Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Mkwasa amesema kwamba uamuzi huo umetokana na kazi nzuri ya Samatta kuitangaza Tanzania na Taifa Stars kimataifa.
“Anastahili kuwa Nahodha wa Taifa Stars kuanzia sasa, na ingawa tumekuwa na Nahodha ambaye anastahili kuendelea, lakini tumeona kitu pekee cha kumlipa Samatta kwa sasa ni beji ya Unahodha,”amesema Mkwasa.
Mkwasa amesema kuanzia sasa Cannavaro atakuwa Nahodha wa kikosi cha wachezaji wanaocheza nyumbani kwa ajili ya michuano ya CHAN, wakati John Bocco atakuwa Nahodha Msaidizi wa Taifa Stars chini ya Samatta.
Samatta ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika katika sherehe zilizofanyika usiku wa Alhamisi ukumbi wa mikutano wa Kimataifa mjini Abuja.
Samatta alipata pointi 127, mbele ya mchezaji mwenzake wa TP Mazembe, kipa Robert Muteba Kidiaba wa DRC, aliyepata pointi 88, wakati mshambuliaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia na timu ya taifa ya Algeria, Baghdad Bounedjah amepata pointi 63.
Mafanikio ya Samatta anayeweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa ukanda w Afrika Mashariki na Kati kushinda tuzo kubwa ya Afrika, yanakuja baada ya kuiwezesha Mazembe kutwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake nane.
Aidha, Samatta sasa ndiye anaweza kuitwa Mchezaji Bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania – bada ya miaka mingi ya kutokuwa na uhakika wa nani apewe sifa hiyo.
Samatta alijiunga na Mazembe mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa msimu mmoja akitokea African Lyon iliyomtoa Mbagala Market, ambayo ilimuibua Kumbagulile FC ya kwao, Mbagala.
No comments:
Post a Comment