Mwana hip hop na Bongo Fleva nchini, Afande Sele, ameweka wazi kwamba
hata kama atakuwa mwakilishi wa wananchi katika bunge la mwakani,
hataweza kuacha kufanya muziki kwa kuwa ndiyo njia ya kumuingizia
kipato.
Alisema licha ya kuwa bungeni, atakuwa akitegemea zaidi fedha
zinazotokana na muziki wake badala ya kufikiria mishahara minono na
posho zinazopatikana bungeni.
“Kazi yangu ya muziki siwezi kuiacha, ndiyo itakayoniongoza katika
maisha yangu, kwa kuwa nitakapokuwa bungeni licha ya kuwa na utetezi
mwingine kwa wananchi, lakini pia nitapinga na kukataa posho na
mishahara minono wanayopata wabunge kiasi kwamba wanasahau
walipotokea,’’ alieleza Afande
Afande, ambaye sasa ni mwanachama wa chama Kipya ya ACT, aliongeza
kwamba ili wasanii waweze kuwatumikia vema wananchi, baada ya kuwa
wabunge lazima wakatae posho na mishahara minono.
“Wasanii wengi waliopo bungeni wanajisahau kwa kuwa wanapopata posho na
mishahara minono wanasahau walipotoka na kujitofautisha na wananchi na
ukishachukua fedha hizo huwezi kuwatetea wananchi, lakini mimi nikienda
huko nitapiga vita dhidi ya posho na mishahara hiyo minono ili fedha
hizo zielekezwe kwenye shughuli nyingine za maendeleo,’’ alieleza.
Aliongeza kwamba hatajali hata akilipwa kiasi kidogo cha mshahara kwa
kuwa lengo lake la utetezi litakuwa limekamilika na wananchi wengi
Tanzania watanufaika nalo kama posho na mishahara minono itapunguzwa ama
kufutwa kabisa.
No comments:
Post a Comment