19 January, 2016

Serikali yatoa Tamko Kuhusu Mwenendo Wa Ugonjwa Wa Kipindupindu Nchini


Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara yangu iliahidi kuendelea kutoa taarifa kwa umma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini kila wiki.

Kuanzia Mwezi Agosti 2015 ugonjwa ulipoanza hapa nchini hadi tarehe 17 Januari 2016, jumla ya watu 14,105 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 218 wamepoteza maisha kwa ugonjwa huu.

Karibia mikoa yote ya Tanzania Bara ilikwisha athirika na ugonjwa huu isipokuwa mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mtwara ambayo haijawahi kuripoti mgonjwa yoyote wa kipindupindu.

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, kuanzia tarehe 11 hadi 17 Januari 2016, kulikuwa na wagonjwa wapya 549 na vifo 10 na mikoa ambayo imeripoti kuwa na ugonjwa imeongezeka kutoka 11 hadi 16 ukilinganisha na wiki iliyopita.

Mikoa hiyo iliyoongezeka kwa kurudia kuripoti wagonjwa wapya baada ya kudhibiti ugonjwa kwa wiki zilizopita ni Dar es Salaam, Lindi, Rukwa, Kagera na Kilimanjaro.

Mikoa mingine ambayo bado imeendelea kuripoti wagonjwa ni pamoja na Morogoro, Arusha, Singida, Manyara, Pwani, Dodoma, Geita, Mara, Tanga, Mwanza na Simiyu.

 Kati ya hiyo, mkoa wa Morogoro umeendelea kuongoza kwa kuripoti idadi kubwa ya wagonjwa (Manispaa ya Morogoro 120, Halmashauri ya Morogoro 40), ukifuatiwa na Simiyu (Bariadi 50), Manyara (Simanjiro 41), Mwanza (Ukerewe 24) na   Halmashauri ya Arusha (19).

Ndugu Waandishi wa Habari,
Napenda kuikumbusha jamii kuwa kipindupindu ni ugonjwa unaoambukizwa kwa kula chakula au kinywaji chenye vimelea ambavyo hupatikana kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote kilichochafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.

Aidha dalili kuu za ugonjwa huu ni kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji meupe kama maji yaliyooshea mchele na kinaweza kuambatana na kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu.

Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapata huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji.

Vilevile, jamii ina fursa ya kujifunza  zaidi  kuhusu ugonjwa wa kipindupindu kupitia njia ya simu kwa kupiga namba   117 na kusikiliza ujumbe wa sauti au kuandika neno “kipindupindu/cholera” kwenda namba 15774 ili kupata habari zaidi. Hakuna malipo kwa mtumiaji wa huduma hii.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea kusisitiza kwa jamii kuzingatia yafuatayo:

-  kunywa maji yaliyo safi na salama
- kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama
-  kunawa mikono kwa sabuni na maji safi  yanayotiririka.
- kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa.

Napenda kurudia kutoa agizo kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji wake kote  nchini kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa kwa mlipuko ambazo ni pamoja na:
  1. Ushirikishwaji wa viongozi ngazi mbali mbali, hasa ngazi za Halmashauri kwa kushirikisha madiwani na viongozi wa kata, vijiji, na mitaa.
  2. Mamlaka husika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na uwekaji wa dawa ya klorini kwenye maji na kupima usalama wa maji mara kwa mara.
  3. Upatikanaji wa dawa za kutibu maji (Water Guard, Aqua Tabs) katika maeneo ya mlipuko.
  4. Juhudi kubwa ziongezwe kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya vyoo bora kwa kila kaya.
  5. Uelimishwaji wa Baba na Mama Lishe, na wauzaji wengine wa vyakula kuhusu kanuni za afya.
  6.  Kusimamia utekelezwaji wa Sheria ya Afya ya Mazingira na Sheria ndogo ndogo (By-Laws).
  7.  Uhamasishaji wa Wananchi wanaopata ugonjwa kuwahi kutumia maji ya chumvi  chumvi (ORS) na kuripoti mapema katika vituo vya huduma
  8.  Ushirikishwaji wa wadau mbali mbali huko Mikoani, Wilayani, na kwenye Halmashauri, ikiwemo Sekta Binafsi, na Viongozi wa dini, katika jitihada za kupambana na Kipindupindu.

Hitimisho
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inatoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kila mmoja kutimiza wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa huu.

 Aidha napenda kusisitiza umuhimu wa Mikoa kutuma taarifa sahihi zinazohusu mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu na kuwachukulia hatua kali watumishi watakao zembea au kujaribu kuficha taarifa hizo.

Napenda kumalizia kwa kuahidi kwamba Wizara yangu itaendelea kushirikiana na sekta zote husika pamoja na wadau mbalimbali katika kuudhibiti ugonjwa huu.

 Aidha tunawashukuru wadau wote, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kupambana na Kipindupindu.

Pamoja tukishirikiana tutaweza kuutokomeza ugonjwa huu.

Nawashukuru kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...