31 December, 2015

Nkurunziza: Nitashambulia majeshi ya AU


Rais wa Burundi ametishia kupigana na kikosi cha Muungano wa Afrika cha kulinda amani pindi wanajeshi hao watakapoingia nchini humo.
Akihutubia taifa kwa njia ya radio, rais Pierre Nkurunziza amesema kuingia kwa wanajeshi hao nchini Burundi kutakuwa ukiukaji wa uhuru wa taifa hilo na pia shambulizi dhidi ya serikali yake.
Rais huyo alisusia ufunguzi wa mazungumzo ya amani nchini Uganda siku ya Jumatatu.
Nkurunzinza aliyeshinda muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu uliokumbwa na utata na maasi mwezi julai mwaka huu anakana kuwepo kwa visa vya mauaji nchini mwake.
Viongozi wa kidini kutoka kanda ya Afrika Mashariki Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda ambao wamekuwa wakikutana mjini Nairobi ,wameelezea wasiwasi wao na jinsi usalama unavyozidi kudorora katika taifa hilo.
Archbishop wa Gulu, John Baptist Odama, ameiambia BBC kuwa wameiomba serikali ya Burundi kupatia mazungumzo ya amani fursa ya kuwapatanisha mahasimu nchini humo.
John Baptist Odama alisema ''Tunaisihi serikali ichukue hatua za kukomesha mauaji ya kiholela nchini humo.
Tafadhali tunawataka wakomesha mauaji zaidi ya watu.
Njia bora ya kusuluhisha mtafaruku huu ni kwa serikali na upinzani kujadiliana.
Mazungumzo ya amani labda ndio suluhisho la kudumu la pekee la mzozo huu.'' alisema Odama.
Umoja wa Mataifa unakadiria watu 400 wameuawa tangu machafuko kuzuka mwezi Aprili Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kwamba angewania urais kwa muhula wa tatu.
AU huenda ikalazimika kutuma walinda amani bila kupewa idhini na taifa mwenyeji, muungano huo utatumia kwa mara ya kwanza kifungu kwenye mkataba wake, kinachouruhusu kuingilia kati katika mataifa mengine nyakati za hatari kubwa.
Baadhi ya mambo ambayo muungano huo unaruhusiwa kuingilia kati kuzuia ni uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu.
Maafisa wa UN wameonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na hatari ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mauaji mabaya zaidi yalitokea Ijumaa wiki iliyopita wapiganaji waliposhambulia maeneo ya jeshi Bujumbura.
Jeshi lilisema watu 87 waliuawa.
AU hata hivyo bado itahitaji kupewa idhini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati.

No comments:

Post a Comment

Samsung kurejesha fedha kwa wanunuzi wa Note 7

KAMPUNI ya Vifaa vya Elektoriniki ya Samsung ya Afrika Mashariki (SEEA) itarejesha fedha kwa wateja wa simu za Note 7, ambao wataweza kuthib...