Barcelona wamefika fainali ya Copa
del Rey baada ya kutoka sare na klabu ya Gary Neville Valencia na
kukamilisha ushindi wa jumla wa 8-1.
Barca walitoka sare 1-1 na
Valencia kwenye mechi ya marudiano katika uwanja wa Mestalla. Mechi ya
kwanza walikuwa wamepata ushindi wa 7-0 uwanjani Nou Camp, ushindi
uliowafanya wengi kutoa wito kwa Neville, nyota wa zamani wa Manchester
United, kujiuzulu.Valencia ndio waliotangulia kufunga mechi hiyo ya Jumatano kupitia Alvaro Negredo.
Lakini nguvu mpya wa Barca Wilfrid Kaptoum alisawazisha dakika za mwisho na kumnyima Neville ushindi.
Matokeo hayo yana maana kwamba Barcelona sasa hawajashindwa katika mechi 29, ambayo ni rekodi Uhispania.
Wapinzani wao kwenye fainali watakuwa mshindi kati ya Celta Vigo na Sevilla.
Sevilla wanajivunia uongozi wa 4-0 kabla ya mechi hiyo ya Alhamisi.
Neville hajashinda mechi hata moja tangu kuchukua usukani Valencia tarehe 2 Desemba.
Alikuwa ameweka wazi kwamba ataangazia zaidi mechi ya Jumamosi ya La Liga dhidi ya Espanyol na alibadilisha sana kikosi chake, ingawa Barca pia hawakuchezesha wachezaji wao nyota.
Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar wote walipumzishwa na Luis Enrique.
Ni mashabiki 16,200 pekee waliofika uwanjani Mestalla kutazama mechi hiyo. Uwanja huo hutoshea mashabiki 55,000.
No comments:
Post a Comment