Pamoja na kupanda kwa bei za pembe za ndovu kuanzia mwaka 2010
kufikia mwaka 2014, thamani ya meno ya tembo imeshuka kwa kiasi kubwa
nchini China jambo ambalo ni habari njema kwa Tanzania katika harakati
zake kukomesha ujangili wa pembe za ndovu.
Taarifa mpya ya utafiti uliofanywa na watafiti Esmond Martin na
Lucy Vigne wa shirika la Save the Elephants na kutolewa wiki hii
imeainisha kwamba bei za meno ya tembo ghafi nchini China zimeshuka kwa
zaidi ya nusu katika kipindi cha miezi 18 iliyopita kutoka dola za
Marekani 2,100 kwa kilo moja hadi kufikia dola 1,100. Katika utafiti wao
uliofanya katika majiji nane nchini, watafiti hao wamegundua kwamba
mahitaji ya meno ya tembo na bidhaa zitokanazo na pembe za ndovu
yanaendelea kushuka kwa kasi kubwa kuliko ilivyowahi kutokea.
Viwanda vinavyotengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na pembe
za ndovu vimeripoti kuwepo na uhaba wa pembe za ndovu na vibali
vinavyotolewa na serikali kuwaruhusu wafanyabiashara kuuza pembe za
ndovu kihalali vimecheleweshwa. Matokeo ya utafiti huu mpya yanaenda
sanjari na ongezeko kubwa la uelewa wa watu nchini China ambapo sasa
sehemu kubwa ya jamii inaelewa madhara ya tatizo la ujangili kwa tembo
wa Afrika na uelewa huu umeongezeka maradufu kati ya mwaka 2012 na 2014
kwa mujibu wa taarifa ya Wildaid, Save the Elephants na African Wildlife
Foundation.
‘Wakati hali hii ikijitokeza, serikali ya China imepiga hatua
kubwa katika kudhibiti soko la pembe za ndovu tangu mwezi Septemba
ambapo Rais wa nchi hiyo Xi Jinping alitangaza kwamba China na Marekani
zitashirikiana kukomesha biashara ya pembe za ndovu. Akizungumza kuhusu
utafiti huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Wildaid, Peter Knights
amesema:
“Kuanguka kwa bei ya pembe za ndovu nchini China ni habari nzuri
tuliyotaka kusikia japo bado kuna kazi kubwa hii ni hatua muhimu sana
katika kukomesha janga la ujangili. Kupigwa marufuku biashara hii nchini
China na Marekani vitatoa shinikizo kwa Hong Kong, Thailand na Japan
nazo kupiga marufuku biashara hii. Pia hii itazipa moyo nchi za Kenya na
Tanzania kuendelea kupambana na ujangili.”
Tangu mwaka 2012, mashirika ya WildAid, Save the Elephants na
African Wildlife Foundation yaliungana kufanya kazi ya uhamasishaji juu
ya ujangili nchini China kwa kuwatumia watu maarufu nchini humo kama Yao
Ming mcheza mpira wa kikapu NBA zamani na muigizaji Li Bingbing ambao
kupitia matangazo mbalimbali wamekuwa wakihamasisha jamii kuacha
kununua, kugawa au kupokea pembe za ndovu kama zawadi. Mashirika makubwa
ya habari nchini China ya CCTV na Xinhua nayo yametoa msaada mkubwa
katika jitihada hizi kwa kutoa matangazo yenye thamani ya dola za
Marekani milioni 42 bure ambapo matangazo hayo yamewafikia mamilioni ya
wananchi wa China.
Vilevile jitihada hizi pia zimesaidiwa na Mwanamfalme wa
Uingereza Prince William ambaye alitoa hotuba ya kihistoria mwezi Oktoba
na kuwaomba wananchi wa China kukataa kabisa biashara ya pembe za
ndovu. Akizungumza kuhusu anguko hilo la bei ya meno ya tembo Balozi wa
WildAid Jacqueline Mengi amesema:
“Upunguaji wa mahitaji ya pembe za ndovu huko nchini China ni
ishara kwamba jitihada za Wildaid pamoja na serikali za nchi tofauti
zinaendelea kuzaa matunda. Mwaka jana tulizindua kampeni maalum ya
kuongeza ufahamu na kuielimisha jamii kuhusu tatizo la ujangili
linaloikabili Tanzania. Kwa matokeo ya utafiti huu ni dhahiri kwamba
mwamko wa kulinda tembo wetu umeongezeka.”
Mashirika ya WildAid, African Wildlife Foundation na Save the
Elephants yamekuwa yakiipa shinikizo kubwa Hong Kong nchi inayodaiwa
kuwa kituo kikubwa cha biashara hiyo duniani. Baada ya mashirika hayo
hivi karibuni kutoa filamu iliyochukuliwa kwa siri ikionyesha jinsi
ambavyo Hong Kong imeshindwa kudhibiti biashara hiyo haramu, maafisa wa
serikali hiyo wameonyesha dalili za kuwa tayari kukomesha biashara hiyo
jambo ambalo linaungwa mkono na Baraza a Sheria la Hong Kong.
No comments:
Post a Comment