesi hiyo namba 68 ya 2015, Makonda
alitakiwa kuwasilisha utetezi wake mahakamani jana, lakini wakili
kupitia wakili wake, Lusiu Peter, ameomba Mahakama kumuongezea muda.
Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa amekubali ombi la utetezi na ametoa siku saba kwa Makonda kuwasilisha uetetezi wake hadi Aprili 23, mwaka huu.
Hakimu Riwa alisema kesi hiyo itatajwa Aprili 27,mwaka huu.
Katika kesi ya msingi, Msindai na
Guninita wanaiomba mahakama hiyo kumuamuru Makonda awaombe msamaha na
kumlipa kila mmoja Sh. milioni 100.
Wanadai fidia hiyo kutokana na maneno
ya kuwadhalilisha yanayodaiwa kutolewa na Makonda kama Katibu
Uhamasishaji na Chipukizi wa CCM katika mkutano wake na waandishi wa
habari.
Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Benjamini Mwakagamba,
wanaiomba Mahakama pamoja na mambo mengine itoe zuio la kudumu kwa
Makonda asizungumze tena maneno ya kashfa wala kuyasambaza kama
alivyofanya awali.
MWANANCHI
Wakati msikiti wa Sunni uliopo Kidatu wilayani Kilombero ukimkana Hamadi Makwendo
aliiyeuawa katika tukio la kuwakamata watu 10 wanaotuhumiwa kuhusika na
vitendo vya ugaidi, dereva wa bajaji iliyowabeba baadhi ya watuhumiwa
hao, amemuelezea mtu huyo kuwa alikuwa hana shughuli za kikazi zaidi ya
kucheza karate.
Polisi aliyejeruhiwa kwenye sakata hilo
na ambaye amehamishiwa kwenye hospitali ya polisi mjini Morogoro, pia
amesimulia mkasa uliosababisha ajeruhiwe huku kukiwa na taarifa kuwa
watuhumiwa hao 10 wamehamishiwa jijini Dar es Salaam kwa mahojiano
zaidi.
Watu hao walimakatwa mapema juzi usiku
kwenye msikiti wa Sunni uliopo Kidatu baada ya wasamaria wema
kulitaarifu Jeshi la Polisi kuhusu kuwapo kwa watu wanaojihusisha na
vitendo vya uhalifu.
Habari za uhakika zilizopatikana ndani
ya Jeshi la Polisi zinasema watuhumiwa hao wamehamishiwa jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kamanda wa polisi wa mkoani hapa, Leonard Paul
hakupatikana kuzungumzia suala hilo na hata alipotafutwa kwa simu,
mlinzi wake alipokea na kueleza kuwa bosi huyo wa polisi alikuwa kwenye
kikao kuanzia asubuhi na hakujua angemaliza wakati gani.
Mmoja wa viongozi wa msikiti wa Masjid Salah Al – Fajih, Mohamed Manze
alisema wao kama viongozi na waumini hawakuwa na taarifa zozote za ujio
wa watuhumiwa hao, na kwamba katika msikiti huo wapo vijana wanne ambao
huwa wanalala na kujisomea.
Alisema siku ya tukio watuhumiwa hao
walifika msikitini hapo saa 4:00 usiku wakati ibada ya mwisho ikiwa
imeshafanyika na waumini kutawanyika.
Alisema walitumia mwanya huo kuingia na
kujihifadhi bila taarifa zozote kwa uongozi wa msikiti huo, jambo ambalo
ni kinyume na utaratibu za msikiti.
Hata hivyo, kiongozi huo alisema
hawakupendezwa na suala hilo na kwamba limewachafua na kuwaharibia sifa
waumini na msikiti wao. Alisema mtu aliyeuawa hakuwa muumini wa msikiti
huo na hafahamiki.
Alisema hawana nasaba na kikundi
chochote kinachojihusisha na uhalifu, na kulaani vikali watu wanaotumia
dini hiyo katika masuala aliyoyaita kuwa ya kihalifu.
MWANANCHI
Moja ya magari yanayotumiwa na chama cha ACT Tanzania baada ya kugonga na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoani Tabora Susan Kaganda
alisema gari hilo lilikuwa linaendesha na mmoja wa madereva
anayejulikana kwa jina la Mabona Kabwe lilikuwa likitokea Nzega kwenda
Tabora mjini.
Alipofika eneo la Magiri lilimgonga
mwanamke mmoja aliyekuwa akivuka barabara baada ya kushuka kwenye gari
alilokuwa amepanda akiwa na mtoto wake wa miezi 10 ambaye aliumia vibaya
na kufariki dunia wakati akitibiwa.
“Gari hilo lilikuwa kwenye mwendo kazi na haikuwa rahisi kuweza kumkwepa mama huyo na kumgonga hapo hapo” Kaganda.
Hata hivyo mama huyo amehamishwa hospitali ya Kitete kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment